Aisha Yerima: 'Kwanini niliamua kurudi Boko Haram hata baada ya kutoroka'

Aisha Yerima

Chanzo cha picha, A T Nwaubani

Katika mfululizo wetu wa barua kutoka kwa waandishi wa Kiafrika, mwandishi wa habari na mwandishi wa riwaya Adaobi Tricia Nwaubani anazungumza na mwanamke mmoja kuhusu maisha yalivyokuwa wakati akiishi na wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram katika maficho yao msituni kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Mnamo mwaka wa 2017, Aisha Yerima alishangaza familia yake alipokubali kurejea katika mikono ya Boko Haram baada ya kuachiliwa huru na kundi hilo. Miaka minne baadaye na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 30 sasa ametoroka na kurejea nyumbani kwa wazazi wake huko Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno.

Alitekwa nyara na Boko Haram akiwa na umri wa miaka 21 kutoka mji wa kusini-mashariki mwa Maiduguri na kwenda kuolewa na mmoja wa makamanda wa kundi hilo, ambaye alisema alimpenda kwa dhati na kumvutia kimapenzi na zawadi zake.

Alikuwa ameenda vitani wakati wanajeshi waliposhambulia kambi yao katika Msitu wa Sambisa, na kumuokoa Aisha na makumi ya wanawake waliokuwa wake za wanamgambo wa kundi hilo.

Wanawake wote waliwekwa katika mpango wa mwaka mmoja wa kuondoa itikadi kali, lakini miezi minne tu baadaye, Aisha aliona kuwa maisha na Boko Haram yalikuwa bora zaidi.

Women and children rescued by Nigerian soldiers from Islamist militants Boko Haram at Sambisa Forest receive treatment - 2015

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Baadhi ya waliookolewa kutoka kwenye mikono ya Boko Haram wanapitia mpango maalumu wa kuondoa itikadi kali

"Ilikuwa vigumu kwangu kupata riziki," aliniambia. "Mambo yalikuwa magumu na ilinibidi kuwategemea wazazi wangu." Pia mwanamke huyo aliona kuwa ni ngumu kulisha mtoto wake wa miaka miwili, aliyeokolewa pamoja naye, mtoto aliyeza na katika ndoa yake na kamanda wa Boko haramu.

"Nilimpigia simu mume wangu na alifurahi sana kunisikia," alisema Aisha.

"Aliniambia lini atakuja Maiduguri kununua mafuta na gesi, na tukakubaliana kwamba nitaungana naye," alisema.

Siku waliyokubaliana, aliondoka nyumbani kwa wazazi wake pamoja na mtoto wake mdogo, bila kumwambia mtu yeyote na kuchukua vitu vichache tu.

Sherehe za milio ya risasi

Alikutana na mume wake mahali pa faragha na akampa pesa za kununua nguo mpya. Alijiunga naye tena mwendo wa saa 1:30 usiku katika eneo tofauti ambapo alikuwa akisubiriwa na wapiganaji wapatao 20 ndani ya basi.

"Wote walikuwa wamejihami kwa bunduki," alisema.

Kisha wakaanza safari ndefu kuelekea msitu wa Sambisa, wakalitelekeza basi hilo kwenye gereji ya mbali kutoka pale lilipotakiwa kuchukuliwa na mtu ambaye wapiganaji hao walikuwa wamemkodi, na kuendelea na safari iliyobaki kwa miguu.

"Tulipofika kwenye kambi yetu msituni, kulikuwa na sherehe. Kila mtu alifurahi kuniona nimerudi na walikuwa wakifyatua risasi," alisema.

Aisha mara moja alianza tena kuisha maisha kama mke wa kamanda - akipewa heshima, na wahudumu maalumu 'watumwa' ambao walikuwa wamwetekwa waliokuwa wakimsaidia kila kitu, yeye na mtoto wake. Muda mfupi baada ya kurudi, alifurahi kujigundua kuwa amepata ujamzito, lakini bahati mbaya mtoto alikufa wakati wa kujifungua.

A soldier

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Jeshi la serikali Nigeria, limekuwa na wakati mgumu wa kulikomboa jimbo la Borno, ambalo lina ukubwa sawa na nchi ya Sierra Leone.

Alipokuwa na mimba nyingine ya miezi miwili, mume wake aliuawa vitani. Wanamgambo hao waliamini kuwa mtoto wake ambaye alikuwa tumboni alikuwa na haki ya kupata sehemu ya mali ya baba yake na hivyo kusubiri hadi mtoto ajifungue kabla ya kugawana urithi.

"Walitaka kuona ikiwa ni mvulana au msichana kwa sababu mvulana ana haki ya kupewa mara mbili ya urithi ambao angepewa mtoto wa kike," Aisha alieleza.

Alijifungua mtoto wa kiume, lakini msiba ulitokea tena. Na huyu nae alikufa wakati wa kuzaliwa. Aisha alikata tamaa.

Kulazimishwa kuolewa tena

Sehemu ya urithi alioupata ilimruhusu kuendelea kuishi vizuri - ingawa hilo liliwafanya watu wengine kuwa na wivu. "Walianza kuuliza kwa nini nifurahie na kuishi peke yangu. Sikutaka kuolewa na mtu mwingine yeyote lakini walinilazimisha kuolewa."

Mume wake mpya alikuwa tajiri pia, mfanyabiashara aliyehusika na usambazaji wa bidhaa kwa Boko Haram, biashara ambayo ilihusisha safari za mara kwa mara kwenda Maiduguri. Alipopata ujauzito mwingine kwa mumewe mpya, Aisha aliogopa sana kupoteza mtoto mwingine msituni.

"Nilimsihi tuhamie Maiduguri, lakini alikataa," alisema.

Map of Nigeria

Tamaa yake ya kuondoka katika msitu huo wakati mapigano yalipozidi, huku mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu yakiwalazimisha wanamgambo hao na familia zao kuendelea kuhama kila mara. Isitoshe, mapigano makali yalisababisha Boko Haram kusambaratika, huku makundi hayo mawili yakizidi kushambuliana. Kwa kuhofia maisha yake na ya mtoto wake aliyekuwa tumboni, Aisha aliamua kutoroka.

Saa 3:00 asubuhi moja mwezi wa Agosti, alitoroka msituni pamoja na mwanawe na wanwake wengine wawili ambao walikuwa wake za wanamgambo na ambao walitaka maisha tofauti. Lakini wote walitekwa njiani na Boko Haram, na kurudishwa kwenye kambi yao. Ili kumzuia asijaribu kukimbia tena, mume wa Aisha na wanamgambo hao walimkamata mtoto wake wa miaka sita na kumpeleka kusikojulikana.

"Wakati wanamkokota mwanangu, alikuwa akinishikilia na kupiga kelele: "Mama, tafadhali, usiniache hapa! Tafadhali, usiniache!" Aisha alisema.

Kwa siku kadhaa, aliwasihi wanamgambo hao wamrudishe na kujaribu kumtafuta bila mafanikio. Hatimaye akili ikambia kwamba jitihada zake hazitaweza kuzaa matunda. Alipopata nafasi nyingine ya kutoroka aliamua kutoroka bila mtoto huyo.

Kutoroka na wema

Kwa kulipa pesa, mwanamgambo ambaye alijua njia ya siri ya kupiaa kwenye msitu huyo ili kutoroka alikuwa tayari kumsaidia yeye na zaidi ya wanawake kumi na wawili ambao walitaka kukimbia. Aisha alimpa pesa zote alizokuwa nazo. Wiki moja baadaye aliwaongoza kupita mbali na kituo cha wanamgambo, kupitia miji ya mbali na kuwaacha mahali ambapo waliweza kuendelea na safari wenyewe hadi kituo cha kijeshi.

"Askari walikuwa wema sana," Aisha alisema.

"Walinisifu kwa kuwa na ujasiri wa kutoroka na kunichangia pesa za kulipa nauli kwenye gari ili kunipeleka nyumbani kwa wazazi wangu. Hawakufikiri kulikuwa na haja yoyote ya kunisindikiza."

Walipofika Maiduguri, ikabidi amuombe dereva asimame ili ampigie simu mama yake na kumuuliza njia kwani jiji lilikuwa limebadilika sana muda ambao hakuwepo: "Kulikuwa na madaraja mapya ya barabara za juu na barabara za lami kila mahali."

Three girls

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Zaidi ya watu milioni 2 wameyakimbia makazi yao kutokana na uasi wa Boko Haram , wengi wakikimbilia Maiduguri

Familia nzima ilikuwa mwakati ndugu mkubwa kati ya ndugu zake wanane walipopita kwenye mlango wa mbele. Walimkimbilia Aisha na kumkumbatia.

Kila mtu alikuwa mwenye fadhili na msaada tangu aliporudi, Aisha alisema, huku baadhi ya majirani wakimchangia pesa kwa ajili ya kumtunza. Lakini bahati mbaya mtoto aliyejifungua mapema Oktoba amefariki dunia.

Hadi sasa, Aisha hajasikia lolote kutoka kwa mume wake aliyemtelekeza msituni. Alipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wanawake waliotoroka hivi majuzi kwamba alikamatwa na kundi pinzani la Boko Haram, na hatima yake haijulikani.

Akiwa amedhamiria kujitengenezea maisha mapya, Aisha anatarajia kutafuta fedha ili kuanza biashara ya manukato na uvumba.

"Namuomba Mwenyezi Mungu amnusuru mwanangu, lakini sitarejea tena Boko Haram," alisema.