Nigeria: Boko Haram wawaua wanavijiji mkesha wa Krismasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu kadhaa wameuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria baada ya wanamgambo wa Boko Haram kushambulia vijiji vya Wakristo na kuteketeza Kanisa mkesha wa Krismasi.
Vyanzo vya habari katika eneo hilo vinasema karibu watu wa 11 wameuawa, kulingana na shirika la habari la AFP.
Wapiganaji waliingia Pemi katika jimbo la Borno, kwa kutumia magari na piki piki na kuanza kufyatua risasi kiholela, mmoja wa viongozi katika kijiji hicho aliambia shirika hilo la habari.
Pemi iko karibu na Chibok ambako wasichana 200 wa shule walitekwa mwaka 2014.
Boko Haram wamefanya mashambulio kadhaa kaskazini mwa Nigeria ambako wanapigana kupindua serikali ili kubuni taifa la Kiislamu.
Siku ya Alhamisi, wapiganaji walivamia Pemi kama walivyokuwa wameonya maafisa wa usalama huenda kukatokea mashambulio hasa wakati wa Siku kuu ya Wakristo
Wanavijiji walitorokea msituni na baadhi yao bado hawajulikani waliko.
"Magaidi waliwaua watu saba, kuchoma moto nyumba 10 na kuiba bidhaa za chakula ambazo zilikuwa zigawanyiwe wakaazi wakati wa sherehe ya Krismasi ,"kiongozi wa wanamgambo Abwaku Kabu alisema.
Wasambuliaji walichoma moto kanisa, kumteka mchungaji na kuiba bidhaa za matibabu katika hospitali moja kabla ya kuiteketeza moto.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mzozo wa Boko Haram ambao umedumu kwa miongo kadhaa umesababisha kuuawa kwa watu karibu 36,000 na wengine milioni mbili kufurushwa makwao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Ili kujilinda, jamii katika eneo la kaskazini mwa Nigeria zimeamua kubuni makundi yaliyojihami na wanamgambo ambao wanafanya kazi kwa ushirikianao na majeshi.
Hivi karibuni, kundi hilo lilidai kuwateka nyara wavulana zaidi ya 300 wa katika jimbo la Katsina, japo mamlaka nchini Nigeria zilisema waliohusika na utekaji huo ni magenge ya wahalifu wanaoshirikiana na wanamgambo wa Kislam.
Mwezi uliyopita, wapiganaji wa Boko Haram pia walisema wamewaua wafanyakazi kadhaa wa mashamba.














