Moja kwa moja, Maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta yashika kasi Kenya, mgomo wa usafiri ukiendelea

Waziri wa nishati wa Kenya Opiyo Wandayi awarai wakenya kuwa na subira akiwaahidi kuwa serikali inashughulikia suala la mafuta, huku upinzani ukimtaka ajiuzulu.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma & Mariam Mjahid

  1. Maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta yashika kasi Kenya, mgomo wa usafiri ukiendelea

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta yashuhudiwa katika baadhi ya sehemu nchini Kenya

    Ghasia zimeripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya huku maandamano dhidi ya ongezeko la bei ya mafuta na mgomo wa usafiri wa umma ukiendelea kushika kasi.

    Katika eneo la Makavazi yaliyoko Jijini Nairobi, maafisa wa polisi wamerusha mabomu ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika nje ya eneo hilo.

    Katika mji wa Meru, waandamanaji wamefunga baadhi ya barabara na kuzuia magari kupita, hali inayosababisha usumbufu mkubwa wa usafiri wa umma.

    Huko Kaunti ya Murang'a, kundi la vijana linaripotiwa kufanya vurugu na kuwashinikiza wafanyabiashara kufunga maduka yao wakati wa maandamano hayo.

    Katika mji wa Mombasa, vijana wamejaribu kuweka vizuizi barabarani katika eneo la stendi ya magari ya Lights wakitekeleza mgomo wa usafiri wa umma. Hata hivyo, polisi wamewatawanya baadhi ya wahudumu wa matatu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo.

    Katika kaunti ya Makueni, waandamanaji wanaripotiwa kuteketeza ofisi za chama cha UDA zilizoko Wote wakilalamikia ongezeko la bei ya mafuta.

    Wakati huo huo katika kaunti ya Kisii, maafisa wa polisi wamewataka madereva wa malori kuondoa magari yaliyokuwa yakizuia barabara ya Kisii kuelekea Oyugis huku mgomo wa matatu ukiendelea kushuhudiwa eneo hilo.

    Katika eneo la Kitengela, baadhi ya waandamanaji wanadaiwa kugeuza maandamano hayo na kuanza kupora maduka yaliyokuwa yamefunguliwa. Hata hivyo, milio ya helikopta za polisi zimeanza kusikika angani huku maafisa wa usalama wakijaribu kudhibiti hali.

    Haya yakijiri Waziri wa nishati Opiyo Wandayi amewataka wakenya kuvuta subira akiwaahidi kuwa serikali inashughulia suala la mafuta.

    ''Naomba wakenya wawe na subira.Serikali inashughulikia suala la mafuta'', anasema Waziri Opiyo.

    Soma zaidi:

  2. Kiongozi wa upinzani Kenya Kalonzo Musyoka amtaka waziri wa nishati ajiuzulu

    Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka

    Chanzo cha picha, Socials/Kalonzo

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka

    Maandamano ya kupinga kuongezeka bei za mafuta nchini Kenya yakiendelea kutanuka katika kaunti mbalimbali nchini humo na kuathiri usafiri wa umma Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amemtaka waziri wa nishati kujiuzulu.

    ''Waziri wa Nishati, Opiyo Wandayi, anapaswa kuchukua hatua muhimu zaidi katika kipindi chake cha uongozi, hatua ambayo historia na wananchi wa Kenya wataikumbuka, kupunguza mara moja bei ya mafuta na kujiuzulu, amesema Kalonzo Musyoka.

    Awali waziri wa fedha wa Kenya amesema hakukuwa na haja ya kufanya mgomo wa usafiri kwa sababu tayari serikali ilishakua hatua kudhibiti athari kali za kupanda kwa mafuta zaidi kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Polisi jijini Nairobi wanaendelea kutawanya waandamanaji kwa kutumia bomu za kuwasha.

    Soma zaidi:

  3. Hakukuwa na haja ya mgomo wa usafiri wa umma – Waziri wa Fedha Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Fedha nchini Kenya amesema hakukuwa na haja ya kufanya mgomo wa usafiri kwa sababu tayari serikali ilishakua hatua kudhibiti athari kali za kupanda kwa mafuta zaidi kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Akizungumza Jumatatu, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema serikali inazingatia kuchukua hatua mpya za kuwalinda Wakenya kutokana na athari za kupanda kwa bei ya mafuta na kuwa Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza mkutano wa ngazi ya juu kuhusu bei ya mafuta atakaporejea kutoka ziara rasmi nchini Azerbaijan.

    "Tunaweza tu kutumaini kwamba vita hivi vitaisha, lakini hata tunavyotarajia, lazima tufanye maamuzi fulani. Nina uhakika serikali itakaa tena mara tu Rais atakaporudi kutathmini ni nini zaidi kinachoweza kufanywa," Mbadi alisema.

    "Kwa maoni yangu, hakukuwa na haja ya kufanya mgomo wa usafiri, ingawa bei za mafuta zimepanda. Wasiwasi wangu ni kwamba tunajaribu kutatua tatizo la kimataifa kwa kutumia njia za ndani, jambo ambalo halifai," alisema.

    "Kama tungeacha bei bila kuingilia kati, dizeli leo ingekuwa inagharimu si chini ya Sh35 zaidi, na petroli ingekuwa inagharimu Sh70 zaidi."

    Mbadi ametoa matamshi hayo hata baada ya maelfu ya Wakenya kulazimika kutembea hadi kazini leo Jumatatu asubuhi baada ya mgomo wa kitaifa wa matatu kuathiri usafiri wa umma katika miji mikubwa, kupinga ongezeko kubwa la bei ya mafuta lililotangazwa wiki iliyopita.

    Soma zaidi:

  4. Mwimbaji nyimbo za Injili aliyeshambiliwa kwa petroli afariki dunia Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rachel Wandeto, mwimbaji wa nyimbo za injili ambaye alishambuliwa kwa petroli na watu wasiojulikana ameaga dunia.

    Wandeto alikuwa akipigania maisha yake katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta baada ya watu wasiojulikana kumvamia na kummwagia petroli kabla ya kumchoma moto huko Mwiki.

    Huduma ya Kitaifa ya Polisi Kenya ilitoa taarifa na kulaani shambulio hilo.

    Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumapili, Mei 17, Huduma ya polisi ilisema tukio hilo lilitokea Jumamosi, Mei 16, 2026 katika eneo la Mwiki katika kaunti Ndogo ya Kasarani, ambapo mwanamke mmoja anadaiwa kumwagiwa kile kinachoaminika kuwa petroli na kuchomwa moto.

    Polisi walisema mwathiriwa anapigania maisha yake katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), wakiongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa shambulio hilo huenda lilihusishwa na mitazamo yake ya kisiasa.

    "Suala hili linachunguzwa na timu maalum kutoka Makao Makuu ya DCI," NPS ilisema.

    Katika ripoti ya tukio kutoka Kituo cha Polisi cha Mwiki, polisi walisema umma uliripoti kwamba mwanamke mmoja alikimbizwa katika Hospitali ya Uzima Uhai baada ya kuchomwa moto katika Barabara ya Obama, Mtaa wa 11, yapata kilomita moja kusini mwa kituo hicho.

    Maafisa waliokimbilia hospitalini walimtambua mwathiriwa kuwa Rachael Wandalo, ambaye alikuwa amepelekwa huko na mumewe, Peter Njaramba.

    Polisi walisema inadaiwa kwamba mwanamke huyo alivamiwa na kundi la wanaume watatu waliommiminia petroli na kumchoma moto.

    Ripoti hiyo ilionyesha kuwa mwathiriwa alipata takriban asilimia 70 ya majeraha ya moto na baadaye akapelekwa hospitali kuu ya Kenyatta kwa matibabu maalum. Kesi hiyo iliwekwa chini ya uchunguzi katika Kituo cha Polisi cha Mwiki.

  5. Baadhi ya shule zaahirisha masomo juu ya maandamano Kenya

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Baadhi ya shule za mjini Nairobi na vitongoji vyake zimeahirisha masomo siku ya leo huku usafiri wa barabarani ukiwa umetatizika kutoka na mgomo wa usafiri wa umma.

    Shule hizo zimetaja usalama wa wanafunzi kama sababu kuu ya kufuta shughuli za masomo siku ya Jumatatu, na kuwasihi wazazi kuhakikisha watoto wao wanaendelea na shughuli za msingi wakiwa nyumbani.

    Ujumbe ambao umekuwa ukisambaa mtandaoni juu ya mgomo wa usafiri umesababisha hali ya wasiwasi kwa wazazi wakihofia usalama wa watoto hasa wanaotumia usafiri kwenda shuleni au wale ambao shule zao ziko katikati ya jiji.

    Wachezaji wanagoma kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

    Wahudumu wa usafiri wa umma wameitisha mgomo wakipinga bei ya juu ya mafuta kuwahi kushuhudiwa nchini kenya.

    Soma zaidi:

  6. Raia wachoma magurudumu ya magari barabarani huku mgomo wa usafiri ukiendelea Kenya

    .

    Chanzo cha picha, NMG

    Wahudumu wa uchukuzi wa umma wamesema watalemaza sekta ya usafiri hadi pale mamlaka ya udhibiti bei wa mafuta EPRA itabatilisha uamuzi wa kupandisha bei ya lita moja ya mafuta ya petroli iliyopanda kwa senti 16 za dola moja ya Marekani na lita moja ya mafuta ya dizeli ambayo imeongezwa kwa senti 23 za dola moja ya Marekani.

    Kulingana na vyombo vya habari vya ndani nchini Kenya, mitaa yenye idadi kubwa kama Rongai, Kawangware, Kitengela imeshuhudia ukosefu wa usafiri wa umma, huku baadhi ya wahudumu wakiwasha moto magurudumu ya magari na kufunga barabara.

    Katika barabara ya Ngong, baadhi ya wahudumu wamefunga barabara kwa kutumia mawe na pia kuchoma moto magurudumu. Polisi wako katika eno hilo kwa sasa kudhibiti hali.

    Katika barabara kuu ya Thika, baadhi ya wenye magari wamelazimika kubadili mwendo kujilinda dhidi ya waandamanaji ambao wamewasha moto barabarani.

    Polisi wamelazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi katika mtaa wa Kayole ambapo wahudumu hao walikuwa wamefunga barabara.

    Abiria waliozungumza na vyombo vya habari walisema kwamba wanatakiwa kulipa shilingi elfu moja za kenya kutumia bodaboda kufika mjini Nairobi, gharama ambayo ni ya juu sana kwa wengi kumudu.

    Msemaji wa huduma ya polisi Muchiri Nyaga katika tarifa aliyochapisha usiku wa kuamkia Jumatatu hii, alisema kwamba polisi hawatakubali utovu wa usalama wa aina yoyote huku wakitambua kwamba haki ya kufanya maandamano ipo katika Katiba ya nchi.

    Katika mtaa wa Zimmerman, wahudumu hao wamewasha moto kwa magurudumu ya gari huku wakiweka mawe pia barabarani.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Mgomo wa usafiri waanza Kenya kupinga bei ya mafuta

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Raia wengi nchini Kenya wamejikuta wakipata ugumu wa kufika kwenye maeneo yao ya kazi asubuhi ya leo baada ya wamiliki wa mabasi ya abiria pamoja na waendesha bodaboda kuanza mgomo wa kushinikiza serikali kushusha bei ya mafuta.

    Waandaaji wa mgomo huo wanasema ongezeko la gharama za mafuta limeendelea kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida. Aidha, wametaka mamlaka ya udhibiti wa nishati na mafuta, EPRA, kuvunjwa wakidai imeshindwa kudhibiti bei hizo.

    Mbali na sekta ya uchukuzi wa umma, shughuli za usafirishaji wa mizigo na utalii pia zinatarajiwa kuathirika kutokana na mgomo huo unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini humo.

    Mgomo huo umeanza siku chache baada ya wahudumu wa usafiri wa umma kutangaza kuongeza nauli kwa asilimia 50 kufuatia bei mpya za mafuta zilizotangazwa Mei 14.

    Kwa sasa, lita moja ya petroli jijini Nairobi inauzwa kwa shilingi 214.25 huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 242.92.

    Soma zaidi:

  8. UAE yaripoti shambulio karibu na kituo cha nishati ya nyuklia cha Abu Dhabi

    Mashambulizi ya droni yaligonga karibu na Kituo cha Nguvu za Nyuklia cha Barakah kilichopo Abu Dhabi, maafisa walisema

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema shambulio la droni lilisababisha moto karibu na kituo chake cha nishati ya nyuklia siku ya Jumapili, na kulielezea tukio hilo kama “ongezeko hatari la mzozo.”

    Maafisa wanasema wanafanya uchunguzi kubaini chanzo cha shambulio hilo. Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema droni tatu zilivuka kuingia UAE kutoka “upande wa mpaka wa magharibi.”

    Iliongeza kuwa droni mbili zilidunguliwa, lakini moja iligonga jenereta ya umeme “nje ya eneo la ndani la uzio wa usalama” wa Kituo cha Barakah kilichopo Abu Dhabi, na kusababisha moto.

    Hakukuwa na majeruhi walioripotiwa, na pia hakukuwa na athari katika viwango vya usalama wa mionzi, mamlaka za eneo hilo zilisema.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ililaani shambulio hilo na kulielezea kama “kitendo kisichokubalika cha uchokozi,” ikisema ina haki ya kujibu vitendo vyovyote vya uhasama.

    Pia iliongeza kuwa “kulenga vituo vya nishati ya nyuklia vya amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, katiba ya Umoja wa Mataifa, na misingi ya sheria za kibinadamu.”

    Wizara ya Ulinzi pia ilisema nchi hiyo “itakabiliana kwa nguvu dhidi ya majaribio yoyote ya kudhoofisha usalama wa taifa.”

    Maafisa bado hawajasema droni hizo zilipotoka. UAE hapo awali imeishutumu Iran kuwa nyuma ya mashambulio dhidi ya miundombinu yake ya nishati na uchumi tangu vita vilipoanza katika eneo hilo mwezi Februari.

    Unaweza kusoma;

  9. Taiwan haitachochea mgogoro wala kuachia mamlaka yake ya kujitawala, asema rais

    Lai Ching-te

    Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

    Taiwan haitachochea mgogoro wowote lakini pia haitaacha uhuru wake, amesema rais wake Lai Ching-te baada ya mkutano kati ya Donald Trump na Xi Jinping ambapo walijadili suala la uhuru wa Taiwan.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China, Xi alimwambia Trump kwamba Taiwan, kisiwa kinachojitawala lakini kinachodaiwa na Beijing, ilikuwa “suala muhimu zaidi” katika uhusiano wa pande mbili, na kwamba kushughulikia vibaya suala hilo kunaweza kusababisha mgogoro.

    Baada ya ziara yake mjini Beijing, Trump alitoa onyo kwa Taiwan, akiiambia Fox News: “Sitafuti kuona mtu yeyote akitangaza uhuru.”

    Marekani ni mshirika wa muda mrefu wa Taiwan na imefungwa kisheria kuipa kisiwa hicho njia za kujilinda.

    Katika mahojiano yake, Trump alisema kuwa sera ya Marekani kuhusu Taiwan haijabadilika, huku akiweka wazi kwamba hataki mgogoro na Beijing.

    Trump pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba Xi alikuwa na msimamo “mkali sana” kuhusu Taiwan lakini Trump “hakutoa ahadi yoyote upande wowote”.

    Chini ya uongozi wa Lai na mtangulizi wake Tsai Ing-wen, serikali ya Taiwan kwa miaka mingi imekuwa ikisisitiza kwamba hakuna haja ya kutangaza rasmi uhuru kwa sababu tayari inaichukulia Taiwan kama taifa lenye mamlaka yake.

    Lai alirudia msimamo huo katika chapisho lake la Facebook, ambalo lilikuwa jibu lake la kwanza la moja kwa moja kuhusu mkutano huo, akisema kwamba “hakuna suala la ‘uhuru wa Taiwan’.”

    Unaweza kusoma;

  10. Donald Trump aonya kuwa “muda unakwisha” kwa Iran huku maendeleo ya kutafuta amani yakikwama

    Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Iran kwamba “muda unakwenda” huku mazungumzo ya kumaliza vita yakikwama.

    “Ni bora waanze kuchukua hatua haraka, la sivyo hakutakuwa na chochote kitakachosalia kwao,” aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social. “MUDA NI WA MUHIMU!”

    Ujumbe huo ulitolewa wakati rais huyo alipotarajiwa kuzungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumapili.

    Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa Marekani imeshindwa kufikia makubaliano ya maana katika majibu yake kuhusu mapendekezo ya hivi karibuni ya Tehran ya kumaliza mzozo huo.

    Ukosefu wa maridhiano kutoka Washington utasababisha “kukwama kwa mazungumzo,” shirika la habari la nusu rasmi la Mehr liliripoti.

    Rais huyo alionya mapema wiki hii kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yalikuwa kwenye “hatua mbaya sana ya kuendelea kuwepo” baada ya kukataa matakwa ya Tehran, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa.”

    Esmail Baghaei, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, alisisitiza kuwa mapendekezo hayo yalikuwa “ya kuwajibika” na “ya ukarimu.”

    Kwa mujibu wa shirika la habari la nusu rasmi la Tasnim nchini Iran, mapendekezo hayo yalijumuisha kusitishwa mara moja kwa vita katika maeneo yote, ikimaanisha mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon, kusimamishwa kwa mzingiro wa kijeshi wa majini wa Marekani kwenye bandari za Iran, pamoja na dhamana kwamba hakutakuwa na mashambulizi mengine dhidi ya Iran.

    Pia yalidaiwa kujumuisha ombi la fidia kwa uharibifu uliosababishwa na vita na kusisitiza mamlaka ya Iran kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

    Shirika la habari la Fars nchini Iran lilisema Jumapili kuwa Washington iliweka masharti matano kujibu pendekezo la Tehran.

    Masharti hayo yanadaiwa kujumuisha kuitaka Iran kubakiza kituo kimoja tu cha nyuklia kikiendelea kufanya kazi na kuhamisha akiba yake ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu kwenda Marekani.

    Unaweza kusoma;

  11. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo