Uchaguzi Tanzania 2025: Wapinzani kukamatwa, vurugu na 'ushindi wa kihistoria'- matukio muhimu

th

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake na ushindi huu unampa muhula mwingine
    • Author, Yusuf Jumah
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Msimu wa uchaguzi wa Tanzania wa 2025 ulijitokeza kama dhoruba ya kisiasa iliyodhihirishwa na hofu, kuzimwa kwa sauti za wapinzani na ukosefu wa imani katika mchakato mzima wa kidemokrasia.

Kuanzia kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu hadi ushindi unaopingwa wa Samia Suluhu Hassan, ambaye ametangazwa mshindi kwa takriban 98% ya kura - 31,913,866 kati ya kura 32,678,844 zilizopigwa, soma kuhusu matukio muhimu yaliyoibua kipindi kibaya cha machafuko ya hivi karibuni katika historia ya nchi hiyo .

Aprili 9: Kukamatwa kwa Tundu Lissu

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Hali ya uchafuzi wa mazingira ya kisiasa ilianza wakati Tundu Lissu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, alipokamatwa wakati wa mkutano wa kisiasa. Kuzuiliwa kwake kulileta mshtuko nchini kote, kuashiria msimamo mkali dhidi ya upinzani.

Aprili 10: Mashtaka ya Uhaini yafunguliwa

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku moja tu baadaye, Lissu alifunguliwa mashtaka rasmi ya uhaini-kosa lisilokuwa na dhamana. Hatua hii ilimuondoa mpinzani mkuu wa chama tawala kutoka kwa kinyang'anyiro cha urais.Mawakili wake baadaye walijaribu kutafuta msaada wa mashirika makuu kama vile Umoja wa Mataifa kuitilia shinikizo serikali kumwachilia huru

Oktoba 6: Humphrey Polepole atekwa nyara

th

Chanzo cha picha, The Citizen

Wakati hali ya mvutano ikiendelea, Humphrey Polepole, aliyekuwa balozi na mkosoaji mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan, alitoweka nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Ripoti za ghasia katika makazi yake zilizidisha hofu kwa usalama wa wakosoaji wa serikali.

Oktoba 22: Pigo jingine kwa upinzani

th

Chanzo cha picha, Facebook/Heche

John Heche, Naibu Mwenyekiti wa CHADEMA, alikamatwa akihudhuria kesi ya uhaini ya Lissu. Msako mkali ulizidi wiki moja tu kabla ya uchaguzi.

Oktoba 29: Siku ya Uchaguzi yageuka kuwa na vurugu

th

Chanzo cha picha, Reuters

Ghasia zilizuka siku ya uchaguzi mkuu . Pamoja na CHADEMA na ACT-Wazalendo kuzuiwa kugombea urais, maandamano yalienea Dar es Salaam na Zanzibar. Vikosi vya usalama vilijibu kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi za moto na kuacha mitaa imejaa hofu na hasira.

Oktoba 30: Jeshi latoa onyo

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Ghasia zilipozidi, Mkuu wa Majeshi Jacob Mkunda alitoa onyo kali, akiwataja waandamanaji kuwa ni "wahalifu" na kuahidi kurejesha utulivu kwa gharama yoyote ile.

Novemba 1: Samia Suluhu atangazwa mshindi

th

Chanzo cha picha, SCREENGRAB/TBC TANZANIA

Maelezo ya picha, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania INEC, Jacobs Mwambegele amemtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais

Licha ya misukosuko hiyo, Samia Suluhu Hassan atangazwa mshindi na hivyo kupata dhamana ya kuhudumu kwa muhula mwingine. Mwenyekiti wa INEC, Jacobs Mwambegele amesema kuwa Samia Suluhu Hassan ameibuka Mshindi kwa kupata 31,913,866 kati ya 32,678,844 zilizopigwa.

Matokeo hayo yaliyotangazwa na INEC yanampa Samia Suluhu Hassan fusra ya kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Samia Suluhu Hassan ameweka historia nchini Tanzania kwa kuwa Rais Wa Kike Wa Kwanza aliyechaguliwa .

Uchambuzi: Ni nini sasa mustakabali wa Tanzania?

th

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uchaguzi wa 2025 umeiacha Tanzania katika njia panda. Mkono mzito wa serikali katika kukabiliana na upinzani na kutengwa kwa vyama vikuu vya upinzani kumezua wasiwasi mkubwa juu ya kurudi nyuma kwa demokrasia. Wachambuzi wanaonya kuwa:

Mgawanyiko wa Kisiasa Utazidi Kuongezeka: Mbinu za ukamataji na vitisho zimeondoa imani katika taasisi za serikali, na kufanya maridhiano kuwa magumu zaidi.

• Nchi kuangaziwa/Kutazamwa kwa karibu zaidi Kimataifa: Makundi ya haki za binadamu na serikali za kigeni zinaweza kushinikiza uwajibikaji, uwezekano wa kuathiri misaada na uhusiano wa kidiplomasia.

• Uthabiti wa Kiuchumi upo hatarni: Machafuko ya muda mrefu na kutokuwa na uthabiti wa kisiasa unaweza kuzuia uwekezaji na kuzorotesha uchumi ambao tayari unakabiliana na mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira.

• Kujipanga upya kwa Upinzani: Licha ya ukandamizaji, vuguvugu la upinzani linaweza kujipanga upya kwa siri au kutafuta ushirikiano mpya na hivyo kuweka mazingira ya makabiliano katika siku zijazo.

• Mwanzo mpya : Licha ya hali ya wasi wasi iliyopo sasa ,pia kuna uwezekano wa awamu hii ya historia ya Tanzania ikachangia hatua kama ushirikiano kati ya serikali na upinzani kuleta marekebisho katika taasisi kama vile tume ya uchaguzi na hata katiba mpya na kukomeshwa kwa ukandamazaji wa wapinzani na uhuru zaidi wa kujieleza na wa vyombo vya habari.

Kwa Watanzania wa kawaida, swali linabaki: Je, miaka mitano ijayo italeta utulivu na mageuzi au misukosuko zaidi?

.