Utekaji nyara wazua hofu ya kurejea kwa siku za 'giza' Kenya

.

Chanzo cha picha, Gerald Karicha

Maelezo ya picha, Billy Mwangi, anayeonekana hapa akiwa na mamake baada ya kuachiliwa, amekuwa kimya kuhusu utekaji nyara wake
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kutoweka kwa zaidi ya wakosoaji 80 wa serikali katika kipindi cha miezi sita iliyopita kumesababisha taharuki kubwa ya umma nchini Kenya.

Jaji ameonya kuwa atawafunga maafisa wakuu wa usalama kwa kudharau mahakama siku ya Jumatatu iwapo watakosa kufika kwa mara ya tatu kujibu msururu wa madai ya utekaji nyara wa hivi majuzi.

Kesi hiyo inahusishwa na kupotea kwa raia kama ilivyoangaziwa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya tangu maandamano ya kitaifa dhidi ya mapendekezo ya nyongeza ya ushuru kuanza Juni mwaka jana.

Takriban watu 24 wanasemekana kuwa bado hawajulikani walipo.

Polisi na serikali wanakanusha utekaji nyara na kuwazuilia waandamanaji kinyume cha sheria, lakini nchi hiyo ina historia ya utekaji nyara unaofadhiliwa na serikali, na baadhi ya Wakenya wanahofia kwamba taifa hilo linarudi nyuma katika maisha ya giza.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai Mohamed Amin waliamriwa kuwasilisha mahakamani watu saba wenye ushawishi wa mitandao ya kijamii waliotoweka mwezi Desemba.

Watano walionekana tena ghafla mapema Januari katika maeneo mbalimbali nchini.

Mawakili wa Bw Kanja waliomba mahakama muda zaidi ili kurekodi taarifa kutoka kwao na kuandikisha ripoti.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Billy Mwangi ni mmoja wa wale watano. Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 24 aliachwa na watu wanaodaiwa kumteka nyara umbali wa kilomita 75 kutoka mji aliozaliwa wa Embu, katikati mwa Kenya, katika kitendo kinachoonekana cha vitisho.

Babake Billy, Gerald Mwangi Karicha, aliambia BBC mwanawe alikuwa na kiwewe.

"Mvulana hajasema mengi mengi," alisema. "Ninachoweza kusema ni kwamba alipokuja, hakuwa kawaida. Alionekana kushtuka."

Billy, mwanafunzi wa chuo kikuu ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali kwenye mitandao ya kijamii, alitoweka tarehe 21 Desemba 2024 akiwa katika duka la kinyozi huko Embu.

Kwa mujibu wa mashahidi, watu waliokuwa wamejifunika kofia walifika wakiwa na gari aina ya Toyota Fielder na pick-up moja, wakamfunga kwenye moja ya magari hayo na kuondoka kwa kasi.

Baada ya saa chache, hofu kuu ya familia yake ilianza kufichuka.

"Wikendi nyingi, tuko pamoja kutazama soka. Klabu yake ni Chelsea; yangu ni Arsenal," Gerald alisema.

Alimpigia simu Billy kujadili mechi ya mpira wa miguu jioni ya kutoweka kwake, na akakuta simu ya mtoto wake imezimwa.

Mmiliki wa duka la kinyozi baadaye alimjulisha juu ya utekaji nyara huo, na hivyo kusababisha msako mkali.

Mama yake Billy alizirai aliposikia habari hizo na wiki zilizofuata zilikuwa na huzuni kwa familia.

Mara tu alipopatikana, Billy alipelekwa hospitali kwa uchunguzi wa kawaida. Familia yake inasema bado anapata nafuu kutokana na kiwewe hicho, lakini kuachiliwa kwake kumewaletea afueni fulani.

Sawa na wengi ambao wamejitokeza tena baada ya madai ya kutekwa nyara, Billy amesema machache kuhusu masaibu yake, labda kwa hofu.

.
Maelezo ya picha, Ndugu wa Longton - Aslam (L) na Jamil (Kulia) - walishikiliwa kwa siku 32. Aslam aliambia BBC kwamba alipigwa mara kwa mara na watekaji nyara wake

Jamil na Aslam Longton pia walinyamaza baada ya kuachiliwa mwezi Septemba baada ya kuhudumia siku 32 utumwani.

Ndugu hao walionywa, asema Jamil, kwamba wangeuawa ikiwa wangezungumza na vyombo vya habari.

Miezi mitatu baadaye, afisa wa serikali alitaja hadharani kesi yao kuwa kukamatwa kwa halali.

Ndugu hao walichukua hili kama uthibitisho kwamba chombo cha serikali kiliwajibika kwa yale waliyopitia na kupata ujasiri wa kusema.

"Katiba ya Kenya iko wazi sana," anasema Jamil. "Unapaswa kukamatwa na kupelekwa mahakamani ndani ya saa 24. Yetu ilikuwa siku 32. Hatukuwahi kupewa wakili wa kutuwakilisha popote.

"Hatukuruhusiwa kuiona familia yetu wala kuwasiliana na familia yetu. Kwa hiyo huku sio kukamatwa, huu ni utekaji nyara."

Ndugu hao waliambia BBC kwamba Aslam alisaidia kuandaa maandamano dhidi ya kupanda kwa ushuru katika mji wa Kitengela karibu na mji mkuu, Nairobi, na alikuwa ameonywa na maafisa wa usalama kukomesha harakati zake.

Siku moja mwezi Agosti wawili hao walitolewa ndani ya nyumba yao wakatiwa ndani ya gari , wakiwa wamefunikwa kofia na kufungwa pingu, na kupelekwa mahali pasipojulikana ambapo walizuiliwa katika seli ndogo za giza.

Aslam anasema alikuwa akipigwa mara kwa mara, mtesaji wake akitaka kujua ni nani aliyekuwa akifadhili maandamano hayo.

"Niliogopa sana," anasema. "Mlango ulipofunguliwa mtu huyo alikuja na waya ya stima na chuma.

"Niliogopa kwasababu sijui alikuja kunipiga au kunimaliza - kulikuwa na chaguzi mbili tu za kunipiga au kuniua."

Jamil anawaelezea watekaji nyara wao kuwa watu wenye silaha nyingi, wanaoweza kufuatilia simu zao za rununu na wanajiamini vya kutosha kuwateka mchana kweupe, wakifanya kazi bila kuogopa suala ambalo vikundi vya haki za binadamu vimeripoti mara nyingi.

Lakini hii haimaanishi kuwa wao ni maafisa rasmi wa usalama, anasema msemaji wa serikali Isaac Mwaura, akikana kwamba serikali inahusika na utekaji nyara.

"Usalama uliopangwa pia unaweza kuwa sehemu ya uhalifu uliopangwa," aliambia BBC.

"Pia inaweza kuwa kwa sababu za kisiasa… Wapinzani wetu wa kisiasa wamekashifu sana suala hili. Kwa hakika wanalitumia kutukabili kisiasa."

Bw Mwaura alikataa kuzungumzia kesi ya waziri wa serikali Justin Muturi, mojawapo ya mashtaka mabaya zaidi ya idara ya usalama ya Kenya.

Muturi anasema mwanawe alichukuliwa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) na kuachiliwa baada ya kukata rufaa moja kwa moja kwa Rais William Ruto.

"Hilo ni suala la uchunguzi, kwa sababu huo ndio upande wake," alisema Bw Mwaura. "Lakini ni nini hadithi ya kupingana na Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi?

"Ningependa kusema kimsingi kwamba rais wa jamhuri ya Kenya, ambaye ndiye mkuu wa serikali, hajaidhinisha aina yoyote ya utekaji nyara, kwa sababu ni mtu anayeamini katika utawala wa sheria."

Kwa hakika, Ruto ameahidi hadharani kukomesha utekaji nyara, kulazimishwa kujibu ghadhabu ya umma, na wasiwasi kutoka kwa washirika wa Magharibi.

Wengi wanasikitishwa kwamba kutoweka kulikopangwa kwa wanaharakati wanaoipinga serikali kumeibuka tena kwa njia hii, wakikumbuka mbinu kama hizo chini ya uongozi wa kimabavu wa Daniel arap Moi katika miaka ya 1980 na 1990.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Hasira za umma zinaongezeka kuhusu kutekwa nyara kwa wakosoaji wa serikali

Gitobu Imanyara, mwanahabari na mwanaharakati aliyefanya kampeni za vyama vingi vya siasa mwanzoni mwa miaka ya 1990, alikamatwa na kupigwa na utawala wa Moi. Hana shaka kuwa anaona "kitabu cha mbinu za Moi" kikifanya kazi.

Lakini, anasema, nyakati zimebadilika. Marekebisho ya katiba yameanzisha mifumo zaidi ya uwajibikaji na "kuna sehemu kubwa zaidi ya jamii ya Kenya ambayo haitatishwa".

"Nafasi ya kidemokrasia imepanuka kiasi kwamba serikali haiwezi kupuuza sauti za kidemokrasia za upinzani," aliiambia BBC.

Pamoja na mitandao ya kijamii, "neno huenea mara moja", alisema.

"Hatuwezi kuchunguzwa jinsi tulivyokuwa tukidhibitiwa siku hizo wakati tungeweza kutumia simu za mezani pekee."

Ripoti za kupotea kwa watu zimepungua katika wiki za hivi karibuni.

Lakini pamoja na kutangazwa kwa uchunguzi wa polisi, hakuna aliyefunguliwa mashtaka na kuhukumiwa, kwa kutekeleza kitendo hicho .

Mashirika kadhaa ya utetezi yamewasilisha ombi kwa mwanasheria mkuu wakiomba kesi za utekaji nyara zipelekwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kuhusu familia za wale ambao bado hawajapatikana, jinamizi hilo linaendelea kuwakabili.

"Tumevunjika moyo sana," anasema Stacey Mutua, dadake Steve Mbisi, mmoja wa wale saba waliotoweka Desemba.

"Tunatumai watamtoa. [Wengi] wa waliotekwa nyara waliachiliwa, lakini bado hayupo. Tunaomba atapatikana."