Utekaji nyara Ethiopia: Waliowatoroka watekaji wasimulia hali ilivyokuwa

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Kalkidan Yibeltal
- Nafasi, BBC
Majina ya watu katika makala hii yamebadilishwa kwa sababu za kiusalama.
Dadake Bekele ni mmoja wa wanafunzi kadhaa wa Chuo Kikuu cha Debark nchini Ethiopia, ambao wametoweka kwa wiki moja sasa - alipanda basi kurudi nyumbani mwishoni mwa mwaka wa masomo, lakini hakufika anakokwenda.
Hakuna hata mmoja katika familia yake aliyeweza kumpata kupitia simu, lakini ghafla simu ya Bekele ikipigwa na namba ya dada yake, alibonyeza upesi kuipokea.
Alipokea akitamani kusikia sauti ya dada yake, lakini sauti ya mtu asiyemfahamu ndio ikasikika, ikimwambia ikiwa anataka kumuona tena dada yake, atoe birr 700,000, sawa na dola za Kimarekani 12,000.
Makumi ya abiria wa basi, wengi wao wakiwa wanafunzi, walitekwa nyara na watu wenye silaha siku ya Jumatano iliyopita.
Baadhi walifanikiwa kutoroka - na watatu kati ya hao waliiambia BBC, kuwa zaidi ya watu 100 bado wanashikiliwa.
Watekaji nyara walimpigia simu Bekele mara tatu. Bekele anasema akiwa kama mfanyakazi, hawezi hata kumudu kuwalipa watekaji birr 7,000, seuze birr 700,000.
Hayuko peke yake - katika miaka ya hivi karibuni, Ethiopia imeshuhudia ongezeko la utekaji nyara kwa ajili ya fidia.
Oromia, mkoa mkubwa zaidi wa Ethiopia ambao unauzunguka mji mkuu Addis Ababa, umeathirika zaidi.
Utekaji ulivyofanyika
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vikosi vya usalama vimesambazwa katika juhudi za kudhibiti migogoro mingi ambayo imezuka katika taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, na hilo limesababisha kuongezeka kwa uvunjifu wa sheria katika maeneo mengine.
Watu waliotekwa nyara Jumatano iliyopita walikuwa wakisafiri kwa mabasi matatu, wakielekea Addis Ababa kutoka Chuo Kikuu cha Debark katika Milima ya Simien, kivutio maarufu cha watalii.
Magari hayo yalisimama ghafla karibu na mji wa Garba Guracha, mji mdogo wa Oromia.
"Kulikuwa na milio ya risasi na nikasikia amri ya mara kwa mara ikiamuru tukimbie,” anasema Mehret, mwanafunzi wa sayansi ya wanyama aliyekuwa akisafiri kwenye moja ya mabasi hayo.
Mwanafunzi wa sheria Petros aliongeza: “Waliwaambia watu washuke. Walianza kumpiga kila mtu [kwa fimbo] na kutulazimisha kukimbilia msitu wa karibu. Hali ilikuwa ya kutisha.”
Watu hao wenye silaha waliwatembeza mateka wao katika safari ya kwenda eneo la mbali ambako kundi la waasi la Oromo Liberation Army (OLA) linaaminika kushikilia.
OLA inasema inapigania "kujitawala" watu wa kabila la Oromo, kabila kubwa zaidi la Ethiopia, lakini kundi hilo limetajwa kama kundi la kigaidi na bunge la shirikisho.
Mehret na Petros wanasema, OLA ndiyo iliyohusika na utekaji nyara huo, lakini kundi hilo la waasi halijatoa maoni yoyote.
Msemaji wa OLA, Odaa Tarbii, alikanusha siku za nyuma, madai kwamba OLA inafanya utekaji nyara ili kufadhili shughuli zake, akisema serikali dhaifu ya shirikisho imeruhusu uhalifu kushamiri.
Baada ya kulazimishwa kukimbia na kutembea kwa takribani kilomita mbili (maili 1.2), Mehret, Petros na baadhi ya watu waliotekwa nyara walifanikiwa kutoroka.
“Watu wenye silaha walikuwa wakipambana kudhibiti kundi hilo kubwa la watu, "hivyo baadhi yetu tulijificha chini ya vichaka na kusubiri hadi wafike mbali," anasema Petros.
Mwanafunzi mmoja, ambaye bado anashikiliwa na watu hao wenye silaha, alifanikiwa kuiba simu na kuipigia familia yake. Aliwaambia ameshuhudia watekaji wakiwaua baadhi ya wanafunzi.
Mtukio mengine ya utekaji
Mwaka mmoja uliopita, zaidi ya abiria 50 waliokuwa wakisafiri kutoka eneo la Amhara kwenda Addis Ababa walitekwa nyara.
Afisa wa eneo hilo alisema wale ambao waliweza kulipa fidia waliachiliwa, lakini hakusema kilichotokea kwa wale ambao hawakuweza.
Katika kisa kingine, wanafunzi 18 wa chuo kikuu cha Oromia walielezwa kutekwa nyara na watu waliokuwa na silaha mwishoni mwa 2019. Hawajapatikana hadi leo.
Miezi michache baada ya wanafunzi kutoweka, Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliwaambia wabunge kwamba watekaji nyara ni "watu wasiojulikana" na hakuna ushahidi wa "kusema kitu kibaya kilifanyika" kwa wanafunzi.
Ingawa Oromia ni mahali panaposhuhudia zaidi utekaji nyara, watekaji nyara pia wanafanya kazi kwingineko, kama vile maeneo yenye makovu ya vita ya Tigray na Amhara.
Machi, watekaji nyara huko Tigray walimkamata msichana wa shule mwenye umri wa miaka 16 na kuwataka wazazi wake walipe fidia ya birr milioni tatu.
Familia iliripoti utekaji nyara huo kwa polisi, lakini maiti ya msichana huyo ilipatikana mwezi Juni, na kusababisha kilio cha kitaifa.
Mamia ya watu waliotekwa nyara kote Ethiopia mara nyingi hupitia ukatili, ikiwa ni pamoja na kuteswa, Tume ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia (EHRC) imesema.
Serikali bado haijatoa maoni yoyote kuhusu utekaji nyara wa Jumatano iliyopita na maafisa hawajajibu maombi ya BBC ya kutoa maoni yao.
Baadhi ya ndugu wa waliotekwa nyara wameishutumu serikali kwa kutotilia maanani tukio hilo.
"Inachanganya, kwa nini serikali inapuuza suala hilo huku watoto wetu wakichukuliwa," anasema Dalke, mkulima ambaye binti yake alitekwa nyara.
Baba mwingine alisema wanataka tu wapendwa wao warudi.
"Hatuna pesa za kuwapa [watekaji nyara]. Nilijitolea sana kuwapeleka watoto wangu shule. Sasa tunachofanya ni kulia na kuomba,” anasema.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












