Vita vya wenyewe kwa wenyewe Ethiopia: Tigray yafikia makubaliano na Waziri Mkuu Abiy Ahmed

Chanzo cha picha, FANA BROADCASTING CORPORATE
Mataifa ya kigeni yamepongeza makubaliano yaliyotiwa saini na serikali ya Ethiopia na viongozi wa Tigray ili kumaliza vita vya kikatili kaskazini mwa nchi hiyo na kufungua mkondo wa misaada kwa wale walio katika hatari ya njaa, lakini maswali yanabaki juu ya iwapo vitafaulu.
Siku moja baada ya kufanyika kwa hafla ya utiaji saini katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, sauti ya mizinga bado inavuma juu ya milima ya Tigray.
Makubaliano hayo yanaafikiana kwa mapana na malengo ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipozindua kile alichokiita ‘’operesheni ya kutekeleza sheria’’ dhidi ya chama kinachotawala eneo hilo - Tigray People’s Liberation Front (TPLF) – karibu miaka miwili iliyopita.
Kutakuwa na mchakato wa kuwapokonya silaha wapiganaji wa Tigray kwa mazungumzo.
Kuwepo kwa Bw Abiy madarakani kunadhihirishwa na ukweli kwamba makubaliano ni ya TPLF, si - kama Watigray walivyotaka – "Serikali ya Tigray".
Inakataa uchaguzi wa 2020 huko Tigray, ulioshinda na TPLF, na inapanga uchaguzi mpya.
Hata hivyo, serikali ya kuu ilikuwa imedai kujisalimisha kikamilifu kwa TPLF.
Haikufanikiwa hilo.
Imeahidi kuondoa jina la TPLF kama shirika la kigaidi, na kuingia nao kwenye meza ya mazungumzo ya kisiasa kuhusu jinsi Tigray inapaswa kuendeshwa.
Makubaliano hayo yanasisitiza kuwa pande zote mbili zitatii katiba ya nchi iliyopo.
Hii ni pamoja na kusuluhisha hali ya maeneo kama vile eneo tajiri la kilimo la Tigray magharibi - lililotekwa na eneo jirani la Amhara wakati wa wiki za mwanzo za vita - kwa njia za kikatiba.
Haisemi kama utawala wa Tigray - na wakulima waliofukuzwa - watarejea kwanza.
Kipengele cha kibinadamu katika makubaliano hayo kinafungua mlango wa kukomesha njaa na kunyimwa vitu ambavyo vimegharimu maisha ya takriban watu milioni moja.
Hii inajumuisha labda 10% ya wakazi wa Tigray karibu milioni sita, kulingana na utafiti uliochapishwa na wasomi nchini Ubelgiji.

Baada ya miaka miwili ya vizuizi na njaa, na chini ya shinikizo la kijeshi lisilokoma kutoka kwa vikosi vya pamoja vya jeshi la Ethiopia na Eritrea pamoja na vikosi kutoka mkoa wa Amhara, viongozi wa Tigray walifanya makubaliano makubwa.
Hesabu yao inaonekana kuwa maisha ya watu wa Tigray yalikuwa hatarini.

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya milioni moja wamekimbia makazi yao tangu mapigano yalipoanza tena mwezi Agosti, na kushindwa kuvuna mazao yao.
Watu wanafariki kwa magonjwa yanayotibika kwani hospitali hazina dawa za kimsingi kama vile insulini na viua vijasumu.
Hakukuwa na dalili ya mwisho huu.
Kwa mamilioni ambao wamenyimwa chakula, dawa na huduma zingine za kimsingi, misaada muhimu haiwezi kuja haraka sana.

Maswali muhimu
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa.
Matatu yakiwa muhimu sana.
Jina la kwanza Eritrea. Kulingana na wanadiplomasia wa Magharibi, mashambulizi ya kijeshi ambayo yalivunja safu za ulinzi za Tigray yalikuwa operesheni ya pamoja ya Eritrea-Ethiopia iliyoelekezwa kutoka Asmara.
Eritrea haijatajwa kwa jina katika makubaliano hayo.
Lakini makubaliano hayo yanajumuisha kipengele cha kukomesha "kuungana na wanajeshi wengine wowote wa nje", ambayo inaweza kumaanisha Eritrea.
Wengi watakuwa na mashaka kuwa serikali ya kuu ina mbinu za kutekeleza hili.
Rais wa Eritrea Isaias Afewerki hashiriki katika makubaliano hayo na ana mbinu za kuendeleza vita bila kujali makubaliano yoyote yaliyoafikiwa na Bw Abiy.
Pili ni ufuatiliaji na uhakiki.
Makubaliano hayo ni ushindi kwa mkakati wa kidiplomasia wa Ethiopia wa kuweka jumuiya ya kimataifa pembeni.
Utaratibu wa ufuatiliaji, uhakiki na uzingatiaji unajumuisha tu kitengo kidogo - watu wasiozidi 10 - ambao wanaripoti kwa jopo la Umoja wa Afrika (AU) linaloongozwa na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.
Kwa upande wake, mamlaka ya Bw Obasanjo yanatoka kwa mwenyekiti wa Tume ya AU Moussa Faki, si Baraza la Amani na Usalama la AU.
Umoja wa Mataifa umetengwa kabisa.
Kutathmini ripoti za ukiukwaji na kusuluhisha mizozo itakuwa kwa uamuzi wa wanaume wawili - Bw Obasanjo na Bw Faki – kwa ufupi tu tunaweza kusema utaratibu usio wa kawaida wa uangalizi.
Ni jambo la kawaida kwa makubaliano ya kiwango cha juu cha amani kushuhudiwa na washirika wa kimataifa.
Katika kesi hiyo, AU iliruhusu tu Umoja wa Mataifa, Marekani na chombo cha kanda ya Afrika Mashariki (IGAD) kuwa waangalizi, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetia saini makubaliano hayo.

Chanzo cha picha, AFP
EU ilizuiwa kushuhudia makubaliano hayo, ingawa ndio wafadhili wakuu wa AU.
Ethiopia na AU zinategemea uidhinishaji wa kimataifa hata hivyo - kwa sababu Ethiopia inahitaji sana misaada ya kigeni.
Tatu ni haki na uwajibikaji.
Makubaliano hayo yanatoa nafasi kwa serikali ya Ethiopia kuanzisha "sera ya kitaifa ya mpito ya haki", bila kutaja uchunguzi wowote wa kimataifa, kwa mfano na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa au Tume ya Afrika ya Haki za Kibinadamu.
Bw Obasanjo aliona kwamba kutia saini mkataba ni hatua ya kwanza tu, na kuutekeleza ni kazi ngumu zaidi.
Matarajio ya amani na mwisho wa ukatili na njaa huko Tigray na utulivu wa Ethiopia unategemea sana imani nzuri ya serikali ya kuu.
Jaribio la mapema litakuwa ni ahadi yake tu ya kutoa matamko ya pamoja kwa umma na TPLF na kukomesha "propaganda za uadui, maswali yasiyokuwa na majibu na matamshi ya chuki".

‘Masharti ya kudhalilisha’
Watigray nyumbani na ughaibuni wamepokea mpango huo kwa kufadhaika.
Inawezekana kwamba baadhi ya makamanda wa Tigray wangependelea kuendelea na vita vya msituni kuliko kujisalimisha kwa kile wanachokiona kama masharti ya amani ya kufedhehesha.
Wengi katika jumuiya ya kimataifa wamedhani kuwa Bw Abiy ana nia njema, na kwamba atarejea kwenye njia ya amani, demokrasia na utulivu iwapo atapewa nafasi.
Wengine wanahofia kwamba somo ambalo Bw Abiy, Bw Isaias na wengine watakuwa wamejifunza ni kinyume chake - yaani kwamba nguvu nyingi, njaa inayoendelea na kukatika kwa mawasiliano ni silaha madhubuti katika kutimiza malengo yao.
Waethiopia watakuwa na matumaini kwamba mbinu hizi hazitatumika kutatua changamoto nyingine za kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa uasi katika eneo la Oromia.
Makubaliano hayo yanatokana na imani kwamba Bw Abiy ataiongoza Ethiopia kutoka katika mgogoro wake.
Jaribio la kwanza kabisa la makubaliano hayo ya matumaini lilikuwa ikiwa bunduki zingenyamaza siku ya Alhamisi.
Hilo halikutokea.
Badala yake siku hiyo ilishuhudia mapigano makali, ikiwa ni pamoja na mashambulizi makubwa ya majeshi ya Ethiopia na Eritrea katika pande tatu, vyanzo katika eneo hilo vinasema.
Watigray wanapinga na wanaripotiwa kushikilia msimamo wao.
Uaminifu wa AU na waangalizi wa kimataifa katika mazungumzo hayo - Umoja wa Mataifa, Marekani na IGAD - unatokana na utayari wao wa kuzungumza na wanaokiuka kutoka pande zote.















