'Ni kutawazwa sio ushindani' - Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania akabiliwa na upinzani mdogo

,

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    • Author, Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC Africa, Dar es Salaam
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Huku kukiwa hakuna mgombea maarufu wa upinzani aliyeidhinishwa kushiriki katika uchaguzi wa Jumatano, 29/10/2025, Watanzania wengi wanahisi kura hiyo si mashindano bali ni kama kutawazwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akikabiliwa na uchaguzi wake wa kwanza wa urais.

Samia mwenye umri wa miaka 65 amekuwa rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya kifo cha rais John Magufuli mwaka 2021. Alisifiwa kwa upande mmoja kwa dhamira yake ya kukomesha ufisadi lakini alikosolewa kwa ukandamizaji wake wa kimabavu juu ya upinzani na mtazamo wa kutatanisha dhidi ya janga la Covid.

Rais Samia, ambaye alikuwa makamu wa rais, alionekana kama pumzi ya hewa safi - na kwa mtindo wake wa kirafiki, alianzisha mageuzi ambayo yalionekana kuwa mabadiliko makubwa kutoka kwa sera za mtangulizi wake.

Sera yake yenye 'R nne' - "reconciliation, resilience, reform and rebuilding" yaani "maridhiano, uthabiti, mageuzi na kujenga upya" - ilifungua tena Tanzania kwa wawekezaji wa kigeni, kukarejesha uhusiano wa wafadhili na kuvutia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

"Alifanya mabadiliko, uhusiano uliopotea kati ya Tanzania na mashirika ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia ulirejeshwa," mchambuzi wa kisiasa Mohammed Issa aliiambia BBC.

Lakini katika kipindi cha miaka miwili hivi iliyopita, nafasi ya kisiasa imepungua kwa kiasi kikubwa - na kulengwa kwa wakosoaji wa serikali na sauti za upinzani kunasemekana kuwa katika hali mbaya zaidi sasa kuliko ilivyokuwa chini ya Magufuli, huku utekaji nyara na mauaji ya mara kwa mara sasa yakiripotiwa.

"Samia aliingia kwa sauti ya maridhiano, lakini sasa amekuwa amekuwa mwenye kufanya maamuzi magumu ambayo wengi hawakutarajia kutoka kwake," alisema Bw Issa.

"Sasa analaumiwa pakubwa kwa baadhi ya mambo kama vile utekaji nyara, mauaji, ukandamizaji wa upinzani na masuala mengine kuhusu usalama."

Hii imeakisiwa katika ripoti za Freedom House, shirika la utetezi wa demokrasia na haki za binadamu lenye makao yake nchini Marekani, ambalo liliiweka Tanzania kama taifa "huru kwa kiasi fulani" mwaka 2020 na "lisilo huru" mwaka jana.

Serikali haijazungumzia tuhuma hizo.

.
Maelezo ya picha, Godfrey Lusana, mkazi wa Dar es Salaam
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

CCM ya Samia imeshinda kila chaguzi tangu kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa mwaka 1992, lakini kampeni huwa na mijadala mikali kati ya vyama pinzani.

Wakati tume ya uchaguzi ikiwa imewaachia wagombea urais 17 kugombea urais wakati huu, chama kikuu cha upinzani Chadema kimezuiwa huku kiongozi wake Tundu Lissu akikabiliwa na kesi ya uhaini.

Alikuwa akitoa wito wa mageuzi ya uchaguzi kabla ya kukamatwa kwake mnamo mwezi Aprili - na chama sasa kinawataka wafuasi wake kususia uchaguzi huo.

Makamu wake, John Heche, naye alikamatwa wiki iliyopita - na aliiambia BBC kabla tu ya kuwekwa kizuizini kwamba kile kinachoitwa mageuzi ya Rais Samia ni mambo yasio na msingi: "Ndiyo, mikutano ya hadhara iliruhusiwa tena, lakini leo Chadema haiwezi kutekeleza wajibu wake kwa sababu ahadi zilikuwa za uongo."

Wakati huo huo, mgombea urais Luhana Mpina, kutoka chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani, ACT Wazalendo, pia ameenguliwa - mara mbili.

Alifaulu kurejeshewa ugombeaji wake na Mahakama Kuu baada ya kuzuiliwa kutokana na suala la kiutaratibu - lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipokata rufaa mwezi uliopita, tume ya uchaguzi iliamua kuunga mkono upande wake.

Hii inaviacha vyama vidogo vya upinzani kama vile CHAUMMA na CUF kwenye kinyang'anyiro hicho, lakini kiuhalisia hakuna nafasi ya kumzuia Samia kushinda wadhifa wake wa sasa.

"Udhibiti wa chama tawala, kutengwa kwa upinzani na upendeleo wa kitaasisi kunadhoofisha uaminifu wa uchaguzi. Fursa finyu ya ushiriki wa umma na uhamasishaji mdogo wa wapiga kura hudhoofisha ushirikishwaji wote," alisema mchambuzi wa kisiasa Nicodemus Minde katika ripoti ya hivi majuzi ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS).

Hii imewaacha baadhi ya wapiga kura, kama mkazi wa Dar es Salaam, Godfrey Lusana, kukata tamaa.

"Hatuna uchaguzi bila upinzani thabiti. Mfumo wa uchaguzi hauko huru. Tayari tunajua nani atashinda. Siwezi kupoteza muda wangu kupiga kura," aliambia BBC. "Kama tume ya uchaguzi ingekuwa huru kweli, ningepiga kura."

.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Hii ni kinyume kabisa na kampeni zinazoendelea kushika kasi kwenye visiwa vya Tanzania ambayo nusu inajitawala, visiwa vya Zanzibar - ambako Rais Samia anatoka.

Wananchi wa visiwani humo wanamchagua rais wao wa eneo na anayemaliza muda wake Hussein Mwinyi wa CCM anatafuta kuwania muhula mwingine, lakini anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Othman Masoud wa ACT-Wazalendo - ambaye amekuwa naibu wake katika utawala wa umoja.

Katika kampeni za Tanzania bara, Rais Samia ametumia sifa za awali alizopokea kwa mtazamo wake kama mama - kutaka kutawala kwa njia ya mazungumzo badala ya kuamrisha.

Hili lilimpa jina la utani la "Mama Samia" - na katika mikutano yake amekuwa akiahidi kuleta maendeleo makubwa kupitia miundombinu bora, afya na elimu.

.
Maelezo ya picha, Queen Castoric, mpiga kura kwa mara ya kwanza kutoka jiji la kaskazini mwa Tanga.

Wanawake wengi, hasa wale wa vijijini, wanamwona kama nguvu ya kuleta utulivu.

"Analeta staha, sisi wanawake vijana tunamuangalia yeye kama kioo cha jamii. Tunahisi uwepo wake kama rais na hiyo inatupa imani kwamba tunaweza kuwa wa kutegemewa kwa jamii zetu sasa na siku zijazo," mpiga kura kwa mara ya kwanza Malkia Castoric kutoka jiji la kaskazini mwa Tanga aliambia BBC.

Lakini baadhi ya wanawake katika maeneo ya mijini, kama Celina Ponsiana, ambaye pia atapiga kura yake kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, ana mtazamo tofauti: "Uongozi si tu kuhusu sauti.

"Naamini rais ana kazi ya kufanya, kwanza kuhusu ukosefu wa ajira. Amekuwa akiwasaidia baadhi yao lakini wengi bado wanahitaji msaada," alisema.

Mwanamke mwingine kijana mjini Morogoro, karibu na Dar es Salaam, alisema anamuunga mkono rais lakini alikataa kutaja jina lake kwa BBC.

"Samia alitufanya tuamini wanawake wanaweza kuongoza. Ningependa kusema zaidi, lakini vijana wengi hawamzungumzii kwa mtazamo chanya," alisema.

Vijana ndio wengi kati ya watu milioni 37.7 waliojiandikisha kupiga kura nchini Tanzania - na kuna hasira kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu ukimya wa rais kuhusu masuala kama vile utekaji nyara unaoshtua wengine.

Na huku wengine wakimpa sifa Rais Samia kwa kuimarisha uchumi, baadhi ya maeneo hata wanamtamani Magufuli kutokana na kuibuka kwa taarifa za ufisadi.

Katika jamii ya kitamaduni inayotawaliwa na wanaume, amekumbana na matatizo ya kuthibitisha mamlaka yake. Katika mikutano ya hivi majuzi amekuwa akiwakumbusha wapiga kura ambao ndio matajiri kwenye suala zima la uchaguzi: "Msisahau mimi ni mkuu wa majeshi ya ulinzi."

Anaweza pia kuhisi kudhoofishwa na wenzake. Ndani ya CCM, kulikuwa na upinzani kwa kuwa mgombea urais wa chama hicho bila kupingwa.

.
Maelezo ya picha, Mabango ya Rais Samia ndio yanayotawala jijini Dar es Salaam

Mwanachama mmoja mkuu wa chama ambaye alikosoa kugombea kwake moja kwa moja - Humphrey Polepole - alitekwa nyara katika mazingira ya kutatanisha.

Pia kuna tetesi kwamba amekuwa miongoni mwa walio kwenye mtandao wenye nguvu wa wafanyabiashara wakubwa na wafuasi wengine wenye ushawishi wa CCM, wanaojulikana kwa mazungumzo kama Mtandao, kulingana na Bw Minde katika ripoti yake ya ISS.

"Demokrasia ya ndani ya chama cha [CCM] imebinywa kutokana na hatua iliyoratibiwa ya kumfanya Rais Samia kuwa mgombea pekee. Wakati hili likizidisha migawanyiko ndani ya chama, sura ya kuwa na umoja inawasilishwa kwa umma," alisema.

Inaaminika kuwa Magufuli alikataa kupokea maagizo kutoka kwa Mtandao, akipendelea kushikamana na ajenda yake ya kupambana na ufisadi.

Bw Minde anaonya kuwa hayo yote yamechangia hali ya hofu katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Kwa kudhibiti vyombo vya habari na kupungua kwa mijadala ya kisiasa, mijadala ya umma imerejea kwenye mazungumzo ya faragha na mitandao ya kijamii.

Wachambuzi wanaonya kuwa utengano wa aina hiyo, hasa miongoni mwa vijana, unaweza kuathiri demokrasia ya Tanzania zaidi - na kuleta matatizo kwa Rais Samia ikiwa hakutakuwa na idadi kubwa ya watu watakaojitokeza na iwapo maandamano yangejitokeza.

Kwa Tito Magoti, mwanasheria na mwanaharakati kijana wa kisiasa, madai bado ni rahisi kabisa.

"Tunataka Tanzania huru ambapo kila mtu ana uhuru wa kuzungumza," aliambia BBC.

"Uhuru wa kutembea na uhuru wa kufanya chochote wanachotaka."

Pia unaweza kusoma:

Imefasiriwa na Asha Juma