Mstari mwembamba kati ya dini na siasa unavyotikisa uchaguzi Tanzania

k

Chanzo cha picha, Ikulu

Muda wa kusoma: Dakika 6

Katika kila jukwaa la siasa, utasikia maneno ya maombi; katika kila madhabahu, maneno ya haki, amani, uadilifu au uwajibikaji. Lugha hizi, zenye mizizi ya kiimani, mara nyingi huibua mijadala ya kisiasa.

Kwa miaka mingi, viongozi wa dini nchini Tanzania wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii, kupinga rushwa, kudai haki za binadamu, na kuhimiza uadilifu wa kisiasa. Lakini mara nyingine sauti hizo huchukuliwa kama za upinzani ama harakati za kisiasa, hali inayofanya mstari kati ya dini na siasa kuwa mwembamba mno na changamoto kuutambua.

Tanzania inaingia katika mwaka wa uchaguzi mkuu wa 2025, kipindi ambacho mijadala kuhusu nafasi ya dini katika siasa inachukua sura mpya.

Kadiri kampeni za kisiasa zinavyozidi kupamba moto, viongozi wa dini wanazidi kujikuta katikati ya mgongano wa maadili na mamlaka. Wengine wanahusishwa na upendeleo wa kisiasa, wengine wakilalamikiwa kuingilia siasa, huku wananchi wengi wakitazama dini kama dira ya maamuzi yao ya kisiasa. Na hivyo hoja ya mstari kati ya dini na siasa unachorwa wapi, nani anauvuka, na kwa sababu gani? inaendelea kuwepo

Nadharia na uhalisia

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria kadhaa, zinasisitiza kuwa nchi hiyo ni ya 'kisekula' yaani isiyoendeshwa kidini japo inaheshimu dini za raia wake.

Hatahivyo, kwa miaka nenda rudi, wanasiasa "wanavaa" majoho ya dini, na viongozi wa dini wanavaa "kofia" za kisiasa. Wakati mwingine kwa Pamoja wakati mwingine kwa nyakati tofauti. Na hapo ndipo penye 'ukakasi' juu ya mstari huu mwembamba wa dini na siasa.

Japo si kwa kiwango kikubwa kama ilivyo kwa nchi kama Kenya au Nigeria, viongozi wa dini nchini Tanzania wamekuwa wakizungumza masuala ya kisiasa, na wanasiasa wakijitokeza katika ibada au matukio ya kidini.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, Mohamed Issa, anasema kutenganisha siasa na dini ni dhana yenye asili ya Ulaya, iliyobuniwa wakati kanisa lilipokuwa na nguvu za kisiasa na kiuchumi. "Suala la kutenganisha dini na siasa liko kinadharia zaidi kuliko vitendo," anaeleza.

Kabla ya kampeni, mikutano au vikao vya bunge, maombi hutangulizwa. Wananchi wengi ni waumini wa dini, na viongozi wao wanapohubiri, hawahubiri kuhusu dhambi pekee bali pia kuhusu amani, haki, rushwa na uwajibikaji.

Makanisa na Misikiti pia yanamiliki shule, hospitali na taasisi za kijamii, mambo ambayo yanagusa kiini cha maisha ya kisiasa na kiuchumi. Swali ni, je, unaweza kutenganisha maadili hayo na siasa wakati yanazungumzia ustawi wa jamii?

Muongo mmoja uliopita, Baraza la Maaskofu Katoliki kupitia Tume ya Haki na Amani, liliwahi kutoa tamko kuhusu wajibu wa kijamii wa Kanisa. Sehemu ya ujumbe huo ilisomeka: "Kila mara Kanisa linapotimiza wajibu huu, linashutumiwa kuingilia siasa. Tafsiri hiyo ni potofu."

Mvutano wa mamlaka na hofu ya ushawishi

a

Chanzo cha picha, Gwajima Insta

Maelezo ya picha, Askofu Josephat Gwajima, mbunge wa zamani wa chama tawala (CCM)
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika nchi yenye historia ya amani, mstari wa dini na siasa unavutwa kwa tahadhari kubwa, mara nyingine ukitetereka bila kudhibitiwa.

Askofu Josephat Gwajima, mbunge wa zamani wa chama tawala (CCM) katika Jimbo la Kawe, ni mfano halisi wa kiongozi aliyevaa kofia zote mbili. Baada ya kulaani vitendo vya utekaji nchini akisema, "Utekaji si utamaduni wa Watanzania," Serikali ilifuta usajili wa Kanisa lake la Ufufuo na Uzima kwa madai ya kuingilia masuala ya kisiasa. Hadi leo, Kanisa hilo limefungwa.

Kwa upande mwingine, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), chini ya Rais wake Wolfgang Pisa, hivi karibuni lilisema kuwa chaguzi za 2019, 2020 na ule wa 2024 hazikuwa za haki. "Hii haiwezi kumuhakikishia mwananchi kwamba uchaguzi mkuu wa 2025 utakuwa wa haki," alisema.

Kauli hiyo ilizua mjadala mkali kwamba Kanisa hilo linaingilia siasa? huku Serikali ikisisitiza kuwa chaguzi hizo zote zilikuwa huru na haki. Hapo ndipo mstari kati ya dini na siasa unapoonekana kuwa na ukakasi, hasa wakati wa kuelekea uchaguzi.

Mwaka 2017, afisa wa ngazi za juu Serikalini, Projest Rwegasira, alitishia kufungia taasisi za dini kwa madai ya kuingilia siasa. Vitisho hivyo vilikosolewa vikali na wanaharakati na wasomi.

Onesmo Olengurumwa, mmoja wa wanaharakati hao, alisema: "Kuna tofauti kubwa kati ya kushiriki katika siasa na kutoa maoni ya kisiasa."

Kwa upande wake, Profesa Bakari Mohammed wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema: "Kinachoshangaza ni kwamba vitisho na onyo hutolewa pale viongozi wa dini wanapokosoa serikali, si wanapoipongeza."

Kwa namna yoyote ile kuli hizi zinaonyesha hofu ya ushawishi wa kidini katika maamuzi ya kisiasa.

Hata hivyo, wanasiasa nao hawako mbali na dini. Wengi huomba baraka za viongozi wa dini, kuhudhuria ibada, au kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada kama njia ya kujijenga kisiasa.

Wapi mstari unapaswa kuchorwa?

A

Chanzo cha picha, ACT

Maelezo ya picha, Sheikh Issa Ponda (kulia), mwanachama wa ACT Wazalendo na mgombea ubunge jimbo la Temeke akisalimia na kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe

Kisheria, dini hairuhusiwi kuhusika moja kwa moja na siasa za vyama: kugawa kadi, kuendesha kampeni au kuhubiri kwa misingi ya chama. Hata hivyo, kuhubiri uadilifu, ukweli na haki ni wajibu wa kimaadili mambo ambayo mara nyingi hubeba uzito wa kisiasa.

Mchambuzi Mohamed Issa anasisitiza: "Huwezi kutenganisha dini na siasa mia kwa mia. Kinachotakiwa ni namna ya lugha na ukosoaji, si ukimya."

Askofu Gwajima si wa kwanza. Marehemu Christopher Mtikila, aliyekuwa mchungaji na mwanasiasa wa chama cha Democratic Party (DP), aliongoza kanisa lake sambamba na kugombea urais mwaka 2005. Vivyo hivyo, marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare alikuwa mbunge wa CCM na kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B.

Nje ya Tanzania, Pastor Chris Okotie wa Nigeria amewahi kugombea urais mara tatu, na Mchungaji Jesse Jackson wa Marekani alijaribu urais kupitia Democratic Party.

Kwa upande wa sasa, Sheikh Issa Ponda kiongozi wa muda mrefu wa Kiislamu amejitosa kugombea ubunge wa Temeke kupitia chama cha upinzani, ACT Wazalendo. Wakati huo huo, Sheikh Seif Hassan Sule, Mwenyekiti wa Taasisi ya Islaah Islamic na mwanachama wa CCM, alichukua fomu za kuwania ubunge Mbagala mwaka huu, hata hivyo kura hazikutosha kuteuliwa na chama chake kwenye kura za maoni ndani ya chama.

Sule, ambaye pia aliwahi kuwa kiongozi wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA), amewahi kuonya dhidi ya maandamano ya wapinzani, akisisitiza umuhimu wa amani msimamo unaoonyesha mchanganyiko wa imani na siasa.

Mwingine ni Mchungaji Emanuel Mgaya, maarufu kama Masanja Mkandamizaji, ambaye mara kadhaa amekuwa akipigia debe chama tawala CCM na mgombea wake wa urais, Samia Suluhu Hassan, katika majukwaa ya kidini. Huku Nabii Mkuu wa Kanisa la Ngurumo na Upako, Geo Davie akichangia shilingi milioni 50 za kitanzania kwa CCM mkoa wa Arusha, kwa ajili ya kuwezesha kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan.

Kwa mazingira haya mstari wa dini na siasa unazidi kuwa mwembamba.

Mwisho wa mstari huo mwembamba

A

Chanzo cha picha, ACT

Maelezo ya picha, Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud (katikati) na mgombea urais wa visiwa hivyo kupita ACT akiwa na viongozi wa dini

Bado ni kizungumkuti kutenganisha dini na siasa licha ya maonyo kadhaa kutoka kwa viongozi wa kisiasa na serikali hasa katika utawala wa miaka ya hivi karibuni.

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliwahi kuonya miaka miwili iliyopita akiwa mkoani Mara kuhusu kuchanganya dini na siasa. "Siku ikifika uanachama wa chama cha siasa au uumini thabiti wa dini ukawiainishwa na chama cha kisiasa anachokifuata ndiyo mwisho wa nchi yetu".

Hata hivyo mtazamo wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ulikuwa tofauti kidogo ingawa na yeye alihimiza dini na siasa kutenganishwa, Lakini aliongeza viongozi wa dini washiriki kukemea yale maovu yanayofanywa na wanasiasa, wasikae kimya: "Kama Kanisa halitashiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya mifumo dhalimu inayosababisha umasikini na udhalilishaji, basi halitakuwa na maana kwa watu wake."

Naye Askofu Pierre Whalon wa Makanisa ya Ulaya anaandika katika makala yake "Religion and Politics Are Inseparable": "Haiwezekani kutenganisha dini na siasa; yeyote anayejaribu kufanya hivyo aidha anadanganya au hajafikiria vizuri."

Na kitabu cha Kent Greenawalt cha Religious Convictions and Political Choice kinathibitisha hoja hiyo, kikionyesha jinsi imani za dini zinavyoathiri maamuzi ya kisiasa hata katika nchi zilizo na demokrasia thabiti zaidi.

Ili kuuheshimu mstari mwembamba huu wa dini na siasa, wachambuzi wanasema, kinachotakiwa si kuzuia dini kuzungumza, bali kuhakikisha kwamba maonyo au mafundisho ya kidini hayaingilii mchakato wa kidemokrasia. Lakini pia wanasiasa waheshimu ushiriki wa dini na viongozi wa dini kwnye masuala ya kisiasa kwa sababu ni sehemu ya jamii na wanaguswa na maamuzi yote ya kisiasa.

Tanzania inabaki kuwa mfano wa kipekee kama nchi yenye dini nyingi, lakini yenye amani isiyotikisika. Lakini kadiri taifa linavyosogea kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, ni wazi kwamba uhusiano kati ya dini na siasa utazidi kuibua mijadala mikali. Kinachohitajika si ukimya wa dini wala ukali wa mamlaka za kisiasa, bali hekima ya mazungumzo kama anavyosisitiza Issa "Viongozi wa dini wazungumze kwa busara; viongozi wa siasa wasikilize kwa unyenyekevu".

Upo msemo unaosema kama 'ukikimbia kivuli chako, bado kinakufuata' Vivyo hivyo kivuli hicho, katika Tanzania ya leo ya kuelekea uchaguzi Mkuu, ni ule mstari mwembamba kati ya dini na siasa, mstari usiovukika, lakini usioweza kuepukika.