Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche akamatwa na kupelekwa Tarime Tanzania

John Heche

Chanzo cha picha, John Heche

Muda wa kusoma: Dakika 2

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, amesafirishwa hadi Tarime na Jeshi la Polisi baada ya kukamatwa leo asubuhi.

Gaston Garubindi, wakili mkurugenzi wa Sheria wa Chama cha CHADEMA, amethibitisha hilo na kusema "Mheshimiwa Heche alipokuja mahakamani asubuhi alikamatwa na jeshi la Polisi kwa makosa ambayo hawajasema…".

Jambo la John Heche halipo Dar es Salaam bali lipo Tarime na kuwa tayari ameshasafirishwa kuelekea huko, kulingana na Wakili Gaston.

Wakili Gaston aliongeza kuwa kama chama wanajipanga kwa ajili ya mawakili waliopo mkoa wa Mara na wengine kutoka Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma za kisheria.

Akizungumza leo asubuhi, Katibu Mkuu alisema makamu mwenyekiti hakuwa amepewa wito wowote wakuitwa.

Heche alikamatwa akiwa njiani kuelekea kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu.

''Tumekwishaelekeza mawakili wetu, waelekee moja kwa moja polisi kwenda kufuatilia suala hili.'' alisema Mnyika.

Unaweza kusoma

Jeshi la polisi halijasema sababu za kukamatwa kwake.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Heche alikamatwa mwishoni mwa juma lililopita mkoani Mara kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya huko Isibania One Stop Border alipokuwa anataka kuingia Kenya.

Kwa mujibu wa CHADEMA, Heche alikuwa akiingia nchini Kenya kukiwakilisha chama kwenye shughuli za mazishi ya mwanasiasa nguli wa Kenya,Raila Amolo Odinga.

Pamoja na kumuweka kizuizini taarifa ya chama hicho ilisema kuwa, Mamlaka ya Uhamiaji Tanzania ilimnyang'anya hati yake ya kusafiria.

Idara ya Uhamiaji ilisema kwenye taarifa yake kuwa Heche aliondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za Uhamiaji.

Ilitoa wito kwa Watanzania na wageni wanaotoka na kuingia Tanzania kufuata utaratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wawatu nchini ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

John Mnyika amesema madai ya Idara ya Uhamiaji kuwa Heche alivuka mpaka kuingia Kenya kinyume cha utaratibu si ya kweli na kuhusisha madai hayo na kitendo cha kumkamata hii leo.

''Kama kukamatwa kwake kunahusiana na taarifa hiyo ni jambo la kusikitisha sana polisi kutumia taarifa isiyo ya kweli ya uhamiaji kumkamata. Mimi ninafahamu kulikuwa tayari kuna njama huko nyuma kutafuta namna ya kutukamata viongozi kabla ya tarehe 29 Oktoba hivyo vitatumika visingizio mbalimbali''. Alisema Mnyika.