Tundu Lissu ashitakiwa kwa uhaini Tanzania

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Na Alfred Lasteck, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, Tundu Lissu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, na kusomewa shitaka la uhaini.

Tundu anayetetewa kwa sasa na Mawakili sita ambao ni Dk. Rugemeleza Nshalla, Dickson Matata, Jebra Kambole, Michael Lugina, Hekima Mwasipu, na Gaston Garubindi, alisomewa shitaka hilo la uhaini Wakili Nassoro Katuga

Mbali na Shitaka hilo anatuhumiwa kwa kuchapisha taarifa za uongo kuhusu kuharibiwa kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, kutumika kwa Polisi kuipa kura na Majaji kutotenda haki kwa kuwa ni wateule wa Rais.

Hata hivyo Mahakama hivyo imesema haina uwezo wa kusikiliza makosa ya uhaini na kuhairisha kesi mpaka April 24, 2024.

Awali Jeshi la Polisi nchini Tanzania lilisema lilimkamata Lissu jana mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kufanya uchochezi wa kutofanyika Uchaguzi Mkuu 2025.

Aidha Polisi nchini humo kupitia taarifa yake ilitoa onyo kwa vyama vyote vya siasa kutotoa maneno ya uchochezi, kashfa kwa Polisi na Serikali au viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Mapema Polisi walipiga mabomu ya machozi na kuwatawanya wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema huku wakizua viongozi wa chama hicho kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kushikiliwa pia kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche, Mjumbe wa Kamati kuu, Godbless Lema, Mwenyekliti wa chama hecho kanda ya Kusini, Aden Mayala na Mkurugenzi wa Mawasiliano na uenezi, Brenda Rupia.

Lissu alikamatwa hapo jana baada ya kumaliza mkutano wa hadhara mkoani Ruvuma, kusini mwa Tanzania. Akiendelea kunadi msimamo wa chama hicho wa 'No Reforms, No Election,

No Reforms, No Election, ni msimamo wa kisera wa chama hicho uliopitishwa na Kamati Kuu katika kikao chake cha Disemba 2-3, 2024 unaodai kuwa CHADEMA haitoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama hakutafanyika mabadiliko ya kimfumo katika uchaguzi, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya katiba, sheria, na kuhakikisha kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi.

Zaidi Lissu na chama hicho unaeleza kwamba uchaguzi hautafanyika nchini humo kama marekebisho wanayodai hayatafanyika.

Taarifa ya jana ya chama hicho inadai kutofanyiwa haki na jeshi hilo.