Samia ashinda uchaguzi Tanzania huku mamia wakihofiwa kufariki katika maandamano

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais Samia Suluhu Hassan ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Tanzania na kupata muhula mwingine licha ya ghasia zilizoshuhudiwa nchini humu.

Samia alipata karibu 98% ya kura katika uchaguzi wa Jumatano, Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC ya ilisema.

Katika hotuba yake ya ushindi Jumamosi alisema uchaguzi ulikuwa "huru na wa kidemokrasia", akiwashutumu waandamanaji kwa "kutokuwa wazalendo".

Vyama vya upinzani vimepinga matokeo hayo, vikiutaja uchaguzi huo kuwa kejeli kwa mchakato wa kidemokrasia kwani wapinzani wakuu wa Samia walikuwa wamefungwa au kuzuiwa kugombea.

Kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maenedeleo CHADEMA, anazuiliwa jela baada ya kushtakiwa kwa uhaini na chama chake kususia uchaguzi. Naye Luhaga Mpina wa ACT- Wazalendo alienguliwa kwa sababu uteuzi wake haukukidhi matakwa ya kikanuni za uchaguzi.

Waangalizi wa kimataifa wameelezea wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa uwazi na machafuko makubwa ambayo yameripotiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu na wengine kujeruhiwa.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Matokeo ya Uchaguzi Tanzania 2025 Bonyeza hapo chini:

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuminywa kwa mtandao wa intaneti kote nchini kunafanya iwe vigumu kuthibitisha idadi ya waliofariki.

Serikali imepuuzilia mbali ukubwa wa maadandano dhidi yake - na kuongeza muda wa kutotoka nje kwa nia ya kumaliza machafuko ya siku tatu yaliyoshuhudiwa nchini humo.

Akipokea cheti chake cha ushindi siku ya Jumamosi, Samia, 65, aliaani vikali vitendo vya vurugu vilivyofanywa na waandamanaji.

Alisema: Matukio haya hayakuwa ya kizalendo hata kidogo," alisema."Tunashukuru vyombo vya usalama kwa kuhakikisha kwamba vurugu hazikuathiri shughuli ya upigaji kura.

"Matukio yaliyofanywa katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe hayakuwa ya kiungwana wala ya kizalendo. Uzalendo ni kujenga nchi wala si kubomoa." Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kupokea cheti chake cha ushindi huko Dodoma.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Samia kuonekana hadharani tangu siku ya uchaguzi -Jumatano Oktoba 29.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alisema kupitia televisheni ya taifa TBC kwamba: Samia alipata takribani kura milioni 31.9, sawa na asilimia 97.66 ya kura zote zilizopigwa, na 87% ya wapiga kura milioni 37.6 waliojiandikisha nchini wakijitokeza kupiga kura

Matokeo hayo yanampa Samia nafasi ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Samia aliingia madarakani mnamo 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake hayati Rais John Pombe Magufuli.

Visiwani Zanzibar Hussein Mwinyi wa CCM, ambaye ni rais aliyeko madarakani, alishinda uchaguzi kwa karibu asilimia 80 ya kura.

Upinzani huko Zanzibar imedai kuwa uchaguzi ulikumwa na "udanganyifu mkubwa", shirika la habari la AP liliripoti.

Sherehe za kuapishwa kwa Mwinyi zinaendelea katika uwanja wa Amaan Complex Zanzibar.

Hakuna maandamano yaliyoripotiwa Jumamosi asubuhi, lakini hali ya wasiwasi iliendelea kushuhudiwa jijini Dar es Salaam, ambapo vikosi vya usalama viliweka vizuizi vya barabarani.

Siku ya Ijumaa maandamano yalifanyika jijini Dar es Salaam na katika miji mingine ambabo vijana waliingia barabarani na kuharibu mabango ya Samia na kushambulia polisi na vituo vya kupigia kura licha ya Mkuu wa Majeshi kuwaamuru wakomesha machafuko hayo.

Waandamanaji wanaishutumu serikali kuwa kuhujumu demokrasia.

Msemaji wa chama cha upinzani cha Chadema siku ya Ijumaa aliiambia shirika la habari la AFP kwamba "takriban watu 700" wameuawa katika makabiliano na vikosi vya usalama, huku chanzo cha kidiplomasia nchini Tanzania kikiambia BBC kuwa kuna ushahidi wa kuaminika kwamba takribani watu 500 walifariki.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Kombo Thabit aliiambia BBC kwamba serikali ya Tanzania bado haijaweza kudhibitisha idadi ya watu waliouawa katika maandamano hayo.

''Kwa sasa hakuna mtu anaweza kusema ni watu wangapi wamefariki au kujeruhiwa. Tunaendelea kupokea ripoti kuhusu mali binafsi ya watu iliyoharibiwa, magari, mali ya umma, magari ya TANESCO ambayo ni kampuni yetu ya umeme yalichomwa. Kwa sasa hakuna hesabu kamili, mpaka serikali itakapopokea ripoti kamili na itatoa idadi kamili,' alisema Mahmoud Thabit.

Alitaja ghasia hizo kuwa ni "matukio michache ya hapa na pale" na kusema "vikosi vya usalama vilichukua hatua haraka na madhubuti kushughulikia hali hiyo".

"Pia tunaendelea kupokea ripoti za mali zilizoharibiwa," Waziri aliiambia BBC Focus on Africa, akiongeza kuwa kuzimwa kwa mtandao kulikuwa muhimu kukomesha uharibifu huo na kuokoa maisha.

''Wakati tulipowasha mtandao wa intaneti ilileta shida kwa watu wachache 'wahuni' ambao walikuwa wakitumia mtandao kuhamasisha vurugu. Sasa kwa mujibu wa sheria za mamlaka ya kusimamia mawasiliano Tanzania - kuna sheria ambazo zinatumiwa wakati kuna hofu ya usalama wa kitaifa kuhusu mtandao wa intaneti ndani ya nchi.''

Baadhi ya makundi ya upinzani yalidai kuwa mamia ya watu waliuawa, huku umoja wa mataifa ukisema kuwa watu kumi wameuawa, madai ambayo Thabit Kombo amekanusha.

.
.