Serikali ya Tanzania yatangaza kurejea kwa shughuli kama kawaida
Chanzo cha picha, Gerson Msigwa
Msemaji wa
Serikali Gerson Msigwa ametoa ujumbe kuwajulisha wananchi kuwa shughuli za
kijamii na kiuchumi zinarejea kama kawaida kuanzia kesho, Jumanne tarehe 4
Novemba 2025.
"Wananchi
wanaaswa kuendelea kuzingatia tahadhari ya miongozo ya kiusalama kadri
itakavyokuwa inatolewa na vyombo vya Ulinzi na Usalama katika maeneo yao,"ujumbe
huo umesema.
Katika
hotuba ya kuapishwa kwake, Rais Samia aliagiza kurejea kwa hali ya kawaida mara
moja.
Marais wa Afrika waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Samia
Chanzo cha picha, Zambia State House
Rais wa
Zambia Hakainde Hichilema amewapongeza Rais Samia Hassan na makamu wake Emmanuel John Nchimbi kwa kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika 29/10/2025.
Akizungumza katika hafla ya kumuapisha rais Samia mjini Dodoma nchini Tanzania, Hakainde
amezungumzia amani, usalama na uthabiti ambao sio tu muhimu kwa nchi hiyo
pekee lakini pia kwa majirani zake.
"Ukosefu
wa utulivu popote ni ukosefu wa uthabiti kila mahali. Tunaelewa kuwa ikiwa
tutakosa utulivu kwa nchi moja, kila mmoja ataathirika
Hichilema alikumbusha
jinsi Tanzania na Zambia zilivyopitia nyakati ngumu katika harakati zake za
ukombozi wa baadhi ya nchi za Afrika," Hichilema alisema.
Akikemea uvunjifu
wa amani, Hichilema alitoa wito wa upendo katika maeneo ya Tanzania.
"Nataka
kutoa wito kwa watu wa Tanzania bara, visiwani Zanzibar, Pemba na kwingineko
kwamba kile ambacho mumekifurahia kwa miaka mingi, lazima kilindwe kwa hali
yoyote ile," alisema Hichilema.
"Kama
tunachangamoto, kama tuna malalamiko tuje kwenye meza moja tu, ya mazungumzo,"
aliongeza Hichilema.
Rais wa
Burundi Évariste Ndayishimiye pia alitoa hotuba yake ambapo alifananisha
uchaguzi na mtihani ambao Watanzania wamefaulu.
Alizungumzia
uhusiano wa nchi hizo mbili akiutaja kuwa wa tangu jadi na jinsi Tanzania
ilivyopokea wakimbizi wa Burundi punde tu baada ya uchaguzi.
Ndayishimiye
aliahidi kuendelea na miradi ya maendeleo kati ya nchi hizo mbili na kusema
kuwa anaamini "Chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania itaendelea kuwa
nyota kwenye njia ya kudumisha amani, kuimarisha maendeleo na umoja wa kikanda.
Hatimaye mtandao
umerejea nchini Tanzania baada ya kufinywa kwa siku sita.
Hili imehjiri
baada ya Rais Samia kuapishwa na kuchukua majukumu yake rasmi.
Katika
hotuba aliyotoa wakati wa kuapishwa kwake Rais Samia alitoa maagizo kwa vyombo
vya usalama kuhakikisha hali imerejea kama kawaida kwa Watanzania.
"Kamati ya kitaifa na kamata za ulinzi za mikoa na wilaya nawataka muhakikishe, kuanzia leo maisha ya wananchi yanarejea mara moja," alisema Rais Samia.
Kuzimwa kwa mtandao kuliathiri mawasiliano, biashara, kudorora kwa utalii mbali na hata kuwa vigumu kujua
hali inavyoendelea nchini humo Tanzania.
Demokrasia haipimwi kwa ni nani aliyeshinda uchaguzi - Rais Samia
Chanzo cha picha, Photothek via Getty Images
Rais wa awamu ya sita nchini Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kwamba kuapishwa kwake hakufanyiki kwa ajili ya walioshinda bali kupitia utekelezaji wa katiba na sheria.
Akihutubia Watanzania punde tu baada ya kula kiapo cha kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili, aliwataka
Watanzania kuendeleza umoja, upendo, amani na kuheshimu sheria za nchi.
"Nawasihi
Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko,
upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya vinyongo, umoja badala ya migawanyiko
na amani badala ya vurugu," alisema Rais Samia.
"Demokrasia
haipimwi kwa ni nani aliyeshinda uchaguzi, bali kwa jinsi tunavyoendesha mambo
yetu baada ya uchaguzi," Aliongeza Samia.
Alitoa wito kwa
watu wote kuungana bila kujali marengo ya kidini wala kisiasa.
"Ushauri wa Waangalizi tutauzingatia ila Maagizo tumeyakataa" – Rais Samia
Chanzo cha picha, Screen grab/TBC
Maelezo ya picha, Rais Samia Suluhu akila kiapo cha uongozi
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kwamba taifa hilo halitakubali maagizo yaliotolewa na waangalizi katika uchaguzi uliokamilika na badala yake akasema kuwa taifa lake litazingatia ushauri wao.
Akiwashukuru punde tu baada ya kuapishwa , kiongozi huyo ameweka wazi kuwa sio kila jambo walilotaka linaweza kutekelezwa ila Tanzania yenyewe ndio yenye uwezo wa kuamua nini cha kufanya na kunukuu maneno ya Rais wa awamu ya Tatu Benjamin Mkapa wakati akiapishwa kuwa rais mwaka 2000.
"Nawashukuru watazamaji wetu wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika,walipotusifu tumepokea sifa hizo kwa nyenyekevu mkubwa. Tumesikia pia waliodhani hayakwenda saw ana mengine hata sisi wenyewe tumeyaona. Maagizo ya kutuelekeza nini cha kufanya tumeyakataa," mwisho wa nukuu ya Rais Benjamin Mkapa iliyosomwa na Rais Samia.
Rais Samia aliongeza kuwa hakuna aliyemkamilifu duniani.
Waangalizi
waliokuwepo kutoka Afrika ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya nchi za
Mawiza Makuu (ICGLR), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) na wengineo kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Waangalizi wa SADC wamesema kwamba uchaguzi wa Tanzania uligubikwa na dosari .
Rais Samia ametoa
hotuba yake baada ya kuapishwa kama rais wa awamu ya sita nchini Tanzania.
Wakati
anazungumza alikiri kuwa kipindi cha kampeni kulikuwa na migawanyiko lakini baada ya
uchaguzi wote wamekuwa kitu kimoja.
"Nawasihi
tuendelee kuilinda itikadi yetu ya umoja na mshikamano," alisema Rais Samia.
Aidha, Samia amezungumzia matukio ya vurugu yaliyochangia watu kupoteza maisha, kupoteza
mali ya umma na watu binafsi katika baadhi ya maeneo nchini humo.
Akikemea
vikali matendo hayo alisema "kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za
Kitanzani akidai kuwa wengine waliokamatwa wakati wa vurugu hizo ni raia kutoka nje
ya Tanzania.
Rais Samia
ametoa onyo kwa wote waliofanya vurugu.
"Sasa
tuchague lenye manufaa kwetu kwani usalama wa taifa lolote hulindwa kwa wote,
kwa nguvu zote na kwa gharama zozote."
Viongozi waliohudhuria uapisho wa Rais Samia watoa wito wa amani
Viongozi mbali mbali barani Afrika wamehudhuria hafla ya kumuapisha na kumpongeza rais wa sita wa muungano wa Tanzania Samia Suluhu eneo la Dodoma nchini humo.
Akitoa hotuba katika hafla ya uapisho wa rais Samia Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ameeleza kuwa anafurahia mshikamano wa Tanzania hasa amani na kumpongeza Rais Samia.
'Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ametoa wito kwa wanachama wa bara la Afrika kudumisha amani ili kuimarisha uchumi.
''Viongozi wa bara Afrika tuendekeze maridhiano hasa wakati wa ghasia ili kuhakikisha uchumi hautatiziki'' asema Hichilema.
Akiongezea amemtaka Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kujumuisha wapinzani wake kwa serikali bila ubaguzi.
Habari za hivi punde, Samia Suluhu Hassan aapishwa kuongoza Tanzania kwa muhula wa pili
Chanzo cha picha, TBC
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepishwai kwa muhula wa pili chini ya ulinzi mkali, kufuatia uchaguzi uliokumbwa na ghasia na kupingwa na upinzani.
Hafla ya uapisho wake huo zinafanyika katika uwanja wa kijeshi katika mji mkuu wa Dodoma.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania huu ni muhula wa pili wa Rais Samia japokuwa ameongoza kwa miaka minne baada ya kumrithi mtangulizi wake Hayati John Magufuli.
Viongozi mbalimbali barani Afrika wamehudhuria ni pamoja na Naibu rais wa Kenya Kindiki Kithure, Rais wa Jamhuri ya Somalia Hassan Sheikh Mahmoud , Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, Rais wa Usumbuji Daniel Chapo na wanadiplomasia.
Samia alitangazwa mshindi Jumamosi kwa asilimia 98 ya kura.
Alikabiliwa na upinzani mdogo huku wagombea wakuu waliokuwa wakishindana nao wakifungwa au kuzuiwa kugombea.
Waangalizi wa kimataifa wameibua wasiwasi kuhusu uwazi wa uchaguzi huo, huku mamia ya watu wakiripotiwa kuuawa na kujeruhiwa.
Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2025: Rais wa Kenya William Ruto ampongeza rais Samia Suluhu kwa ushindi
Chanzo cha picha, Ikulu Kenya/Facebook
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Samoei Ruto, ametuma salamu za pongezi kwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kufuatia kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Rais Ruto amewataka wananchi wa Tanzania kudumisha amani na kuheshimu utawala wa sheria.
Aidha, alihimiza wadau wote wa kisiasa na jamii kuchukua hatua za kujadiliana kwa heshima na kuvumiliana ili kutatua changamoto zozote zinazoweza kujitokeza, kwa lengo la kulinda demokrasia na kudumisha uthabiti wa taifa.
Rais Ruto alisisitiza kuwa Kenya iko tayari kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania katika kutimiza ndoto ya pamoja ya Afrika Mashariki yenye amani, ustawi, na mshikamano.
“Kwa niaba ya Serikali ya Kenya, nawapongeza kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wote wa Tanzania kwa kufanikisha uchaguzi huu kwa njia ya kidemokrasia. Ushirikiano wetu utaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi wetu na ustawi wa eneo zima la Afrika Mashariki,” alisema Rais Ruto.
Malori ya mizigo ya Kenya yazuiwa kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Namanga
Wafanyabiashara kutoka Kenya wamepata pigo kubwa kufuatia vurugu za uchaguzi mkuu zilizotokea nchini Tanzania.
Hii ni baada ya idara ya uhamiaji ya Tanzania kupiga marufuku magari yote ya usafiri wa abiria na Mizigo kuingia nchini Tanzania.
Katika mpaka wa Namanga,foleni ndefu ya malori kutoka Nairobi Kenya imeendelea kushuhudiwa baada ya kukatazwa kuingia Tanzania.
Ghalib Ahmed dereva wa Lori la mizigo kutoka Nairobi Kenya anaenunuwa machungwa nchini Tanzania na kusambaza jijini Nairobi amekwama mpakani kwa karibu wiki sasa.
"Mimi hununuwa machungwa Tanzania na kuuza Nairobi,lakini tangu uchaguzi uchaguzi ulipofnayika wametukataza kuingia wakidai tunaweza kuwa na dhamira mbaya, siwezi kurudi Nairobi nitapata hasara ya mafuta, nasubiri kuangalia iwapo watafungua mpaka Samia akiapishwa."alisema.
Maafisa wa forodha katika mpaka wa Namanga wanasema hiyo ni amri kutoka uongozi kwa ajili ya usalama.
Upande wa usafiri wa umma, Kampuni za mabasi ya usafiri wa abiria kama vile Tahmeed,Modern Coast na nyinginezo zinazosafirisha abiria kutoka Kenya hadi Tanzania pia zimekadiria hasara kubwa baada ya usafiri huo kusimamishwa kwa zaidi ya siku 6 sasa.
Leila Menza, mhudumu wa kukata nauli za mabasi ya umma kutoka Nairobi anasema, wanatumai baada ya Samia kuapishwa hii leo, shughuli zitarejea katika hali ya kawaida waendelee na safari hapo kesho" alimalizia.
Katika mpaka huu wa Namanga, upande wa uchukuzi ,wafanyabiashara wa malori ya mizigo kutoka Kenya ndio waliothirika zaidi na kusitishwa kwa shughuli za kazi baada ya uchaguzi wa Tanzania.
Kwa kawaida,kila siku mpaka wa Namanga hupitish malori mia 3 kutoka na kuingia Tanzania kwa uchukuzi wa bidhaa mbalimbali.
Sherehe ya kumuapisha Rais mteule wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu yaanza
Chanzo cha picha, Screengrab
Maelezo ya picha, Gwaride la Jeshi la Tanzania kutumbuiza katika hafla ya uapisho wa rais mteule
Hafla ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan imeanza katika uwanja wa kijeshi lakini raia wa kawaida hawatahudhuria.
Rais mteule wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuapishwa wakati wowote kutoka sasa baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Jumatano uliokumbwa na utata.
Viongozi mbalimbali barani Afrika wamehudhuria ni pamoja na Naibu rais wa Kenya Kindiki Kithure, Rais wa Jamhuri ya Somalia Hassan Sheikh Mahmoud , Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, Rais wa Usumbuji Daniel Chapo na wanadiplomasia.
Sherehe hizi zinafuata itifaki za kijeshi.
Kilele cha sherehe ni kiapo cha uongozi na mizinga 21 kufyatuliwa.
Ni mara ya kwanza kwa rais mwanamke kula kiapo baada ya kushinda uchaguzi nchini Tanzania.
Kuwepo kwa gwaride kunaashiria mamlaka ya rais ambaye pia atakuwa amri mkuu wa majeshi.
Hata hivyo, upinzani umeutaja uchaguzi wa 2025 uliofanyika juma lililopita kama kejeli kwa demokrasia.
Hafla hiyo inafanyika katika uwanja wa kijeshi na haitakuwa wazi kwa umma.
Picha ambazo BBC imezipata ni gwaride la jeshi tayari liko uwanjani kwa shughuli hiyo nzima ikitarajiwa kutumbuiza wageni mashuhuri watakaokuja kushuhudia uapisho wa rais mteule Samia.
TBC inapeperusha matangazo hayo mubashara kutoka Dodoma kwa taifa.
Rais Samia alitangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 kwa kujinyakulia asilimia 97.66 ya jumla ya kura zote zilizopigwa.
INEC imetangaza kwamba ushindi mkubwa wa Rais Samia ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Tanzania katika awamu tano za kwanza za uongozi wa nchi hiyo.
Wapiga kura milioni 37 walisajiliwa kushiriki kwenye uchaguzi wa mwaka huu huku INEC ikisema kwamba Samia alipata jumla ya kura milioni 31.
Aidha tume hiyo imesema pia kwamba asilimia 87 ya waliosajiliwa kupiga kura walijitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo ambao ulishuhudia maandamano huku mji wa Dar es Salaam ukikabiliwa na amri ya kutotoka nja kati ya saa 12 jioni na saa 12 asubuhi.
Tayari Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi ameapishwa baada ya kumshinda mpinzani wake wa chama cha ACT-Wazalendo Othman Masoud.
Sherehe hiyo ya uapisho wa rais wa Zanzibar ilihudhuriwa na maafisa wakuu wa serikali, akiwemo Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango, wanadiplomasia, na maelfu ya raia wa Zanzibar.
Maelezo ya picha, Wageni wahudhuria uapisho wa urais lakini raia wa kawaida hawajaruhusiwa
Ubalozi wa Marekani waongeza kiwango cha tahadhari ya usafiri kuelekea Tanzania
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kwa mara ya nne ubalozi wa Marekani na Uingereza umekuwa ukitoa tahadhari kwa raia wake walioko Tanzania
Ubalozi wa Marekani umetangaza kuongezwa kwa kiwango cha tahadhari ya usafiri kwenda Tanzania kutoka Kiwango cha 2 hadi Kiwango cha 3, ikimaanisha kuwa ina shauriwa kuepuka safari zisizo za lazima kuelekea nchini humo.
Kiwango hiki kipya kimeongezwa kufuatia kuongezwa kwa kiashiria cha hatari ya “machafuko”, pamoja na sababu nyingine za kiusalama ikiwemo uhalifu, ugaidi, na unyanyasaji dhidi ya watu wa jinsi moja (LGBTQ+).
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa wito kwa wasafiri kutembelea tovuti yao kwa taarifa zaidi kuhusu hatari ya ugaidi hasa katika mkoa wa Mtwara.
Pia tahadhari hiyo imetolewa kwa watu wanaojitambulisha kama jinsi moja walioko nchini humo wakisema wanakamatwa, kunyanyaswa, au wanalengwa na vyombo vya usalama.
Wasafiri wanaopanga kuelekea Tanzania wanahimizwa kuwa na mpango wa dharura wa kuondoka ambao hautegemei msaada wa serikali ya Marekani.
Taifa kuwekewa tahadhari ya usafiri inamaanisha nini?
Tahadhari ya usafiri mara nyingi hutolewa kwa mataifa ambayo yako katika ghasia, uhalifu na unyanyasaji wa kibinadamu wa hali ya juu.
Tahadhari hizi hutolewa kwa viwango, cha juu zaidi kikiwa ni cha nne.
Kiwango cha 1 - Chukua tahadhari za kawaida
Hiki ndicho kiwango cha chini kabisa cha tahadhari.
Inamaanisha kuwa hali ya usalama ni ya kawaida. Wasafiri wanashauriwa kuchukua tahadhari zile zile za kawaida wanazochukua popote, kama vile kuepuka maeneo yasiyojulikana usiku au kutokuwa na vitu vya thamani hadharani.
Kiwango cha 2 - Chukua tahadhari ya juu
Hiki ni kiwango cha tahadhari kinachoonyesha kuwa kuna hatari fulani, ingawa si kubwa sana. Wasafiri wanashauriwa kuwa makini zaidi kuliko kawaida, hasa katika maeneo yenye matukio ya uhalifu, migogoro ya kisiasa, au hatari za kiafya.
Kiwango cha 3 -“Epuka safari zisizo za lazima.”
Kiwango hiki kinaashiria hatari kubwa zaidi kwa usalama wa msafiri.
Kiwango cha 4 – Epuka safari zote
Hiki ndicho kiwango cha juu zaidi cha tahadhari. Kinaonyesha kuwa kuna hatari kubwa sana kwa maisha au usalama binafsi. Safari kuelekea eneo hilo hazipendekezwi kabisa, kwa kuwa mazingira yanaweza kuwa hatarishi.
Athari ya tahadhari ya usafiri kwa nchi
Baada ya Marekani kutoa tahadhari ya usafiri ya Kiwango cha 3 kuelekea Tanzania, wachambuzi wanaonya kuhusu athari za moja kwa moja na za muda mrefu kwa taifa.
Tahadhari hiyo inaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya watalii, kwani wasafiri huchagua maeneo salama zaidi, hivyo kupunguza mapato ya sekta ya utalii.
Pia, inachafua taswira ya kimataifa ya Tanzania kwa kuashiria kutokuwa na usalama au uthabiti.
Onyo hilo pia linaweza kuwazuia wawekezaji, wataalamu na mashirika ya kimataifa kuingia nchini, pamoja na kuathiri mahusiano ya kidiplomasia.
Pia linaibua wasiwasi kuhusu hali ya usalama na haki za binadamu nchini.
Tuiombee Tanzania kumekuwa na vurugu na maafa - Papa Leo
Chanzo cha picha, EPA
Kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo, amewataka waumini wa Kikatoliki kote duniani kuiombea nchi ya Tanzania kufuatia “vurugu zilizotokumba taifa hilo siku ya uchaguzi mkuu kusababisha maafa makubwa”.
Waangalizi wa kimataifa wameelezea wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa uwazi na machafuko makubwa ambayo yameripotiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu na wengine kujeruhiwa.
Vyanzo vya kidiplomasia vimeiambia BBC kuwa kuna ushahidi wa kuaminika unaoonyesha kuwa takriban watu 500 wamepoteza maisha tangu ghasia hizi zilipoanza.
Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Thabit Kombo, amekanusha ripoti hiyo akiongeza kuwa hazijathibitishwa rasmi na serikali.
Kuminywa kwa mtandao wa intaneti kote nchini kunafanya iwe vigumu kuthibitisha idadi ya waliofariki.
Tanzania inasubiri kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan kuanza muhula wake wa pili baada ya kutangazwa mshindi na Tume ya uchaguzi, INEC.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam asema kwamba vyakula kuletwa kutoka mikoani
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila anasema kwamba vitengo vya usalama vimejitahidi kurejesha hali ya utulivu katika mji huo ambao umeshuhudia maandamano tangu Oktoba 29 – siku ya uchaguzi mkuu.
“Inawezekana mukaona kama ni kifungo cha adhabu. Lakini ukweli ni kwamba ni muda mfupi sana ili tuweze kukabiliana vizuri na ipasavyo na makundi hayo ambayo yangeweza kuleta madhara makubwa sana kwa nchi yetu.’
Chalamila alitoa tamko hilo kwenye mahojiano na runinga moja nchini Tanzania.
Miungano ya Ulaya na Jumuiya ya Madola imelaani hali ya maafa na ukiukaji wa haki za kimsingi za raia ambao wamesema wana haki ya kuandamana chini ya uongozi wa sheria za nchi.
Mapema leo, vyanzo vilivyo Tanzania viliiambia BBC kwamba kwa mara ya kwanza Jumapili hii, raia walionekana nje ya majumba yao huku wakikubaliwa kukusanyika kwa makundi ya watu angalau watatu barabarani.
Hata hivyo, maduka yaliyokuwa yamefungwa yalifunguliwa mjini humo Jumapili hii, ila wengi waliofika kununua bidhaa walilalamikia hali kwamba maduka hayo yalikuwa hayana bidhaa nyingi kwa kuwa hakujakuwa na usafiri wowote barabarani kutoka mkoa huo kwa siku tatu sasa.
Lakini Bwana Chalamila anasema kwamba hivi karibuni bidhaa kama vyakula zitakuwepo sokoni na madukani kwa kuwa mipango ya kusafirisha chakula kutoka mikoani imeanza. “
Watu wamezidi kulalamika kwamba sokoni hakuna vyakula. Tumeweka na utaratibu mzuri wa vyakula vinavyotoka mikoani. Tumezungumza mimi na mkuu wa mkoa wa pwani na yule wa mkoa wa Morogoro ili kurahisisha magari yote yaliyobeba vyakula kupita kwa haraka katika njia hizo na kuingia katika mkoa wetu vizuri,” alisema Chalamila.
Aidha mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salama amesema kwamba katika siku chache zijazo huduma muhimu kama maduka makuu yatakubaliwa kufunguliwa ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuwa na bidhaa muhimu madukani mwao kwa ajili ya kuifaa jamii.
Vyanzo ndani ya Dar es Salaam vimeiambia BBC kwamba bei ya mafuta ya petroli imepanda maradufu huku baadhi ya vituo vya kuuza mafuta vikisalia vimefungwa.
Hali hiyo imesababisha magari mengi kutoweza kuwa barabarani ambapo pia kuna vizuizi vya polisi na jeshi.
Kuhusu taarifa zinazopeperushwa na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu hali ya kiusalama mjini Dar es Salaam. Chalamila aliwataka raia wa Tanzania kuzingatia ripoti zinazotolewa na vyombo vya ndani pekee kwa kuwa ndivyo vinavyotoa taarifa sahihi.
Rais mteule wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuapishwa asubuhi hii baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Jumatano ulikumbwa na utata.
Upinzani umeutaja uchaguzi huo kama kejeli kwa demokrasia.
Hafla hiyo tafanyika katika uwanja wa kijeshi na haitakuwa wazi kwa umma.
Kulingana na taarifa ya serikali iliyotangazwa kupitia runinga ya kitaifa ya TBC, sherehe ya uapisho itafanyika katika uwanja wa kijeshi ambapo raia wa kawaida hawatakubaliwa kuhudhuria.
TBC itapeperusha matangazo hayo mubashara kutoka Dodoma kwa taifa.
Rais Samia alitangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 kwa kujinyakulia asilimia 97.66 ya jumla ya kura zote zilizopigwa.
INEC imetangaza kwamba ushindi mkubwa wa Rais Samia ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Tanzania katika awamu tano za kwanza za uongozi wa nchi hiyo.
Wapiga kura milioni 37 walisajiliwa kushiriki kwenye uchaguzi wa mwaka huu huku INEC ikisema kwamba Samia alipata jumla ya kura milioni 31.
Aidha tume hiyo imesema pia kwamba asilimia 87 ya waliosajiliwa kupiga kura walijitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo ambao ulishuhudia maandamano huku mji wa Dar es Salaam ukikabiliwa na amri ya kutotoka nja kati ya saa 12 jioni na saa 12 asubuhi.
Karibu tena katika matangazo yetu ya moja kwa moja, hii leo Jumatatu 03/11/2025
Uingereza na Marekani zatoa tahadhari kwa raia wao nchini Tanzania
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mara ya tatu wiki hii Ubalozi wa Uingereza umetoa taarifa ya tahadhari kwa raia wake wanaoishi nchini Tanzania.
Katika taarifa ya hivi punde iliyochapishwa muda mfupi kwenye ukurasa wa mtandao wa X. Ubalozi wa Tanzania @UKinTanzania umesema kwamba Wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza kupitia idara ya masuala ya kigeni, jumuiya ya madola na meendeleo ya Uingereza imeongeza hali ya tahadhari kuhusiana na hali ya usalama nchini Tanzania.
“Tungependa kuwaomba kutosafiri ila katika hali ya dharura nchini Tanzania. Hii ni kwa sababu ya fujo na vurugu zilizoshuhudiwa kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Kuna uhaba mkubwa wa chakula, mafuta ya petroli na pesa taslimu. Hali hii imezidi kuwa mbaya kutokana na kuminywa kwa mitandao wa intaneti.’ Ilisema taarifa hiyo ya Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.
Hapo jana Ubalozi wa Marekani ulitoa tahadhari nyingine katika muda wa siku tatu na kupandisha kiwango cha tahadhari kuwa RED ALERT ikiwaomba raia wa Marekani kutofika maeneo ambapo maandamano yanashuhudiwa, kwenye umati mkubwa wa watu , kutotoka nje pasipo na dharura, kufuatilia matangazo ya habari kujuwa hali ilivyo nchini humo na kuangazia kwa ukaribu mazingira ya ndani kwa ajili ya usalama wao.
“Kwa sasa kuna amri ya kutotoka nje ambayo inatekelezwa kati ya magharibi na alfajiri .
Katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salam vyombo vya usalama vinaripotiwa kudhibiti vikali usafiri katika baadhi ya barabara kuu za mji huo.
Mtandao wa intaneti umeminywa , hali ambayo inadhibiti mawasiliano ya siku na uwezo wa kufanya malipo kupitia kadi za kimataifa.
Viwanja wa ndege vya kimataifa vina fanya kazi kwa sasa japo safari za ndege ni chache mno .
Hakikisha umethibitsha kwamba safari yako ipo kabla ya kufika uwanja wa ndege. Jiandae kuchukuwa muda mrefu kufika uawnja wa ndege kwa sababu ya vizuizi vya jeshi na polisi vilivyowekwa barabarani,’ ilisema taarifa ya Ubalizi wa Marekani nchini Tanzania.
Umoja wa Ulaya wasikitishwa na hali ilivyo Tanzania , yataka Polisi kutotumia nguvu kupitia kiasi
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Umoja wa Ulaya
Kwa mara ya pili tangu uchaguzi mkuu kufanyika nchini Tanzania Oktoba 29, Umoja wa Ulaya umetoa taarifa kueleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Katika taarifa iliyochapishwa Novemba 2, ofisi ya katibu mkuu wa EU imesema kwamba japo imepokea ripoti za tume huru ya uchaguzi INEC kutangaza ushindi wa wadhfa wa Urais Tanzania na tume ya ZEC kutangaza mshindi wa Urais visiwani unguja, imesikitishwa na hali ya kiuslama ambayo imeshuhudiwa nchini humo tangu siku ya kupiga kura.
Kumekuwa na maandamano na hali ya kutokuwa na utulivu tangu siku hiyo ambapo ghasia na vurugu zimeriporiwa. Pia intaneti imeendelea kuzimwa huku kukiwa na ripoti kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari na maeneo mengine yakishuhudia hali ngumu ya kiuslama wakati wa kupiga kura,’ taarifa hiyo ilisema.
Umoja wa Ulaya aidha umeitaka serikali ya Tanzania kutekeleza majukumu ya kiuslama bila ya kutumia nguvu kupitia kiasi na kuhakikisha kwamba maisha ya binadamu yanalindwa.
Serikali ya Tanzania imesema kwamba uchaguzi huo ulifanyika katika njia ya uwazi huku ikitetea uamuzi wake wa kuminya intaneti nchini humo kwa sababu za ,’kiusalama.’
EU imeeleza wasiwasi mkubwa kutokana na kile imekitaja kutokuwa na hali sawa ya ushindani kwenye uchaguzi huo ambapo Chama kikuu cha upinzani CHADEMA hakikushiriki
Kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani na mgombea wa ACT Wazalendo Luhaga Mpina alienguliwa.
“Kumekuwa na madhila mengine ya utekaji nyara na watu kupotea na vile vile ghasia ambazo zinabana nafasi ya kidemokrasia.
Umoja wa Ulaya unataka wanasiasa wote wanaozuiliwa na serikali ya Tanzania kuachiliwa huru na wale ambao wanakabiliwa na kesi mahakamani, kesi zao kusikizwa kwa misingi ya kufuata sheria na uchunguzi kamili kutekelezwa kuhsiaiana na madai yote ya uvunjaji wa sheria na ukiukaji wa haki za kimsingi za kibinadamu hasa mauaji, utekeaji nyara na watu kupotea,’iliendelea kusema taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya.
Umoja huo umeeleza kwamba ina uhusiano mwema na ushirikiano mkubwa na Tanzania na imehimiza serikali ya nchi hiyo kuhakikisha kwamba mfumo wa siasa za vyama vingi unakubaliwa kuwepo katika mazingira yanayofaa.
CHADEMA yaalani mauaji ya watu kwenye maandamano Tanzania
Chanzo cha picha, X
Maelezo ya picha, John Mnyika
Chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kimetoa taarifa kulaani kile ilichotaja kuwa mauaji ya raia wengi nchini humo kufuatia maandamano ya vijana ya tangu Oktoba 29.
Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika amesema kuwa : ‘kutokana na Ushahidi wa picha za video na nyinginezo, miili ya watu iliyotapakaa barabarani na mitaani na kuwepo kwa ripoti kwamba baadhi ya hospitali zimesema kwamba hifadhi zao za maiti zimejaa – ni ishara kwamba kumekuwa na mauaji ya mamia ya watu ambayo yanatekelezwa na serikali iliyopo kwa sasa.”
CHADEMA aidha imesema kwamba imepokea ripoti kwamba jeshi la polisi linapitia kila hospitali kuchunguza miili iliyohifadhiwa huko ambayo inasemekana ni ya waliouawa kwenye maandamano.
Polisi haijatoa taarifa kuhusu madai hayo japo imesema kwamba kuna baadhi ya raia wa kigeni ambao wanaripotiwa kuingia nchini Tanzania kupitia njia zisizo rasmi na kuhusika katika vurugu na ghasia zinazoshuhudiwa nchini humo.
Baadhi ya wakuu wa mikoa katika meneo kama Mbeya na Arusha wamekielezea kituo cha Habari cha kitaifa TBC kwa njia ya simu kwamba hali ya utulivu imerejea huko na kwamba hakujakuwa na maandamano huko leo.
Hathivyo kuna taarifa kutoka kwa baadhi ya wanaharakati ambazo zimesema kwamba hali bado haijakuwa ya utulivu huku wakitoa picha za video zenye kuonyesha watu waliofyatuliwa risasi wakiwa barabarani.
CHADEMA imelaani hali hiyo na kuitaka polisi kutotumia nguvu kupita kiasi katika majukumu yao wanapokabiliana na waandamanaji ambao wametajwa kuwa wanatekeleza haki yao ya kikatiba.
‘Tungezitaka taasisi za kiusalama kusitisha mara moja utumizi mbaya wa nguvu dhidi ya raia ambao wanaandamana kwa amani. Na Tuneiomba jamii ya kimataifa na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC kuanzisha uchuguzi wa mauaji ya raia wa Tanzania yaliyotekelezwa na serikali na waliopatikana na hatia kuchukuliwa hatua kali za kisheria.”
Pia wanaitaka serikali kurejesha intaneti nchini Tanzania ili kuwawezesha raia kuwasiliana na wapendwa wao kuwezesha huduma muhimu kuendelea.
Hapo jana rais Samia alilaani machafuko yaliyoshuhudiwa tangu Jumatano Oktoba 29 na kusema kwamba hatokubali wachache kuvuruga amani ambayo muungano wa Tanganyika na Zanzibar imefurahia kwa miongo mitano sasa.
Polisi Tanzania yadai raia wa kigeni wameingia nchini humo kuzua vurugu
Chanzo cha picha, AFP Via Getty Images
Maelezo ya picha, Maafisa wa polisi Tanzania wakipiga doria
Msemaji wa polisi nchini Tanzania ametoa taarifa inayodai kwamba jeshi la polisi nchini humo lina ripoti kwamba kuna watu ambao sio raia wa Tanzania ambao wameingia nchini humo kwa njia zisizo rasmi kwabnia mbovu ya kufanya uhalifu ikiwepo vurugu.
Katika taarifa hiyo iliyochapishwa jioni ya Jumapili Novemba 2, polisi nchini Tanzania wanasema kwamba watu hao wapo katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Songwe na mikoa mingeo.
‘Wakati jeshi la polisi linaendelea kuwafuatilia ili kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria, mwananchi yeyote ambaye amempangisha au anaishi na raia yeyote wa kigeni asiyefahamika na anafanya shughuli gani na mienendo yake nia ya kutilia shaka atoe taarifa haraka sana kwa viongozi wa serikali za mitaa, wakuu wa vituo vya polisi, wakuu wa polisi wilaya, makamanda wa polisi mikoa au apige simu polisi.’ Taarifa hiyo ilendelea kusema.
Taarifa hiyo ya polisi imesemekana kutia hofu katika jamii na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uongozi bora ambao wanahisi huenda raia wa kigeni wakalengwa bila ya kuwepo kwa ushahidi wa kutosha.
Polisi nao wametoa onyo kwa raia wa Tanzania kwamba; “ Asipotoa taarifa na watu hao wakakutwa nyumbani kwake au eneo lake la biashara hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.”