'Uchaguzi umeisha tusimame pamoja kama Taifa' – Hotuba ya Kwanza ya Samia Suluhu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais Mteule Samia Suluhu Hassan ametoa hotuba yake ya kwanza baada ya kupewa cheti cha ushindi kwenye uchaguzi wa 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo Samia aliwashukuru wananchi kwa kumchagua.

"Chama cha Mapinduzi kupitia mimi, Tumepokea cheti hiki cha Ushindi cha Uchaguzi Mkuu kwa heshima na unyenyekevu mkubwa sana. Cheti hiki ni uthibitisho wa imani ya wananchi kunikabidhi mimi na chama cha Mapinduzi dhamana ya kwenda kutekeleza ahadi yetu ya kuimarisha, kuilinda na kuijengea heshima na utu wa Mtanzania," alisime Samia.

Rais Samia akizungumza katika hotuba yake, alisema kuwa uchaguzi wa 2025, ni wa kwanza katika historia kufanyika nchini humo kwa nguvu yao wenye, "kwa raslimali zetu wenyewe" na pia kuwa kati ya wagombea 17, wanne ni wanawake.

Vile vile aliwapongeza wagombea wote wa nafasi ya Rais walioshiriki uchaguzi huo akisema kuwa "wameendesha kampeni safi na kiistaarabu".

Aliwakumbusha Watanzania kuwa zoezi la uchaguzi limeisha.

"Wagombea wenzangu, uchaguzi wa mwaka 2025 ndani ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania umehitimishwa. Sasa ni wakati wa kusimama pamoja kama taifa…," alisema Rais Samia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Samia aligusia uchaguzi huo kuwa kipimo cha ukomavu wa demokrasia nchini humo akiashiria kuwa ni ushindi wa kila mmoja.

Wakati anazungumzia hili, vyama vikuu vya upinzani viliondolewa kwenye uchaguzi wa 2025.

Luhanga Mpina aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo alizuiwa kushiriki uchaguzi baada ya INEC kuunga mkono pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu.

Wakati huo huo, Tundu Lissu ambaye alikuwa mgombea wa chama cha CHADEMA - alikamatwa Aprili 9, 2024, na kupelekwa Dar es Salaam. Siku iliyofuata, Aprili 10, 2024, alishitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Lissu alipinga hatua hii akisema ni kinyume cha sheria.

Lissu anakabiliwa na shitaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, kilichotokana na maneno aliyoyatamka yanayohusiana na mpango wa kudhibiti au kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025.

Kesi ya Lissu imevutia hadhira kimataifa na vyombo vya habari.

Samia Suluhu Hassan pia amepongeza Tume Huru ya Uchaguzi kwa namna alivyosimamia uchaguzi kwa sheria na Katiba ya Tanzania.

"Wameweza kusimamia uchaguzi kwa Uhuru, Uwazi na Haki."

Soma zaidi:

Samia alizungumzia waangalizi wa uchaguzi waliokuwa nchini Tanzania kufuatilia uchaguzi huo.

Waangalizi wa uchaguzi huo waliokuwepo ni pamoja na Umoja wa Afrika, SADC, ICGLR ya maziwa makuu na waangalizi wa Afika Mashariki.

"Kuwaalika waangalizi hawa kunathibitisha dhamira yetu ya kuhakikisha kwamba tulikusudia kufanya uchaguzi katika mazingira ya uhuru na uwazi."

Wakati akizungumza hayo, dunia imeshuhudia vyombo vingine kama vile Bunge la Ulaya likisema kuwa uchaguzi wa Tanzania 'haukuwa huru na wa haki'.

"Tunataka washirika wa kidemokrasia kusimama kidete kutetea demokrasia na haki za binadamu," Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Bunge hilo ilisema.

"Watanzania walipokwenda kupiga kura, Jumuiya ya Kimataifa imefuatilia mchakato kwa masikito makubwa. Kile ambacho kingekuwa kufurahia demokrasia, badala yake kimebadilika kuwa ukandamizaji, vitisho na hofu. Uchaguzi huu haukuwa huru na wa haki. Udanganyifu haukuanza kwenye sanduku la kupigia kura," taarifa ya Bunge la Ulaya iliongeza.

Bunge hilo pia lilizungumzia suala la viongozi wa upinzani kunyanyaswa na kukamatwa, vyama vyao kutengwa, na uhuru wa kujieleza kuingiliwa na kumtaja Lissu kama mfano.

"Hakuna uchaguzi ambao unaweza kuwa wa kuaminika wakati chama kikuu cha upinzani kimenyamazishwa," Taarifa hiyo iliendelea.

Akiendele ana hotuba yake, Samia alizungumzia matukio ya uvunjifu wa amani yaliofanyika siku ya uchaguzi.

Hii ni mara ya kwanza azungumzia suala hili na kudai kuwa lengo la wahusika lilikuwa kuvuruga uchaguzi usifanyike.

Alisifu vyombo vya usalama kwa kuhakikisha kuwa shughuli ya siku ya uchaguzi haijaathirika.

"Matukio yaliyofanywa kwenye maeneo ya miji, Dar es laam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe hayakuwa ya kiungwana na kizalendo," Alisema Samia.

Kauli hii inathibisha ripoti za kutokea kwa maandamano tangu siku ya uchaguzi 29/10/2025.

Umoja wa mataifa kitengo cha haki za kibinadamu ulitoa taarifa ikidai kuwa idadi ya waandamanaji waliofariki dunia tangu maandamano yaanze ni kumi peke yake.

''Ripoti tulizopokea zinaashiria kwamba watu takribani 10 wameuawa," yasema Umoja wa Mataifa.

Vile vile maandamano yameshudiwa Namanga mpaka wa Kenya na Tanzania.

Kulingana na timu ya BBC aliyokita kambi eneo hilo, inasemeka kuwa Mtu mmoja anahofiwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mapambano makali kati ya waandamanaji na polisi.

Polisi katika mji wa Dar es Salaam nchini Tanzania, risasi na vitoa machozi vilishuhudiwa kutawanya waandamanaji wakilalamikia kukamatwa kwa viongozi wakuu wa upinzani na kuzuiliwa kushiriki katika uchaguzi wa Urais mbali na madai ya ukandamizaji wa wakosoaji wa serikali, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Reuters.

Samia alisema kuwa yeye na wengine wamesikitishwa na vitendo hivyo na kutoa wito wa ushirikiano.

''Tanzania ndio lulu pekee barani Afrika… watu wake wameishi kwa umoja na kudumisha muungano kwa zaidi ya miaka 61 na kupiga hatua pamoja…,'' amesema Samia.

Alitoa wito wa umoja baada ya kumalizika kwa uchaguzi na kuishi kwa amani.

''Tuimarishe umoja na mshikamano wetu'', Samia alimaliza hotuba kwa maneno hayo.