Masuala yaliyoibuliwa na waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Tanzania

Chanzo cha picha, MWANANCHI
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC News Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
"Nawashukuru waangalizi wetu wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifu tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu mkubwa. Tumesikia pia waliodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi wenyewe tumeyaona. Maagizo ya kutuelekeza nini cha kufanya tumeyakataa,".
Hii ilikuwa sehemu ya hotuba ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kuapishwa kufuatia ushindi wake wa kishindo katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 iaka mitano ijayo, akimnukuu Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamini Mkapa.
Kauli hiyo ilionekana kujibu ripoti kutoka kwa waangalizi wa jumuiya mbalimbali za kimataifa ambazo zinasema kuwa uchaguzi huu haukuwa huru wala wa haki na uligubikwa na dosari nyingi.
Ni takriban juma moja sasa tangu Tanzania imalize uchaguzi mkuu wake. Hata hivyo matukio yaliyofanyika nchini humo wakati na baada ya uchaguzihuo Mkuu bado yanaendelea kujadiliwa ndani na nje ya Tanzania.
Vurugu zilizokumba uchaguzi mkuu na athari zake ni kitu ambacho hakikutarajiwa.
Kwa miaka mingi Tanzania imeonekana kuwa tofauti kwa jinsi inavyoendesha mambo yake kijamii na kisiasa. Rais Samia mwenyewe alikubaliana na hoja hiyo hata wakati mambo yalionekana kwenda mrama.
''Tanzania ndio lulu pekee barani Afrika… watu wake wameishi kwa umoja na kudumisha muungano kwa zaidi ya miaka 61 na kupiga hatua pamoja…,'' alisema Samia katika hotuba yake alipopokea cheti cha ushindi wa uchaguzi uliokumbwa na vurugu.
Katika taarifa hii tunaangazia masuala yaliyoibuliwa na waangalizi kuhusu uchaguzi huo Mkuu.
Maandamano siku ya uchaguzi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waandamanaji wengi wao vijana walijitokeza barabarani kote nchini Tanzania kupinga uchaguzi mkuu wa Jumatano Oktoba 29 ambao walisema haukuwa wa haki.
Vijana hao waliishutumu Serikali kwa kukandamiza demokrasia kwa kuwazuia viongozi wakuu wa upinzani kushiriki – mmoja yuko jela, Tundu Lissu (CHADEMA) na mwingine kuenguliwa, Lugaha Mpina (ACT Wazalendo) kwa kutokidhi vigezo vya kisheria na hivyo kumuongezea Rais Samia Suluhu Hassan nafasi ya kushinda akiwa na chama chake tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Kombo Thabit alija ghasia hizo kuwa ni "matukio michache ya hapa na pale" na kusema "vikosi vya usalama vilichukua hatua haraka na madhubuti kushughulikia hali hiyo".
Katika ripoti yake ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrka AU, ulieleza maandamano hayo kama dosari kubwa na ikatamaushwa na vifo vilivyotokana na maandamano ya baada ya uchaguzi, na kutoa wito kwa mamlaka husika kuchunguza matukio hayo kwa uwazi, na kuhakikisha haki inatendeka kwa wote walioathirika.
Uchaguzi kutokuwa ''huru na wa haki''
Suala la uchaguzi Mkuu wa Tanzania kutozingatia kanuni zinazokuza demokrasia liliangaziwa katika ripoti iliyotolewa na Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
Waangalizi wake walibainisha kuwa uchaguzi huo "haukifikia Kanuni na Miongozo ya SADC ya Kusimamia Uchaguzi wa Kidemokrasia (2021)", kigezo cha uchaguzi huru, wa haki, na wa kuaminika miongoni mwa nchi wanachama.
Kulingana na Jumuiya hiyo uchaguzi haukukidhi viwango vya kidemokrasia kutokana na visa vya viongozi wa upinzani kutishiwa na wengine kuzuiwa kushiriki.
"Katika baadhi ya maeneo, wapiga kura hawakupewa nafasi ya kuwachagua viongozi waliowataka kidemokrasia." wakiashiria maeneo yaliyo na wafuasi wengi wa upinzani
SADC pia ilimesema ingawa siku ya upigaji kura kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya amani mchakato huo hukuendeshwa kwa uwazi. Hoja ambayo pia iliungwa mkono na Umoja wa Afrika AU, ambayo ilisema katika baadhi ya vituo wapiga kura walikuwa na karatasi zaidi ya moja ya kupigia kura
Ujumbe huo pia uliripoti kuhusu kutoshiriki kwa wagombea wa upinzani walioonekana kuwa na nguvu. Tundu Lissu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, yuko jela akituhumiwa kwa kosa la uhaini. Japo chama chake kilitangaz akutoshiriki uchaguzi wowote mpaka pale mifumo ya uchaguzi itakapobadilishwa na kutopendelea chama chochote, kesi yake hasa wakati wa uchaguzi imezua mjadala.
Vitendo hivyo kulingana na SADC vinadhoofisha demokrasia ya vyama vingi vya Tanzania na kukatisha tamaa ushiriki wa wapiga kura.
Vyombo vya habari kutoangazia kampeni kwa usawa
Vyombo vya habari nchini Tanzaia, hasa redio, televisheni na magazeti, vilionyesha kuegemea upande wa chama tawala cha CCM, na hivyo kuzuia kuonekana kwa vyama vya upinzani na wagombea.
SADC imesema kwamba, vyombo vinavyomilikiwa na serikali vilipendelea chama tawala, wakati vyombo vya habari vya kibinafsi vilijishughulisha na kujidhibiti kwa sababu ya kuogopa kuchukuliwa hatua baada ya uchaguzi.
Masuala haya yaliangazia kutofautiana kwa kiasi kikubwa na Kifungu cha 17 cha ACDEG, ambacho kinatetea ufikiaji sawa wa vyombo vya habari vya umma na binafsi kwa wahusika wote wa kisiasa wakati wa uchaguzi.
Hii imewaacha baadhi ya wapiga kura, kama mkazi wa Dar es Salaam, Godfrey Lusana, kukata tamaa.
"Hatuna uchaguzi bila upinzani thabiti. Mfumo wa uchaguzi hauko huru. Tayari tunajua nani atashinda. Siwezi kupoteza muda wangu kupiga kura," aliambia BBC. "Kama tume ya uchaguzi ingekuwa huru kweli, ningepiga kura."
Kuzimwa kwa intaneti baada ya uchaguzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Tarehe 29 Oktoba, 2025, Watanzania walipiga kura kuwachagua viongozi katika nyadhifa mbalimbali kuanzia Urais, Ubunge na udiwani.
Alhamisi Oktoba 30, waliamkia kufungwa kwa mtandao wa ntaneneti katika hatua ambayo ilifanya iwe vigumu kujua kinachoendelea nchini humo.
Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ripoti yao kwa kiwango kikubwa ilionekana kuunga mkono juhudi zilizofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC kwa jinsi ilivyoendesha uchaguzi huo, nao pia walielezea jinsi kuminywa kwa mtandao wa intaneti kulivyokatiza mawasiliano na kuwafanya kushindwa kushughulikia ripoti yao kwa muda kama walivyopanga.
Waangalizi wa EAC pia walisema baadhi yao hawakuweza kufuatilia uchaguzi kwa karibu kutokana na vurugu zilizoshuhudiwa karibu na vituo vya kupiga kura
Kauli ya Bunge la EU

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa kimataifa, Bunge la Ulaya limesema Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025, ''haukuwa huru na wa haki'' na kuelezea kusikitishwa kwao na mchakato huo kwa ujumla.
Katika historia ya Tanzania, uchaguzi wa mwaka 2025, uligubikwa na maandamano pamoja na vurugu.
"Kukamatwa na kesi inayoendelea ya uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu - mtu ambaye bunge hilo imesema uhalifu wake pekee ni kudai uchaguzi huru na wa haki ni mfano wa kuporomoka kwa maadili ya kidemokrasia na uhuru wa mahakama nchini Tanzania.
"Hakuna uchaguzi ambao unaweza kuwa wa kuaminika wakati chama kikuu cha upinzani kimenyamazishwa,"ilisema katika taarifa yake wiki iliyopita.
Bunge hilo limemeishauri Tanzania kutoa kipaumbele kwa mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi na kisasa, wameshauri pia serikali na bunge kuongoza mchakato wa wazi wa mabadiliko ya katiba unaohusisha wananchi.
Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa Oktoba, 29, 2025, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA ambacho kiongozi wake Tundu Lussu yuko rumande kwa mashataka ya uhaini, kilipinga matokeo hayo na kudai kuwa uchaguzi huo ni kejeli kwa demokrasia.
Bunge la Ulaya limetoa wito wa "kuhimiza washirika wote wa Kidemokrasia kutetea kikamilifu demokrasia na haki za binadamu. Iliongeza kuwa Ukimya sio sawa na kutoegemea upande wowote - ni kufanya mambo kuwa mugumu zaidi."
Pamoja na kauli hizi zote, Rais Samia mara baada ya kutangazwa mshindi aliweka wazi kuwa uchaguzi ulikuwa huru, wa haki na wa kidemokrasia", akiwashutumu waandamanaji kwa "kutokuwa wazalendo". Pia ushiriki wa wagombea wengi zaidi wa urais mwaka huu (17) kuliko chaguzi zote sita zilizopita ni ishara kwamba demokrasia imepanuka.















