Maandamano Tanzania: Familia zahaha kupata miili ya ndugu zao

A
Maelezo ya picha, Mhariri Msaidizi wa Baraka Fm, Kelvin Lameck Mwakangondya mmoja wa waliopoteza maisha katika ghasia za maandamano anazikwa Mbeya Novemba 6, 2025 makaburi ya Iwambi
Muda wa kusoma: Dakika 3

Tangu vurugu za maandamano kufuatia uchaguzi mkuu nchini Tanzania, majonzi na hofu vimeendelea kutawala katika baadhi ya familia. Wengi bado hawajapata majibu kuhusu hatima ya wapendwa wao waliopotea, huku baadhi wakithibitisha vifo lakini wakishindwa kupata miili kwa ajili ya maziko.

Baadhi ya familia zimeelezea kupoteza wapendwa wao katika mazingira ya sintofahamu. Wengine wamethibitisha kuuawa, lakini wengine hadi leo bado hawajui ndugu zao wako wapi, hai ama wamekufa licha ya kutafuta hospitali, mochwari na vituo vya polisi. Madaktari wa hospitali kadhaa binafsi na za serikali ambao hawakutaja kutambuliwa kwa sababu za kiusalama walithibitisha kushuhudia majeruhi na miili ya waliofariki katika ghasia hizo huku miili mingine ikichukuliwa magari.

Walisema kuwa: magari "yamekua yakichukua miili na kupeleka maeneo yasiyojulikana." Serikali hadi sasa haijatoa maelezo yoyote rasmi kuhusu madai hayo, licha ya maombi ya vyombo vya habari na familia nyingi. BBC ilimtafuta Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa kwa ajili ya ufafanuzi, bado juhudi zimegonga mwamba.

Mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam ambaye hadi sasa familia yao bado haijapata taarifa za ndugu yao. Ni familia ya kijana Shabani Bakari Hamisi, mwenye miaka 25, mkazi wa Mbagala na fundi aliyekuwa akifanya kazi Ubungo. Kwa siku tano sasa wamekuwa wakitafuta bila mafanikio katika hospitali, polisi na mochwari.

"Tumeenda hospitali zote na baadhi ya vituo vya Polisi vikubwa vikubwa, hana mtoto na hajaoa bado, tunaomba Serikali ingetupa namna yoyote kama kuna watu waliopotea kutokana na maandamano yaliyotokea," alisema ndugu yake kwa huzuni.

Kwa familia kama hizi, kila siku inavyopita ni mateso mapya. Wengine wamekosa hata nguvu ya kuendelea kutafuta kutokana na kukata tamaa na ukimya wa mamlaka.

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Mazishi yenye maumivu

Kwa wale waliofanikiwa kupata miili ya ndugu zao, wameendelea kuzika katika maeneo mbalimbali, lakini haikuwa rahisi kuipata. Alhad Mussa Salum, Sheikh mkuu wa zamani wa mkoa wa Dar es Salaam, alitoa ushuhuda wa kugusa moyo wakati wa msiba wa Sheikh Mohamed Msopa maarufu kama Sheikh Sharif Majini, mmoja wa waliopoteza maisha, pamoja na kushukuru Mungu aliongeza 'Ili kunyanyua jina la Mwenyezimungu juu yeye ndiye aliyesaidia mchakato zote za Muhimbili (hospitali) maana mazingira yaliyokuwepo yalikuwa ni magumu kidogo kupata mwili wowote ule lakini hatimaye tumeweza kupata mwili leo.'"

Mmoja wa waandishi wa habari waliopoteza maisha katika ghasia za maandamano, Kelvin Lameck, mwili wake ulipatikana katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mbeya na anzikwa Novemba 6, 2025 katika makaburi ya Iwambi, Mbeya.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Meneja wa Baraka Media, Charles Amulike, chombo alichokuwa akifanya kazi Lameck kama Mhariri msaidizi anasema ndugu zake waliwapa taarifa ya kukuta mwili huo katika hospitali hiyo ukiwa na majeraha yanaodhaniwa kuwa ni risasi kifuani baada ya kutoonekana kwa zaidi ya saa 24.

Katika hospitali za kibinafsi, madaktari wamesema hali ilikuwa ngumu mno. Wengine walilazimika kutumia sehemu za wodi za watoto kuhifadhi majeruhi kutokana na wingi wa majeruhi na miili. mmoja wao alisema:

"Hali ilikuwa mbaya, tulikua hapa kazini kwa siku tano, wagonjwa na majeruhi wengi, sitasahau katika maisha yangu, yalikuwa mazingira magumu zaidi ya kazi maishani mwangu. Miili tulipeleka sehemu nyingine, hospitali nyingine wakakataa kwa sababu nao wamejaza".

Kwa upande wake, mwanasiasa na mtaalamu wa udhibiti majanga, Mhandisi James Mbatia, alitoa wito kwa serikali kutoa miili ya waliofariki ili jamii iweze kuwapumzisha kwa heshima. Alisema:

"Tupewe miili yetu ya mashujaa wetu waliouawa, ambao ni utamaduni na uungwana wetu wa kiimani, ili twende tukawasitiri ndugu zetu, tukawazike kwa heshima mashujaa wetu bila kuendeleza ghadhabu zaidi, kwa kuwa mdharau mwimba mguu uota tende."

Katika maandamano hayo yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi, watu kadhaa wamepoteza maisha, wakitaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Thabit Kombo, aliiambia BBC kuwa serikali haiwezi kuthibitisha idadi hiyo rasmi. Wengine wanasemekana kukamatwa au hawajulikani walipo, huku mashuhuda walioko Dar es Salaam wakieleza kusikia milio ya risasi katika siku mbili za mwanzo za maandamano. Juhudi za kumtafuta Msemaji wa Serikali zinaendelea.