Urusi lazima ishindwe lakini ‘isisambaratishwe’ asema Macron

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema hataki kuona Urusi ikisambaratishwa kwa kushindwa vita Ukraine.
Akizungumza na vyombo vya habari Ufaransa, Macron ameomba mataifa ya magharibi yaongeze usaidizi wa kijeshi kwa Kyiv na kuongeza kwamba yupo tayari kwa vita vya muda mrefu.
"Nataka Urusi ishindwe Ukraine, na ninataka Ukraine iweze kulinda ardhi yake," alisema.
Lakini aliwashutumu wale ambao alisema wanataka kuviendeleza vita hadi Urusi kwenyewe katika jitihada za ‘kulisambaratisha’ taifa hilo.
Matamshi hayo yanakuja wakati viongozi duniani wanakutana mjini Munich Ujerumani kwa mkutano wa usalama, ulioshuhudia kutolewa ahadi za kuharakisha usambazaji wa silaha kwa Kyiv na kuidhinisha vikwazo vikali zaidi dhidi ya Moscow.
"Sidhani kama wanavyofikiria baadhi ya watu, kwamba tulenge kuishinda kikamilifu Urusi, kuishambulia Urusi katika ardhi yake," Macron ameliambia jarida la Le Journal du Dimanche.
"Waangalizi hao wanataka sana kuiangamiza Urusi. Huu haujawahi kuwa msimamo wa Ufaransa na hautowahi kuwa msimamo wetu."

Chanzo cha picha, Getty Images
Akihotubia mkutano wa Munich siku ya Ijumaa, Macron alisisitiza kwamba sasa sio muda wa mazungumzo na Moscow.
Lakini hakusita kutaja mazungumzo ya amani kama lengo la mwisho.
Rais alipendekeza kuwa jitihada za kijeshi za Ukraine, zinazoungwa mkono na washirika, ndio njia pekee ya " kuirudisha Urusi katika meza ya mazungumzo na kujenga amani ya kudumu".
Pia alipuuzilia mbali uwezekano wa mageuzi ya utawala nchini Urusi, akielezea jitihada kama hizo kote duniani "zilishindwa".
Mazungumzo ya amani
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya matamshi yake Macron, uwezekano wa majadiliano upo mbali sana kwa viongozi wa Ukraine.
Siku ya Ijumaa Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba alikaribisha uamuzi wa kutoialika Moscow kwenye mkutano huo wa usalama Munich.
Viongozi wa Urusi hawapaswi kualikwa mezani ilimradi "taifa hilo la kigaidi linaua, linatumia mabomu na makombora kama kitetezi cha siasa za kimataifa ", alisema.
Rais Volodymyr Zelensky ameondoa uwezekano wa mazungumzo ya sasa hivi na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, akisistiza kuwa "hakuna imani" kati ya pande husika.
Katika mahojiano na BBC mapema wiki hii, pia alipuuzilia mbali fikra ya kutoa ardhi katika kufikia makubaliano ya amani na Moscow.
Macron amewahi kushutumiwa na baadhi ya washirika wa jumuiya ya kujihami Nato kwa kile wanachoamini ni kutuma ujumbe usioeleweka kuhusu Ukraine.
Mnamo Juni mwaka jana alishutumiwa na Bwana Kuleba kwa kusema kuwa ni muhimu Urusi " isiaibishwe kwa uvamizi ".
Wakati huo, Kuleba alijibu kuwa Urusi – ambayo "inajiaibisha" inahitaji kuwekwa mahala pake.













