Vita vya ukraine: Vifaru vya kisasa vya Ujerumani kuwasili muda wowote Ukraine

Lepard Tank

Chanzo cha picha, Getty Images

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Ujerumani hivi karibuni itaweza kupeleka vifaru vyake vya kwanza vya Leopard nchini Ukraine. Akizungumza katika Mkutano wa kila mwaka wa Usalama wa Munich siku chache kabla ya maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa uvamizi wa Urusi, aliwaambia washirika wenzake kwamba watarajie vita vya muda mrefu. Emmanuel Macron wa Ufaransa pia alisema sasa sio wakati wa mazungumzo na Urusi juu ya uvamizi wake wa Ukraine. Tukio hili ni mkusanyiko wa kila mwaka wa viongozi na wanadiplomasia kujadili masuala ya usalama Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris na Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken wanahudhuria na wajumbe wengi wa bunge, pamoja na wakuu wa serikali takribani 30 wa Ulaya.

Mkutano

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika mkutano huo, Bw Scholz alisema ni jambo la busara kujiandaa kwa vita vya muda mrefu na kumuonyesha Rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba Ujerumani na washirika wake hawataiacha Ukraine.

Maafisa wa Ukraine wamesema wanahitaji haraka silaha nzito zaidi, na kwamba vifaru vya kutosha vya vita vinaweza kusaidia vikosi vya Kyiv kurejeshamaeneo yaliyotekwa na Urusi

Ujerumani - ambayo katika miezi ya hivi karibuni ilikabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na kusita kwake kupeleka silaha Ukraine - ilikubali mwezi Januari kuruhusu vifaru vilivyotengenezwa na Ujerumani na vizito vya Leopard kutumwa Ukraine.

Leopard tank

Chanzo cha picha, Getty Images

Pia iliruhusu nchi zingine kutuma vifaru vya Leopard 2 kwe Ukraine - ambapo ilikuwa vimezuiliwa hadi sasa chini ya kanuni za usafirishaji za kimataifa. Bw Macron alisema wiki chache zijazo zitakuwa za maamuzi, akiongeza washirika wanahitajika "kuongeza uungaji mkono wetu" kwa Ukraine kuweza kuanzisha mashambulizi ya kukabiliana na warusi, ili baadaye nchi hiyo iweze kuingia katika mazungumzo ya amani ikiwa na nguvu. Hapo awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye alizungumza na viongozi waliokusanyika kwenye mkutano huo kupitia video, aliwahimiza washirika kuharakisha usambazaji wa silaha, akionya hakuna njia mbadala ya ushindi dhidi ya Moscow. Hakuna maafisa wa Urusi walioalikwa kwenye mkutano huo. Ajenda ni pana - kutoka China hadi mabadiliko ya hali ya hewa - lakini mkutano huo utawapa washirika wa Ukraine nafasi ya kutathmini uvamizi wa Urusi ikiwa ni karibu mwaka mmoja sasa. Kutakuwa na majadiliano ya moto kuhusu misaada kwa Kyiv. Lakini pia kutakuwa na maswali juu ya kiwango na muda wa azimio la Magharibi kadiri shinikizo za kiuchumi linavyokua.