'Jeshi kivuli' linavyomsaidia rais wa muda mrefu wa Uganda kusalia madarakani

Rais Yoweri Museveni (katikati) aliingia madarakani kama kiongozi wa waasi na anatumikia muhula wake wa sita baada ya uchaguzi wa 2021.
Muda wa kusoma: Dakika 7

Wakijihami kwa bunduki ndogo na wakati mwingine kuvaa barakoa wanapofanya doria barabarani nchini Uganda, wanajeshi wa kikosi maalumu cha kijeshi wanazidi kutazamwa kama jeshi la binafsi kumuweka madarakani Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81, pamoja na nasaba ya familia yake inayoendelea kukua.

Museveni ameiongoza Uganda tangu 1986, wakati vikosi vyake vya waasi vilipoingia mji mkuu, Kampala. Tangu wakati huo ameshinda chaguzi nne, zote zimegubikwa na madai ya ghasia na wizi wa kura.

Lakini hili si jambo geni nchini humo, tangu Uganda ilipopata uhuru wake mwaka 1962, mamlaka imewahi kubadilishana tu kupitia uasi au mapinduzi ya kijeshi.

Museveni anataka kuchaguliwa tena mwaka ujao na upinzani unahofia kuwa Kamandi ya Kikosi Maalumu (SFC) inaweza kutumika kuizuia kufanya kampeni, kama inavyosema ilivyokuwa mwaka 2021.

Lakini SFC, ambayo kwa miaka mingi iliongozwa na mwanawe Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, imeshutumiwa na wakosoaji wa serikali kwa kuwateka nyara, kuwatesa na kuwaua wanaharakati wa upinzani mwaka mzima, na sio tu wakati wa uchaguzi. SFC inakanusha madai haya.

"Ni kama jeshi kivuli ndani ya jeshi ambalo linawajibika kwa rais na mwanawe pekee. Kupanda kwake na ushawishi wake kunasababisha chuki miongoni mwa majenerali wakuu," chanzo kimoja cha kijeshi kiliiambia BBC.

Hii inachangiwa na ukweli kwamba Jenerali Kainerugaba, 51, ambaye sasa ni mkuu wa jeshi, na amesema anataka kumrithi baba yake siku moja, amemsajili mwanawe mwenyewe jeshini.

Jenerali Kainerugaba pia amekuwa akiwadharau baadhi ya majenerali waliohudumu kwa muda mrefu, akimwita mtu kama "mpuuzi".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Matamshi yake yalileta mshtuko kupitia duru za kijeshi na kisiasa, lakini serikali ilizidharau kama "soga tu kwenye mitandao ya kijamii".

Miaka kadhaa iliyopita alitoa matamshi ya mzaha kuhusu kuvamia nchi jirani ya Kenya, na kuwasikitisha majenerali.

Wadadisi wanasema kitengo hicho kimekuwa na ushawishi mkubwa kiasi kwamba kinashindana na nguvu ya jeshi la kawaida, ambalo bado lina makamanda waliopigana katika vita vya msituni vilivyomwingiza Museveni na chama chake cha National Resistance Movement (NRM) madarakani.

Waangalizi hawa wameibua hofu kwamba wawili hao wanaweza kugombana siku moja, kama vile huko Sudan ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vimezuka kufuatia mzozo wa madaraka kati ya jeshi na kundi la wanamgambo lililowahi kuungana nalo, Rapid Support Forces (RSF).

Kitengo hicho ambacho sasa kinajulikana kama SFC kilianzishwa wakati Museveni alipochukua madaraka kwa mara ya kwanza, na kina kauli mbiu inayosema "hakuna mbadala wa uaminifu".

"SFC ndicho kitengo chenye nguvu zaidi ndani ya jeshi la Uganda, kinachojumuisha [maofisa] waliofunzwa zaidi, walio na vifaa bora, na wanaofadhiliwa vyema zaidi nchini," Dk Gerald Bareebe, msomi mzaliwa wa Uganda anayeishi katika Chuo Kikuu cha York cha Kanada, aliiambia BBC.

Jeshi la Uganda na SFC walikataa kutoa maoni yao walipoulizwa na BBC.

Jenerali Muhoozi Kainerugaba

Chanzo cha picha, Getty Images

Museveni amewahi kuitetea SFC akisema iliundwa kwa ajili ya Waganda. Alisema ni watu tu ambao hawaitakii Uganda mema ndio wanaweza kutofurahishwa na jeshi kama hilo.

Lakini wakosoaji wa Museveni wanaona tofauti, wakisema kwamba rais ametawala kwa mkono wa chuma tangu atwae mamlaka, na ameigeuza nchi hiyo kuwa miliki ya familia yake.

Wanabainisha kuwa mke wa rais, Janet, ni waziri wa elimu na Jenerali Kainerugaba ndiye mkuu wa jeshi. Uandikishaji wa mjukuu wake katika jeshi, uliotangazwa mnamo Julai, unaonekana kuendeleza nasaba ya familia.

Jenerali Kainerugaba ameongoza SFC mara mbili na anasifiwa kwa kuipanua na kuwa kikosi chenye makadirio ya askari zaidi ya 10,000. Jeshi la kawaida linafikiriwa kuwa na askari wapatao 40,000.

"Wanapitia mafunzo maalum. Na pia wana silaha za hali ya juu, tofauti na jeshi la kawaida," afisa mkuu wa zamani wa kijeshi aliiambia BBC.

Ingawa baba yake alimpandisha cheo na kuwa mkuu wa vikosi vya ulinzi Machi mwaka jana, Jenerali Kainerugaba anasemekana kudumisha udhibiti wa kweli wa SFC, huku kamanda wake wa sasa, Meja Jenerali David Mugisha, akiripoti kwake.

Jenerali Kainerugaba anafanya kazi zaidi kutoka makao makuu ya kitengo, katika jengo lililopewa jina la baba yake, huko Entebbe, karibu kilomita 34 (maili 21) kusini mwa mji mkuu, Kampala.

Walio katika SFC wana mafunzo ya hali ya juu na kitengo kinakadiriwa kuwa na nguvu 10,000

Chanzo cha picha, State House Uganda/X

Maelezo ya picha,

SFC inajivunia kwenye tovuti yake kwamba inafanya misheni maalum "kwa taarifa ya muda mfupi", na imepewa kazi ya kulinda maeneo muhimu kama vile uwanja wa ndege mkuu na maeneo ya mafuta.

Inashukiwa kuvuka hadi Kenya Novemba mwaka jana ili kumkamata mwanasiasa wa upinzani Kizza Besigye, aliyekuwa daktari wa Museveni, na kumrejesha Uganda kujibu kesi ya uhaini, ambayo bado haijaanza. Mwendesha mashtaka wa jeshi amekiri kuhusika kwa vikosi vya usalama vya Uganda.

Wachambuzi kama Dk Bareebe wanahisi kazi ya msingi ya SFC "ni kuhakikisha uhai wa serikali" kwa kujikinga na vitisho, sio tu kutoka kwa upinzani lakini pia majenerali wa jeshi.

"Ina jukumu kubwa kwa kiasi kikubwa katika kukandamiza uhamasishaji dhidi ya serikali na kukinga chama tawala cha NRM dhidi ya upinzani wa ndani na vitisho vya nje," Dk Bareebe alisema.

Ingawa SFC imekanusha kuhusika na wimbi la utekaji nyara na mateso ya wanachama wa upinzani, baadhi ya maafisa wake wamepatikana na hatia ya kutumia mamlaka yao vibaya.

Kesi iliyojulikana zaidi ni ile ya mwanajeshi wa SFC mwenye umri wa miaka 32, ambaye alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifo Novemba mwaka jana kwa kuwapiga risasi watu watatu na kuwajeruhi wengine wawili, akiwemo mtoto wa mwaka mmoja.

Mwezi Mei, ofisi ya rais ilisema inachunguza tukio lililoripotiwa ambapo askari wa SFC walishtakiwa kwa kumtesa dereva wa boda boda.

Dereva huyo alikuwa akikimbia kumfikia mkewe mjamzito aliponaswa kwenye msafara wa rais.

Mwezi huo huo, Jenerali Kainerugaba alizua hasira za umma baada ya kuthibitisha kuzuiliwa kwa mlinzi wa kiongozi wa upinzani, ambaye alikuwa ametoweka kwa siku kadhaa.

Alisema "wavulana" wake walikuwa wamemshikilia Edward Sebuufu, almaarufu Eddie Mutwe, "katika basement yangu", na katika chapisho la mtandao wa kijamii, aliambatanisha picha ya mlinzi huyo akiwa na kichwa kilichonyolewa.

Jenerali Kainerugaba alimdhihaki Bw Sebuufu, akisema "siku hizi anaonekana mwerevu sana" kwani ndevu zake zilikuwa zimenyolewa na "mvulana wangu", akimaanisha mwanajeshi mdogo.

Chama cha Wanasheria wa Uganda kilisema masaibu ya Bw Sebuufu hayakuwa ya pekee, lakini ni "sehemu ya kampeni ya kunyamazisha upinzani na kukandamiza matarajio ya watu wanaotamani uhuru".

Iliongeza kuwa tukio hilo lilisisitiza "mwelekeo hatari wa nguvu za kijeshi na ukandamizaji wa kisiasa".

Shughuli zake mara nyingi zimesababisha shutuma kwamba kuwepo kwake ilikuwa kinyume cha sheria.

Lakini mwezi Juni, bunge lilipitisha marekebisho ya sheria yenye utata, na kutambua SFC kama moja ya huduma nne rasmi za kijeshi, pamoja na vikosi vya nchi kavu, jeshi la anga na jeshi la akiba.

Wabunge wa upinzani walikosoa hatua hiyo wakisema kitengo hicho hakifai kupewa uhalali huo na badala yake kivunjwe.

"Sheria mpya inaidhinisha chombo ambacho kimekuwa kikifanya kazi kinyume cha sheria," alisema mbunge wa upinzani Ibrahim Ssemujju Nganda.

Wasiwasi huu ulioneshwa na mchambuzi anayeheshimika wa Uganda Godber Tumushabe. Hivi karibuni alionya kuwa licha ya nchi hiyo kuwa na uthabiti, "tulicho nacho ni kutokuwepo kwa vita".

 Mwaka huu, bunge lilitambua SFC kama mojawapo ya huduma nne rasmi za kijeshi

Chanzo cha picha, State House Uganda/X

Afisa mkuu wa jeshi, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia madhara, aliiambia BBC kwamba kumekuwa na hali ya kutoridhika ndani ya jeshi kuhusu mchakato wa kuajiri kikosi hicho kwani inaonekana ni ya kikabila.

Vyanzo mbalimbali, vikiwemo vile vya jeshi, viliiambia BBC kwamba SFC ilitawaliwa sana na maafisa wa kabila la Rais Museveni la Banyankore, na jamii zinazohusiana, ili kuhakikisha uaminifu.

"Ukiangalia makamanda wote wa SFC tangu kuanzishwa kwake, wanatoka katika kabila la Museveni," anasema Nganda, mbunge wa upinzani.

Kati ya makamanda sita ambao wameshika wadhifa huo tangu 2007, ni mmoja tu ambaye hatoki magharibi, ambako wanaishi Banyankore.

Kwa kuzingatia maslahi haya yanayoshindana, wachambuzi wanahofia kuwa huenda mzozo wa kuwania madaraka ukazuka kati ya makundi hasimu ya kijeshi katika zama za baada ya Museveni.

"Hofu yangu kubwa ni kwamba hatujui kitakachotokea Museveni atakapokwenda na kuna upinzani ndani ya jeshi," Nganda alisema.

Dk Bareebe alikariri wasiwasi huu: "Mgogoro kati ya SFC na jeshi la kawaida, kila moja ikiwa na uaminifu wake, maslahi, na miundo ya amri, inaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na hata vurugu, hasa kwa kukosekana kwa mpango wazi wa urithi."

Lakini wachambuzi wengine hawakubaliani, wakisema kwamba hapa ndipo Jenerali Kainerugaba atakapokuja kivyake kutokana na maisha yake ya muda mrefu akiwa na jeshi na SFC.

Wanahoji kuwa yuko katika nafasi nzuri ya kushikilia pande zinazohasimiana pamoja na kuhakikisha kuwa ukoo wa Museveni unaendelea, na kuhakikishia utulivu nchini Uganda.

Matokeo kama hayo bila shaka yataonekana kuwa yasiyo ya kidemokrasia na upinzani.

Robert Kyagulanyi, nyota wa zamani wa pop anayejulikana zaidi kama Bobi Wine ambaye anachuana na Rais Museveni kwa mara ya pili mwaka ujao, anakielezea kitengo hicho kama "kikosi cha mateso".

Mapema mwaka huu Jenerali Kainerugaba alitishia kumkata kichwa kiongozi huyo wa upinzani, ingawa baadaye alifuta ujumbe huo wa "utani" na kuomba msamaha.

Bobi Wine aliambia BBC kuwa yeye na wenzake mara nyingi walilengwa na kupigwa na maafisa wa SFC, na anataka kikosi hicho kivunjwe.

"Hii inaonekana kama sehemu ya jeshi ambayo inawajibika kwa maisha ya serikali kupitia ukatili," alisema. "Wanafanya kazi bila kuadhibiwa na wanafanya kazi chini ya ulinzi wa Jenerali Museveni na mwanawe."