Je, mpango wa kusitisha mapigano Gaza unakaribia kuafikiwa?

th

Chanzo cha picha, SHUTTERSTOCK

Na Paul Adams, Mwanahabari wa Kidiplomasia, mjini Jerusalem

BBC News

Katika eneo la tamasha la Nova kusini mwa Israeli, lililoshambuliwa na wapiganaji wa Hamas tarehe 7 Oktoba, familia na marafiki wa mateka wa Israel walianza safari ndefu kuelekea Jerusalem siku ya Jumatano.

Mahali pa tamasha, karibu na Kibbutz Re'im, ndipo mamia ya Waisraeli waliuawa na mamia zaidi kuburutwa hadi Gaza.

Waandamanaji hao, wakiwa wamebeba picha za wale ambao bado hawajapatikana, wanaitaka serikali yao kufanya zaidi kuwarudisha mateka 134 waliosalia nyumbani.

Matumaini yao yamekuzwa kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano.

"Siku na usiku mia moja na arobaini na tano zisizo na mwisho za kutamani wapendwa wetu," Ronen Neutra alisema, akihutubia umati.

Mtoto wa kiume wa Ronen mwenye umri wa miaka 22, Omer, yuko mahali fulani huko Gaza.

"Tunawatakia nguvu, na tunawaomba washikilie kwa muda mrefu zaidi," Ronen alisema.

"Omer, vumilia tena kidogo. Makubaliano yanaweza kupatikana"

TH

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu wapatanishi wa Marekani, Misri na Qatar kukutana mjini Paris mwishoni mwa juma lililopita, vyombo vya habari vya Israel vimekuwa na mazungumzo mengi juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Hakuna waraka wowote ambao umetolewa kwa umma, unaoelezea mapendekezo ya hivi punde, lakini Joe Biden aliposema makubaliano yanaweza kutekelezwa kufikia Jumatatu , uvumi uliongezeka zaidi.

Lakini mpango huo utasheheni nini?

Inafikiriwa usitishaji mapigano unaweza kudumu kwa wiki sita, wakati ambapo mateka 40 wa Israeli wataachiliwa polepole. Raia wa kike na askari wataachiliwa kwanza.

Kwa upande wake, karibu wafungwa 400 wa Kipalestina, baadhi yao waliopatikana na hatia ya makosa makubwa ya kigaidi, wataachiliwa kutoka jela za Israel.

Wanajeshi wa Israel wanaweza kuondoka katika baadhi ya maeneo yenye wakazi wengi zaidi Gaza, na baadhi ya Wapalestina milioni 1.8 waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano tangu Oktoba wanaweza kurejea makwao kaskazini mwa nchi hiyo.

Lakini huku mazungumzo bado yakiendelea nchini Qatar wiki hii - ambapo wapatanishi wa Misri na Qatar wanazunguka kati ya wajumbe wa Israel na Hamas - ni wazi kuwa masuala mengi bado hayajaafikiwa.

Ripoti zinaonyesha kuwa bado kuna mzozo kuhusu idadi ya wafungwa wa Kipalestina watakaoachiliwa kwa kila mateka wa Israel.

Wala bado haijafikiriwa kuwa na makubaliano juu ya kutumwa tena kwa wanajeshi wa Israeli au kurejea kwa Wapalestina kwenye makazi yao.

Lakini Haim Tomer, mkuu wa zamani wa kitengo cha Mossad, mwenye uzoefu wa mazungumzo ya awali, aliniambia alikuwa na matumaini.

"Nadhani tuko karibu sana," alisema.

"Sisemi hivyo kwa uhakika tutaona kuachiliwa kwa mateka na wafungwa wa Kipalestina. Lakini nadhani mazungumzo yanaendelea."

Alinukuu maoni ya kiongozi wa Hamas mwenye makao yake nchini Qatar, Ismail Haniyeh, ambaye alitoa dokezo la kwanza siku ya Jumatano kwamba kundi hilo linaweza kulegeza msimamo wake kuhusu makubaliano.

"Ulegezi wowote wa msimamo wetu tunaoonyesha katika mazungumzo," alisema katika hotuba ya televisheni, "ni kulinda damu ya watu wetu na kukomesha maumivu yao makubwa na kujitolea katika vita vya kikatili vya kuwaangamiza."

Bw Haniyeh aliendelea kusema kuwa Hamas iko tayari kuendelea na mapigano ikibidi, na akawataka Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem kukaidi vikwazo vya Israel na kuandamana kuelekea msikiti wa al-Aqsa mjini Jerusalem wakati wa mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhani.

Kuzungumzia 'uwezekano wa kulegeza msimamo' ilionyesha kuwa Hamas inaweza kufikiria upya madai - kukomesha kabisa mapigano na kuondolewa kabisa kwa wanajeshi wa Israeli kutoka Ukanda wa Gaza - ambayo Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ameiita "ndoto."

Lakini Hamas bado haijajibu rasmi mapendekezo yaliyotolewa mjini Paris.

Haijulikani pia kiongozi wa Hamas huko Gaza, Yahya Sinwar, anafikiria nini kuhusu mpango huo.

Mara ya mwisho alirekodiwa kwenye handaki la chini ya ardhi, mahali fulani chini ya Khan Yunis au Rafah.

Jeshi lake la msituni linaangamizwa polepole juu yake na serikali ya Israeli limeapa kumkamata.

Maafisa wa Israel wamependekeza kwamba mamlaka ya Bw Sinwar yamedhoofishwa vibaya na miezi mitano na nusu ya mashambulizi ya mabomu na vifo vya makumi ya maelfu ya watu wake.

Ripoti kama hizo ni ngumu kudhibitisha, lakini jambo moja ni hakika - ni vigumu zaidi kuwasiliana na mtu aliyeanzisha mashambulio ya 7 Oktoba.

Wakati huo huo, familia na marafiki wa mateka waliobaki wako njiani. Wanasema watafika Jerusalem siku ya Jumamosi.

Je, habari njema itawasubiri watakapofika huko?

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah