Njaa ni nini, hutangazwa wakati gani na kwa nini Gaza, Sudan ziko hatarini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamilioni ya watu huko Gaza wako kwenye hatari ya kupata baa la njaa huku wakihangaika kupata chakula.
Umoja wa Mataifa (UN) pia umeonya kuwa mzozo unaoendelea nchini Sudan unaweza kusababisha janga kubwa la njaa duniani.
Njaa ni nini na hutangazwa wakati gani?
Njaa hutokea wakati nchi ina uhaba mkubwa wa chakula kiasi kwamba wakazi wake wanakabiliwa na utapiamlo mkali, njaa, au kifo.
Hadhi hiyo kwa ujumla hutangazwa na Umoja wa Mataifa (UN), wakati mwingine kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo, na mara nyingi pamoja na mashirika mengine ya kimataifa ya misaada au mashirika ya kibinadamu.
Inaamuliwa kwa kutumia mizani ya Umoja wa Mataifa iitwayo 'Integrated Food Security Phase Classification' yaani ni mpango bunifu wa wadau mbalimbali ili kuboresha uchambuzi na kufanya maamuzi kuhusu usalama wa chakula na lishe.
Lakini ili njaa itangazwe rasmi, mambo matatu yanahitajika kutokea katika eneo maalum la kijiografia:
- Takribani 20% ya kaya zinakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula
- Takribani 30% ya watoto wanakabiliwa na utapiamlo mkali
- Watu wazima wawili au watoto wanne kwa kila watu 10,000 hufa kila siku "kwa sababu ya njaa moja kwa moja au mwingiliano wa utapiamlo na magonjwa".
Kwa nini Gaza na Sudan ziko hatarini kukumbwa na njaa?
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, njaa iko karibu kaskazini mwa Gaza, na inaweza kutokea wakati wowote kati ya Machi na Mei 2024.
Hali hii ni baada ya miezi kadhaa ya mgogoro kati ya Israel na Gaza baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas.
Nusu ya idadi ya watu, takribani watu 1.1m, wana njaa, kulingana na uainishaji wa IPC. Katika hali mbaya zaidi, wakazi wote wa Gaza watakuwa katika njaa ifikapo Julai 2024.
Umoja wa Mataifa ulisema Gaza ina "sehemu kubwa zaidi ya watu wanaokabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula ambao mpango wa IPC umewahi kuainisha kwa eneo au nchi yoyote".
Kwingineko, maafisa wa Umoja wa Mataifa walionya kwamba mzozo unaoendelea nchini Sudan umeitumbukiza nchi hiyo katika "mojawapo ya jinamizi baya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni", ambalo linaweza kusababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), karibu watu milioni 18 nchini Sudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Aprili 2023.
Unicef ilisema imeona utapiamlo miongoni mwa watoto wadogo "zaidi ya makadirio mabaya zaidi", pamoja na milipuko ya kipindupindu, surua na malaria.
Ni nchi gani nyingine zilizo hatarini kukumbwa na njaa?
Shirika la Kibinadamu la Action Against Hunger lilisema nchi nyingine kadhaa pia "ziko hatarini kukumbwa na njaa''
Nchi hizo ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Pakistan, Somalia, Syria na Yemen.

Mnamo Machi 2024, WFP ilionya kwamba Haiti, ambayo inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa na kiuchumi huku kukiwa na ghasia za magenge, "iko ukingoni kupata janga la njaa".
Takribani watu 1.4m huko wameorodheshwa kuwa karibu kupatwa na njaa, na wengine milioni tatu katika kiwango cha chini. Maelezo ya IPC kuhusu hali ya usalama wa chakula nchini Haiti "yanatisha".
Njaa husababishwa na nini ?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa IPC, njaa na majanga makubwa ya chakula yana sababu nyingi, ambazo zinaweza kusababishwa na binadamu, kuendeshwa kwa asili, au mchanganyiko wa zote mbili.
Action Against Hunger ilisema migogoro inasalia kuwa "kichochezi kikuu cha njaa duniani kote".
Nchini Sudan, vita ni sababu ya uzalishaji duni wa chakula na kusababisha bei ya juu.
Pia imesema mzozo unaoendelea Gaza unazuia chakula, mafuta na maji ya kuokoa maisha kuingia katika eneo hilo.
IPC iliangazia mashirika ya misaada ya kibinadamu "kukosa kufika" kaskazini mwa Gaza.
Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC) imesema ukame na kuharibika kwa mazao kunakosababishwa na hali mbaya ya hewa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kunasababisha uhaba mkubwa wa chakula hasa Afrika Mashariki.
El Niño, muundo wa hali ya hewa ambao unaelezea ongezeko la joto lisilo la kawaida la maji ya uso katika Bahari ya Pasifiki, tayari imeathiri usambazaji wa chakula katika Asia ya Kusini, mashariki na Amerika Kusini.
Je, tangazo rasmi la njaa lina maana gani?
Tangazo la njaa halifungui milango ya ufadhili.
Hata hivyo, mara nyingi husababisha mwitikio mkubwa wa kimataifa kutoka kwa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na serikali za kimataifa, ambazo zinaweza kutoa chakula na ufadhili wa dharura.
Baadhi ya mashirika ya kibinadamu kama IRC hutoa matibabu ya utapiamlo. Oxfam imefanya kazi na washirika huko Gaza kusambaza vocha na pesa taslimu kwa chakula na bidhaa za usafi.
WFP inafanya kazi nchini Sudan kurejesha miundombinu kama vile barabara na shule. Pia ina timu za mwitikio wa simu zinazosafiri hadi maeneo ya mbali kupeleka chakula na usaidizi mwingine.
Mashirika mengi kwa kawaida huanza kupanga na kutoa misaada kabla ya njaa kutangazwa ili kuepusha athari mbaya zaidi, kwa kawaida wakati nchi imepewa uainishaji wa awamu ya tatu au zaidi.
Awali njaa ilitangazwa wapi?
Mara ya mwisho njaa kutangazwa rasmi ilikuwa Sudani Kusini mnamo mwaka 2017.
Takribani watu 80,000 walikabiliwa na njaa na milioni nyingine walikuwa kwenye ukingo wa kukumbwa na njaa baada ya miaka mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wakati huo, Umoja wa Mataifa ulilaumu madhara ya vita kwenye kilimo. Wakulima walipoteza mifugo, uzalishaji wa mazao ulipungua sana, na mfumuko wa bei uliongezeka.

Chanzo cha picha, Getty Images
Njaa ilitangazwa awali ni pamoja na kusini mwa Somalia mwaka 2011, kusini mwa Sudan mwaka 2008, Gode katika eneo la Somalia la Ethiopia mwaka 2000, Korea Kaskazini mwaka 1996, Somalia mwaka 1991-1992 na Ethiopia mwaka 1984-1985.
Kati ya 1845 na 1852, Ireland ilikumbwa na njaa, magonjwa na uhamaji.
Takribani watu milioni moja wanakisiwa kufa wakati zao la viazi nchini humo ambalo lililisha theluthi moja ya wakazi lilipoharibiwa na magonjwa. Usafirishaji wa chakula uliendelea hadi Uingereza, ambayo ilitawala kisiwa cha Ireland wakati huo.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












