Utapiamlo watishia maisha ya watoto 132,000 Gaza-Ripoti

Ripoti ya IPC,shirika linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa linalohusika na ufuatiliaji wa usalama wa chakula, linakadiria kuwa "utapiamlo unatishia maisha ya watoto 132,000.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma na Lizzy masinga & Dinah Gahamanyi

  1. Walaghai wa Kichina wafukuzwa nchini Nigeria

    Raia wa kigeni

    Chanzo cha picha, Economic and Financial Crimes Commission/X

    Nigeria imewafukuza raia wa kigeni, wakiwemo raia 50 wa China, katika msako mkali uliofanyika wiki iliyopita dhidi ya mojawapo ya "makundi makubwa zaidi ya uhalifu wa mtandaoni yanayoongozwa na wageni", wakala wa kupambana na ufisadi nchini humo umesema.

    "Hii inaleta jumla ya raia wa kigeni waliotiwa hatiani kufikia 102 katika zoezi linaloendelea," ilisema, na kuongeza kuwa wamepatikana na hatia ya "ugaidi wa mtandao na udanganyifu wa mtandao".

    Ni miongoni mwa wageni 192 waliokamatwa wakati wa operesheni kali huko Lagos Ijumaa iliyopita.

    Nigeria inajulikana kwa ulaghai kwenye mtandao na ulaghai wa mapenzi.

    Kesi za uhalifu wa mtandaoni zilikuwa miongoni mwa makosa yaliyoenea zaidi nchini Nigeria mwaka jana, kulingana na Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC).

    Katika miaka ya hivi majuzi, EFCC imefanikiwa kuteka maficho kadhaa ambapo vijana wahalifu mtandaoni, wanaojulikana kama "Yahoo Boys", hujifunza ujuzi wao wa kulaghai.

    Pia kumekuwa na kesi kadhaa za juu za ulaghai wa mtandaoni zinazohusishwa na Wanigeria wanaoishi nje ya nchi, baadhi zilifichuliwa na Ofisi ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

    Mwaka jana, mmiliki wa Instagram, Meta, aliondoa maelfu ya akaunti nchini Nigeria ambazo zilikuwa zikijaribu kulenga watu katika miradi ya ulaghai mtandaoni.

    Walaghai kama hao kwa kawaida hujifanya kama wanawake mtandaoni ili kuwalaghai watu kutuma nyenzo chafu za ngono kabla ya kuwachafua.

    Kampuni hiyo ilisema pia iliondoa vikundi 5,700 vya Facebook ambapo walaghai walikuwa wakitoa vidokezo kuhusu jinsi ya kuwalaghai watu.

    Wataalamu na mamlaka hapo awali waliwaonya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuendelea kufahamu na kuwa macho kuhusu hatari za ulaghai huo.

    Unaweza kusoma;

  2. Utawala wa Trump unachunguza viza za wageni wote milioni 55 waliopo Marekani kubaini iwapo ni halali

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Utawala wa Trump ulisema Alhamisi unakagua zaidi ya watu milioni 55 ambao wana visa halali vya Amerika kwa ukiukaji wowote ambao unaweza kusababisha kufukuzwa, sehemu ya ukandamizaji unaokua dhidi ya wageni wanaoruhusiwa kuwa Marekani

    Wizara ya Mambo ya Nje ilisema wote wenye viza ya Marekani, ambao ni pamoja watalii kutoka nchi nyingi, wanakabiliwa na "kukaguliwa mara kwa mara," kwa kuangalia dalili zozote kwamba wanaweza kukosa kibali cha kuingia au kukaa Marekani, The Associated Press imeripoti.

    Taarifa kama hizo zikipatikana, visa itabatilishwa , na ikiwa mwenye viza yuko Marekani, atafukuzwa.

    Tangu Rais Donald Trump aingie madarakani, utawala wake umeelezea kuwatimua wahamiaji kinyume cha sheria nchini Marekani pamoja na wamiliki wa viza za wanafunzi na wageni .

    Lugha mpya ya Wizara ya Mambo ya Nje inaonyesha kwamba mchakato huo wa uhakiki unaoendelea ambao maafisa wanakiri kuwa unatumia muda mwingi, umepanuliwa zaidi na inaweza kumaanisha kwamba hata wale walioidhinishwa kuwa nchini Marekani wanaweza kushuhudia ruhusa hizo zikiondolewa ghafla.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Majaji watupilia mbali mashtaka dhidi ya mke wa rais wa zamani wa Rwanda

    Kanziga

    Chanzo cha picha, AFP

    Majaji wa uchunguzi wa Ufaransa wametupilia mbali mashtaka dhidi ya Agathe Kanziga Habyarimana, mke wa Rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana.

    Bi.Kanziga amekuwa akichunguzwa na mamlaka ya mahakama ya Ufaransa kwa takriban miaka 20 kwa tuhuma za mauaji ya halaiki. Mashtaka hayo yaliwasilishwa na vyama vinavyosaidia manusura wa mauaji ya Kimbari ya mwaka 94 kuwasaka watuhumiwa wa mauaji hayo.

    Kulingana na shirika la habari la AFP ,Katika uamuzi wao Majaji waliandika kwamba hakuna mashtaka ya kutosha dhidi ya Agathe Kanziga (Habyarimana) kuonesha kuwa alikuwa mshiriki wa mauaji ya halaiki" au kushiriki katika "njama ya kufanya mauaji ya kimbari , Bi Agathe Habyarimana, 82, ambaye amekuwa akiishi Ufaransa tangu 1998 na ambaye kurejeshwa kwake nchini Rwanda kumeombwa mara kwa mara na mamlaka ya nchi hiyo, sasa anaonekana kutokuwa na uwezekano mkubwa wa kushtakiwa na mahakama ya Ufaransa kufuatia amri hiyo.

    Waendesha mashtaka wa Ufaransa dhidi ya ugaidi jana waliiambia AFP kwamba wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

    Wakili wa moja ya vyama vya kiraia alielezea uamuzi wa majaji kuwa "wa kusikitisha sana na usioeleweka" akisema, "Kulikuwa na ushahidi wa kutosha" dhidi ya mshtakiwa huku akiongeza kuwa anaweza kukata rufaa.

    Lakini wakili wa Habyarimana, Philippe Meilhac, alisifu uamuzi huo kama "chanzo cha kuridhika sana", akisema "ulirudisha heshima yake".

    Mke wa rais wa zamani aliikimbia Rwanda kwa usaidizi wa Ufaransa siku chache tu baada ya ndege ya mumewe kudunguliwa Aprili 1994, na kusababisha mauaji ya kimbari ambayo yalishuhudia takribani watu lakini 800,000 kwa mjibu wa Umoja wa Mataifa wakiuawa katika moja ya ukatili mbaya zaidi wa karne ya 20.

    Uchunguzi umekuwa ukiendelea tangu mwaka 2008, wakati chama cha waathiriwa wa mauaji hayo chenye makao yake nchini Ufaransa kilipowasilisha malalamiko ya kisheria dhidi ya Agathe Habyarimana, ambaye alihojiwa kutokana na tuhuma kuwa alikuwa sehemu ya Wahutu waliopanga mauaji hayo.

    Alikuwa na hadhi ya shahidi msaidizi, ambayo katika mfumo wa sheria wa Ufaransa ni kati ya kuwa shahidi na kushtakiwa. Uchunguzi huo ulifungwa mnamo 2022, lakini waendesha mashtaka wa Ufaransa dhidi ya ugaidi, waliomba ufunguliwe upya.

    Unaweza kusoma;

  4. Utapiamlo watishia maisha ya watoto 132,000 Gaza-Ripoti

    Gaza

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ripoti ya IPC,shirika linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa linalohusika na ufuatiliaji wa usalama wa chakula, linakadiria kuwa "utapiamlo unatishia maisha ya watoto 132,000 walio chini ya umri wa miaka mitano" huko Gaza hadi Juni mwaka ujao, ikitathmini kuwa wanatarajiwa kukumbwa na "utapiamlo mkali".

    Linaongeza kuwa 41,000 kati yao watapata utapiamlo "mbaya", mara mbili ya idadi iliyokadiriwa katika tathmini ya Mei ya IPC, na kuwaweka katika "hatari kubwa ya kifo".

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imeshutumu IPC kwa kuchapisha "ripoti ya uwongo iliyobuniwa kulingana na kampeni feki ya Hamas".

    Inashutumu shirika hilo kwa "kupindisha sheria zake na kupuuza vigezo vyake ili tu kutoa shutuma za uongo dhidi ya Israel".

    "Waraka mzima wa IPC unatokana na uongo wa Hamas ulioibiwa kupitia mashirika yenye maslahi," inaongeza.

    Wizara hiyo inaendelea kudai "hakuna njaa huko Gaza" ikitoa mfano wa malori 100,000 ya misaada inazoingia Gaza kwa karibu miaka miwili ya vita na "kushuka kwa kasi kwa bei ya chakula" hivi karibuni.

    "Kila utabiri ambao IPC imetoa kuhusu Gaza wakati wa vita umethibitisha kutokuwa na msingi na uongo kabisa. Tathmini hii pia itatupwa kwenye pipa la takataka la kudharauliwa la nyaraka za kisiasa," taarifa hiyo inahitimisha.

  5. Aina za Twiga zazidi kuongezeka: wanasayansi watambua spishi nne badala ya moja

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) umetambua rasmi spishi nne tofauti za twiga kwa mara ya kwanza, na kurekebisha uainishaji wake wa awali ambao ulitambua twiga kama spishi moja.

    Kihistoria, twiga wameainishwa kama spishi moja na spishi ndogo tisa, lakini hili kwa muda mrefu limekuwa suala la mjadala kati ya wanasayansi.

    Mnamo 2024, kikundi maalum cha kazi kilianzishwa ili kukagua kwa kina data ya hivi punde ya maumbile, kimofolojia na biogeografia.

    Kikundi kazi kilichambua data ya kina kutoka tafiti nyingi zilizoidhinishwa na kupata tofauti kubwa kati ya nasaba za twiga, jambo linalounga mkono hadhi yao kama spishi tofauti.

    Sasa wanasayansi wanatofautisha:

    • twiga wa kaskazini (pamoja na spishi ndogo za Afrika Magharibi, wa Kordofa na Nubi),
    • twiga mwenye madoadoa
    • twiga wa Kimasai (pamoja na spishi ndogo za Kimasai yenyewe na twiga wa Thornycroft),
    • twiga wa kusini (pamoja na spishi ndogo za Afrika Kusini na Angola).

    Kulingana na wataalamu, kitengo kipya ni muhimu sana kwa uhifadhi wa asili: kitaruhusu tathmini sahihi zaidi ya vitisho na maendeleo ya hatua za kulinda twiga katika kanda tofauti za Afrika.

  6. Njaa yathibitishwa katika Jiji la Gaza kwa mara ya kwanza

    Mtoto

    Chanzo cha picha, Reuters

    Njaa imethibitishwa katika Jiji la Gaza kwa mara ya kwanza, shirika linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa linalohusika na ufuatiliaji wa usalama wa chakula linasema.

    Ainisho ya Awamu Jumuishi ya Usalama wa Chakula (IPC) imeongeza uainishaji wake hadi Awamu ya 5, kiwango cha juu na kibaya zaidi cha kiwango chake cha uhaba wa chakula.

    Inasema njaa imethibitishwa Gaza, inayojumuisha Jiji la Gaza na eneo linalozunguka, huku "hali mbaya" ikitarajiwa kuenea hadi Deir al-Balah na Khan Younis mwishoni mwa Septemba.

    Zaidi ya watu 500,000 katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na "njaa, umaskini na kifo", inaongeza.

    Tunapitia ripoti na tutakuletea zaidi kuhusu matokeo ya IPC hivi karibuni. Kama ukumbusho, IPC yenyewe haitangazi rasmi kama njaa inatokea, lakini inatoa uchambuzi ambao unaruhusu serikali na mashrikika kutoa matamko kuhusu njaa.

    Unaweza kusoma;

  7. Mji wa Gaza utaangamizwa kabisa ikiwa Hamas haitakubali masharti yetu, waziri wa Israel asema

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa ulinzi wa Israel anasema mji wa Gaza utaangamizwa iwapo Hamas haitakubali kuwapokonya silaha na kuwaachilia mateka wote.

    Maoni ya Israel Katz yalikuja baada ya baraza la mawaziri la Israel kuidhinisha mipango ya mashambulizi makubwa katika mji wa Gaza, licha ya upinzani mkubwa wa kimataifa na wa ndani ya Israel.

    Siku ya Jumatatu, Hamas ilikubali pendekezo la wapatanishi wa Qatar na Misri la kusitisha mapigano kwa siku 60, ambayo kwa mujibu wa Qatar yatatoa fursa ya kuachiliwa kwa nusu ya mateka waliosalia Gaza.

    Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu inaonekana alikataa hili, akisema alikuwa ameagiza mazungumzo kuanza kwa ajili ya kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia na kukomesha vita huko Gaza kwa masharti "yanayokubalika kwa Israeli".

    Israel inaamini kuwa ni mateka 20 tu kati ya 50 ambao bado wako hai baada ya miezi 22 ya vita.

    Vyombo vya habari vya Israel vimemnukuu afisa wa Israel akisema wapatanishi watatumwa kwa mazungumzo mapya pindi eneo litakapoamuliwa.

    Katika taarifa yake ya video alipotembelea makao makuu ya kitengo cha Gaza nchini Israel Alhamisi usiku, Netanyahu alisema "ameagiza kuanza mara moja mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka wetu wote".

    "Nimekuja kuidhinisha mipango ya IDF [Jeshi la Ulinzi la Israel] kuchukua udhibiti wa Mji wa Gaza na kuwashinda Hamas," alisema.

    "Mambo haya mawili - kuwashinda Hamas na kuwaachilia mateka wetu wote - yanakwenda pamoja," Netanyahu aliongeza, bila kutoa maelezo kuhusu hatua inayofuata ya mazungumzo itahusisha nini.

    Soma zaidi:

  8. Israel inaendea kusonga mbele Gaza huku shirika moja likitarajiwa kutoa tathmini ya njaa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirikishi la Usalama wa Chakula (IPC) litatoa taarifa baadaye kuhusu njaa katika Ukanda wa Gaza.

    Chombo kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kinachohusika na ufuatiliaji wa usalama wa chakula, ambacho chenyewe hakitangazi rasmi njaa, kilisema mwezi uliopita kwamba "hali mbaya zaidi ya njaa" ilikuwa "ikishuhudiwa Gaza".

    Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema watu 271 wamekufa kwa "njaa na utapiamlo" tangu tarehe 7 Oktoba 2023 - ikiwa ni pamoja na watoto 112.

    Mashirika ya kibinadamu yametoa wito kwa Israel kuwezesha upatikanaji wa misaada zaidi katika Ukanda huo, na kuonya uhaba wa chakula na maji unaweza kuibuka na kuwa baa la njaa kubwa.

    Israel imekanusha kuwa Gaza kuna njaa, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akisema mapema mwezi huu kwamba "sera ya Israel wakati wote wa vita imekuwa ikizuia mzozo wa kibinadamu …".

    Ripoti hiyo mpya inakuja chini ya saa 24 baada ya Netanyahu kusema kuwa ameidhinisha mipango ya shambulio kubwa katika mji wa Gaza, licha ya upinzani mkubwa wa kimataifa na wa ndani.

    Pia unaweza kusoma:

  9. WHO yaonya juu ya hatari ya joto kali mahali pa kazi

    .

    Chanzo cha picha, CHRISTOPHE ARCHAMBAULT/AFP

    Wafanyakazi duniani kote wanahitaji ulinzi bora dhidi ya joto kali kwani mabadiliko ya hali ya hewa husababisha mawimbi ya joto ya mara kwa mara - hiyo ni hitimisho la ripoti mpya kutoka kwa Shirika la Afya Duniani na Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

    Ripoti hiyo inasema mamilioni ya wafanyikazi wanakabiliwa na joto kali inayoathiri afya na utendakazi wao. Inatoa wito kwa serikali, waajiri, na wafanyakazi kushirikiana ili kuandaa mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

    Ingawa WHO imeonya mara nyingi juu ya hatari za kiafya za joto kali, hii ni ripoti yake ya kwanza tangu 1969 haswa juu ya joto kali kazini.

    Mkurugenzi wa mazingira, hali ya hewa na afya wa WHO Rüdiger Krech alisema ugunduzi huo unapaswa kuwa tahadhari.

    Soma zaidi:

  10. Miili mitano yafukuliwa karibu na Shakahola

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Miili mitano imegunduliwa huko Kilifi kufuatia kumalizika kwa makaburi 6 katika kijiji cha Kwa Binzaro karibu na Shakahola katika mkoa wa pwani wa Kenya.

    Hii inakuja baada ya ugunduzi wa makaburi yenye kuhusishwa na kanisa la ‘Kufunga hadi Kufa’ huko Shakahola lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 400 mnamo 2023.

    Hussein Khalid, mwanaharakati wa haki za binadamu na Mkurugenzi Mtendaji wa Vocal Africa ambaye alikuwa kwenye maeneo ya makaburi alisema:

    "Mwili wa kwanza ambao ulipatikana na wenyewe ulionekana kuzikwa hapo hivi karibuni wiki mbili hadi tatu zilizopita. Lakini minne inaonekana kuwa ilizikwa kitambo kidogo na ilikuwa katika hali ya kuharibika."

    Makaburi 21 yanatarajiwa kufukuliwa hii leo.

    Kwa mujibu wa Bwana Khalid, kuchimbwa kwa kaburi la kwanza jana kulionyesha dalili za mchezo fulani unaoendelea.

    "Hakuna mabaki yaliopatikana lakini ilionekana kana kwamba siku zilizopita, mtu, watu wengine au kundi fulani waliondoa maiti zilizokuwepo hapo. Ishara zilionyesha wazi kwamba kulikuwa na mwili eneo husika. Kitu pekee ambacho tulipata kutoka kaburi la kwanza kilikuwa nguo za ndani za wanawake na watoto. Hiyo ilionyesha kwamba inawezekana mtu au watu waliozikwa hapo walikuwa wanawake na watoto."

    Hayo yanajitokeza baada ya hofu kwamba ‘Kanisa la Kufunga hadi Kufa’ huenda nado linaendeleza shughuli zake licha ya Mchungaji wake Paul Mackenzie kuwa kuzuizini.

    Mwezi uliopita, mahakama ya Kenya ilikuwa imeamuru kufukuliwa kwa miili inayoshukiwa kuwa ni ya watu ambao walikufa kwa njaa na kukosa hewa kaunti hiyo hiyo ambapo mamia ya washiriki wa kanisa la Mackenzie walipatikana miaka miwili iliyopita.

    Soma zaidi:

  11. Iran yafanya zoezi la kwanza la kijeshi tangu vita vya siku 12 na Israel

    .

    Chanzo cha picha, IRIB

    Jeshi la Wanamaji la Iran linasema lilitumia makombora matatu ya baharini, yaliyopewa jina la "Nasir, Ghadir, na Ghader," katika mazoezi ya kombora ya "Eqtdar Paydar 1404".

    Haya ni mazoezi ya kwanza ya kijeshi kwa Iran tangu vita vya siku 12 na Israel.

    Kwa mujibu wa tangazo la Jeshi la Wanamaji la Iran, zoezi hili la kombora lilianza (Alhamisi, Agosti 21) kwa lengo la kuonyesha "nguvu ya ulinzi na kujaribu silaha za hivi karibuni" kaskazini mwa Bahari ya Hindi na Bahari ya Oman, na "vitengo vya ardhini, vitengo vya kuruka, maeneo ya makombora ya ufuo wa Bahari na wengineo".

    Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Iran, wakati wa mazoezi hayo makombora na ndege zisizo na rubani yalirushwa kwenye shabaha katika maji ya Bahari ya Hindi.

    Awali Admiral Abbas Hassani, msemaji wa zoezi hilo, alisema kwamba zoezi hilo litafanyika kwa siku mbili. Hata hivyo, idara ya mahusiano ya umma ya jeshi ilitangaza kuwa zoezi la kombora lilimalizika kwa "kufikia malengo yaliyopangwa mapema".

    Zoezi hili la kombora lilifanyika takriban mwezi mmoja baada ya mazoezi ya pamoja ya Iran na Urusi, ambayo yalifanyika katika maji ya Bahari ya Caspian.

    Soma zaidi:

  12. Lil Nas X akamatwa akizurura mitaani akiwa na suruali ya ndani pekee

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rapa aliyeshinda tuzo nyingi Lil Nas X amekamatwa baada ya kuzozana na polisi huko Los Angeles, mamlaka imethibitisha.

    Polisi waliitwa huko Ventura Boulevard saa 05:30 saa za eneo siku ya Alhamisi baada ya ripoti za mtu kutembea barabarani akiwa amevaa suruali ya ndani pekee, msemaji wa Idara ya Polisi ya Los Angeles (LAPD) alisema.

    Baada ya maafisa kufika katika eneo la tukio, idara ya polisi inadai kwamba mwimbaji huyo "alizozana" nao na kuwekwa chini ya ulinzi kwa tuhuma za kuwashambulia.

    Kisha akapelekwa hospitali kwa matibabu kwa uwezekano wa kunywa dawa kupita kiasi. BBC imewafikia wawakilishi wake kwa maoni yao.

  13. Erik Menendez anyimwa kuachiliwa kwa msamaha miaka 30 baada ya kuwaua wazazi wake huko LA

    .

    Chanzo cha picha, California Department of Corrections and Rehabilitation

    Erik Menendez amenyimwa kuachiliwa kwa msamaha baada ya kutoa ombi lake mbele ya bodi ya msamaha ya California.

    Yeye na mdogo wake ambao wote ni mashuhuri, walipatikana na hatia katika mauaji ya 1989 ya wazazi wao matajiri huko Beverly Hills, na alitoa ombi lake la kwanza kwa bodi ya msamaha Alhamisi asubuhi.

    Kaka yake, Lyle, ombi lake la kuachiliwa kwa msamaha kumeratibiwa kusikilizwa siku ya Ijumaa.

    Ndugu wote wawili walistahiki kuomba kuachiliwa kwa msamaha baada ya kupewa hukumu mpya na hakimu mnamo mwezi Mei.

    Erik Menendez anaweza kujaribu kuomba tena kuachiliwa kwa msamaha katika kesi nyingine baada ya miaka mitatu, bodi iliamua.

    Soma zaidi:

  14. Israel kuanza mazungumzo ya kuachiliwa huru mateka wote, Netanyahu asema

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ameagiza kuanza kwa mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia na kukomesha vita huko Gaza kwa masharti "yanayokubalika na Israel".

    Netanyahu aliwaambia wanajeshi wa Israel Alhamisi usiku kwamba baraza lake la mawaziri pia limeidhinisha mipango ya shambulio kubwa katika mji wa Gaza kaskazini mwa eneo hilo, licha ya upinzani mkubwa wa kimataifa na wa ndani.

    Hamas ilikubali pendekezo lililotolewa na wapatanishi wa Qatar na Misri kwa ajili ya kusitisha mapigano kwa siku 60 siku ya Jumatatu, ambayo kwa mujibu wa Qatar itashuhudia kuachiliwa kwa nusu ya mateka waliosalia huko Gaza.

    Lakini akijibu kwa mara ya kwanza, Netanyahu hajakubali mpango huo uliopo mezani kwa sasa.

    Vyombo vya habari vya Israel vimemnukuu afisa wa Israel akisema wapatanishi watatumwa kwa mazungumzo mapya pindi eneo litakapoamuliwa.

    Katika taarifa yake ya video alipotembelea makao makuu ya kitengo cha Gaza nchini Israel Alhamisi usiku, Netanyahu alisema "ameagiza kuanza mara moja mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka wetu wote".

    "Nimekuja kuidhinisha mipango ya IDF (Vikosi vya Ulinzi vya Israel) kuchukua udhibiti wa Mji wa Gaza na kuwashinda Hamas," alisema.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja. Tarehe ni 22/08/2025