Maswali yanayouliza Waafrika kuhusu marufuku mpya ya usafiri ya Trump

Wakosoaji wanahoji kuwa orodha hiyo wakisema haina uwazi na kwamba iliandaliwa kwa misingi ya kisiasa au ya kikabila.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakosoaji wanahoji kuwa orodha hiyo wakisema haina uwazi na kwamba iliandaliwa kwa misingi ya kisiasa au ya kikabila.
    • Author, Jelilat Olawale
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza marufuku mpya ya usafiri dhidi ya mataifa 12 - na saba kati hayo yanatokea barani Afrika.

Tumekuwa tukifuatilia kile ambacho watu katika bara zima wanauliza mtandaoni kwa kutumia Google Trends na kwenye majukwaa ya kijamii ya BBC Afrika.

Haya ni baadhi ya maswali yanayoulizwa ambayo yanazua wasi wasi.

Ni nchi gani zimejumuishwa katika marufuku ya hivi punde ya usafiri?

Saba kati ya mataifa 12 yaliyoathiriwa na marufuku mpya ya Usafiri ya Marekeni yako Afrika:

  • Chad, Congo-Brazzaville, Equatorial Guinea, Eritrea, Libya, Somalia, na Sudan.

Mengine ni Afghanistan, Myanmar, Haiti, Iran, na Yemen.

Amri hiyo pia imeiwekea vikwazo vya muda mataifa kadhaa ikiwa ni pamoja na:

  • Burundi, Togo, naSierra Leone barani Afrika, pamoja na Cuba, Laos, Turkmenistan, na Venezuela.

Raia wa nchi hizi wamezuiwa kutuma maombi la aina fulani za viza, kama vile viza ya wanafunzi na watalii, lakini aina zingine za viza bado zinaweza kupatikana.

Je, kuna tarehe ya mwisho ya marufuku hii? Na nchi zinahitaji kufanya nini ili kuondolewa marufuku?

Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu, tarehe 9 Juni, 2025.

Marufuku hiyo haina tarehe ya mwisho lakini viza zilivyotolewa kabla ya tarehe hiyo hazitabatilishwa, agizo hilo lilisema.

Rais wa Marekani alisema orodha hiyo inaweza kurekebishwa ikiwa "maboresho" yatafanywa na nchi za ziada pia zinaweza kuongezwa huku "vitisho vikiibuka kote ulimwenguni".

Kwa nini nchi hizi za Afrika zililengwa?

Kwa kila nchi iliyowekewa marufuku,Trump alisem zina mifumo ya utoaji pasipoti na hati ya kiraia zinazotiliwa shaka au wamekataa kuwachukua raia wao wenyewe.

Sababu nyingine zilizotajwa ni pamoja na madai ya kuvunjwa kwa sheria za viza za Marekani na watu kutoka nchi husika nakwamba baadhi yao tishio kwa usalama na wa Wamarekani.

Msemaji wa Ikulu ya White House Abigail Jackson anasema vikwazo hivyo "vitawalinda Wamarekani dhidi ya wahamiaji hatari."

"Vikwazo hivi ni vya kawaida na vinalenga nchi binafsi ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo hayana uhakiki mzuri, yaliyo na viwango vya juu vya visa vya kukawia, au kushindwa kushiriki utambulisho na habari za vitisho," msemaji huyo aliiambia BBC mshirika wa Amerika CBS.

Hatua hii kweli inahusiana na usalama, au imechochewa kisiasa?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rais Trump aliangazia shambulizi la hivi majuzi linalodaiwa kuwa la kigaidi huko Boulder, Colorado, akidai liliangazia hatari zinaazoletwa na raia wa kigeni ambao "hawajachunguzwa ipasavyo."

Hata hivyo, mshukiwa wa tukio hilo ni raia wa Misri - na Misri sio miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na marufuku mpya ya usafiri.

Wakosoaji wanahoji kuwa orodha hiyo haina uwazi na inaonekana kuwa na msukumo wa kisiasa au ubaguzi wa rangi, hasa ikizingatiwa kuwa si nchi zote zinazokabiliwa na masuala ya usalama zilijumuishwa - na mataifa mengi yaliyoorodheshwa hayana historia ya hivi karibuni ya matukio ya ugaidi yanayohusisha Marekani.

Umoja wa Afrika ulisema "una wasiwasi kuhusu athari mbaya zinazoweza kutokea" za hatua hizi na kuitaka Marekani kutumia "mbinu ya mashauriano zaidi... na nchi husika."

Amnesty International Marekani iliitaja hatua hiyo kuwa ya "kibaguzi, ubaguzi wa rangi, na ya kikatili", wakati shirika la Human Rights First lenye makao yake nchini Marekani, likiita "hatua nyingine ya kuwadhibiti wahamiaji iliyochukuliwa" na rais.

Balozi wa Somalia nchini Marekani alisema katika taarifa yake kwamba serikali yake "iko tayari kufanya mazungumzo ili kushughulikia matatizo yaliyotolewa." Somalia imetajwa kama "mahali salama kwa magaidi" na Rais Trump.

Marufuku hii itakuwa na athari gani kwa familia na wahamiaji wanaoishi Marekani?

Chini ya marufuku hii mpya ya usafiri, misamaha kadhaa imeainishwa ili inapunguza athari zake kwa makundi maalum ya wahamiaji na familia ambazo tayari zinaishi nchini Marekani.

  • Walio na kibali maalum (Green card) hawataathiriwa na hatua hii na wanaweza kuendelea kuzuru Marekani.
  • Watoto walioasiliwa na raia wa Marekani.
  • Watu walio na uraia pacha na ambao pia wana uraia wa Marekani hawataaathiriwa na marufuku hii.
  • Jamaa wa karibu wa raia wa Marekani - mwenza, watoto, na wazazi -wanaweza kuwasilisha maombi ya viza.
  • Baadhi ya wafanyakazi wa kigeni wa serikali ya Marekani ambao wamehudumu nje ya nchi kwa walau miaka 15 na wenzi wao na watoto.
  • Watu walio na viza ya uhamiaji kwa jamii au dini ya walio wachache na ambao wanakabiliwa na mateso nchini Iran pia wameponea marufuku ya usafiri ya Trump.
  • Raia wa Afghanistan walio na visa maalum ya uhamiaji pia wanaruhusiwa kuingia Marekani.

Misamaha hii ina maana kwamba wakati marufuku hiyo inazuia kuingia kutoka nchi 12 nyingi za Kiafrika, watu ambao wako katika kundi hili hawataathiriwa na vikwazo.

Je, kuna uwezekano marufuku hii mpya kukumbwa na changamoto za kisheria?

Jeff Mason, mwandishi wa Reuters katika Ikulu ya Marekani, aliambia BBC kwamba marufuku hii mpya ni sawa na ile iliyotolewa wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, mwaka wa 2017, ambayo ililenga nchi nyingi za Waislamu, ingawa orodha ya sasa inajumuisha mataifa mengi zaidi.

Mason alidokeza kuwa marufuku hiyo ilipitishwa kupitia tangazo la rais - sawa na amri ya utendaji - na kwamba utawala unaamini kuwa una mamlaka ya kutekeleza hatua hiyo. Hata hivyo, pia anatarajia marufuku hiyo mpya kukabiliwa na changamoto za kisheria, sawa na ilivyoshuhudia katika hatua ya awali, na iliyoibua maswali kuhusu athari zake kwa watu kutoka nchi zilizoathirika.

Je, hatua hii ni ya kushangaza?

Kwa wa ambao wamekuwa wakimfuatilia Trump kwa miaka kadhaa tangazo la marufuku ya kuingia Marekani sio la kushangaza.

Tangu arejee katika Ikulu ya White House, Trump amezindua kampeni ya utekelezaji wa ahadi yake ya kuwafurusha wahamiaji na hii inaonekana kama hatua ya hivi punde ya kuendeleza ukandamizaji huu.

Tayari alikuwa ametekeleza marufuku kama hiyo wakati wa muhula wake wa kwanza mwaka 2017, wakati nchi mbili ambazo sasa zimejumuishwa katika orodha hiyo mpya, Somalia na Chad, pia zililengwa.

Je, marufuku hii inaweza kuathiri timu za kitaifa zinazopanga kuhudhuria Kombe la Dunia la 2026 nchini Marekani?

Habari njema kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, ni kwamba agizo kuu la Trump linajumuisha msamaha wa wazi kwa wanariadha, wanachama wa timu, makocha, wafanyikazi wa usaidizi, na jamaa zao wa karibu wanaosafiri kwa hafla kuu za michezo kama vile Kombe la Dunia na Olimpiki.

Hii ina maana Iran, ambayo tayari imefuzu kwa Kombe la Dunia la 2026, itaweza kutuma timu yake na wasaidizi muhimu kwa mashindano hayo.

Hata hivyo, wachezaji wa Iran hawataruhusiwa kuleta marafiki au jamaa ambao pia ni raia wa Iran - jamaa wa karibu pekee ndio watakaoruhusiwa.

Je, hii inatofautiana vipi na marufuku ya usafiri ya 2017?

Wakati wa muhula wake wa kwanza, Rais Trump alitoa marufuku ya usafiri iliyolenga nchi saba zilizo na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu, ambazo wakosoaji waliziita "marufuku dhidi ya Waislamu." Amri hiyo ilikabiliwa na changamoto nyingi za kisheria na ilirekebishwa mara kadhaa kabla ya kuidhinishwa na Mahakama ya Juu Zaidi ya Marekani mwaka wa 2018. Rais Joe Biden baadaye alibatilisha marufuku hiyo mwaka wa 2021.

Toleo la sasa limeundwa kimkakati zaidi. Kulingana na mwandishi wa Amerika Kaskazini Jake Kwon, inaondoa mantiki ya kidini kwa kuzingatia mambo kama vile ukosekafu wa utulivu wa kisiasa na kadhalika.

Ingawa nchi kama vile Iran, Libya, na Somalia zilijumuishwa kwenye orodha zote mbili, marufuku hii mpya imepanuliwa na kujumuisha mataifa 12.

Tofauti na marufuku ya awali, ambayo makataa yake ilitakiwa kutekelezwa kwa kati ya siku 90 hadi 120, toleo hili halina tarehe maalum ya mwisho.

Maelzo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi