Kufunga mpaka kufa: 'Mke wangu na watoto sita walimfuata Mchungaji Mackenzie'

Chanzo cha picha, Reuters
Mhubiri wa Kenya Paul Nthenge Mackenzie anatarajiwa kufikishwa mahakamani kufuatia kupatikana kwa miili ya watu katika eneo lake lenye pori.
Anatumiwa kwa kuhimiza wafuasi wake kujiua kwa njaa - mamia ya jamaa sasa wanashangaa kile kilichowapata wapendwa na ndugu zao.
Mchungaji huyo ambaye niongozi wa Kanisa la Good News International Church, Mchungaji Mackenzie, aliposema kwamba ulimwengu utafika mwisho Juni 2023, mke wa Stephen Mwiti alimuamini.
Sasa, ana hakika kwamba mkewe alikufa kwa njaa akiwa pamoja na watoto wao sita.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye anajipatia riziki yake kwa kuuza maandazi na mikate, amekuwa na picha iliyokunjwa mkononi ya mke wake na watoto wake wanne akiuliza kama kuna mtu yeyote amewaona.
Amekuwa akifanya hivi mara kwa mara katika mji wa Malindi, kusini-mashariki mwa Kenya, tangu mkewe alipotoweka Agosti mwaka jana.
Bw Mwiti pia amekuwa akimtafuta pamoja na watoto katika msitu wa Shakahola, ambapo waumini wa kanisa la Mchungaji Mackenzie walikuwa wamejitenga huko kwa ibada maalumu.
Mkewe, Bahati Joan, alikuwa mjamzito alipoondoka mwaka jana na watoto wao: Hellen Karimi (9), Samuel Kirimil (7), Jacob Kimathi (3), Lillian Gatumbi (miezi 18), na Angelina Gatumbi (miezi saba).
Baadaye Bw Mwiti aligundua kuwa mkewe alikuwa amejifungua mtoto wa kiume ambaye pia alifariki.
Alikuwa mfuasi mwenye bidii wa Mchungaji Mackenzie tangu 2015 na alikuwa ameenda Shakahola kwa mara ya kwanza mnamo 2021, kisha akaendelea kuwa anakwenda na kurudi.
Baada ya kuwatahadharisha polisi mara nyingi na kushindwa kujaribu kuwaokoa, alifahamu hivi majuzi kutoka kwa watoto wengine waliotoroka na waliokuwa wakishikiliwa na polisi wa Kenya, kwamba watoto wake walikuwa wamefariki.
"Waliweza kuwatambua kutokana na picha. Walijua majina yao na mahali Jacob na Lillian walikuwa wamezikwa," anasimulia, akibubujikwa na machozi.
"Niliambiwa nisijaribu tena kuwatafuta watoto wangu. Wote walikuwa wamekufa. Nilichelewa sana."
Anaamini walizikwa msituni lakini miili yao bado haijatambuliwa.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shakahola ni neno la Kiswahili ambalo kwa tafsiri rahisi ni "mahali pa kuondoa mazonge na wasiwasi".
Inapatikana katika eneo kubwa la ekari 50,000 (hekta 20,000) la Chakama Ranch katika kaunti ya pwani ya Kilifi.
Mchungaji Mackenzie anaripotiwa kumiliki ekari 800 za eneo la msitu huo.
Mlango wa kuingia msituni, kwa kutumia njia mbovu kando ya barabara kuu, ni mwendo wa saa mbili kwa gari kutoka Malindi, mji mkuu ulio karibu zaidi.
Vichaka vya miiba na vichaka vingi hutanda kwenye mandhari na kufanya safari ya kuingia Shakahola kuwa ngumu. Ni kawaida tembo kuzurura katika eneo hilo.
Hakuna mtandao wa simu, hakuna muunganisho wa intaneti. Lakini hapa ndipo nchi takatifu mpya ilipoanzishwa.
Eneo hilo lilikuwa limegawanywa katika vijiji, kila kimoja kikipewa majina ya mahali kibiblia.
Baadhi ya wafuasi wa Mchungaji Mackenzie waliishi maisha ya kunyimwa vitu huko Yudea. Wengine walijificha huko Bethlehemu. Kulikuwa pia na Nazareti.
"Niligundua kuwa mke na watoto wangu waliishi na kufa Yerusalemu," Bw Mwiti asema. Lakini hajaonekana mpaka sasa tangu maafisa walipoanza kufukua miili kutoka kwenye makaburi yaliyoko katika eneo hilo na yaliyowekwa alama.
Katika msitu huo, wachunguzi walikuwa wamechora awali maeneo 65 ambapo watu walizikwa. Kila moja lilikuwa na makaburi kadhaa yenye kina kifupi huku miili ikiwa imejibana.
'Watoto walikuwa wa kwanza kufa'
Waliofukua maiti hizo wanasema hali ya kuwaona watu waliozikwa bila utu inawaandama. Kufikia sasa watu 110 wamethibitishwa kufariki, lakini kuna hofu kwamba huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka zaidi huku msitu huo ukiendelea kupekuliwa.
Uchunguzi wa maiti bado unapaswa kufanywa lakini polisi na waendesha mashtaka wa serikali wanasema pamoja na watu hao kufa kutokana na njaa, baadhi ya wafuasi wanaweza kuwa wameuawa kwa kunyongwa, kuzidiwa au kupigwa hadi kufa kwa vitu butu.
Waumini wa zamani wa Kanisa la Good News International wamesema walilazimika kukaa na njaa kama sehemu ya kufuata mafundisho yake.
Titus Katana, ambaye alifanikiwa kutoroka, anasema waliojaribu kuondoka kwenye ibada hiyo walitajwa kuwa wasaliti na walishambuliwa vikali.
Pia alisema kuwa kuna utaratibu ambao watu walipaswa kufa kabla ya mwisho wa dunia.
"Watoto walikuwa wa kwanza kufa. Kisha baada ya watoto, walifuata wasio katika ndoa. Kisha, akina mama na wazee walikuwa wanafuata."
Viongozi wa kanisa walipaswa kuwa wa mwisho kufa.
Akifafanua kilichomvutia kwenye kanisa hilo, Bw Katana alisema alifikiri kuwa Mchungaji Mackenzie alikuwa "anahubiri neno la Mungu vyema".
Kivutio cha ziada kilikuwa kwamba "Mackenzie pia alikuwa akiwauzia ardhi wafuasi wake. Hilo lilinivutia. Nilinunua ekari 15. Lakini nilipoona mahubiri yake yalikuwa ya ajabu, nilichagua kuondoka."

Chanzo cha picha, Youtube
Bw Mwiti anasema alikuwa amesikia habari za jinsi mtoto wake mchanga kwamba alinyonyeshwa mara moja pekee. Kisha akazibwa pumzi hadi kufa.
“Nilisikia wakati mwanangu alipouawa, badala ya waumini wa ibada hiyo kuhuzunika, walipiga makofi na kushangilia kwamba anakwenda kukutana na Yesu,” anasema.
Uchambuzi wa BBC wa mahubiri ya Mchungaji Mackenzie kwenye video hauonyeshi akiamuru watu moja kwa moja wafunge, lakini kuna marejeleo mengi ya wafuasi kujitoa, ikiwa ni pamoja na maisha yao.
Mwishoni mwa juma lililopita, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya liliripoti kwamba watu 410, wakiwemo watoto 227, ambao walidhaniwa kuwa na uhusiano fulani na kanisa la Mchungaji Mackenzie, walipotea.
Ndugu zao sasa wanazunguka katika hospitali na kituo cha polisi cha Malindi, wakisubiri habari za wapendwa wao.
Hakuweza kumshawishi mama kuondoka
Miongoni mwao ni Patrick Ngumbau.
Mama yake alipotea miaka miwili iliyopita na aliamua kwenda kumtafuta Shakahola, lakini licha ya kumpata hakuweza kumshawishi aondoke.
"Nilimuuliza ikiwa kama atakubali kurudi nyumbani. Aliniambia alikuwa huko kwa lengo moja, kumtafuta Yesu," Bw Ngumbau asema huku akiwa miongoni mwa mamia ya watu waliokuwa wakisubiri taarifa kuhusu jamaa zao.
"Niliondoka Shakahola mnamo 2021 nikiwa na huzuni sana kwa sababu nilihisi tayari tumempoteza mama yetu."
Alikuwa ametoka kaunti ya Makueni - 270km (maili 170) - ili kupata taarifa zaidi. Ndugu wa waliotoweka wamekusanyika Malindi kutoka nchi nzima na hata nchi jirani za Tanzania na Uganda, pamoja na Nigeria ambao ni upande wa pili wa bara hilo.

Chanzo cha picha, Reuters
Christine Nyanchama alifika Malindi akitokea Nyamira, karibu kilomita 800, kumtafuta dadake, shemeji yake na ndugu zake wengine sita. Watoto wa dada yake tayari wamepatikana wamekufa, lakini Bi Nyanchama anadhani wengine bado wanaweza kuwa hai.
“Popote alipo dada yangu anahitaji kusaidiwa haraka iwezekanavyo, kabla hajafa, naelewa kuwa tayari amefunga siku 22,” anasema akirejea ujumbe mfupi wa mwisho aliopokea.
Mafundisho ya Mchungaji Mackenzie mtandaoni na kwenye vipindi vya Televisheni yalionekana kuwagusa baadhi ya watu. Miongoni mwa mambo mengine, alihubiri dhidi ya elimu rasmi na tiba ya kisasa.
Alikuwa anasema kwamba alikuwa amelifunga Kanisa lake miaka minne iliyopita baada ya takriban miongo miwili ya uendeshaji, lakini mahubiri yake, ambayo mengine bado yanapatikana mtandaoni, yanaonekana kurekodiwa baada ya muda aliyoutaja.
Baadhi ya wafuasi wake wenye utii walichana vyeti vyao vya elimu, wakaacha kazi na kukataa kuwachanja watoto wao chanjo mbalimbali.
Dk Susan Gitau, mwanasaikolojia na mshauri nasaha anaamini kwamba watu wengi waliomfuata Mchungaji Mackenzie - ikiwa ni pamoja na wahitimu wa chuo kikuu na afisa wa polisi wasomi - walikuwa wakitafuta faraja, matumaini, nguvu na usaidizi.

Chanzo cha picha, Reuters
Mchungaji Mackenzie alikamatwa mwezi Machi wakati watoto wawili walipatikana wakiwa wamekufa huko Shakahola. Yeye na wazazi wa watoto hao walishtakiwa kwa kuwashindisha njaa na kuwaziba pumzi na kufa kabla ya kuwazika msituni.
Hata hivyo, aliachiliwa huru kwa kukosekana ushahidi.
Sasa amerejea rumande lakini hajazungumzia mashtaka ya mauaji, itikadi kali na kutishia usalama wa umma ambayo anakabiliwa nayo.
Rais William Ruto ameahidi kuunda tume ya kuchunguza kilichotokea lakini mamlaka zenyewe zinakabiliwa na maswali magumu. Moja kipi kimefanywa kuchukua muda mrefu kugundua kitu kilichokuwa kinaendelea.
"Hakuna kisingizio kwa mamlaka kutogundua hili," anasema Hussein Khalid, mkurugenzi mtendaji wa Haki Africa, kundi ambalo liliibua hoja kuhusu vifo hivyo.
"Tumedhamiria na tunataka kuhakikisha kila mwathirika anapata haki."
Bw Mwiti analaumu serikali, polisi na mamlaka za mitaa huko Malindi kwa kukosa kuchukua hatua.
"Tayari nina umri wa miaka 45. Dakika niliposikia kwamba wamekufa, nilihisi kwamba na mie nimekufa pia."
Sasa amewapa mamlaka sampuli ya DNA yake kwa matumaini kwamba watoto wake wanaweza kutambuliwa. Hapo ndipo ataweza kuanza kuomboleza.















