Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?

Chanzo cha picha, YOUTUBE
- Author, NA Peter Mwai, Deka Barrow na Rose Njoroge
- Nafasi, BBC NEWS
Kiongozi wa dhehebu tata la Kikristo nchini Kenya anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo, huku shughuli ya uchimbaji wa miili iliyopatikana kwenye makaburi ya pamoja kwenye ardhi yake ikiendelea. Zaidi ya miili 100 imefukuliwa kufikia sasa.
Kasisi Paul Nthenge Mackenzie amesema alifunga Kanisa lake la Good News International miaka minne iliyopita baada ya kuhudumu kwa takriban miongo miwili.
Lakini BBC imefichua mamia ya mahubiri yake ambayo bado yanapatikana mtandaoni, ambayo baadhi yanaonekana kurekodiwa baada ya wakati huo.
Mahubiri hayo yanatoa taswira gani kumhusu mtu huyo ambaye wafuasi wake wamejiua kwa njaa?
'Mtu yeyote asirudi nyuma'
Kwa sauti ya shauku, Mchungaji Mackenzie anatoa mahubiri yake mbele ya mkusanyiko makubwa wa watu kwa msisimko wa mada zake zilizo na itikadi kali.
"Tunakaribia kushinda vita... mtu yeyote asirudi nyuma... safari inakaribia kukamilika," bango kwenye skrini huwa imeandikwa hivyo.
Mojawapo ya video kwenye chaneli ya YouTube ya kanisa lake inasema na nukuu: "End Time Kids" na unaonyesha vikundi vya watoto wadogo wakitoa ujumbe mbele ya kamera.

Chanzo cha picha, YOUTUBE
Zingine huishia kwa kutoa pepo ambapo wafuasi - hususan wanawake - hujigaragaza sakaduni wakati yeye "anakabiliana" na nguvu za mapepo ndani yao.
Chaneli yake ya YouTube ina maelfu ya watu waliojisajili na ukurasa wa Facebook imesheheni mahubiri ya kanisa lake na sehemu kubwa ikiwa ni video.
Haijulikani ni lini mahubiri hayo yalirekodiwa, lakini kuna marejeleo ya tukio lijalo jijini Nairobi mnamo Januari 2020, ambalo linakinzana na madai ya Mchungaji Mackenzie kuwa alimaliza shughuli zake za kuhubiri mwaka uliotangulia.
'Watoto wanalia kwa sababu wana njaa, waache wafe'
Waumini wa zamani wa kanisa hilo wamedai kuwa walilazimika kufunga kama sehemu ya kufuata mafundisho yake.
Hakuna ushahidi wa moja kwa moja katika video kadhaa ambazo tumeona za Mchungaji Makenzie akiamuru watu moja kwa moja wafunge, lakini kuna ujumbe unaorejelewa mara kwa mara kuwasihi wafuasi kutolea sadaka kile wanachothamini, ikiwa ni pamoja na maisha yao.

Chanzo cha picha, Reuters
"Kuna watu ambao hawataki hata kuhubiri [kuhusu] Yesu. Wanasema watoto wao wanalia kwa sababu wana njaa, waache wafe. Je, kuna tatizo hapo?"
Katika mahojiano na gazeti Kenya la Daily Nation wiki chache zilizopita, Mchungaji Makenzie alikanusha kuwa aliwalazimisha wafuasi wake kufunga.
"Je, kuna nyumba labda au boma au uzio mahali fulani ambao umepatikana [kwenye shamba] ambapo watu wanaweza kuwa wamefungiwa ndani?" alijibu mwandishi alipomuuliza kuhusu hili.

'Elimu ni mbaya'
Mada nyingine ya mahubiri ya Mchungaji Mackenzie imekuwa ni wazo kwamba elimu rasmi ni ya kishetani na hutumiwa kupora pesa.
"Wanajua elimu ni mbaya. Lakini wanaitumia kujinufaisha," anasema katika mojawapo ya mahubiri. "Wale wanaouza sare, wanaoandika vitabu ... wale wanaotengeneza kalamu ... kila aina ya takataka. Wanatumia pesa zako kujitajirisha huku wewe ukiwa maskini."
Mnamo 2017 na tena 2018, alikamatwa kwa kuhimiza watoto wasiende shule kwani alidai elimu "haitambuliki katika Biblia".
Mchungaji Mackenzie pia amelaani elimu kwa kuendeleza mapenzi ya jinsia moja kupitia programu za elimu ya ngono.
"Niliwaambia watu elimu ni mbaya…. Watoto wanafundishwa kuhusu mapenzi ya jinsia moja," aliambia gazeti la Nation.
Madaktari 'humtumikia Mungu tofauti'
Pia amewahimiza akina mama kuepuka kutafuta matibabu wakati wa kujifungua na kutowachanja watoto wao.
Katika mojawapo ya video hizo, mwanamke mmoja anasimulia jinsi alivyosaidia kujifungua mtoto kwa njia ya maombi na bila kuhitaji upasuaji, akiongeza kwamba baadaye alipata “msukumo” kutoka kwa roho mtakatifu ili kumwonya jirani yake dhidi ya kumchanja mtoto wake.
Kisha mchungaji anaunga mkono maoni yake kwamba chanjo si lazima, akidai kwamba madaktari "humtumikia Mungu tofauti".
Pia anawakatisha tamaa wanawake kusuka nywele zao, kuvaa mawigi na kuvalia mapambo.

Alama za Shetani na njama za kimataifa
Mengi ya mahubiri ya Mchungaji Mackenzie yanahusiana na utimizo wa unabii wa Biblia kuhusu Siku ya Hukumu.
Maudhui ya kanisa mtandaoni pia yanaangazia machapisho kuhusu mwisho wa dunia, maangamizi yanayokaribia na hatari zinazodhaniwa kuwa za sayansi.
Na kuna mara kwa mara onyo hutolewa kuhusu nguvu ya kishetani yenye uwezo na ambayo inasemekana imejipenyeza kwenye ngazi za juu zaidi za mamlaka kote duniani.

Chanzo cha picha, FACEBOOK
Anarejelea mara kwa mara "New World Order" - nadharia ya njama kuhusu njama ya wasomi wa kimataifa kuleta serikali ya kimabavu ya ulimwengu, kuchukua nafasi ya mataifa - akidai kwa uwongo Kanisa Katoliki, UN na Amerika ziko nyuma yake.
Pia ana mashaka makubwa na teknolojia ya kisasa, hapo awali akidai mpango wa serikali ya Kenya kutoa nambari ya kipekee ya utambulisho kwa raia kupata huduma za serikali ilikuwa 'alama ya mnyama'.















