Nchi 5 duniani ambazo taasisi zake ziliwahi kudukuliwa mitandaoni

S

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Serikali ya Tanzania kupitia Jeshi la Polisi na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa tahadhari kali kufuatia ongezeko la matukio ya udukuzi na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii.

Hii ni baada ya taarifa potofu kuchapishwa kwenye akaunti zinazodaiwa kuwa za taasisi muhimu za umma kama vile Jeshi la Polisi, kitu ambacho kimeibua taharuki na sintofahamu kwa wananchi.

Taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi zimekanusha kuhusika na taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), na kueleza kuwa watu wasiojulikana waliingia kwenye akaunti yao na kuchapisha ujumbe wa uongo na usio na maadili.

Serikali imethibitisha kuwa akaunti feki zinazofanana majina na zile halali zimeongezeka, na kuwaasa wananchi kuwa waangalifu kabla ya kusambaza taarifa zozote mtandaoni.

Lakini je, hili ni jambo la kipekee kwa Tanzania? Ukweli ni kwamba nchi mbalimbali duniani zimekumbwa na matukio ya aina hii, baadhi yakiwa na athari kubwa zaidi.

Hapa chini ni mifano ya nchi tano kati ya nyingi ambazo taasisi zake ziliwahi kudukuliwa

1. Marekani: SolarWinds hack (2020)

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nembo ya SolarWinds Corp, inaonekana katika makao makuu huko Austin, Texas mnamo Aprili 15, 2021, huko Austin, Texas.

Udukuzi wa mitandao ulioitwa SolarWinds hack ni mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya kimtandao, likihusisha taasisi kadhaa za serikali ya Marekani kama Wizara ya biashara, hazina, na mambo ya Nje.

Wadukuzi walitumia programu ya kampuni ya SolarWinds kuingiza virusi kwenye mifumo ya ndani.

Tukio hili liliathiri pia kampuni binafsi na lilituhumiwa kufanywa na wadukuzi wanaohusishwa na serikali ya Urusi. Marekani ilichukua hatua za kidiplomasia na kiusalama kulinda mifumo yao.

Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya Urusi na kufukuzwa kwa wanadiplomasia 10 kama kisasi kwa kile ambacho Washington inasema ni uingiliaji wa Kremlin katika uchaguzi wa Marekani, shambulio kubwa la mtandaoni na shughuli nyingine za uhasama. Ikulu ya White House ilisema vikwazo hivyo vilevile vinajibu "shughuli za uhalifu wa mtandaoni dhidi ya Marekani na washirika wake," ikirejelea udukuzi huu mkubwa unaojulikana kama SolarWinds wa mifumo ya kompyuta ya serikali ya Marekani mwaka 2020.

2. India - Tovuti za Serikali (2021,2022 na 2023)

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni hivi majuzi tu India imekumbana na udukuzi ambapo tovuti rasmi 59 za wizara na taasisi zake mbalimbali zilidukuliwa.

Taarifa ya Wizara ya Mawasiliano, teknolojia ya habari bungeni, iliyotolewa February 2023 ilieleza kwamba tovuti 50 za serikali zilidukuliwa katika mwaka wa 2022-23.

Akijibu swali la bunge lililoulizwa na Mbunge wa CPI Binoy Viswam, Waziri wa wizara hiyo, Ashwini vaishnaw, alisema kuwa, kulingana na taarifa zilizoripotiwa na kufuatiliwa na Timu ya kukabiliana na uhalifu mitandaoni ya India (CERT-In), jumla ya tovuti 59 za Wizara, 42 za Idara za na 50 za Serikali kuu na Serikali za majimbo zilidukuliwa katika miaka ya 2020, 2021 na 2022.

3. Ujerumani: Udukuzi wa bunge (2015)

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Bunge la Ujerumani (Bundestag) lilidukuliwa, na maelfu ya barua pepe na nyaraka za serikali kuibiwa. Tukio hilo lilihusishwa na kundi la wadukuzi wanaotajwa kuwa na uhusiano na serikali ya Urusi. Tukio hilo lililazimisha uboreshaji wa haraka wa mifumo ya ulinzi mtandaoni wa taifa hilo.

Mpaka leo linabaki kubwa tukio la kukumbukw ala taasisi kubwa kama bunge nchini Ujerumani.

4. Ukraine: Mashambulizi kwa mfumo wa umeme (2015 & 2016)

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukraine ilishambuliwa kwa mara mbili mfululizo kwenye mifumo ya nishati, na kusababisha maelfu ya watu kukosa umeme kwa saa kadhaa.

Disemba 23, 2015, gridi ya umeme katika mikoa miwili ya magharibi mwa Ukraine ilidukuliwa, na kusababisha kukatika kwa umeme kwa takriban watumiaji 230,000 nchini Ukraine kwa saa 1-6.

Shambulio hilo lilitokea wakati wa vita vya wkati huo kati ya Urusi na Ukraine na linahusishwa na kundi la Urusi lenye tishio sugu linalojulikana kama "Sandworm".

Hili lilikuwa mojawapo ya mashambulizi ya kwanza ya kihistoria ambapo udukuzi ulileta madhara ya moja kwa moja kwa huduma muhimu ya umma.

5. Kenya: Mfumo wa huduma za Serikali (2023)

s

Mwaka 2023, Kenya ilishuhudia mashambulizi ya mtandaoni yaliyolenga mifumo ya serikali ikiwemo eCitizen, jukwaa la utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi. Tovuti hiyo ilikwama kwa siku kadhaa, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Serikali ya Kenya ilithibitisha kuwa kulikuwa na shambulio la mtandaoni kwenye mfumo wa eCitizen, unaotumiwa na umma kupata huduma zaidi ya 5,000 za serikali. Huduma hizi ni pamoja na maombi na wa hati ya kusafiria (Pasipoti), utoaji wa visa za kielektroniki kwa wageni wanaotembelea nchi humo , utoaji wa leseni za udereva, vitambulisho na rekodi za kitaifa za afya.

Hata hivyo Serikali ya Kenya ilichukua hatua za haraka za kuimarisha miundombinu ya usalama wa kidigitali.