'Shujaa' aliyepigana na mshambuliaji ufukwe wa Bondi amefahamika kwa jina, Ahmed al Ahmed
"Shujaa" aliyeshuhudia, aliyerekodiwa akinyang'anyana bunduki na mmoja wa washambuliaji wa Bondi Beach ametajwa kuwa Ahmed al Ahmed mwenye umri wa miaka 43.
Video iliyothibitishwa na BBC ilimuonesha Bw. Ahmed akimkimbilia mshambuliaji huyo na kumnyang'anya silaha yake, kabla ya kumgeuzia bunduki, na kulazimisha kujisalimisha.
Bw. Ahmed, mmiliki wa duka la matunda na baba wa watoto wawili, bado yuko hospitalini, ambapo amefanyiwa upasuaji wa majeraha ya risasi kwenye mkono wake, familia yake iliiambia 7News Australia.
Watu kumi na watano walifariki na makumi kadhaa walijeruhiwa katika tukio la ufyatuaji risasi Jumapili usiku, ambao ulifanyika wakati zaidi ya watu 1,000 wakihudhuria tukio la kusherehekea Hanukkah. Polisi wametangaza kuwa ni tukio la kigaidi linalolenga jamii ya Wayahudi.
Binamu yake Bw. Ahmed, Mustafa, aliiambia 7News Australia usiku wa Jumapili: "Yeye ni shujaa, 100% yeye ni shujaa. Ana risasi mbili, moja mkononi mwake."
Katika taarifa mpya mapema Jumatatu, Mustafa alisema: "Natumai atakuwa sawa. Nilimwona jana usiku. Alikuwa sawa lakini tunasubiri kuona daktari (anasema nini)."
Wazazi wake waliliambia Shirika la Utangazaji la Australia kwamba alikuwa amepigwa risasi nne au tano.
"Tunaomba Mungu amuokoe," mama yake alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baba yake aliongeza: "Alipofanya alichofanya, hakuwa akifikiria kuhusu historia ya watu anaowaokoa, watu wanaokufa mitaani.
"Habagui kati ya utaifa mmoja na mwingine. Hasa hapa Australia, hakuna tofauti kati ya raia mmoja na mwingine."
Walisema walikuwa wametenganishwa na mtoto wao wa kiume tangu 2006 alipokuja Australia. Walikuwa wamesafiri hadi Sydney kutoka Syria miezi michache iliyopita.
Polisi wanasema kwamba wapigaji risasi wawili waliohusika walikuwa baba na mwanawe wa miaka 50 na 24.
Walithibitisha kwamba mwanaume huyo wa miaka 50 alifariki papo hapo huku mwanaume huyo wa miaka 24 akiwa hospitalini akiwa katika hali mbaya.
Picha za Bw. Ahmed zimesambazwa sana mtandaoni.
Inamwonesha mmoja wa watu wenye bunduki akiwa amesimama nyuma ya mtende karibu na daraja dogo la watembea kwa miguu, akilenga na kufyatua bunduki yake kuelekea shabaha isiyoonekana.
Bw. Ahmed, ambaye alikuwa amejificha nyuma ya gari lililokuwa limeegeshwa, anaonekana akimrukia mshambuliaji, ambaye anamkabili.
Anafanikiwa kupokonya bunduki kutoka kwa mshambuliaji, anamsukuma chini na kumwelekezea bunduki. Mshambuliaji anaanza kurudi nyuma kwenye daraja.
Kisha Bw. Ahmed anashusha silaha na kuinua mkono mmoja hewani, akionekana kuwaonyesha polisi kwamba hakuwa mmoja wa wapigaji risasi.
Mshambuliaji huyo huyo anaonekana baadaye kwenye daraja akichukua silaha nyingine na kufyatua risasi tena.
Mtu mwingine mwenye bunduki pia anaendelea kufyatua risasi kutoka darajani. Haijulikani ni nani au wanalenga nini.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumapili jioni, Waziri Mkuu wa New South Wales Chris Minns alitoa heshima kwa ushujaa wa Bw. Ahmed, ambaye hakutajwa jina wakati huo.
"Mtu huyo ni shujaa wa kweli, na sina shaka kwamba kuna watu wengi sana walio hai usiku wa leo kutokana na ushujaa wake."
Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese alisema: "Tumewaona Waaustralia leo wakikimbilia hatarini ili kuwasaidia wengine.
"Waaustralia hawa ni mashujaa, na ushujaa wao umeokoa maisha."
Akizungumza katika sherehe ya Krismasi ya Ikulu ya White House, Rais wa Marekani Donald Trump pia alimsifu Bw. Ahmed, akisema alikuwa na "heshima kubwa" kwake.
"amekuwa mtu shujaa sana, kwa kweli, ambaye alienda na kumshambulia mmoja wa wapiga risasi, na kuokoa maisha mengi," alisema.













