'Tulidhani ni mwisho wa dunia': Marekani ilipodondosha mabomu manne ya nyuklia Uhispania 1966

p;

Chanzo cha picha, Alamy

    • Author, Myles Burke
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Tarehe 7 Aprili 1966, karibu miaka 60 iliyopita, bomu la nyuklia lililopotea ambalo jeshi la Marekani ililikuwa ikilitafuta kwa siku 80 hatimaye lilipatikana. Bomu la nyuklia, lenye uwezo mara 100 zaidi ya bomu lililotupwa Hiroshima, lilitolewa kwa uangalifu kutoka kwenye kina cha futi 2,850 (869m) katika Bahari ya Mediterania na kuingizwa kwenye manowari ya USS Petrel.

Mara tu lilipoingizwa, maafisa walikata nyaya na kulitegua. Ndipo kila mtu akapumua – kwani bomu la mwisho kati ya mabomu manne ya hidrojeni ambayo Marekani iliyadondosha kwa bahati mbaya nchini Hispania lilikuwa ndilo hilo limepatikana.

"Hii haikuwa ajali ya kwanza kuhusisha silaha za nyuklia," alisema mwandishi wa BBC, Chris Brasher aliporipoti kutoka eneo la tukio mwaka 1968. "Pentagon inasema kuna angalau ajali tisa ndege kudondosha bomu la nyuklia kwa bahati mbaya. Lakini hii ilikuwa ni ajali ya kwanza nje ya Marekani, na ya kwanza kuhusisha raia na ya kwanza kusisimua hisia za ulimwengu."

Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Marekani ilianzisha mradi wa kumzuia mpinzani wake wa wakati wa Vita Baridi, Muungano wa Kisovieti, kwa kujitayarisha na mashambulizi ya mapema. Doria za ndege za B-52 zenye silaha za nyuklia zilifanyika mara kwa mara. Lakini kufanya doria hizo ndefu, ndege zilihitaji kujaza mafuta zikiwa angani.

Tarehe 17 Januari 1966, ndege moja kama hiyo ilikuwa ikiruka kwa urefu wa futi 31,000 (9.5km) juu ya eneo la Almería, kusini mwa Uhispania, na ilikuwa ikijaza mafuta angani kutoka ndege ya mafuta ya KC-135.

"Naamini kilichotokea ni kwamba ndege ya kivita ilikuwa ikiruka kwa kasi sana, na hivyo haikuwa na utulivu," anasema Meja Jenerali wa Marekani, Delmar Wilson, msimamizi aliyeshughulikia ajali hiyo. Anasema "na matokeo yake, ndege hizo mbili zikakaribiana sana na kugongana."

Madhara ni kuzuka kwa moto, wafanyakazi wanne wa KC-135 waliokuwemo ndani walifariki. Pia Mlipuko uliwaua wanaume wawili katika sehemu ya mkia ya B-52. Na watatu alifanikiwa kujitoa kwa parachuti, lakini alikufa wakati parachuti yake iliposhindwa kufunguka.

Wahudumu wengine wanne wa ndege ya mafuta iliyokuwa ikiungua walifanikiwa kuvuka, kabla ya ndege kuvunjika na kuanguka chini, na kudondosha vipande vya ndege na shehena yake ya hatari ya nyuklia kwenye kijiji cha Uhispania cha Palomares.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Moto ulionekana maili moja. Kwa bahati nzuri, haikusababisha mlipuko wa nyuklia. Katika tukio la ajali, mabomu yalikuwa na miamvuli iliyounganishwa, iliyoundwa ili kuzuia athari wakati wa kutua na kuzuia uchafuzi wa mionzi. Bomu moja ambalo lilitua kwa usalama kwenye mto, lilipatikana siku iliyofuata. Kwa bahati mbaya, miamvuli miwili ya mabomu mengine mawili ilishindwa kufunguka.

Asubuhi hiyo, mkulima Mhispania Pedro Alarcón alikuwa akitembea kuelekea nyumbani kwake na wajukuu zake wakati bomu moja la pili la nyuklia lilipotua kwenye shamba lake la nyanya.

"Watoto walianza kulia. Nilipooza kwa hofu. Jiwe lilinipiga tumboni, nilifikiri nimekufa. Nililala pale nikihisi kama kifo huku watoto wakilia," aliambia BBC mwaka 1968.

Bomu la tatu lilitua kwenye ardhi karibu na makaburi. Kudondoka huku kulizusha shimo, na kutawanya vumbi la plutonium lenye sumu, lenye mionzi katika ekari kadhaa.

Mabaki ya ndege pia yalimwaga katika kijiji cha Uhispania. "Nilikuwa nalia na kukimbia huku na huku," mwanakijiji anayeitwa Señora Flores aliiambia BBC mwaka 1968. "Msichana wangu mdogo alikuwa akilia, 'Mama, Mama, angalia nyumba yetu, inaungua.'

Pia unaweza kusoma

Operesheni kubwa

Mara tu habari juu ya silaha za nyuklia za jeshi la Marekani kuenea, operesheni kubwa ilianzishwa. Wanajeshi wa Marekani walipelekwa hadi kijiji hicho kwa helikopta. Sehemu kubwa ya ndege ya B-52 iliyokuwa ikiungua, ilitua katika ua wa shule.

Licha ya ajali hiyo, hakuna mtu katika kijiji hicho aliyeuawa. Takriban tani 100 za mabaki yanayowaka moto yalianguka kijijini lakini hakuna hata kuku aliyekufa.

Mwalimu na daktari wa shule ya eneo hilo walipanda hadi kwenye mlima wa mabaki ya moto ili kuopoa mabaki ya wanajeshi wa anga wa Marekani waliokuwa wameuawa.

Watatu kati walioruka walifanikiwa kupaa kwa parachuti na kutua katika bahari ya Mediterania, kisha waliokolewa na boti za wavuvi ndani ya saa moja baada ya ajali.

Wa nne, alitoka wakati wa mlipuko wa ndege, na kumwacha akiwa ameungua vibaya, na hakuweza kujiondoa katika kiti chake. Pamoja na hayo, alifanikiwa kufungua parachuti yake na kupatikana akiwa hai karibu na kijiji hicho na kupelekwa hospitali.

Mabomu ya nyuklia

Mabomu matatu ya nyuklia yaliweza kupatikana kwa urahisi. Lakini bado kulikuwa na moja lililopotea. Kufikia siku iliyofuata, lori zilizojaa wanajeshi wa Marekani zimetumwa kutoka kambi za wanajeshi wa anga wa Marekani, wanajeshi 700 na wanasayansi walipambana kuzuia uchafuzi wowote wa mionzi na kutafuta bomu la nne.

Askari wa Marekani walipokuwa wakilitaja eneo kuwa na mionzi, hukwangua nchi tatu za udongo wa juu na kuutia kwenye mapipa ili kusafirishwa kurudi Marekani. Tani 1,400 za udongo wenye miale zilitumwa kwenye kituo cha kuhifadhia mionzi huko Carolina Kusini.

Marekani na Uhispania, ambayo wakati huo ilikuwa chini ya utawala wa kikatili wa udikteta wa kijeshi wa Francisco Franco, ilikuwa na nia ya kuficha athari ya ajali hiyo mbaya.

Franco alikuwa na wasiwasi kwamba hofu ya mionzi ingeumiza sekta ya utalii ya Uhispania, chanzo kikuu cha mapato kwa serikali yake. Katika juhudi za kuwahakikishia wakazi wa eneo hilo na dunia nzima kwamba hakukuwa na hatari yoyote, Balozi wa Marekani nchini Uhispania, Angier Biddle Duke, alikwenda kuogelea katika pwani ya Palomares mbele ya vyombo vya habari vya kimataifa wiki chache tu baada ya ajali hiyo.

Licha ya mamia ya wanajeshi wa Marekani kufanya utafutaji wa kina, katika eneo hilo kwa wiki moja, bado hawakuweza kupata bomu la nne.

Kisha Marekani ilizungumza na mvuvi wa eneo hilo ambaye alikuwa amesaidia kuwaokoa baadhi ya maafisa wa anga waliokuwa na maparachuti baharini. Ndipo walipogungua kuwa mvuvi huo aliona bomu la nyuklia lililopotea.

Msako huo ulihamia haraka kwenye Bahari ya Mediterania, huku Jeshi la Wanamaji la Marekani likitumia meli zaidi ya 30, pamoja na meli za kutegua mabomu na nyambizi, ili kwenda chini ya bahari.

Utafutaji wa maili chini ya bahari ulikuwa mgumu na ulikwenda polepole sana, lakini baada ya wiki za utafutaji, chombo kipya kilichoundwa cha kuzamia, Alvin, hatimaye kililipata bomu lililopotea kwenye mtaro chini ya maji.

Karibu miezi minne baada ya kupotea, hatimaye bomu hilo lilirudi salama mikononi mwa Marekani. Siku iliyofuata, licha ya usiri ambao jeshi la Marekani liliufanya wakati wa utafutaji, ilichukua hatua isiyo ya kawaida ya kuonyesha bomu hilo kwa vyombo vya habari vya ulimwengu.

Balozi Duke alisema watu wasipojionea wenyewe bomu hilo, hawataamini kuwa kweli limepatikana.

Marekani na Hispania zilikubali kufadhili ukaguzi wa afya wa kila mwaka kwa wakazi wa Palomares. Pia waliahidi kufuatilia udongo, maji, hewa na mazao ya ndani.

Lakini hadi sasa bado kuna baadhi ya ekari 100 (hekta 40) za ardhi ambayo ina mionzi huko Palomares, ambayo imesalia kuzungushiwa uzio.

Na licha ya Uhispania na Marekani kutia saini makubaliano ya pamoja mwaka 2015 ya kusafisha eneo hilo, hata hivyo hilo bado halijatekelezwa.