Ukraine iliachana na silaha zake za nyuklia. Lakini sasa inauliza kwanini ilifanya hivyo

Chanzo cha picha, BBC/Kostas Kallergis
Chini ya wingu zito la kijivu na kutanda kwa theluji, mabaki ya kijivu na kijani ya Vita baridi yanakumbusha siku zilizoshuhudiwa hapo nyuma nchini Ukraine.
Makombora, na silaha nzito za kivita vimesalia kama ukumbusho wa enzi ambazo Ukraine ilikuwa na jukumu muhimu katika mpango wa silaha za kinyuklia katika muungano wa Kisoviet.
Hata hivyo makombora hayo ya asili, yana nyufa na kujaa vumbi.
Kwa zaidi ya miaka 30 handaki hilo limejaa vumbi.
Ngome nzima, karibu na jiji la Pervomais’k katikati mwa Ukraine, limegeuka kuwa jumba la makumbusho kwa muda mrefu.
Ukraine mpya ilipoibuka kutoka chini ya kivuli cha Moscow mwanzoni mwa miaka ya 1990, Kyiv ilikataa silaha za nyuklia.
Lakini karibu miaka mitatu baada ya uvamizi kamili wa Urusi, na bila makubaliano ya wazi kati ya washirika kuhusu jinsi ya kudhamini usalama wa Ukraine vita vitakapomalizika, wengi sasa wanahisi hilo lilikuwa kosa.
Takriban miaka 30 iliyopita, mnamo 5 December 1994 katika maadhimisho ya Budapest, Ukraine iliungana na Belarus na Kazakhstan katika kuachana na silaha za kinyuklia kama hatua ya kuhakikisha usalama kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uchina na Urusi.
Kwa msisitizo, makombora yalikuwa ni ya muungano wa Kisoviet si ya jamhuri za zamani.
Lakini theluthi moja ya hifadhi ya nyuklia ya USSR ilikuwa kwenye ardhi ya Ukraine na kukabidhi silaha kulizingatiwa kama wakati muhimu, unaostahili kutambuliwa kimataifa.
"Ahadi juu ya uhakikisho wa usalama ambao [tume]toa mataifa haya matatu...tunasisitiza kujitolea kwetu kwa uhuru, mamlaka na uadilifu wa eneo la mataifa haya," Rais wa Marekani wakati huo Bill Clinton alisema huko Budapest.
Akiwa kijana aliyehitimu katika chuo cha kijeshi huko Kharkiv, Oleksandr Sushchenko aliwasili Pervomais'k miaka miwili baadaye, mchakato wa kumvua uanachama ulipokuwa ukiendelea.
Alitazama jinsi makombora yalivyokuwa yakitolewa na kusafishwa.
Sasa amerejea kama mmoja wa wasimamizi wa jumba la makumbusho.

Chanzo cha picha, BBC/Kostas Kallergis
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akiangalia nyuma baada ya miaka kumi ya taabu iliyosababishwa na Urusi, ambayo jumuiya ya kimataifa imeonekana kushindwa au kutotaka kuzuia, hufikiria hatma isiyoepukika.
Nikishuhudia kinachoendelea Ukraine sasa, mtazamo wangu ni kwamba ilikuwa kosa kubwa kuteketeza kabisa silaha za nyuklia'', anasema
''Hata hivyo ilikuwa ni suala la kisiasa''. Uamuzi ulifanywa na uongozi wa juu na sisi tulitekeleza tu''.
Wakati huo ulionekana kuwa sawa. Hakuna aliyefikiria kwamba Urusi ingeishambulia Ukraine ndani ya miaka 20.
"Hatukufahamu vizuri lakini pia tuliamini," alisema Serhiy Komisarenko, ambaye alikuwa akihudumu kama balozi wa Ukraine huko London mwaka wa 1994.
Wakati Uingereza na Marekani na baadaye Ufaransa ikajiunga ''anasema tulikuwa tunafikiri imetoka, unajua, na Urusi pia.
Kwa nchi masikini kuibuka tu kutoka kwenye miongo ya utawala wa Kisoviet, wazo la kuendeleza mradi ghali wa silaha za nyuklia haukuonekana wa maana sana.
"Kwa nini utumie pesa kutengeneza silaha za nyuklia au kuzihifadhi," Komisarenko asema, "ikiwa unaweza kuzitumia kwa viwanda, kwa maendeleo?"
Lakini maadhimisho ya makubaliano mabaya ya 1994 sasa yanatumiwa na Ukraine kutoa hoja.
Akitokea katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Nato mjini Brussels wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiha alitangaza nyaraka yenye nakala ya Mkataba wa Budapest.
"Hati hii imeshindwa kuhakikishia usalama Ukraine na barani Atlantic," alisema. "Lazima tuepuke kurudia makosa kama haya."

Maghala ya makombora ya nyuklia nchini Ukraine sasa yote yameondolewa.
Taarifa kutoka kwenye wizara yake iliita Mkataba huo "kumbukumbu ya iliyokosa maono ya mbali katika kufanya maamuzi ya kimkakati ya kiusalama".
Swali sasa, kwa Ukraine na washirika wake, ni kutafuta njia nyingine ya kuhakikisha usalama wa nchi.
Kwa Rais Volodymyr Zelensky, jibu limekuwa dhahiri kwa muda mrefu.
"Dhamana bora zaidi ya usalama kwetu ni Nato," alirudia Jumapili.
"Kwetu sisi, Nato na EU hazina mjadala."
Licha ya msisitizo wa mara kwa mara wa Zelensky kwamba kuwa mwanachama wa muungano wa Magharibi pekee ndio kunaweza kuhakikisha kuinusuru Ukraine dhidi ya jirani yake mkubwa, ni wazi wanachama wa Nato wanasalia kugawanyika katika suala hilo.
Pamoja na pingamizi kutoka kwa wanachama kadhaa, muungano huo hadi sasa umesema tu kwamba hatua ya Ukraine ya kupata uanachama hatimaye "haiwezi kutenguliwa", bila kuweka utaratibu.

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati huo huo, mazungumzo yote kati ya washirika wa Ukraine ni "amani kuliko matumizi ya nguvu" ili kuhakikisha kwamba Ukraine iko katika nafasi imara zaidi kabla ya mazungumzo yanayoweza kusimamiwa na Donald Trump, baadae mwaka ujao.
"Kadiri uungwaji mkono wetu wa kijeshi kwa Ukraine ulivyo sasa, ndivyo mkono wao utakavyokuwa na nguvu kwenye meza ya mazungumzo," Katibu Mkuu wa Nato Mark Rutte alisema Jumanne.
Bila uhakika ni mbinu gani Donald Trump ataitumia kwa Ukraine, watoa msaada wa kijeshi wakuu, ikiwa ni pamoja na Marekani na Ujerumani, wanatuma shehena kubwa mpya ya vifaa nchini Ukraine kabla hajaingia madarakani.
Bado haijafahamika ni vipi Donald Trump atashughulikia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine
Wakitazama mbele zaidi, baadhi ya watu nchini Ukraine wanaona kwamba nchi yenye nia ya kujilinda haiwezi kukataa kurejea kwa silaha za nyuklia, hasa wakati mshirika wake muhimu zaidi, Marekani, anaweza kuthibitisha kukosa uhakika katika siku za usoni.
Mwezi uliopita, maafisa walikanusha ripoti kwamba nyaraka inayozunguka katika Wizara ya Ulinzi ilipendekeza kifaa rahisi cha nyuklia kinaweza kutengenezwa katika kipindi cha miezi tu.
Ni wazi haiko kwenye ajenda sasa, lakini Alina Frolova, aliyekuwa naibu waziri wa ulinzi, anasema uvujaji huo unaweza kuwa haukuwa wa bahati mbaya.
"Huo ni uamuzi ambao unajadiliwa nchini Ukraine, miongoni mwa wataalam," anasema.
"Iwapo tutaona kwamba hatuna msaada na tunashindwa vita hivi na tunahitaji kulinda watu wetu ... naamini inaweza kuwa uamuzi wa kuchukua."
Ni vigumu kuona silaha za nyuklia zikirejea hivi karibuni kwenye taka za theluji nje ya Pervomais'k.
Moja tu ya handaki ya silaha yenye kina cha 30m imesalia kuwa sawa, ikihifadhiwa kama ilivyokuwa mnamo 1979.
Ni muundo ulioimarishwa sana, uliojengwa ili kustahimili mashambulizi ya nyuklia, na milango ya chuma nzito na vichuguu vya chini ya ardhi vinavyoiunganisha na sehemu nyingine ya msingi.
Mtaalamu wa zamani wa makombora Oleksandr Sushchenko anaonyesha jinsi wataalamu wawili wangezungusha ufunguo na kubofya kitufe (kijivu, si chekundu), kabla ya kufyatuka mithili ya mtindo wa video za Holywood.
Ni kichekesho kidogo, lakini pia cha kutisha sana.
Kuondoa silaha za ICBM kubwa zaidi, Oleksandr anasema, ilikuwa na maana. Katikati ya miaka ya 1990, Marekani haikuwa adui tena.
Lakini silaha za nyuklia za Ukraine zilijumuisha aina mbalimbali za silaha, zenye masafa kati ya 100 na 1,000km.
"Kama ilivyotokea, adui alikuwa karibu zaidi," Oleksandr anasema.
"Tungeweza kuweka mbinu kadhaa za makombora ya kivita. Hilo lingehakikisha usalama wa nchi yetu."
Imetafsiriwa na Martha Saranga












