Mwanajeshi aliyetoroka vita Urusi afichua siri za kulinda kambi ya silaha za nyuklia

.

Chanzo cha picha, Russian defence ministry

Maelezo ya picha, Kombora la balestiki kwenye kambi ya nyuklia nchini Urusi
Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika siku ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari 2022, Anton anasema kambi ya silaha za nyuklia aliyokuwa akihudumu iliwekwa katika hali ya tahadhari tayari kwa vita.

"Kabla ya hapo, tulikuwa na mazoezi tu. Lakini siku ambayo vita vilianza, silaha zilikuwa zimewekwa tayari ,” alisema afisa huyo wa zamani katika vikosi vya nyuklia vya Urusi. "Tulikuwa tayari kupeleka vikosi baharini na angani na, kutekeleza shambulio la nyuklia."

Nilikutana na Anton katika eneo la siri nje ya Urusi. Ili kumlinda, BBC haitafichua ni wapi. Pia tumebadilisha jina lake na hatutaonyeshi sura yake.

Anton alikuwa afisa katika kituo cha siri kuu ya silaha za nyuklia nchini Urusi.

Ametuonyesha nyaraka zinazothibitisha kitengo chake, cheo na kambi aliyokuwa.

BBC haiwezi kuthibitisha kwa uhuru matukio yote aliyoyaeleza, ingawa yanafanana na taarifa za Kirusi wakati huo.

.
Maelezo ya picha, Afisa huyo wa zamani (kushoto) alizungumza na BBC katika eneo la siri - uso wake umewekewa ukungu ili kuficha utambulisho wake.

Siku tatu baada ya wanajeshi kumiminika kwenye mipaka ya Ukraine, Vladimir Putin alitangaza kwamba vikosi vya kuzuia nyuklia vya Urusi vimeagizwa kuwa katika "hali maalum ya huduma ya mapigano".

Anton anasema kuwa tahadhari ya mapigano iliwekwa siku ya kwanza ya vita na anadai kitengo chake "kilifungiwa ndani ya kambi".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

“Tulichokuwa nacho tu ni TV ya serikali ya Urusi,” alisema afisa huyo wa zamani, “sikujua hatua yote hii ilikuwa ikimaanisha nini. Nilitekeleza majukumu yangu moja kwa moja. Hatukuwa tukipigana vitani, tulikuwa tukilinda silaha za nyuklia.”

Hali ya tahadhari ilighairiwa, anaongeza, baada ya wiki mbili hadi tatu.

Ushahidi wa Anton unatoa ufahamu juu ya utendaji wa siri wa juu wa vikosi vya nyuklia nchini Urusi. Ni nadra sana kwa wanajeshi kuzungumza na waandishi wa habari.

"Kuna mchakato mkali sana wa kuajiri. Kila mtu ni mwanajeshi kitaaluma - hakuna askari," anaelezea.

"Kuna ukaguzi wa mara kwa mara na vipimo vya kugundua uwongo kwa kila mtu. Malipo ni makubwa zaidi, na askari hawapelekwi vitani. Wapo ili kudungua, au kutekeleza, mashambulizi ya nyuklia.

Afisa huyo wa zamani anasema maisha yalidhibitiwa vikali.

"Ilikuwa jukumu langu kuhakikisha wanajeshi walio chini yangu hawatumii simu yoyote kwenye kituo cha nyuklia," anaeleza.

"Ni jamii iliyofungiwa, hakuna wageni huko. Ikiwa ungependa wazazi wako wakutembelee, unahitaji kuwasilisha ombi kwa Huduma ya Usalama ya FSB miezi mitatu kabla.”

.

Chanzo cha picha, Russian Defence Ministry

Anton alikuwa sehemu ya kitengo cha usalama cha kambi hiyo - kikosi cha mwitikio wa haraka ambacho kililinda silaha za nyuklia.

"Tulikuwa na mazoezi ya mara kwa mara. Wakati wetu wa kujibu ulikuwa dakika mbili, "anasema, na ishara ya majivuno.

Urusi ina karibu vichwa 4,380 vya nyuklia vinavyofanya kazi, kulingana na Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani, lakini ni 1,700 tu "ambavyo viko tayari kutumika. Nchi zote wanachama wa Nato kwa pamoja zina idadi sawa.

Pia kuna wasiwasi kuhusu iwapo Putin anaweza kuchagua kupeleka silaha "zisizo za kimkakati", ambazo mara nyingi hujulikana kama silaha za nyuklia. Haya ni makombora madogo ambayo kwa ujumla hayasababishi athari ya mionzi iliyoenea.

Matumizi yao hata hivyo yangesababisha kuongezeka kwa hatari katika vita.

Kremlin imekuwa ikifanya yote iwezayo kujaribu kuzipima nchi za Magharibi.

Wiki iliyopita Putin aliidhinisha mabadiliko ya kanuni za nyuklia - sheria rasmi inayoelekeza jinsi na lini Urusi inaweza kurusha silaha za nyuklia.

Maelezo hayo sasa yanasema Urusi inaweza kurusha makombora hayo chini ya "mashambulizi makubwa" kutoka kwa makombora ya kawaida na nchi isiyo ya nyuklia lakini "kwa ushiriki au msaada wa serikali inayomiliki nyuklia".

Maafisa wa Urusi wanasema maelezo hayo hayazungumzii kikamilifu uwezekano wa kushindwa kwenye uwanja wa vita.

Lakini je, silaha za nyuklia za Urusi zinafanya kazi kikamilifu?

Wataalam wengine wa Magharibi wanasema silaha zake nyingi ni za enzi ya Soviet, na kuna uwezekano hazifanyi kazi.

Afisa huyo wa zamani wa vikosi vya nyuklia alipinga maoni hayo kama "maoni rahisi kuzungumzia kutoka kwa wale wanaoitwa wataalamu".

"Kunaweza kuwa na aina za silaha za kizamani katika baadhi ya maeneo, lakini Urusi ina silaha kubwa za nyuklia, idadi kubwa ya vichwa vya vita, ikiwa ni pamoja na doria ya kivita ya kila mara ardhini, baharini na angani."

Silaha za nyuklia za Urusi zilikuwa zikifanya kazi kikamilifu na ziko tayari kwa vita, alisema. "Kazi ya kudumisha silaha za nyuklia inafanywa kila wakati, haisitishwi hata kwa dakika moja."

Muda mfupi baada ya vita kamili kuanza, Anton alisema alipewa kile anachoeleza kama "amri ya uhalifu" - kufanya mihadhara na askari wake kwa kutumia miongozo maalum iliyoandikwa.

"Walisema kwamba raia wa Ukraine ni wapiganaji na wanapaswa kuangamizwa!" anashangaa. "Huo ni mstari mwekundu kwangu - ni uhalifu wa kivita. Nilisema sitaeneza propaganda hii.”

Maafisa wakuu walimkaripia Anton kwa kumhamisha kwa kikosi cha mashambulizi ya kawaida katika sehemu nyingine ya nchi. Baadaye aliambiwa atapelekwa vitani.

Imetafsiriwa na na kuchapishwa na Seif Abdalla