Kwanini Urusi inazidisha vitisho vya nyuklia kwa Magharibi?

Chanzo cha picha, getty images
Katika wiki za hivi karibuni, Urusi imeongeza malengo yake ya nyuklia na kutoa vitisho zaidi dhidi ya nchi za Magharibi.
Kuongezeka vitisho hivi kunakuja kutokana na mazungumzo kuhusu uwezekano wa kutumwa wanajeshi nchini Ukraine na kuongeza uungaji mkono wa haki ya Kiev ya kutumia silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kufanya mashambulizi ndani ya Urusi.
Hivi karibuni, Vladimir Putin alieleza uwezekano wa kutuma silaha katika nchi tatu zilizo karibu na Magharibi, na kisha akajisifu juu ya uwezo wa nyuklia wa nchi yake.
Maafisa wa Urusi

Chanzo cha picha, REUTERS
Kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi za Magharibi na Urusi, umekuwa wazi katika hotuba za maafisa wakuu wa Urusi.
Juni 11, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Ryabkov, anayesimamia diplomasia ya nyuklia ya nchi hiyo, alieleza uwezekano wa mabadiliko juu ya sababu za Urusi za kutumia silaha za nyuklia.
Maoni ya Ryabkov yalikuja muda mfupi baada ya vitisho vya Vladimir Putin dhidi ya Magharibi katika Kongamano la Kiuchumi la Kimataifa la St. Petersburg
Wakati wa kikao cha mashauriano cha Juni 7, Sergey Karaganov, mtaalamu wa siasa, anayejulikana kwa kutetea mashambulizi ya nyuklia ya mapema dhidi ya Magharibi, alimuuliza Putin mara kwa mara juu ya uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia katika mzozo na Ukraine.
Putin alijibu Urusi haihitaji silaha za nyuklia ili kuhakikisha ushindi dhidi ya Ukraine, lakini alisema zinaweza kutumika "katika kesi maalumu, pale uhuru wa nchi na mipaka vitakapokuwa hatarini."
Maoni ya Putin ya nyuklia yalifuatia vitisho vyake vya kutumia silaha za masafa marefu za Urusi dhidi ya maeneo nyeti ya Magharibi, kufuatia ripoti kwamba washirika wa NATO wanafikiria kuiruhusu Ukraine kutumia silaha zao kushambulia ndani ya Urusi.
Ujumbe huo wa nyuklia pia uliambatana na mazoezi yanayoendelea ya vikosi vya nyuklia vya Urusi, ambayo Putin alikuwa ameyatangaza mapema Mei.
Wanapropaganda wa Urusi wanasema nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wanapropaganda wa Urusi pia wamezidisha vitisho vyao dhidi ya nchi za Magharibi.
Mwishoni mwa mwezi Aprili, Dmitri Kiselyov, mtangazaji mashuhuri wa chaneli inayoendeshwa na serikali ya "Russia 1," alieleza uwezekano wa kutumika silaha za nyuklia dhidi ya Magharibi ikiwa vikosi vya NATO vitaingia Ukraine.
Mtangazaji wa kipindi cha runinga, Vladimir Solovyov alisema "kuongezeka kwa mzozo, kunaweza kusababisha mashambulizi dhidi ya Magharibi.’
Wageni wa kipindi cha mazungumzo ya kisiasa kwenye televisheni ya serikali ya Urusi, pia wametoa wito wa matumizi ya silaha za nyuklia.
Kwa mfano, mbunge wa Urusi Andrei Goroliev alipendekeza shambulio la nyuklia dhidi ya Uholanzi, lango kuu la haidrokaboni ya Ulaya, kwa lengo la kulifanya bara hilo lipige magoti.
Mikhail Kovalchuk, mshirika wa karibu wa Putin na mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Kurchatov, pia aliibua vitisho vingine vya nyuklia, akitangaza katika mahojiano, ‘Urusi pekee ndio ina uwezo wa kuigeuza Marekani kuwa rundo la majivu ya mionzi."
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mtangazaji wa televisheni Dmitry Suslov, alizitaka mamlaka za Urusi kufikiria kufanya majaribio ya mlipuko wa nyuklia kama njia ya kuzuia kuongezeka kwa mzozo nchini Ukraine.
Katika makala ya Aprili 29, aliandika: "Athari za kisaikolojia na kisiasa za majaribio ya nyuklia, yakitangazwa moja kwa moja kwenye kila mtandao wa televisheni ulimwenguni, yanaweza kuwarudisha wanasiasa wa Magharibi kwenye kile kilichozuia vita kati ya mataifa yenye nguvu baada ya 1945. Lakini kwa sasa wengi wamepoteza hofu juu ya vita vya nyuklia."
Wachambuzi wanasemaje?

Chanzo cha picha, Adalberto Roque / AFP
Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanasema mzozo wa nyuklia haujakaribia, lakini wanatambua wasiwasi wa Moscow kuhusu mipango mipya ya Magharibi ya kuiunga mkono Ukraine.
Mchambuzi wa masuala ya ulinzi Valery Shiryav anasema, kupeleka makombora zaidi ya nchi za Magharibi kwenda Ukraine na kuondoa vikwazo vyovyote vya matumizi yake, "makombora hayo yanaweza kuharibu maeneo kadhaa ya kimkakati ya kijeshi na kiviwanda katika mikoa ya Belgorod, Bryansk, Kursk na Rostov nchini Urusi.’’
Anasema Urusi inaweza kulipiza kisasi kwa kulenga madaraja na vifaa vya mawasiliano vya Ukraine, na kushambulia maeneo katika Mashariki ya Kati ili kudhoofisha masilahi ya NATO.
Vasily Kashin, mchambuzi wa masuala ya kijeshi anayeunga mkono Kremlin, alisema teknolojia ya kisasa itaruhusu nchi za NATO kutoa maelekezo ya mashambulizi ya Ukraine ili "kuua wanajeshi wa Urusi."
Anaendelea kusema, kuondoa vikwazo vyovyote vya matumizi ya silaha za masafa marefu kwa Ukraine kutaifanya Urusi kufanya mashambulizi kwenye vituo vya NATO".
Anasema, mashambulizi ya Urusi dhidi ya ndege za upelelezi za Magharibi kwenye Bahari Nyeusi au dhidi ya satelaiti za Magharibi, yanaweza kuwa jibu ikiwa washirika wa NATO wataondoa vikwazo vya matumizi ya silaha za Ukraine."
Kuhusu chaguo la mwisho la matumizi ya silaha za nyuklia ya Urusi dhidi ya Ukraine au nchi za Magharibi - Shiryav anatilia shaka ufanisi wa hatua hiyo.
Katika safu yake ya gazeti la Novaya Gazeta, Shiryav ansema, mstari wa mbele wa vita vya Urusi na Ukraine ni mpana sana, hivyo shambulio moja au kadhaa ya nyuklia hayataisaidia Moscow kushinda vita hivyo.
"Leo hii, dunia iko kwenye ngazi ya kwanza ya tishio la nyuklia," anaonya Shiryav "ni muhimu kukumbuka [Nikita] Khrushchev na [John F.] Kennedy walikuwa na hekima ya kushuka ngazi hii."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na Kuhaririwa na Seif Abdalla












