Kwanini silaha mpya ya nyuklia ya anga za juu ya Urusi inaitia wasiwasi Marekani?

ds

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Marekani imesema ina wasiwasi kuwa Urusi imetengeneza silaha mpya inayoweza kushambulia satelaiti.

Lakini Urusi imekanusha madai hayo ya Marekani, ikisema ni njama ya kutoa shutuma ili kulilazimisha Bunge la Marekani kutoa fedha za ziada kwa ajili ya Ukraine.

Katika mitandao ya habari ya New York Times, ABC na CBS - ripoti zilisema tishio hilo lilitokana na silaha za nyuklia zilizotengenezwa na Urusi. Kuna hofu kuwa zinaweza kutumika kushambulia satelaiti za Marekani angani.

Akizungumza na waaandishi wa habari hivi karibuni kuhusu silaha hii, msemaji wa usalama wa taifa katika Ikulu ya Marekani John Kirby, alisema hakuna tishio la moja kwa moja kwa watu wa Marekani.

John Kirby, amesema Rais Joe Biden amefahamishwa kuhusu suala hilo, alisema utawala wa Biden umelichukulia suala hilo 'kwa uzito mkubwa'.

Kadhalika alisema, Rais Biden ameamuru mawasiliano ya moja kwa moja ya kidiplomasia na Urusi juu ya suala hili.

John Kirby aliwaambia wanahabari hakuna ushahidi kwamba silaha hiyo imetumiwa.

Mbali na maoni ya John Kirby, maafisa wa serikali ya Marekani bado hawajatoa taarifa zozote kuhusu tishio hilo.

Mshauri wa Usalama wa Taifa, Jake Sullivan amedokeza kuwa serikali ya Marekani imekuwa kimya kwa makusudi.

Pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba mashirika ya kijasusi ya Marekani yatafanya kazi kukusanya taarifa kuhusu tishio hilo.

Kwa nini Marekani ina wasiwasi?

wds

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wataalamu na maafisa wa zamani wa serikali wameonya kuwa tishio lolote kwa satelaiti za Marekani litakuwa na madhara makubwa. Jeshi la Marekani linategemea sana mawasiliano ya satelaiti.

Marekani hutumia satelaiti kwa kila kitu kuanzia uchunguzi, utambuzi wa maeneo ya kurusha makombora, mashambulizi ya angani na baharini hadi mabomu yanayoongozwa na GPS na mawasiliano katika uwanja wa vita.

Afisa wa zamani wa ngazi ya juu wa ujasusi katika idara ya Marekani, Gary Bingken akizungumzia hilo alisema, ''jinsi jeshi letu linavyopigana leo na silaha tunazowekeza zinategemea uwezo wetu wa anga, bila hivyo tungekuwa katika hali ngumu."

Mbali na mahitaji ya kijeshi, satelaiti pia hutumiwa katika maeneo mengi kama vile huduma ya usafiri ya GPS, huduma za upelekaji bidhaa na taarifa za hali ya hewa. Inahitajika katika kila kitu - kilimo hadi miamala ya mtandaoni ya kifedha.

"Satelaiti ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Wamarekani na watu duniani kote wanaitegemea," alisema Gary Bingken.

Kwa miaka mingi, maafisa wa Marekani na wataalamu wa anga wamekuwa wakidai kuwa Urusi na China zimekuwa zikipanua uwezo wao wa kijeshi angani ili kushindana na Marekani.

Marekani, Urusi na China tayari wana uwezo wa kushambulia satelaiti duniani kote.

Hata hivyo, nchi hizo tatu zimetia saini Mkataba wa Anga za Juu wa 1967, ambao unakataza kutuma kitu chochote cha silaha kwenye mzunguko wa Dunia.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah