Saa ya Siku za Mwisho za dunia iko sekunde 90 kabla ya janga

- Author, Jane Corbin
- Nafasi, BBC
Saa ya Siku ya Mwisho - ni saa ya ishara ambayo inaonyesha jinsi dunia ilivyo karibu kuharibiwa na silaha za nyuklia. Mwaka 2024 saa hiyo itasalia kwenye sekunde 90 kufikia uharibifu wa dunia kutokana na shughuli za kibinaadamu.
Wanasayansi wameorodhesha sababu za kuiweka karibu zaidi kuwahi kuwa na siku ya mwisho. Wakieleza ushindani katika uundaji wa silaha mpya za nyuklia, vita vya Ukraine na wasiwasi wa mabadiliko ya tabia nchi, yote yametajwa kama sababu.
Saa hiyo husetiwa kila mwaka na wanachama wa Bulletin of the Atomic Scientists.
Sababu za kuwekwa sekunde 90

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu 2007, wanachama wamekuwa na wasiwasi juu ya hatari zinazosababishwa na ujenzi hatari wa akili mnembe (AI), mabadiliko ya tabianchi pamoja na tishio kubwa zaidi la vita vya nyuklia. Katika tangazo lao la 2024 siku ya Jumanne, gazeti la Bulletin lilisema China, Urusi na Marekani zote zinatumia kiasi kikubwa cha fedha "kupanua au kuboresha silaha zao za nyuklia" - jambo ambalo linaongeza hatari ya vita vya nyuklia kuzuka kimakosa au mahesabu mabovu." "Vita vya Ukraine vimeongeza hatari ya kulipuka vita vya nuklia," wanasema. Ukosefu wa hatua za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na hatari zinazohusiana na "kutumia vibaya" teknolojia zinazoibuka za kibaolojia na zana za akili bandi (AI) pia zimetajwa.
Historia ya saa ya siku ya mwisho

Saa ya Siku ya Mwisho iliundwa mwaka 1947 na J Robert Oppenheimer na wanasayansi wenzake wa Marekani ambao walitengeneza bomu la atomiki. Waliona matokeo mabaya ya bomu hilo miaka miwili baadaye, wakati wa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, kwenye majiji ya Japani ya Hiroshima na Nagasaki. Walitaka kuuonya umma na kuweka shinikizo kwa viongozi wa ulimwengu kuhakikisha kuwa silaha za nyuklia hazitumiwi tena. Ujiti wa saa hiyo umebadilishwa mara 25. Mwaka 1947, walianza kwa kuiweka dakika saba kufikia uharibifu. Mwishoni mwa Vita Baridi, katika 1991, ilirudishwa nyuma hadi dakika 17 kufikia uharibifu wa dunia. Rais wa Bulletin Rachel Bronson aliiambia BBC "kila nchi kubwa, ikiwa ni pamoja na Uingereza, zinawekeza katika silaha zao za nyuklia. Huu ni wakati hatari sana na viongozi hawawajibiki." Pavel Podvig, mtaalamu wa silaha za nyuklia wa Urusi ambaye amekuwa akihusika katika kuweka saa ya hiyo kwa miaka mingi, anasema alishtuka Rais Putin alipoweka vikosi vya nyuklia vya Urusi katika hali ya tahadhari baada ya uvamizi wa Ukraine. "Rais wa Urusi aliamini kutoa matamshi ya nuklia kungeweza kuzuia Magharibi kuingilia Ukraine hesabu ambazo zilikuwa sahihi."
Nchi zenye nyuklia

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya miongo kadhaa ya makubaliano ya udhibiti wa silaha bado kuna takriban vichwa 13,000 vya nyuklia ulimwenguni, 90% ni vya Urusi na Marekani. Nchi nyingine sita zimetangazwa kuwa na nguvu za nyuklia: Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan na Korea Kaskazini. Israel inaaminika kuwa na silaha hizi, lakini haijawahi kuthibitisha. Silaha nyingi za kisasa za nyuklia zina nguvu mara nyingi zaidi kuliko zile zilizoharibu Hiroshima na Nagasaki. Mnamo 2021, Uingereza iliongeza vichwa kutoka 225 hadi 260, na kuna uwezekano wa vichwa 35 kuongezwa. Tangu vita vya Ukraine vilipoanza, kumekuwa na minong'ono kutoka kwa wakuu wa Urusi wakipendekeza silaha za nyuklia za Moscow zinaweza kutumika dhidi ya Uingereza. Silaha za nyuklia za Uingereza ziko magharibi mwa Scotland kwenye kambi ya Faslane, kuna nyambizi nne za Vanguard ambazo hubeba makombora ya Trident yenye vichwa vya nyuklia.
Upinzani dhidi ya nyuklia

Tangu bomu la atomiki lilipoundwa kumekuwa na upinzani dhidi ya silaha hizi. Katika miaka ya 1980, wanawake wa kambi ya amani ya Greenham Common walipigana ili makombora yote ya nyuklia ya Marekani yaondolewe katika ardhi ya Uingereza - makombora ya mwisho yaliondoshwa 2008. Wanaharakati wa RAF Lakenheath huko Suffolk, wanaoendesha Kampeni ya Kupunguza Silaha za Nyuklia (CND) wanapinga uwezekano wa silaha za Marekani kurejea Uingereza. Nyaraka za Pentagon - zilizoripotiwa na Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani - zinaonyesha silaha "maalumu" za Marekani zitawekwa kwenye kambi ya ndege za kivita za Marekani na tayari ndege hizo zenye uwezo wa kubeba silaha kama hizo ziliwasili UK mwaka 2021 na sasa kuna mipango ya Jeshi la Anga la la Marekani kujenga kambi kwa wanajeshi wenye uwezo wa kuhudumu katika misheni za nyuklia. Katika muongo mmoja uliopita, hofu ya kutokea vita vya nyuklia imeongezwa na Kim Jong-Un, kiongozi wa Korea Kaskazini, taifa la karibuni zaidi kujiunga na klabu hiyo ya nyuklia. Amejigamba kwa kufanya majaribio ya makombora yenye uwezo wa nyuklia ambayo yanaweza kufika Marekani. Mwanachama wa zamani wa Bulletin of Atomic Scientists na mshauri wa Saa ya Siku ya Mwisho, Sig Hecker, ametembelea vituo vya nyuklia vya Korea Kaskazini mara saba kama sehemu ya mpango wa utafiti wa kisayansi na anakadiria kuwa inaweza kuwa na vichwa vya nyuklia 50 hadi 60 kufikia sasa. "Silaha za nyuklia, ugaidi wa nyuklia, kuenea kwa nyuklia - yote yanakwenda katika mwelekeo mbaya," anasema.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












