Jinsi mitambo ya kufuatilia silaha za nyuklia ilivyogundua nyangumi wa buluu

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa miaka mingi viumbe viliogelea baharini bila kukutana na mwanadamu yeyote. Baadhi yao walikua na urefu wa mita 24 (futi 80) na uzani wa tani 90. Kwa miaka mingi hatukujua uwepo wa viumbe hao hadi hivi karibuni - nyangumi wa buluu katika Bahari ya Hindi.
Ugunduzi wao 2021 ulikuwa wa kushangaza kwa jinsi walivyogundulika. Tusingeweza kukutana nao kama si silaha za nyuklia. Mabomu ya atomiki yana uhusiano gani na aina hii ya nyangumi?
Jibu liko katika mtandao wa kimataifa wa utambuzi, uliowekwa katika baadhi ya maeneo ya mbali zaidi ya dunia. Tangu miaka ya 1990, waendeshaji wa mitambo hiyo katika chumba cha udhibiti huko Vienna, Austria wamekuwa wakifuatilia majaribio ya silaha za nyuklia.
Kadiri miaka inavyosonga, mtandao wao pia umepokea sauti na minong'ono mingi kutoka baharini, ardhini na angani – matokeo hayo yameleta manufaa ya kushangaza kwa sayansi.
Hadithi ya jinsi kundi la nyangumi wa bluu walivyopatikana inaanza miaka ya 1940, wakati wanadamu walipogundua wanaweza kutengeneza mabomu ya nyuklia.
Baada ya jaribio la kwanza la nyuklia la Marekani na kulipuliwa kwa Japan, miongo kadhaa ya kukosekana kwa utulivu na hofu ilifuata, huku mataifa yakishindana kujaza ghala zao kwa silaha na kujaribu silaha zenye nguvu zaidi.
Baada ya miaka 50, serikali nyingi zilikubali kwamba uwazi ulihitajika. Ili kuepuka ongezeko la nyuklia, ulimwengu ulihitaji njia ya kujua ikiwa taifa fulani linafanya majaribio ambayo hayajaidhinishwa. Hapo ndipo wangeweza kuaminiana.
Katika miaka ya 1990, mataifa kadhaa yalitia saini na kuridhia Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia (CTBT), ikijumuisha Uingereza na mataifa mengi yenye nguvu za nyuklia ya Ulaya Magharibi.
Mataifa machche hayakufanya hivyo, ikiwa ni pamoja na China, India na Marekani. Hilo lilifanya mkataba huo uliounda kanuni za kimataifa dhidi ya majaribio ya nyuklia ushindwe kufanya kazi, ingawa ulikuwa chanzo cha harakati za kupinga nyuklia ulimwenguni.
Na muhimu zaidi, ulisababisha kuanzishwa kwa mtandao wenye uwezo wa kusikia, kunusa au kuhisi mlipuko wa nyuklia mahali popote Duniani.
Mfumo huo unafanyaje kazi?

Chanzo cha picha, CTBTO
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mfumo wa Kimataifa wa Ufuatiliaji - unaoendeshwa na Shirika la CTBT huko Vienna - umekuwa ukifanya kazi tangu wakati huo, umepanuka na kuwa na zaidi ya vituo 300 ulimwenguni kote ambavyo vinaweza kugundua sauti, mawimbi na mionzi za milipuko wa nyuklia.
Vituo hivyo vinapatikana katika sehemu tulivu, zisizo na pishapisha. Marekani, kwa mfano, inaendesha kituo kwenye kisiwa cha Wake huko Pasifiki, mojawapo ya visiwa vilivyojitenga zaidi duniani.
Vingine vinapatikana katika bara la Antarctica. Vituo vichache viko karibu na makazi ya watu, kama kituo cha kufuatilia tetemeko kilichopo katika kijiji cha Lajitas huko Texas – kilomita 650 (maili 400) magharibi mwa San Antonio - au kituo cha kufuatilia mionzi huko Sacramento, California.
‘’Hii ina maanisha kama kuna mlipuko wa nyuklia mahali fulani duniani, wafuatiliaji waliopo katika chumba cha udhibiti huko Vienna watajua,’’ anasema Xyoli Perez Campos, mkurugenzi wa CTBTO nchini Austria.
"Iwapo kuna jaribio la nyuklia la chini ya ardhi, basi tuna teknolojia ya kugundua tetemeko. Ikiwa majaribio ya nyuklia yatafanyika chini ya maji, basi tuna vifaa huko. Ikiwa majaribio yatafanyika katika anga, tunao vituo vya mawimbi ya sauti."
Wakati Korea Kaskazini ilipofanya majaribio ya silaha za nyuklia katika miaka ya 2000 na 2010, mitambo hiyo ilichukua mawimbi kutoka katika milipuko, na mtambo wa utambuzi wa mionzi wa angani ulithibitisha hilo.
Vituo hivyo pia hunasa milipuko mikubwa isiyo ya nyuklia, kama vile mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut 2020 au mlipuko wa volkeno ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai Januari 2022.
Sauti za Nyangumi

Chanzo cha picha, CTBTO
Hata hivyo, siku za hivi karibuni mtandao wa nyuklia wa IMS umefichua mengi zaidi ya milipuko mikubwa. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ufuatiliaji umezidi kutanuliwa. Na kupelekea kugundulika kwa sauti za makundi ya nyangumi.
Mwezi Juni, mamia ya wanasayansi walikutana katika mkutano huko Vienna. Watafiti kutoka Ujerumani walionyesha vituo vya baharini vinavyonasa sauti za meli. Timu kutoka Japan iliwasilisha matokeo kuhusu jinsi walivyotumia IMS kuchunguza shughuli za volkeno ya chini ya bahari.
Watafiti wa Brazili walizungumza kuhusu vituo vinavyofuatilia mawimbi ya sauti angani. Wengine walielezea ugunduzi wa sauti za kuanguka kwa milima ya barafu katika bara la Antaktika.
Mwanafizikia Elizabeth Silber wa Maabara ya Sandia, New Mexico alionyesha jinsi vituo vya IMS vilivyonasa sauti ya moto wa ardhini uliowaka Septemba 22, 2020.
Kuhusu nyangumi wa buluu - waligunduliwa wakati watafiti nchini Australia walipoamua kusikiliza kwa ukaribu sauti za baharini kwa kutumia mtandao wa kwenye maji wa IMS.
Mwaka 2021, mtaalam wa sauti Emmanuelle Leroy kutoka Chuo Kikuu cha New South Wales, huko Sydney, na wenzake walichambua sauti za nyangumi mbalimbali katikati mwa bahari ya Hindi.
Miaka michache kabla, sauti mpya iligunduliwa, inajuliikana kama "sauti ya Chagos," au "Diego Garcia Downsweep," ilipewa jina la mahali ilipotambuliwa; kisiwa cha Diego Garcia katika visiwa vya Chagos.
Wakati huo, makundi matano ya nyangumi wa buluu yaligundulika katika Bahari ya Hindi, pamoja na nyangumi wa jamii ya Omura. Lakini haikujulikana sauti ya Chagos ilikuwa ni kutoka kundi gani. Wanasayansi wanajua kwamba kila jamii ya nyangumi ina sauti yake na zinatambulika lakini sauti hii haikulingana na jamii yoyote ya nyangumi.
Leroy na wenzake waligundua kuwa mtandao wa IMS ungewaruhusu kufuatilia sauti ya Chagos kwa karibu miongo miwili, katika maeneo mbalimbali ya bahari, kuanzia Sri Lanka hadi Australia Magharibi. Uchambuzi wao ulihitimisha kuwa sauti ya Chagos ni kundi jipya kabisa la nyangumi wa buluu.
Kupata aina mpya ya kundi la nyangumi ilikuwa ni habari njema - kwa sababu nyangumi wa buluu ni nadra sana. Katika Karne ya 20, nyangumi hao waliwindwa karibu kutoweka, kutoka wastani wa nyangumi 239,000 katika miaka ya 1920 hadi chini ya nyangumi 360 mwaka wa 1973 .
"Kinachonishangaza sana ni kwamba hawa watu werevu waliamua kuwa majaribio ya nyuklia ni hatari kwa wanadamu, na sio tu kwamba waliandika mkataba wa kusema tuachane nayo, lakini walikuja na teknolojia ya kufuatilia. Hiyo ni kuiweka sayansi na teknolojia katika matumizi mazuri kwa binadamu," Perez Campos anasema.












