Watafiti wa Marekani wagundua maeneo ya Urusi ya kurushia kombora la Burevestnik

Chanzo cha picha, Kremlin.ru
Watafiti wawili wa Marekani wanadai kuwa Urusi inajiandaa kutumia kombora la masafa linalotumia nguvu ya nyukilia la 9M370 Burevestnik, ambalo Vladimir Putin alilizungumzia katika hotuba yake kwa bunge mwezi Machi 2018. BBC inaripoti kile tunachokijua kuhusu taarifa hii.
Ripoti ya Reuters, pamoja na tweet kutoka kwa mchambuzi wa utafiti wa CNA Dekker Evelet, zilisema kuwa kwa ushirikiano na Hans Christensen kutoka Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani , waligundua mabadiliko katika picha za satelaiti za kituo kilichopo katika eneo la Sheksninsky huko Vologda ambayo yanaonyesha kusafirishwa kwa makombora hayo.
Kituo hiki kinajulikana kama kitengo cha kijeshi 25594, au hifadhi ya silaha ya Kurugenzi Kuu ya 12 ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi, ambayo inasambaza silaha kwa Vikosi vya nyuklia vya kimkakati. Karibu na eneo hilo kuna mji wa Vologda-20, ambapo kitengo, kambi, na vifaa vyake vipo.
Kituo chenyewe kina maeneo matano na miundo ambayo watafiti huiita vifaa vya kuhifadhia ya kichwa cha nyuklia. Vifaa hivi ambavyo vimekuwepo mahali hapo kwa muda mrefu - vilionekana kwenye picha za satelaiti za Google Earth tangu mwaka 2003.
Watafiti wameona mabadiliko katika eneo hili kwenye picha mpya za satelaiti - lenye ujenzi na maeneo tisa tofauti. Wachambuzi wa picha hizi wameona kitu ambacho wamekitaja kama kifaa kinachoundwa kwa ajili ya ufyatuzi wa makombora.
Kimegawanyika katika makundi matatu.
Kwa mujibu wa chapisho la Reuters, eneo la ufyatuaji wa makombora lipo karibu na maeneo ya kuhifadhi kichwa cha nyuklia.
Kwa mujibu wa Evelet, maeneo haya " yanakusudiwa kutumiwa kwa ajili ya mfumo mkubwa wa makombora, na mfumo pekee mkubwa wa makombora ambao Urusi inauandaa ni Skyfall." SSC-X-9 Skyfall jina uliopewa mradi wa Burevestnik na NATO.

Chanzo cha picha, Reuters
Maeneo haya yanaonekana wazi katika picha za satelaiti zilizochukuliwa mnamo Septemba 3, 2024.
Pia yanaonekana katika picha zilizochukuliwa mapema 2024. Hawakuwepo huko mnamo Agosti 2021, lakini tayari kulikuwa na eneo la ujenzi katika eneo hili.
Hata hivyo, maeneo haya hayaonekani katika picha iliyochukuliwa mnamo Septemba 25, 2020.
Taarifa kuhusu hali ya programu ya Burevestnik ni ya siri mno. Jaribio la mwisho liliripotiwa hadharani kabla ya Oktoba 5, 2023, wakati Putin alipotangaza kuwa Urusi imefanikiwa kuifanyia majaribio silaha ya Burevestnik.
Hata hivyo, maelezo ya vipimo hivi hayajulikani, na hali halisi ya programu ni vigumu kuitambua.
Silaha ya Putin
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sehemu kubwa ya hotuba ya Putin bungeni Machi 1, 2018, ilijikita katika maendeleo mapya katika uwanja wa silaha.
Kombora la nyuklia la Burevestnik, pamoja na torpedo Poseidon, yalionekana kuwa aina ya ajabu zaidi ya silaha wakati huo kwasababu ya injini zake za nyuklia.
Burevestnik ilikuwa ya kuvutia zaidi kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kupiga masafa marefu zaidi.
Mkakati na uwezo wake wa kiufundi ni wa kuvutia. Kombora hili lina uwezo wa kushambulia kwenye maeneo ya masafa marefu zaidi.
Putin alisema katika hotuba yake kwamba "mtambo mdogo wa nyuklia wenye nguvu kubwa" ambao umewekwa katika kombora la hilo huliwezesha " kupaa kwa kiwango cha juu ambacho hakina ukomo."
Inaaminika kuwa linatumia injini ya ramjet, ambapo mtiririko wa hewa utachemshwa na nishati ya kinu kidogo cha nyuklia, na kupelekea kombora hilo kufyatuka kwa msukumo wa kasi kubwa.
Sio lazima kuwa na kichwa cha nyuklia. Faida yake kuu ni uwezo wake wa kusafiri masafa marefu sana, na kutokana na hilo itakuwa na uwezo wa kuvuka njia, na maeneo ya ulinzi wa anga.
Urusi imekuwa ikiendeleza mradi huu kwa muda mrefu, na inawezekana kwamba teknolojia iliyokuwepo kuanzia nyakati za Muungano wa Usovieti ilitumika kama msingi wake.

Chanzo cha picha, Planet Lab

Chanzo cha picha, Planet Lab
Ajali katika Nenoksa
Hata hivyo, wakati wa majaribio ilibainika wazi kwamba kutengeneza silaha kama hiyo sio rahisi sana.
Mnamo Agosti 2019, ajali ilitokea kwenye eneo la majaribio karibu na Severodvinsk.
Mwanzoni, jeshi la Urusi liliripoti kuwa mfumo wa kusukuma maji ulikuwa umelipuka.
Baadaye, shirika la serikali Rosatom lilikiri kuwa mlipuko karibu na Severodvinsk ulitokea wakati wa majaribio ya roketi na kipengele cha radioisotope kwenye injini.
Matokeo yake, wafanyakazi watano wa Rosatom walifariki, na wengine watatu walipata majeraha na kuungua kwa viwango tofauti.
Hakuna mtu aliyeweza kuthibitisha idadi ya waathirika - vipimo na ajali hiyo viliainishwa kwa makini.
Wakati huo huo, kulingana na Idhaa ya Kirusi ya BBC, waathirika ambao walipokea kiwango kikubwa cha mionzi wakati wa ajali walipelekwa katika hospitali ya kiraia huko Arkhangelsk bila kuwaonya madaktari kuhusu hatari ya sumu ya mionzi.
Baadaye, ilibidi ufanyike kile kilichoitwa "mchakato" [usafishaji wa mionzi] katika sehemu ya hospitali na kwenye magari.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Abdallah Dzungu












