Wapiganaji wanaoondoka katika vita Syria na kuwa mamluki Afrika

Kwa zaidi ya miaka 10, Abu Mohammad amekuwa akiishi katika hema na familia yake kaskazini mwa Syria, iliyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu.
Hapati pesa za kutosha kuisadia familia yake. Kama ilivyo kwa mamia ya wapiganaji wengine, naye ameamua kusafiri kupitia Uturuki kwenda Niger kufanya kazi kama mamluki.
Abu Mohammad (sio jina lake halisi), ana umri wa miaka 33. Yeye na mkewe wana watoto wadogo wanne - hawana maji ya bomba wala choo chao wenyewe na wanategemea paneli ndogo ya jua kuchaji simu zao.
Hema lao huwa na joto kali wakati wa kiangazi na hupata baridi kali wakati wa baridi, na huvuja mvua inaponyesha.
"Kupata kazi imekuwa ngumu sana," anasema. Ni mwanachama wa vikosi vya upinzani vinavyoungwa mkono na Uturuki ambavyo vimekuwa vikipambana na Rais Bashar al-Assad kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kikundi anachofanyia kazi kinamlipa chini ya dola za kimarekani 50 kwa mwezi. Hivyo mawakala wa Kituruki walipojitokeza kutoa dola 1,500 kwa mwezi kufanya kazi nchini Niger, aliamua hiyo ndiyo njia bora ya kupata pesa zaidi.
Baada ya kodi kwa kikundi na mawakala, bado atasalia na angalau theluthi mbili ya pesa hiyo. "Na kama nitakufa katika vita [nchini Niger], familia yangu itapokea fidia ya dola 50,000," anaongeza.
Ghasia katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi zimezidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mzozo kati ya makundi ya kijihadi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Niger na majirani zake Mali na Burkina Faso zote zimeathirika - na nchi zote tatu zimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi katika miaka michache iliyopita, ikiwa ni matokeo ya kukosekana kwa utulivu.
Ali (si jina lake halisi), anayeishi katika hema katika kijiji huko Idlib, alijiunga na vikosi vya upinzani vya Syria miaka 10 iliyopita alipokuwa na umri wa miaka 15.
Anasema analipwa chini ya dola 50 kwa mwezi, ambayo hudumu kwa siku tano. Amelazimika kukopa ili kutunza familia yake na anaona Niger ndio njia pekee ya kulipa madeni yake. "Nataka kuacha kazi ya kijeshi kabisa na kuanza biashara yangu mwenyewe," anasema.
Na kwa Raed (sio jina lake halisi), mpiganaji mwingine wa upinzani mwenye umri wa miaka 22, atakayekwenda Niger, anaamini hiyo ndio njia pekee ya kupata pesa za kutosha "kufikia ndoto yangu ya ndoa na kuanzisha familia."
Tangu Desemba 2023, zaidi ya wapiganaji 1,000 wa Syria wamesafiri hadi Niger kupitia Uturuki, kulingana na Shirika la Uangalizi wa Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) lenye makao yake makuu nchini Uingereza, ambalo linafuatilia mzozo wa Syria kupitia mitandao na vyanzo vya habari.
Ni mkataba wa miezi sita, lakini wengine wameongeza mkataba hadi mwaka mmoja.
End of Pia unaweza kusoma
Wanamtumikia nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkataba rasmi ni kwamba wapiganaji hao watakuwa wanalinda miradi ya Uturuki na masilahi yake ya kibiashara nchini Niger.
Uturuki imepanua ushawishi wake wa kisiasa na shughuli za kibiashara katika eneo hilo, ikiuza vifaa kama vile ndege zisizo na rubani kwa Niger ili kusaidia kupambana na vikundi vya wanamgambo wa jihadi.
Pia inajihusisha na uchimbaji wa maliasili za nchi, ambazo ni pamoja na dhahabu, urani na madini ya chuma.
Lakini mamluki wanajua kuwa, wanapofika Niger, mambo yanaweza kuwa tofauti.
SOHR na marafiki wa mamluki ambao tayari wameshafanya kazi nchini Niger waliiambia BBC, Wasyria hufanya kazi chini ya amri ya Urusi kupigana na makundi ya wanamgambo wa jihadi katika mpaka wa pembetatu kati ya Niger, Mali na Burkina Faso.
Rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Niger Mohamed Bazoum alipinduliwa mwaka mmoja uliopita, na tangu wakati huo utawala wa kijeshi umekata uhusiano na Magharibi.
"Niger ilianza kutafuta washirika wapya na Urusi ikawa ndio mbadala," anaelezea Nathaniel Powell, mtafiti wa Sahel katika taasisi ya Oxford Analytica.
"Silaha za Urusi ni za bei nafuu kuliko za Magharibi. Urusi pia inatoa rasilimali na mafunzo ya kijeshi. Na hukubaliana na masharti ya mwenyeji bila kuweka masharti magumu, tofauti na wenzao wa Magharibi."
Kupigana chini ya amri ya Urusi, kunaleta mtanziko kwa wapiganaji wa Syria ambao wanapinga utawala wa Syria na Urusi imekuwa ikimuunga mkono Rais Assad.
"Sisi ni mamluki hapa na mamluki huko," anasema Abu Mohammad, "lakini niko kwenye misheni ya Uturuki, sitakubali amri kutoka kwa Warusi."
Lakini anaweza kukosa chaguo, kama Raed anavyokiri. "Nachukia vikosi hivyo lakini lazima niende kwa sababu za kiuchumi," anasema.
Mchakato wa siri

Chanzo cha picha, Issifou Djibo/EPA-EFE/REX/Shutterstock
Wote bado wanasubiri kusaini mikataba yao kabla tu au wakati wa kusafiri.
Raed anaeleza kuwa mchakato huo ni wa siri na anamfahamu mtu ambaye alifungwa na kundi la upinzani la Syria "kwa kuvujisha baadhi ya maelezo ya operesheni barani Afrika na utaratibu wa usajili."
Mamluki tuliozungumza nao walisema viongozi wa kikundi chao wamewaambia, kampuni ya Kituruki iitwayo SADAT itawasimamia mara tu mikataba itakapotiwa saini na itahusika katika kupanga safari zao na vifaa.
Takribani miaka mitano iliyopita, Abu Mohamad alikwenda Libya ambako alifanya kazi kama mamluki kwa muda wa miezi sita na anasema hilo pia lilipangwa na SADAT.
SOHR pia inadai, kulingana na taarifa kutoka kwa mamluki wengine ambao tayari wamefika Niger, SADAT inahusika katika mchakato huo.
Hatujaweza kuthibitisha madai haya. Tuliwasiliana na SADAT, ambayo ilikanusha vikali kusajili au kupeleka wapiganaji wa Syria nchini Niger, ikisema madai hayo "hayana ukweli, hatufanyi shughuli zozote nchini Niger."
Pia ilisema haina shughuli nchini Libya mbali na mradi wa "michezo ya kijeshi" zaidi ya muongo mmoja uliopita ambao ulimalizika na kujiondoa kwa sababu ya mgogoro huko.
Kampuni hiyo iliongeza kuwa "haikutoa huduma kwa vikosi visivyo vya serikali" lakini badala yake ilitoa "huduma za ushauri, mafunzo na vifaa kwa vikosi vya jeshi na vikosi vya usalama katika uwanja wa ulinzi na usalama kulingana na Kanuni ya Biashara ya Uturuki."
“Makampuni ya kibinafsi yanatumiwa na serikali ya Ankara kuajiri na kutuma mamluki wa Syria nchini Niger,” kulingana na SOHR.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdul Rahman, anaishutumu serikali ya Uturuki kwa kuwanyonya Wasyria bila pesa na matarajio mabaya ya kiuchumi.
BBC ilituma madai haya kwa wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, lakini hatujapata jibu.
Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Uturuki kushutumiwa kuwatuma wapiganaji wa Syria nje ya nchi.
Ripoti kadhaa, ikiwa ni pamoja na ya Idara ya Ulinzi ya Marekani, zimeandika kuwa wapiganaji wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wapo nchini Libya.
Uturuki ilikubali kuwa wapiganaji wa Syria wapo Libya lakini haikukubali kuwa ndiyo iliyowaandishika.
Pia imekanusha kuajiri na kupeleka mamluki wa Syria katika eneo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh huko Caucasus.
Maisha nchini Niger

Chanzo cha picha, Getty Images
Hali nchini Niger inaweza kufanya mchakato wa kuwasiliana na familia nchini Syria kuwa mgumu sana. Mamluki wanapowasili simu zao huchukuliwa, kulingana na Abdul Rahman wa SOHR.
Na Abu Mohammad anasema marafiki zake barani Afrika "wanaweza kuwasiliana na familia zao mara moja kila baada ya wiki mbili, wakati mwingine chini ya wiki hizo."
Anaongeza, hawawezi kuzungumza na wake zao au wazazi wao wenyewe, mawasiliano lazima yapitie kwa wakuu wao nchini Niger "ambao wanazihakikishia familia za wapiganaji kuwa wako sawa."
Ali anaongeza, baadhi ya marafiki zake ambao walisafiri kwenda Niger walimwambia walitumia muda wao mwingi "ndani ya kambi za kijeshi, wakisubiri amri za kupigana."
Na sio wote wanaorudi nyumbani. Kulingana na SOHR, tisa wameuawa nchini Niger tangu Desemba 2023. Miili ya wanne kati yao imerejeshwa Idlib lakini bado haijatambuliwa.
Raed na Ali wanasema familia zao hazitaki waende, kwa hivyo watadanganya na kujifanya wanakwenda Uturuki kufanya mazoezi kwa miezi michache.
Familia ya Abu Muhammad pia haiungi mkono safari hiyo. “Ikiwa ningekuwa na uwezo wa kuishi maisha mazuri, nisingefanya kazi ya aina hii hata kama ungenipa dola milioni moja,” anasema.
“Ikiwa mwanangu ataniomba baiskeli, sina uwezo wa kumudu kumnunulia. Mambo haya ndiyo yananisukuma kwenda."
End of Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












