Je, mwisho wa utawala wa Assad unamaanisha nini kwa wakimbizi wa Syria?

Mwanamume ashikilia bendera ya Syria juu ya kichwa chake huku akisherehekea

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wasyria wanaoishi nchini Ugiriki walikusanyika katika eneo la Syntagma Square mjini Athens kusherehekea matukio nchini mwao.
    • Author, Sanaa Alkhoury
    • Nafasi, BBC Arabic
    • Author, Fundanur Öztürk
    • Nafasi, BBC Turkish
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mamia ya raia wa Syria wanapiga miluzi, wakicheza, kuimba na kusherehekea zikishuhudiwa huko Altındağ, na mjini Ankara, Uturuki. Sherehe zilianza mapema asubuhi wakati taarifa zilipoibuka kuwa utawala wa Bashar al-Assad umeondolewa madarakani.

"Nina furaha sana - hii ni mara ya kwanza kuwa na furaha ya aina hii maishani mwangu," anasema Asif, kijana mwenye umri wa miaka 20 kutoka mji wa Hama nchini Syria. Amebeba bendera za upinzani za Uturuki na Syria mikononi mwake.

"Hatujalala tangu jana usiku. Siwezi kuelezea hisia zangu kwa maneno. Hakuna mtu atakayebaki hapa tena. Kila mtu anataka kurejea nyumbani kwa sababu vita nchi vimekwisha nchini mwetu. Tunaishukuru sana Uturuki."

Rafiki yake Ayham, ambaye anatoka Aleppo, anaunga mkono kauli hizo.

"Hatukuweza kurudi kwa sababu ya ukatili wa Assad. Tulitoroka mikononi mwa dhalimu Assad. Ilibidi tuondoke kwa sababu hatukutaka kulazimishwa kuua raia wetu. Sasa kila kitu kimekwisha, tunarudi."

Kijana mwingine, ambaye ameishi Uturuki kwa miaka 14, anasema amedhamiria kurejea Syria na ataondoka Uturuki mara moja.

"Hapa hakuna kilichobaki kwetu, ni wakati wa kurudi Syria. Tutajenga upya ikibidi hata kuanzia mwanzo, leo siku nilipopanga kuoa Syria ikawa huru, sitaisahau tarehe hii. "

Sherehe kama hizo zilishuhudiwa katika miji mingineiliyo na wakazi wengi wa Syria kote Uturuki, ikiwa ni pamoja na Istanbul. Huko Şişli, umati wa watu ulikusanyika mbele ya ubalozi mdogo wa Syria, wakishusha bendera ya utawala wa Assad.

Uturuki imekuwa nyumbani kwa takriban wakimbizi milioni tatu wa Syria tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria kuanza mwaka 2011.

Wasyria wakisherehekea mjini Istanbul kuanguka kwa utawala wa Assad

Chanzo cha picha, Azra Tosuner / BBC

Maelezo ya picha, Wasyria wakisherehekea mjini Istanbul kuanguka kwa utawala wa Assad

Wasiwasi na hofu

Katikati ya matumaini na msisimko, sio kila mtu ana shauku ya kurudi Syria haraka sana.

Kwenye behewa la treni tulivu huko Berlin, Rasha anazungumza kwa sauti ya chini kwenye kinasa sauti, akiwa mwangalifu asisumbue abiria wenzake. Hadi hivi majuzi, alikuwa amekata tamaa kwa kuamini kwamba hangeweza kuona tena nyumba ya familia yake huko DamasCUS.

Katika muongo mmoja uliopita, mzozo unaoendelea wa Syria ulilazimisha mamilioni kama yeye kukubali kwamba baadhi ya sehemu zao za nyuma zinaweza kubaki bila kufikiwa milele. Lakini habari zikaja.

Kwa wakimbizi wengi wa Syria, taarifa hiyo ilipokelewa kwa hisia mseto: kutoamini, furaha, matumaini, kuchanganyikiwa, na uoga.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa Rasha, msisimko umepungua kutokana na hali halisi ya hatma isiyojulikana. Msukumo wake kwanza ulikuwa "kufunganya virago na kurudi", lakini uwezekano wa kufanikisha uamuzi huo ulififia haraka, kwani tathmini ya jibu hilo ni muhimu zaidi.

"Ninajua jinamizi la kuvuka mpaka na kuogopa kukamatwa au kutoweka limekwisha," anaeleza, "lakini sasa kuna aina nyingine ya hofu: uwezekano wa kulipiza kisasi, mivutano ya kimadhehebu, na vitendo vya kulipiza kisasi."

Akiwa mshiriki wa wachache wa kidini, Rasha anafahamu hasa hatari zinazoweza kutokea. Ingawa bado hakuna ripoti zilizothibitishwa za unyanyasaji unaolenga makundi maalum, bado anahofia.

"Bado tuko katika nyakati za awali kufurahia," anasema kwa tahadhari. "Tunahitaji kufikiria kwa busara."

Hali ya Rasha inazidi kuwa ngumu kutokana na hali yake ya ukimbizi nchini Ujerumani. Akiwa ametumia miaka kujumuika katika jumuiya yake mpya, anaelekea kupokea uraia wa Ujerumani ndani ya mwaka mmoja, hatua muhimu ambayo ingempa uhuru mkubwa wa kutembea.

"Tunataka kurejea bila kupoteza mafanikio ambayo tumepata hapa," anaeleza, akirejelea ujuzi wa lugha, elimu, na utulivu ambao amejenga. "Ikiwa nitarudi sasa na kupoteza hadhi yangu ya kisheria, ninaweza kuhatarisha kila kitu."

Wasiwasi wake pia unahusu hatima ya nyumba ya familia yake huko Damascus.

"Kabla ya jana, nilifikiri sitaiona nyumba yetu tena," anakiri. "Sasa, kuna matumaini. Lakini hali itakuwa vipi ikiwa mtu mwingine ataichukuwa?"

Amefarijika kusikia kwamba hakuna wizi ambao umeripotiwa, lakini bado kuna sintofahamu. "Nina furaha serikali imeanguka," anasema, "lakini ninaogopa mapigano, kuongezeka kwa makundi yenye itikadi kali."

A group of women celebrate in the street

Chanzo cha picha, WAEL HAMZEH/EPA-EFE/REX/Shutterstock

Maelezo ya picha, Wanawake mjini Beirut, Lebanon, wakisherehekea hatua ya waasi kuuchukuwa mji mkuu wa Syria.

Rasha ni mmoja tu kati ya Wasyria zaidi ya milioni 14 ambao wamekimbia makazi yao tangu kuzuka kwa mzozo mwaka 2011. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi UNHCR, mzozo wa wakimbizi wa Syria ndio mkubwa zaidi.

Zaidi ya wakimbizi milioni 5.5 wa Syria wanaishi katika nchi jirani, zikiwemo Uturuki, Lebanon, Jordan, Iraq na Misri. Ujerumani, ikiwa mwenyeji wa zaidi ya Wasyria 850,000, imekuwa nchi iliyo na idadi kubwa ya wakimbizi ambao sio wa taifa jirani.

Kwa wakimbizi wengi, maisha ya nje ya nchi yamekuwa magumu, huku miaka mingi ikitumika kukabili vikwazo vya kisheria, kustahimili matatizo ya kiuchumi, na kukabiliwa na chuki dhidi ya wageni.

People wave Syrian and Danish flags in a town square in Copenhagen, Denmark,

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Maelezo ya picha, Mjini Copenhagen, Denmark, raia wa Syria walisherehekea kuanguka kwa utawala wa Assad

'Kurejea nyumbani haitakuwa rahisi'

Ayah Majzoub, Naibu Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Shirika la Amnesty International, anasisitiza kuwa njia ya kurejea haitakuwa rahisi.

"Wasyria wengi ambao wanaweza kufikiria kurejea wamepoteza nyumba zao, kazi, na wapendwa wao," anaelezea.

"Uchumi nchini Syria umedorora kutokana na migogoro na vikwazo vya miaka mingi. Mashirika ya misaada ya kibinadamu lazima yahakikishe kwa haraka kwamba mapato ni ya hiari, salama na yenye heshima. Waliorejea wanahitaji kupata makazi, chakula, maji, vyoo na huduma za afya."

Majzoub pia anasisitiza umuhimu wa kuepuka kurejeshwa nyumbani kwa lazima. "Serikali mwenyeji lazima zisilazimishe mtu yeyote kurudi," anasema. "Urejeshaji lazima uwe wa hiari kabisa, na tutaendelea kufuatilia hatari zinazowakabili wanaorejea, bila kujali dini zao, kabila, au msimamo wao wa kisiasa."

A Syrian refugee with a face painted with the Syrian flag celebrates in Ankara, Turkey.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mkimbizi wa Syria akisherehekea mjini Ankara, Uturuki

Katika jiji la Jordan la Zarqa, Um Qasim anakumbuka miaka yake kama mkimbizi. "Tumeishi kwa miaka 12 nchini Jordan," anasema. "Watu walitukaribisha kama familia, lakini uhamisho bado ni uhamishoni."

Anaelezea nyakati za furaha zilizojaa huzuni, haswa wakati wa sherehe au huzuni, wakati kutokuwepo kwa jamaa kunahisiwa sana.

Ingawa ana ndoto ya kurejea Syria yenye amani, ana uhalisia kuhusu hali mbaya ya kiuchumi ya nchi hiyo. "Familia yangu bado inateseka. Hakuna umeme thabiti, hakuna maji, na bei ambayo haiwezekani kumudu. Watu wanapaswa kuishi vipi?"

Hisia zake zilizochanganyika zinafanana na za wengi walioko ughaibuni.

"Tuna furaha kuwa utawala umeanguka, lakini kuondoka Jordan, baada ya kujenga familia ya pili hapa, itakuwa ya kuhuzunisha."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi