Kwanini mwaka mpya hauanzi Januari 1 katika nchi zote duniani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Saa inapofika usiku wa tarehe 31 Desemba kila mwaka, si nchi zote duniani husherehekea mwanzo wa mwaka mpya. Tofauti za kitamaduni zimesababisha kila jamii kutumia tarehe ya mwaka wao mpya, kulingana na kalenda wanayotumia, kama vile mzunguko wa mwezi au jua, na mila na desturi zao wenyewe.
Hii inatokana na historia na urithi ambao mataifa yamerithi kwa muda mrefu, kila moja ikitegemea mtazamo wake kuhusu mzunguko wa dunia (Jua na Mwezi), na jinsi muda unavyohusiana na dini, mavuno ya kilimo, au nguvu za kisiasa.
Kalenda ya Kiislamu (Hijri)

Chanzo cha picha, Getty Images
Kalenda ya Kiislamu inategemea mzunguko wa mwezi, ambao ndio unaotumiwa na nchi nyingi za Kiislamu, na mwaka wake huanza na mwezi wa Muharram, mmoja wa miezi mitakatifu ya Uislamu.
Kwa kuwa inategemea mzunguko wa mwezi, mwaka wa Hijri una takriban siku 354, jambo linaloufanya uwe mfupi kwa takriban siku 11 kuliko mwaka wa Gregory.
Waislamu kote ulimwenguni husherehekea mwanzo wa mwaka wa Hijri kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sala, dua, mikusanyiko na jamaa, na kupamba nyumba kwa mishumaa kama ishara ya upya wa kiroho na ukumbusho wa kuhama kwa Mtume (SAW).
Kalenda ya Gregory - Januari 1

Chanzo cha picha, Getty Images
Kalenda hii inategemea mzunguko wa jua, na ndiyo inayotumika sana duniani. Ndio kalenda inayotumiwa na watu wengi duniani.
Inaanza Januari 1. Kihistoria, ilianza katika Milki ya Kirumi, baadaye ikatumiwa na Wakristo, na polepole ikapitishwa na nchi zote ulimwenguni.
Mwaka Mpya wa Kichina

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wa China husherehekea Mwaka Mpya wao kwa kutumia kalenda ya mwezi na jua, ambayo huchanganya mizunguko ya mwezi na misimu ya jua.
Kwa hivyo, mwaka wao hauanzia Januari 1, lakini huanzia mwishoni mwa Januari na katikati ya Februari. Mwaka Mpya wa Kichina unategemea mwezi mpya wa pili baada ya msimu wa baridi, na tarehe hubadilika kila mwaka.
Kwa kawaida sherehe ya mwaka huchukua siku kumi na tano, kuanzia siku ya kwanza ya mwezi wa mwandamo na kuishia usiku wa mwezi mpevu wa tarehe kumi na tano.
Mwaka Mpya wa Kikorea (Seollal)

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa Korea Kusini hutumia kalenda ya Kikristo kama nchi nyingi, Januari 1 kama mwanzo rasmi wa mwaka kulingana na kalenda ya Gregory, Mwaka Mpya wa kitamaduni wa Korea, unaojulikana kama Seollal, ndio tukio muhimu zaidi katika jamii, na hufuata mwaka wa Gregory.
Mwaka Mpya wa Korea hauna tarehe maalum, na huanza siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwandamo, ambao kwa kawaida huangukia mwishoni mwa Januari au katikati ya Februari, karibu na Mwaka Mpya wa Kichina.
Mwaka Mpya wa Kiyahudi (Rosh Hashanah)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka Mpya wa Kiyahudi, unaojulikana kama Rosh Hashanah, si tukio la kalenda, bali ni tukio la kidini na kiroho lenye umuhimu mkubwa kwa Wayahudi kote ulimwenguni.
Kwa kawaida huangukia Septemba au Oktoba kulingana na kalenda ya Gregory, kwani kalenda ya Kiebrania inategemea mfumo wa mwezi na jua, ambao huamua mwaka, misimu ya kilimo, na matukio ya kidini wanayosherehekea.
Nevruus - Mwaka Mpya wa Kiajemi na Asia ya Kati

Chanzo cha picha, Getty Images
Nevruus ni siku ya mwaka mpya ya kalenda ya jua ya Kiajemi, na hutokea kila mwaka wakati mchana na usiku ni sawa na jua liko kwenye ikweta, kihistoria ni Machi 20 au 21.
Sio mwanzo wa Januari, bali ni mwanzo wa majira ya kuchipua, na wakati mwingine muda hutofautiana kulingana na hali ya hewa.
Mwaka Mpya wa Amazigh (Yennayer)

Chanzo cha picha, Getty Images
Waamazigh, watu wa Afrika Kaskazini wenye lugha na utamaduni wao, husherehekea mwaka wao mpya unaoitwa Yennayer, ambao kwa kawaida huangukia Januari 12 au 13 kulingana na kalenda ya Gregory, na unategemea kalenda ya mwezi, ni kalenda ya muda mrefu ambayo imekuwepo kwa karne nyingi.
Sherehe wanazofanya zimepewa jina kutokana na mwezi wa kwanza wa kalenda ya Amazigh, na zinahusishwa na mwanzo wa msimu wa kupanda mazao, kuashiria mwaka mpya wa ustawi na kazi.
Mwaka Mpya wa Ethiopia (Enkutatash)

Chanzo cha picha, Getty Images
Ethiopia na Eritrea husherehekea mwaka wao mpya mwezi Septemba, unaoitwa Enkutatash, na kalenda ya Ethiopia hutofautiana na kalenda ya Gregory kwa idadi ya miezi na urefu wa mwaka.
Ua la manjano ni ishara ya Mwaka Mpya wa Ethiopia, ambalo hupambwa majumbani na mitaani ili kupamba na kuleta mabadiliko, na watu hupeana zawadi.
Maua hayo, pamoja na mila za kidini na sherehe za kitamaduni kama vile nyimbo na densi za kitamaduni, huleta hisia ya matumaini na mwaka mpya.
Kama leo ni Januari 1 na unasherehekea Siku ya Mwaka Mpya, 'Heri ya Mwaka Mpya'.















