Kwanini Israel haitaki vikosi vya Uturuki Gaza?

Chanzo cha picha, Fadel Senna/AFP via Getty Images
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar amesema kuwa Israel haitakubali kuwepo kwa wanajeshi wa Uturuki huko Gaza.
Maneno ya Saar yalikuwa matamshi ya wazi zaidi yaliyotolewa na Israeli kuhusu suala hili.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Hungary, Saar amesema kuwa "Türkiye, chini ya uongozi wa [Rais] Erdoğan, ina mtazamo wa chuki dhidi ya Israel."
"Kwa hiyo, hatutaruhusu vikosi vyao vya kijeshi kuingia Ukanda wa Gaza, na tumewaambia hivi marafiki zetu wa Marekani," Gideon Saar alisema.
Suala hili pia lilijitokeza wakati wa ziara za Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio wiki iliyopita.
Rubio alikariri kwamba "nchi nyingi" zimejitolea kuchangia wanajeshi kwenye kikosi kazi, na kuongeza, "Bila shaka, kikosi hiki kitalazimika kuundwa na nchi ambazo Israel haitasumbuliwa nazo."
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alidokeza Oktoba 22 kwamba alikuwa anapinga kuhusu uwezekano wa wanajeshi wa Uturuki kutumwa Gaza.
Netanyahu alitoa kauli hii wakati wa mkutano wake na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance mnamo Oktoba 21.
Katika mkutano huu, ambao ulikuja siku moja baada ya Vance kusema Uturuki inaweza kuwa na jukumu la "kujenga" huko Gaza, Netanyahu aliulizwa maoni yake juu ya uwezekano wa kuwepo kwa vikosi vya usalama vya Uturuki huko Gaza.
Sentensi ya kwanza ya Netanyahu ilikuwa, "Tutaamua juu ya jambo hili pamoja."
Kisha akasema, "Nina mawazo ya wazi sana kuhusu hili. Je, ungependa kukisia ni nini?"
Wizara ya Ulinzi wa Kitaifa Uturuki ilitoa taarifa ikisema, "Tuko tayari kwa kazi."
Mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa Gaza unajumuisha kuundwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Utulivu.
Indonesia, nchi kubwa zaidi duniani yenye Waislamu wengi, ilitangaza utayari wake wa kutuma wanajeshi katika kikosi hiki.
Rais Recep Tayyip Erdoğan pia alisema kuwa Türkiye itajumuishwa katika kikosi kazi wakati wa mchakato wa kutia saini makubaliano hayo.
Erdoğan alitoa taarifa yake ya mwisho kuhusu suala hili kwenye ndege iliokuwa ikirejea kutoka kwenye ziara yake ya Ghuba na kusema kuwa "mazungumzo ya kina yanaendelea."

Chanzo cha picha, Haroon Sabawoon/Anadolu Agency/Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya hatua hizi, Wizara ya Ulinzi ya Kitaifa inatangaza kwamba Vikosi vya Wanajeshi wa Uturuki vinaendelea na maandalizi yao.
Katika maelezo yaliyotolewa na Wizara ya Ulinzi wa Kitaifa mnamo Oktoba 23, ilitangazwa kuwa walikuwa tayari kufanya kazi katika Jeshi la Kimataifa la Udhibiti.
"Türkiye, ikiwa ni moja ya nchi nne zilizodhamini makubaliano ya kusitisha mapigano, inaendelea na mashauriano ya kidiplomasia na kijeshi na nchi zingine," ilisema taarifa hiyo.
Maafisa wa Wizara ya Ulinzi wa Kitaifa pia waliorodhesha yafuatayo kuhusu dhamira ya Kikosi cha Kimataifa cha Udhibiti:
- Doria ya usalama
- Ulinzi wa miundombinu ya kiraia
- Msaada wa kibinadamu
- Usalama wa mpaka
- Kufanya shughuli za mafunzo ya vikosi vya usalama vya ndani
- Ufuatiliaji wa kusitisha mapigano
Pia kuna mipango kwenye pande za Uturuki na Qatar, ambazo zina ushawishi kwa uongozi wa Hamas, kuhusu kuendelea kwa usitishaji vita na hatua zake nyingine.
Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan na Mkurugenzi wa MIT İbrahim Kalın walikutana na viongozi wa Hamas huko Doha mnamo Oktoba 21.
Afisa wa Uturuki akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP kuhusiana na mkutano huu alisema kuwa hakuna uamuzi madhubuti kuhusiana na mustakabali wa kikosi kazi cha Gaza na Hamas.
Afisa huyo huyo alisema kuwa masuala haya "yatategemea jinsi Israel na Marekani zilivyojikita katika mchakato huo."
Kituo cha Uratibu wa Kijeshi na Kiraia kimeanzishwa

Chanzo cha picha, Nathan Howard - Pool/Getty Images
Kituo cha Uratibu wa Kijeshi na kiraia kilianzishwa huko Kiryat Gat, kusini mwa Israeli, ndani ya mfumo wa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.
Takriban wanajeshi 200 wa Marekani watawekwa katika kituo hiki.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Uingereza mnamo Oktoba 21, ilitangazwa kuwa idadi ndogo ya maafisa wa Uingereza pia watahudumu katika kituo hiki cha uratibu.
Israel na Hamas zinashutumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini Oktoba 12.
Hata hivyo, pande zote mbili zinasema zimejitolea kusitisha mapigano licha ya makabiliano ya hapa na pale.
Suala la mazishi ya mateka pia linaendelea kuzua mvutano.
Kufikia Oktoba 21, inadhaniwa kuwa miili 13 ya mateka wa Israel bado ipo Gaza.















