Je, siasa za Kenya 2026 zinaanzaje bila Raila Odinga?

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Raila Amollo Odinga
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Mwaka 2025 Kenya ilimpoteza mmoja wa watu wake mashuhuri kwa jina la Raila Amolo Odinga, mmoja wa wanasiasa waliodumu nchini humo, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Raila, ambaye alifahamika sana kwa jina la 'Baba' kwa mamilioni ya wafuasi wake, aliaga dunia alipokuwa akipatiwa matibabu nchini India.

Kifo chake kiliashiria mwisho wa enzi ya mtu ambaye alisimama katikati ya maisha ya kisiasa ya Kenya kwa zaidi ya miongo minne.

Mpigania uhuru, mwanamageuzi, na mgombea urais mara tano ambaye alikaribia kushika wadhfa huo zaidi ya mtu mwengine yeyote yule.

Alizaliwa Januari 1945 na Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga, Raila alirithi ujasiri wa babake na shauku ya haki.

Alijipatia umaarufu katika miaka ya 1980 kama mkosoaji asiye na woga wa utawala wa chama kimoja wa Rais Daniel arap Moi, akivumilia miaka ya kizuizini bila kufunguliwa mashtaka kwa harakati yake.

Lakini azma yake lilizidi kuwa na nguvu.

Kenya ilipokumbatia demokrasia ya vyama vingi mwaka wa 1991, Raila aliibuka kuwa mmoja wa wabunifu wake wakuu na sauti kuu ya mageuzi.

Safari ya kisiasa ya Raila ilibainishwa na uvumilivu.

Aligombea urais mara tano.

Mnamo 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022 na kila wakati, alikosa ushindi lakini hakuwahi kukukata tamaa.

Msimamo wake wa karibu zaidi wa madaraka ulikuja mwaka wa 2007 wakati, kama mgombea wa Orange Democratic Movement (ODM), aliaminika na wengi kuwa mshindi kabla ya matokeo ambayo yalibishaniwa kumtangaza Mwai Kibaki kuwa mshindi.

Odinga amekuwa mmoja wa watu mashuhuri nchini Kenya kwa miongo kadhaa, hivyobasi athari ya kifo chake itaonekana katika ulingo wa kisiasa hususan katika , upinzani.

Yafuatayo ni mambo ambayo yanaweza kufanyika nchini Kenya kufuatia kifo cha Raila Odinga .

Mabadiliko ya kisiasa

Kenya itaendelea kufanya kazi kama taifa, lakini hali ya kisiasa itabadilika. Raila mara nyingi amekuwa kiongozi mkuu wa upinzani, hivyobasi kutokuwepo kwake kutatoa fursa kwa viongozi wapya —hasa wanasiasa wachanga—kuinuka na kuendeleza upya siasa za upinzani.

Kutokuwepo kwake kutazua pengo la kisiasa ambalo viongozi wengine watahangaika kulijaza.

Ruto alikuwa akitegemea kuungwa mkono na Raila Odinga ili kushinda uchaguzi wa 2027. Sasa atalazimika kufanya bidii zaidi ili kuweka pamoja muungano utakaoshinda.

Wakati huo huo viongozi hao ambao waliungana kumzunguka Odinga - ikiwa ni pamoja na wale waliomtegemea kwa nyadhifa zao - watahitaji kuamua jinsi gani wanaweza kuhamasishana kwa ufanisi zaidi akiwa hayupo.

Wanapofanya hivyo, viongozi wote watakuwa wanafanya kazi katika kivuli chake, na katika hali ambayo watu na jamii zilizotengwa nchini zitahisi kutowakilishwa na wale walio mamlakani.

Upinzani utagawanyika au kujipanga upya

Raila amekuwa mtu anayeunganisha mavuguvugu mengi ya upinzani. Bila yeye:

Vyama vya upinzani vinaweza kuhangaika na kudumisha umoja wao .

Muungano mpya au viongozi wanaweza kuibuka

Siasa zinaweza kuwa na ushindani mkali ndani ya upinzani

Baada ya muda, hii inaweza kuwa nzuri kwa demokrasia ikiwa itajenga taasisi imara badala ya siasa za kibinafsi .

Siasa zisizo na ubinafsi

Uwepo wa Raila kwa muda mrefu mara nyingi umefanya uchaguzi kuhisi kama kura ya maoni juu yake binafsi. Bila hiyo:

Siasa sasa zinaweza hatua kwa hatua kuwa msingi wa masuala

Wapiga kura wanaweza kuzingatia zaidi sera, utawala na utendaji badala ya ushindani wa kihistoria wa kisiasa.

Athari ya kihisia

Kwa Wakenya wengi, Raila anawakilisha upinzani, mageuzi, na mapambano. Kutokuwepo kwake kungesababisha hali muhimu kihisia, hasa kwa wafuasi wanaomwona kama ishara ya demokrasia na haki.

Kwa ujumla, Kenya haitasambaratika bila Raila Odinga—lakini itaingia katika awamu ya mpito. Nchi itahama kutoka enzi iliyotawaliwa na watu wachache wa kihistoria hadi wakati ambapo viongozi wapya, mawazo, na mitindo ya kisiasa hutengeneza siku zijazo.

Mwaka 2026 ukiwa umeanza, ndugu yake na Raila, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Oburu Oginga, ametangaza wazi kuwa atakuwa mgombea wa urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 endapo ODM itaamua kugombea pekee bila kuingia muungano na vyama vingine.

Mwaka 2026 bila Odinga na mwaka 2027 na Odinga mwingine, Kenya itaamua nini?