Marais watano wa Afrika walioondoka madarakani kwa hiari

,m

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa kwanza Mwafrika kuondoka madarakani kwa hiari, Léopold Sedar Senghor (kushoto) alitangaza kujiuzulu Desemba 31, 1980, baada ya miaka 20 akiwa mkuu wa Senegal.
    • Author, Ousmane Badiane
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Licha ya migogoro mingi ya kisiasa barani Afrika, lakini kuna marais wachache waliojiuzulu kwa hiari yao kabla ya muhula wao kuisha kikatiba.

Tangu uhuru, baadhi ya viongozi wameondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na mauaji. Katika mazingira haya, visa vya marais wa Afrika kuondoka kwa hiari katika nafasi ya juu ya utawala ni nadra.

Viongozi watano katika nafasi ya urais ambao waliondoka kwa hiari yao: Léopold Sédar Senghor, Ahmadou Ahidjo, Julius Nyerere, Thabo Mbeki, na Joachim Chissano.

Pia unaweza kusoma

Léopold Sédar Senghor (Senegal)

,,l

Chanzo cha picha, AFP

Miaka 45 iliyopita, Desemba 31,1980, Léopold Sédar Senghor alitangaza rasmi kujiuzulu urais wa Senegal, na kuwa mkuu wa kwanza wa nchi Mwafrika kuondoka madarakani kwa hiari baada ya miaka ishirini akiwa rais.

Tangazo la uamuzi huu wa kihistoria lilifichuliwa kwa mara ya kwanza Desemba 4, 1980 katika gazeti la kila siku la Le Soleil, kisha akatangaza rasmi katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka kwa taifa.

Mshairi na rais mwenye umri wa miaka 74 alithibitisha kuondoka kwake, kuanzia saa sita usiku. Alitaja umri wake na kanuni ya kisiasa: ile ya kuachia madaraka kwa kizazi kipya, kuwa ndio sababu za kuondoka.

Senghor, rais wa kwanza wa Jamhuri mpya ya Senegali, alirithiwa na Waziri Mkuu wake, Abdou Diouf, mwanachama wa chama hicho hicho, Chama cha Kisoshalisti. Diouf aliapishwa Januari 1, 1981.

Licha ya mashaka ya viongozi kadhaa wa Kiafrika wakati huo, Léopold Sédar Senghor alisisitiza kuandaa kipindi cha mpito cha amani na kwa utaratibu, bila kuingiliwa kijeshi au mgogoro wa kisiasa. Hii ilikuwa mara ya kwanza katika bara ambalo wakati huo lilikuwa na mapinduzi ya kijeshi na urais wa maisha.

Katika ujumbe wake wa kuaga, alitoa wito wa umoja wa kitaifa, heshima kwa haki za binadamu na kulindwa kwa demokrasia, huku akitoa shukrani zake kwa watu wa Senegal kwa kumuamini kwa miongo miwili.

Kuondoka huku kwa hiari kunasalia, kuwa hatua muhimu katika historia ya kisiasa ya Senegal na kumbukumbu ya kipekee katika historia ya mabadiliko ya kidemokrasia barani Afrika.

Ahmadou Ahidjo (Cameroon)

K

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Novemba 4, 1982, Rais wa Cameroon Ahmadou Ahidjo alitangaza kujiuzulu wakati wa hotuba fupi kupitia redio.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Wacomeroon, wapendwa wenzangu. Nimeamua kujiuzulu kutoka nafasi yangu kama Rais wa Jamhuri ya Cameroon. Uamuzi huu utaanza kutekelezwa Jumamosi, Novemba 6."

Novemba 4, 1982, Rais wa Cameroon, Ahmadou Ahidjo alitangaza kujiuzulu kwake katika hotuba fupi ya redio kwa taifa, na kumaliza miaka ishirini na miwili ya madaraka akiwa mkuu wa nchi.

Katika ujumbe huu mfupi uliotangazwa jioni, Ahmadou Ahidjo alitangaza kujiuzulu kwake kwa sababu za kiafya. Kwa mujibu wa Katiba, siku mbili baadaye, Novemba 6, 1982, Waziri Mkuu wake, Paul Biya, alimrithi rasmi kama Rais.

Mpito huu wa amani, bila kuingiliwa kijeshi, ulileta mabadiliko makubwa katika historia ya siasa za Cameroon.

Katika miezi iliyofuata, uhusiano kati ya Ahmadou Ahidjo na mrithi wake ulizorota sana, na kusababisha mgawanyiko wa kisiasa na kisha kufurushwa kwa rais wa zamani.

Kipindi hiki kilikuwa na mvutano mkali, na kufikia kilele cha jaribio la mapinduzi la Aprili 1984, ambalo serikali ililihusisha na wafuasi wa rais wa zamani wa nchi.

Kwa hivyo kujiuzulu kwa Ahmadou Ahidjo kunabaki kuwa tukio la kipekee katika historia ya Cameroon: mpito ambao ulikuwa wa amani, lakini matokeo yake ya kisiasa yanaendelea kuacha alama ya kudumu nchini.

Julius Nyerere (Tanzania)

l

Chanzo cha picha, UPI/Bettmann Archive/Getty Images

Ukurasa wa historia ulifunguliwa nchini Tanzania Novemba 5, 1985, wakati Rais Julius Nyerere alipojiuzulu kwa hiari baada ya miaka 21 akiwa mkuu wa nchi, na kuwa mmoja wa wakuu wa kwanza wa nchi za Kiafrika kujiondoa madarakani kwa hiari yake.

Baada ya kuongoza nchi kwa miaka 23, Rais Julius Nyerere, ambaye wengi wanamwona kama baba wa taifa la Tanzania, aliwashangaza wananchi wenzake kwa kutangaza kujiuzulu, na hivyo kumfungulia njia mrithi wake.

Akitambuliwa rasmi kama "Baba wa Taifa," Julius Nyerere, kama Kwame Nkrumah nchini Ghana au Léopold Sédar Senghor nchini Senegal, alikuwa mmoja wa wasanifu wakuu wa kutofungamana na upande wowote, umajumui wa kiafrika, kupinga ubeberu, na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini.

1967, katika hotuba yake huko Arusha, alizindua Ujamaa, jaribio la "Ujamaa kwa mtindo wa Kiafrika," yaani mshikamano wa jamii na ujumuishaji wa rasilimali muhimu.

Ingawa mfumo huu haukuleta matokeo ya kiuchumi yaliyotarajiwa na ulikosolewa vikali, ulichangia katika kuunda utambulisho imara wa kitaifa katika nchi yenye makabila mengi.

Akiwa mtu muhimu katika harakati za uhuru wa Afrika, Julius Nyerere alipokeza urais kwa makamu wake wa rais, Ali Hassan Mwinyi. Mwinyi alihudumu kama rais, kuanzia 1985 hadi 1995. Chini ya uongozi wake, Tanzania ilianzisha mfumo wa vyama vingi, na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Baada ya kuondoka mwaka 1985, Nyerere alibaki kuwa rais wa chama kimoja Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka mitano kabla ya kustaafu kabisa maisha ya kisiasa. Hadi kifo chake, alibaki kuwa sauti inayoheshimika kuhusu masuala ya Afrika na kimataifa.

Joachim Chissano (Msumbiji)

l

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Joaquim Chissano, rais wa Msumbiji kuanzia 1986 hadi 2005, aliondoka madarakani kwa hiari yake mwaka 2005.

Joaquim Chissano, rais wa Msumbiji kuanzia mwaka 1986 hadi 2005, aliondoka madarakani kwa hiari yake mwaka 2005, akichagua kutogombea muhula wa tatu, na kuashiria mpito mkubwa wa kidemokrasia baada ya miaka 18 kama rais.

Chissano alijiondoa madarakani kwa hiari yake mwishoni mwa muhula wake wa pili, akiheshimu mipaka ya kikatiba na kuwa mmoja wa wakuu wachache wa nchi za Kiafrika waliokataa kurefusha muhula wake.

Baada ya kuingia madarakani mwaka 1986 kufuatia kifo cha Samora Machel, Joachim Chissano aliongoza Msumbiji kipindi muhimu, cha mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mpito hadi mfumo wa vyama vingi. Chini ya urais wake, Makubaliano ya Amani ya Roma ya 1992 yalikomesha vita vya miaka kumi na sita kati ya serikali na waasi wa Renamo.

Alichaguliwa kidemokrasia mwaka 1994 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo, na kisha kuchaguliwa tena mwaka 1999, Chissano alichagua kutogombea muhula wa tatu, ingawa chama chake, Chama cha Ukombozi cha Msumbiji (Frelimo), kilikuwa na wingi wa kisiasa na njia za kikatiba za kufanya hivyo.

2005, alikabidhi madaraka kwa Armando Guebuza, mgombea wa Frelimo, akiimarisha taswira ya Msumbiji kama moja ya nchi chache za Kiafrika zilizopitia mabadiliko ya madaraka bila usumbufu baada ya mzozo mrefu.

Katika ngazi ya kikanda na kimataifa, Joachim Chissano alijiimarisha kama mtu anayeheshimika katika upatanishi na diplomasia ya Afrika, hasa katika michakato ya amani Kusini na Kati mwa Afrika. Baada ya kuondoka katika urais, aliendelea kuhusika katika Umoja wa Afrika na mashirika kadhaa ya kimataifa, kama mwanasiasa aliyejitolea katika utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.

Thabo Mbeki (Afrika Kusini)

k

Chanzo cha picha, Louise Gubb/CORBIS SABA/Corbis kupitia Getty Images

Maelezo ya picha, Thabo Mbeki alimrithi Nelson Mandela kwa dhamira ya kuimarisha demokrasia changa ya Afrika Kusini na kuiweka nchi hiyo katika jukwaa la kimataifa.

Alichaguliwa mwaka 1999 na kisha kuchaguliwa tena mwaka 2004, Thabo Mbeki, rais wa Afrika Kusini na kiongozi mkuu wa chama cha ANC baada ya ubaguzi wa rangi, alijiuzulu Septemba 21, 2008, akikubali shinikizo kutoka kwa chama chake mwenyewe, lililotokana na ushindani wa ndani na kuongezeka kwa ushawishi wa Jacob Zuma.

Kuondoka huku, bila kuingiliwa kijeshi au uasi wa umma, kunaashiria mabadiliko makubwa, yaani rais wa Afrika analazimika kuondoka madarakani kupitia mfumo wa chama.

Thabo Mbeki alimrithi Nelson Mandela kwa dhamira ya kuimarisha demokrasia changa ya Afrika Kusini na kuiweka nchi katika jukwaa la kimataifa. Kuondoka kwake kulisababishwa na mgawanyiko mkubwa wa ndani ndani ya ANC, uliozidishwa na ushindani wake wa kisiasa na Jacob Zuma, ambaye wakati huo alikuwa mwenyekiti wa chama.

Kwa mujibu wa Katiba ya Afrika Kusini, urais wa mpito ulishikiliwa na Kgalema Motlanthe hadi uchaguzi mkuu wa 2009, ambao Jacob Zuma alishinda. Mpito huo ulifanyika bila vurugu au changamoto yoyote kwa taasisi hizo, na kuthibitisha nguvu ya mfumo wa kidemokrasia wa Afrika Kusini.

Kujiuzulu kwa Thabo Mbeki hakukuwa kujiuzulu kwa hiari, bali kujiuzulu kulilazimishwa na chama. Hata hivyo, bado ni tukio muhimu katika historia ya Afrika Kusini, likionyesha ukuu wa chama juu ya ofisi ya rais.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi