Mabinti wa marais wa Afrika wanafanya nini zaidi ya kuwa watoto wa wakuu wa nchi?

Chanzo cha picha, Wanu Hafidh Ameir Suluhu/Instagram
- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 11
Wanazaliwa katika familia maarufu na mazingira ya kifahari. Baadhi ya Mabinti hawa wa wazazi wenye mamlaka zaidi barani Afrika, wameonekana kuwa na mvuto kwa jamii zao kutokana na kazi zao, mafanikio yao katika jamii au hata mtindo wao wa maisha.
Baadhi yao husifiwa kwa mafanikio yao nyuma ya jina la wazazi wao , huku wengine wakijipata katika utata na ukosoaji.
Hawa ni mabinti 8 wa Afrika tunaowaangazia katika makala hii:
Uganda: Natasha Karugire Museveni

Chanzo cha picha, Natasha Karugire/X
Natasha Karugire ni binti na mtoto wa pili wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Mke wa Rais Janet Museveni.
Licha ya malezi yake ya hali ya juu ndani ya Ikulu Natasha alikuwa na ndoto zake kuu ya kuwa mbunifu wa mitindo ya mavazi, akilenga kukuza sanaa na utamaduni wa Uganda, ndoto aliyoanza kuitekeleza tangu alipokuwa msichana mdogo.
Akijiimarisha kama mbunifu mwenye kipawa hicho, kupitia chapa ya Natasha, J&N Couture, huchanganya mambo ya kitamaduni ya Uganda na urembo wa kisasa, na kupata kutambuliwa ndani na kimataifa.
Kutokana na kipaji chake alichokiboresha kwa mafunzo nchini Afrika Kusini, anajulikana kwa mchango wake katika tasnia ya ubunifu na kujitolea kwake kukuza sanaa na utamaduni wa Uganda.
Mbali na ubunifu na mitindo ya mavazi, Natasha anafahamika katika Sekta ya Filamu baada ya kufanikiwa kwa filamu ya tamthilia yake ya kihistoria ya "27 Guns," ambayo aliiandika na kuiongoza.
Filamu hiyo inayoonyesha babake akiinuka mamlakani wakati wa Vita vya Msituni vya Uganda. Filamu hiyo imepata sifa kubwa na kuonyesha vipaji vya Waganda duniani kote. Mnamo mwaka wa 2023, alizindua filamu " "Those Among Us," ambayo inasimulia historia ya Uganda, siasa, na watu mashuhuri.
Bi Natasha pia amesifika kwa Kutumia jukwaa lake kama Binti wa Rais, kutetea uhifadhi na ukuzaji wa sanaa na utamaduni wa Uganda, akiwasaidia wasanii wa ndani na taasisi za kitamaduni, kukuza ushirikiano wa kimataifa.

Chanzo cha picha, Natasha Karugire Museni/Facebook
Kazi ya Natasha katika tasnia ya ubunifu inalenga kuwawezesha wanawake, mitindo yake ikilenga husherehekea nguvu na urembo wa wanawake, huku ushiriki wake katika utengenezaji wa filamu ukitoa fursa kwa wanawake mbele na nyuma ya kamera.
Katika kazi hizo Natasha amepokea sifa nyingi kwa mchango wake katika muundo wa mitindo na utengenezaji wa filamu. Mkusanyiko wake umeonyeshwa kwenye hafla za kifahari za mitindo, na filamu yake ya " 27 Guns" imeadhimishwa katika sherehe mbalimbali za filamu.
Kama Binti wa Kwanza wa Uganda kisanii, Natasha ananaonelewa na wengi kama msukumo kwa wale wanaotaka kuleta matokeo chanya katika jamii zao na kwingineko.
Kitabu chake cha Sowing Mustard Seed ambacho ni wasifu wa namna Rais Museveni alivyoingia madarakani kupitia vita vya msituni, pia kinaonekana na baadhi ya Waganda kama moja ya vitabu vitabu vya kihistoria vya Uganda.
Nigeria: Habibat Oyindamola Tinubu

Chanzo cha picha, Habibat Tinubu/Instagram
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Habibat mwenye umri wa miaka 32 ni binti wa Rais wa Nigeria, Bola Tinubu.
Mbali na kuwa mtoto wa kiongozi mkuu wa taifa la Nigeria, Habibat Oyindamola Tinubu ni mwanamitindo, mwimbaji na mwanamuziki anayeishi Marekani.
Akiwa Mhitimu wa Chuo cha Muziki cha Berklee huko Boston, Massachusetts, nchini Marekani Bi Habibat amejijengea jina kama mwanamitindo anayeonyesha mavazi jukwani (Runway model), kote ulimwenguni akifanya kazi na nembo kubwa kama vile Vague Magazine na kampuni ya vipodozi ya Fenty Beauty
Hatahivyo maisha yake yameibua hisia kali mtandaoni hususan miongoni mwa Wanigeria baada ya kubainika kuwa ni mwanaharakati wa haki za wapenzi wa jinsi moja LGBTQ na kujitambulisha kama "queer". Queer ni neno linalotumika kuwatambulisha watu ambao wasioshiriki mapenzi na watu wa jinsia moja, na watu waliobadili jinsia wote wanaweza kujitambulisha kwa neno queer.
Kwenye mtandao wa X, zamani ikiitwa Twitter, Habibat Tinubu ameelezea mawazo yake, akionyesha kuunga mkono haki za LGBTQ+.
Pia ameonyesha msaada mkubwa kwa jumuiya ya LGBTQ+ kupitia kazi yake ya uanamitindo.

Chanzo cha picha, Habibat Oyindamola Tinubu/ Instagram
Alitoa taarifa kuhusu hali yake ya kijinsia wakati mmoja alipokuwa ameigiza kuwa kama paka na kutoa kelele za paka.
Yeye ni mtoto wa sita kati ya watoto saba wa Rais Tinubu, lakini ni wa pili kati ya watoto watatu wa mkewe, Remi Tinubu.
Nchini Nigeria, ambapo baba yake Habibat ni rais, kushiriki mapenzi ya jinsi moja ni kinyume cha sheria. Sheria ya Kukataza Ndoa za Jinsia Moja ya Nigeria inaharamisha aina zote za maungano ya jinsia moja na ndoa za jinsia moja kote nchini. Kitendo hicho kinaadhibiwa hadi miaka 14 jela.
Adhabu ya juu zaidi kwa mahusiano ya jinsia moja katika majimbo 12 ya kaskazini mwa Nigeria ambayo yamepitisha sheria ya Sharia ni kifo cha kupigwa mawe.
Tanzania: Wanu Hafidh Ameir Suluhu

Chanzo cha picha, Mwanu Hafidh Ameir Suluhu/Instagram
Wanu Hafidh Ameir ni mtoto mashuhuri wa Tanzania anayejulikana sana kwa kuwa binti ya Samia Suluh,- rais wa sita wa Tanzania aliyeingia madarakani tarehe 19 Machi 2021 baada ya kifo cha rais aliyepita, John Pombe Magufuli, siku mbili mapema.
Akiwa ndiye binti wa kwanza wa Rais Samia Suluhu Hassan na Hafidh Ameir, Wanu amefuata nyayo za mama yake kwa kuwa mwanasiasa wa Tanzania na mwanachama wa chama tawala -Chama cha Mapinduzin(CCM).
Kwa sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa chama hicho, nafasi aliyoishikilia tangu mwaka 2010.
Ameshikilia kiti cha Ubunge katika Baraza la wawakilishi la Zanzibar tangu mwaka 2005.
Licha ya nyadhifa hizo Wanu ambaye alizaliwa mnamo 9 Februari 1982 Zanzibar, ameshikilia nyadhifa mbali mbali za kisiasa ambapo kuanzia mwaka 2015 hadi 2018, na alikuwa mjumbe katika Kamati ya Katiba na Masuala ya Sheria. Alikuwa Mwenyekiti wa Vijana CCM- Kusini Unguja kuanzia mwaka 2008 hadi 2012.
Wanu ni Mwenyekiti na Mwanzilishi wa taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) ambayo aliianzisha Juni 2022 Zanzibar kwa lengo la kuwasaidia watoto katika elimu, ili kuhakikisha wanakamilisha ndoto zao kimaisha.
Ana diploma ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia aliyoipata kutoka Kituo cha Mahusiano ya Kimataifa.
Kenya - Charlene Ruto

Chanzo cha picha, Charlene Ruto/Facebook
Charlene Ruto ni binti na mtoto wa tatu wa Rais wa Kenya William Ruto na Rachel Ruto.
Mbali na kuwa mtoto wa rais Bi Charlen amekuwa ajijaribu kuonyesha mchango wake katika maendeleo ya vijana, licha ya kupata ukosoaji mkubwa kutoka kwa jamii.
Alikabiliwa na mtihani mkubwa pale alipolazimika kukanusha tuhuma kwamba pesa za zinatumika kufadhili kile anachoita "Ofisi ya Binti wa Kwanza".
Katika sheria za Kenya, hakuna ofisi kama hiyo.
Tangu baba yake aingie mamlakani, Charlene Ruto aliitisha mikutano kadhaa ya hadhi ya juu chini ya jina hilo.
Hatahivyo Charlene hajasita katika harakati za wezeshaji wa vijana akiitisha mikutano rasmi 31 kwa muda wa mwezi mmoja tu kunaonyesha kujitolea kwake kuhakikisha kuwa sauti na mahangaiko ya vijana wa Kenya yanasikika katika ngazi za juu zaidi za kufanya maamuzi. Utetezi wake unaenea hadi sekta ya kibinafsi, ambapo anakuza ushiriki wa vijana, ushirikiano, na fursa ndani ya jumuiya ya wafanyabiashara.
Akiwa mlezi na mwanzilishi wa Smart Mechanized Agriculture and Climate Action for Humanity and Sustainability Foundation (SMACHs) Foundation, Charlene Ruto anaongoza mipango ya kuwapa vijana ujuzi kwa ajili ya kupata ujuzi wa kilimo cha kisasa.
Taasisi hiyo inashughulikia changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kwa kukuza mbinu endelevu na bunifu za kilimo, ikionyesha dhamira ya Charlene katika kuwawezesha vijana katika sekta mbalimbali.
Binti huyo wa Rais William Ruto aliyezaliwa Januari 1993, aliorodheshwa katika nafasi ya 5 ya Wanawake 100 wa Kiafrika wenye ushawishi zaidi Afrika ya mwaka 2023 ya taasisi ya Avance Media
Ni Binti mwenye maono ya uongozi, hatahivyo alikiri mwaka jana kuwa anakabiliwana shinikizo la kuwa mtu mashuhuri , lakini akasema kuukumbatia utambulisho wake kulimsaidia kukua katika kukabiliana na shinikizo hilo
Pia ana Shahada ya Kwanza katika Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Daystar nchini Kenya na Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara katika masuala ya Hoteli na utalii (Hospitality) kutoka Shule ya Kimataifa ya Usimamizi wa Hoteli ya Les Roches huko Crans-Montana, Uswidi.
Rwanda – Ange Kagame

Chanzo cha picha, Personal Collection
Ange Kagame ni mtoto wa pili na Binti pekee wa Rwanda Paul Kagame.
Mbali na kuwa Binti wa Rais, Bi Ange ameonekana kuhusika katika masuala yanayojumuisha uwezeshaji wa wanawake, elimu, na kupunguza umaskini, uhifadhi wa mazingira, pamoja na kampeni za afya ya umma.
Akiwa msoni wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Smith huko Massachusetts, nchini Marekani aliteuliwa na baba yake Rais Paul Kagame kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Baraza la Mikakati na Sera (SPC) katika Ofisi ya Rais.

Chanzo cha picha, Flickr/Paul Kagame
Tangu 2019, amekuwa akifanya kazi katika Baraza la Rais kama mchambuzi mwandamizi wa sera.
Ana shahada ya uzamili katika maswala ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Columbia, New York, moja ya vyuo vikuu vya kifahari nchini Marekani na ulimwengu.
Ange Kagame amekuwepo katika mikutano muhimu nchini Rwanda, ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Kitaifa wa kujadili maendeleo ya taifa, na kushiriki katika kampeni za kitaifa kama vile kampeni ya kudhibiti maradhi ya Covid -19 na lishe kwa watoto wachanga.
Mwaka 2016, baadhi ya magazeti yaliripoti kwamba alikuwa mwanachama wa timu ya mitandao ya kijamii ya ofisi ya Rais, lakini Ange Kagame na ofisi ya Rais walikanusha hili.
Zimbabwe: Tariro Mnangagwa

Chanzo cha picha, Tariro Mnangagwa/Instagram
Tariro Mnangagwa ni Binti wa Rais wa Zimbabwe Amerson Mnangagwa. Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1998, amejikita zaidi katika sekta ya filamu akiwa mtayarishaji wa filamu wa Zimbabwe, mwigizaji .
Tariro anajulikana kwa jukumu lake katika filamu ya 2020 Gonarezhou The Movie. Amesifika kwa utayarishaji wa filamu kama Gonarezhou Sinema [2020] na Hadithi ya Nehanda. [2021], akiigiza filamu zote mbili. Yeye ndiye binti mdogo wa rais wa sasa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa na mkewe wa kwanza Jayne Matarise, ambaye alifariki mnamo 31 Januari 2002 kwa saratani ya shingo ya kizazi. Tarimo Mnangagwa ana ndugu watano wakubwa.

Chanzo cha picha, Tariro Mnangagwa/ Instagram
Mnangagwa alipata Diploma ya Upigaji Picha wa Kitaalam huko Cape Town. Pia alihitimu shahada ya Usimamizi wa Michezo katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Cape Peninsula
Baada ya kurejea Zimbabwe, Mnangagwa alijiunga na Akashinga, kitengo cha mgambo wa kupambana na uwindaji haramu. Kisha akawa mwanachama wa kitengo cha kupambana na iuwindaji haramu cha wanawake. BINTI mdogo wa Rais Emmerson Mnangagwa, Tariro, amejiunga na kundi la walinzi vijana waliojitolea kupambana na ujangili katika bonde la Zambezi.
Takriban wanawake 36 wanaunda kitengo cha kupambana na ujangili ambacho kinafundishwa na kitengo cha walinzi wa uwanja cha Akashinga cha International Anti-Poaching Foundation kukabiliana na majangili katika eneo hilo.
Amecheza mara tatu katika filamu ya Gonarezhou kama mtayarishaji mwenza wa filamu hiyo, akijulikana kama Sydney Taivashe.
Burundi: Navie Quetsia Madeleine Keza Ndayishimiye

Chanzo cha picha, Good Action BA Umugiraneza Foundation
Mei 11 (5) mwaka huu 2025, bintiye Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alipata shahada yake ya Sayansi ya Siasa na Uhalifu kutoka Chuo Kikuu cha Gonzaga.
Katika ujumbe wake uliowekwa kwenye tovuti ya X, mama yake Mke wa Rais wa Burundi , Angeline Ndayishimiye Ndayubaha alisema kuwa safari yake hiyo inaambatana na kutochoka, kupenda maarifa na uwezo wake wa kustaajabisha wa kukabiliana na changamoto. "Kwa hekima na uvumilivu, alichukua kila hatua kwa dhamira," alisema.
Anasema bintiye ni mfano wa kuigwa kwa vijana wenye malengo na wanaojiheshimu, tayari kutumia ujuzi wake kwa manufaa ya wote.
Mnamo 2021, Quetsia Madeleine Keza alizindua shirika liitwalo Bene Ntare kwa lengo la kusaidia vijana kama yeye, haswa wasichana, kwa kuwasaidia kufikia malengo yao ya kujitegemea.
Pia alizindua kampuni iitwayo Madele Company mnamo 2023, ambayo inalenga kusaidia tasnia ya mitindo nchini. Anasema pia kuwa kampuni yake inasaidia vijana wanaotaka kuwa wabunifu wa mitindo kwa kuwapa ubunifu wa mavazi wanayoweza kutengeneza.
Mnamo Agosti (8) 2024, Quetsia Madeleine aliwasilishwa katika hafla kama msaidizi katika kituo cha Bonne Action Umugiraneza, kinachomilikiwa na Rais Evariste Ndayishimiye.
Cameroon: Brenda Biya

Chanzo cha picha, Brenda Biya /Instagram
Tofauti na Mabinti wengine wa marais,Brenda Biya ni Binti ametokea kujulikana kwa maono na vitendo vyake vinavyokwenda kinyume na matarajio ya jamii ya Wacameroon, hususan ni mtindo wake wa maisha, ulioibua utata.
Akizaliwa 1997, Bi Brenda alisomea katika shule za kifahari, masomo yake ya chekechea akiyaanzia katika Etoudi , shule ya kifahari iliyompo mjini Yaoundé Cameroon, iliyotengwa maalum kwa ajili ya watoto wa rais, na wafanyakazi wengine wa ofisi ya rais.
Alijiunga na shule ya bweni- Collège du Léman, shule ya kibinafsi ya Uswizi katika Versoix, Takriban kilomita kumi kutoka Geneva, ambayo inajulikana kuelimisha watoto wa marais.
Kisha akahamia Los Angeles nchini Marekani, ambako aliendelea na masomo yake.
Akiwa huko, alishutumu ubaguzi wa rangi dhidi ya Weusi wa dereva wa teksi kwenye akaunti yake ya Twitter.
Akiwa huko baadhi ya waandishi wa habari walikosoa mtindo wake wa maisha, maisha yake ya kifahari, karamu zake na pombe kali, na uvutaji wa sigara.
Mnamo 2024, Biya alianza kazi ya mziki wa kurap na kazi ambayo haikutarajiwa kufanywa na Binti wa Rais.
Lakini lililoibua zaidi hisia ni Aprili 2015, alichapisha picha yenye utata kwenye akaunti yake ya Instagram, ikimuonyesha akimbusu mtu mwenye jinsia sawa na yake (ya kike) asiyejulikana. Kufuatia ukosoaji mkubwa wa umma, alilazimika kuondoa picha hiyo, pamoja na picha zingine zote kwenye akaunti yake.

Chanzo cha picha, Btenda Biya /Instagram
Mnamo 2020, Brenda Biya alitangaza kuwa kwa njia ya video kwamba alikuwa kwenye uhusiano na mwishoni mwa mwezi huo 30, 2024, alijitokeza na kujitangaza rasmi kama mpenzi wa jinsi moja kwa kuchapisha picha kwenye ukurasa wake wa Instagram, akimbusu mpenzi wake, mwanamitindo wa Brazil Layyons Valença.
Taarifa hiyo iliibua maoni makali na kuendea kwenye mitandao ya kijamii katika nchi ambayo mapenzi ya jinsi moja ni haramu.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa vitendo vyake vimesababisha aibu kwa Cameroon.
Mwezi Mei 2016, Brenda aliripotiwa kukimbizwa hospitalini huko Los Angeles, Marekani kwa madai ya kutumia dozi zaidi ya dawa za kulevya mnamo Mei 11.
Katika tukio jingine lililoibua maoni makali mtandaoni Brenda aliushirikisha umma video akimrekodi mlinzi ambaye alitaka kumzuia baada ya kutawanya vitu kutoka chumbani kwake. Binti wa Rais Biya alizungumzia jinsi anavyoteseka kwa ajili ya Cameroon, anachoomba hakupewa. Aende hospitali ya Jamot ambako wanatibu vichaa.
Mnamo 2020, aliamua kujikita katika kazi ya muziki na ni shabiki wa wasanii kadhaa wa Kiafrika, kama vile Locko, na wakati mmoja alimualika Wizkid kwenye ikulu ya rais kwa onyesho la kibinafsi.
Brenda Biya pia ni mjasiriamal ambapo Aprili 16, 2020, alizindua duka aliloliita Bree Culture Inc Shopping, duka la kuuza nywele bandia (wigi), huko Beverly Hills, California Marekani.
Bila shaka sawa na kila mmoja wetu Mabinti hawa wa Marais wa Afrika wameonyesha kuwa Mtoto wa Rais sio kizingiti cha kufuata ndoto au maisha yako ya kibinafsi.















