Wake wa marais: Mfahamu Bi Jeanette Nyiramongi Kagame mke wa rais wa Rwanda Paul Kagame

Chanzo cha picha, Rwanda FirstLady /Twitter
- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC Swahili
Ni watu wenye ushawishi katika uongozi wa kila siku wa nchi zao, hata hivyo si kila siku utasikia juu ya maisha yao na vipawa vyao. Hawa ni wenza wa marais, ambao baadhi yao ni wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega katika safari za kisiasa za wenza wao mpaka kushika hatamu za madaraka. Wiki hii tunakuletea mfululizo wa makala kuhusu wenza wa marais katika eneo la Afrika Mashariki na leo tunakupakulia yote unayofaa kujua kumhusu mke wa rais wa Rwanda .
Wengi wanamfahamu kama mke wa Rais wa Rwanda Paul Kagame, lakini kwa Wanyarwanda wengi, Bi Jeannette Nyiramongi Kagame ni zaidi ya kuwa mke wa rais.
Lakini je Janeatte Nyiramongi Kagame, ni nani hasa? na amekuwa na mchango gani katika mafanikio yanayotajwa kumuhusu Rais Kagame ?
Kabla ya kuwa mke wa Rais
Bi Jeanette Nyiramongi Kagame alizaliwa ukimbizini katika nchi jirani na Rwanda ya Burundi tarehe 10 Agosti, 1962.
Wazazi wake walikuwa wakimbizi kufuatia machafuko ya kikabila yaliyoikumba Rwanda.
Alizaliwa kipindi kifupi baada ya Rwanda kupata uhuru wake kutoka kwa ukoloni wa Kibelgiji.
Elimu yake ya msingi na sekondari aliipata nchini Burundi, ambako alisomea katika shule ya sekondari ya St Albert na baadaye aliendelea na masomo yake Nairobi, Kenya ambako wazazi wake walikuwa wanaishi kama wakimbizi.
Alivyokutanana na kuoana na Bw Paul Kagame
Akiwa mjini Nairobi nchini Kenya alikoishi na wazazi wake, Bi Jeanette Nyiramongi alikutana na Bw Paul Kagame wakachumbiana na baadaye kuoana na ndipo alipoanza kuitwa Jeannette Kagame.

Chanzo cha picha, Jeanette Kagame
Harusi yao ya kufana ilifanyika nchini Uganda, ambako pia mume wake Bw Paul Kagame alikuwa akiishi kama mkimbizi, lakini wakati huo akiwa mwanajeshi katika jeshi la Uganda.
Baada ya kuoana Bi Jeanette Kagame alikabiliwa na jukumu la kuwa mke wa mwanajeshi Paul Kagame ambaye baadaye miaka ya 90 alijiunga na mapambano ya vita vya waasi wa RPF vilivyolenga kulikomboa taifa la Rwanda na kuwarejesha nyumbani Wanyarwanda waliokuwa ukimbizini, vita ambavyo aliviongoza mumewe Paul Kagame, baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa kundi la RPF Fred Rwigema.
Mwaka 1994, majeshi ya RPF yalipata ushindi na Bi Jeanette Kagame alirudi Rwanda pamoja na familia yake, kushirikiana na mumewe kulijenga taifa lililokuwa limesabaratishwa vibaya kwa vita na mauaji ya kimbari.
Watoto
Bi Jeanette Kagame na mumewe Paul Kagame wamejaliwa watoto wanne, wa kiume watatu na wa kike mmoja, wa kwanza akiwa ni Yvan Cyomoro Kagame, wa pili Ange Ingabire Kagame, wa tatu Ian Kagame na kitinda mimba akiitwa Brian Kagame. Ana mjukuu mmoja.

Chanzo cha picha, Ange Kagame/Twitter
Mara baada ya kurejea nchini Rwanda kutoka ukimbizini , mke wa rais wa Rwanda, Bi. Jeannette Kagame alijitokeza kama mtu aliyejitolea kuinua maisha ya Wanyarwanda wenye matatizo mbalimbali ya kijamii, hususan maisha ya wajane, mayatima wa mauaji ya kimbari na familia zisizojiweza.
Tarehe 28 Februari 1996 aliunda Shirika la (Unity Club) ambalo lengo lake limekuwa ni kuwaleta pamoja mawaziri na wabunge wanawake na wake wa mawaziri kwa lengo la kuboresha umoja na amani huku wakichangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kufuatia mauaji ya kimbari na sasa shirika hilo lina wajumbe zaidi ya 270 likiwajumuisha viongozi wanaume.
Jeannete Kagame kama mke wa rais
Kuanzia tarehe 24 Machi, 2000, Jeannette Kagame alitambulilika rasmi kama Mke wa rais, baada ya mumewe Paul Kagame kuwa rais nne wa Rwanda.
Mwaka 2002 alianzisha Wakfu wa Imbuto Foundation, ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kutoa usaidizi wa elimu kwa watoto hususan wa kike wanaotoka katika familia masikini.
Imbuto- neno linalomaanisha mbegu-na kwa muktadha wa wakfu huu, neno hili linamaanisha kuwa vijana wanapowezeshwa wanakuwa mithili ya mbegu bora ambayo baadaye italeta matunda mema na ya faida kwa taifa.

Chanzo cha picha, Imbuto Foundation
Kupitia kazi zake Wakfu huu umewasaidia vijana wa kike na wa kiume zaidi ya 7,000 wanaosoma masomo ya sekondari kwa kuwapatia vifaa vya shule, bima ya matibabu, na muhimu zaidi ada ya shule.
Kupitia kazi zake, Wakfu wa Imbuto umekuwa ukibuni ushirika na watu na taasisi kitaifa na kimataifa ili kuendeleza shughuli zake katika jamii za Wanyarwanda.
Katika Wakfu wa Imbuto wasichana na wavulana wanafunzwa juu ya kuweka akiba, nidhamu, na kujiamini, na hufundishwa pia juu ya afya ya uzazi na uongozi.
Wakfu wa Imbuto, huwaandaa vyema kwa kuwajengea uwezo kielimu wasichana wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuwa watu bora siku zijazo kwa kuwapatia msaada wa kielimu ambapo wasichana wanaofanya vyema kielimu huzawadiwa zawadi na wengine kulipiwa ada za masomo ndani na nje ya nchi.
Kwa sasa zaidi ya asilimia 60 ya Wabunge wa Rwanda ni wanawake, na Mke huyu wa rais wa Rwanda ameonyesha mchango mkubwa katika kufanikisha hili.
Kupitia wakfu huo mafunzo ya umoja, maridhiano na uzalendo yamekuwa yakitolewa.
Kutokana na shughuli za Wakfu huo Bi Jeanette Kagame amewavutia wanawake hasa wa maeneo ya mashinani, ambao wamenufaika- hali ambayo pia imeufanya utawala wa mume wake Rais Kagame kupendwa na wanawake.
Wakfu wa Imbuto Foundation umekwenda sambamba na ajenda ya uongozi wa Rais Paul Kagame ya kuwajengea uwezo wanawake na kuwawezesha kushikilia nafasi katika ngazi zinazofanya maamuzi.
Miongoni mwa mafanikio mengine yaliyoafikiwa na Wakfu wa Imbuto ni kufanikisha vita dhidi ya Ukimwi ikiwa ni pamoja na utoaji elimu na taarifa za kuzuia maambukizi ya HIV uliofikiwa kwa kiwango cha 92.4% katika maeneo yaliyofanyiwa utafiti, kulingana na wavuti wa wakfu huo.
Amekuwa na mchango upi Kimataifa?
Licha ya kuwa Mke wa rais, Bi Jeanette Kagame amejitokeza binafsi kama kiongozi mwenye uwezo wa kuwaunganisha watu katika kutekeleza ajenda za kimataifa.

Chanzo cha picha, Jeanette Kagame
Mwaka 2001 aliandaa kikao cha wake wa marais wa Afrika kujadili jinsi ya kuwalinda watoto na maambukizi ya HIV/Ukimwi 2001 mjini Kigali.
Na baadaye mwaka 2002 Bi Jeanette Kagame alikuwa muasisi mwenza wa Shirika la wake wa marais wa Afrika la kupambana na HIV na Ukimwi mwaka 2002, ambalo limekuwa likisaidia katika kuzuia, maambukizi ya mtoto kutoka kwa mama.
Shirika hilo pia limekuwa likisaidia katika upatikanaji wa chanjo ya wasichana dhidi saratani ya mfuko wa uzazi barani Afrika . Na kutokana na jitihada zake Rwanda imeweza kuwachanja wasichana chanjo ya saratani - HPV.

Chanzo cha picha, Jeanette kagame
Bi. Kagame pia ni mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa mashirika mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Muungano wa dunia wa wanawake wanaopambana na HIV/Ukimwi (Global Coalition of Women against HIV/AIDS) pamoja na Bodi ya marafiki wa mfuko wa dunia wa Afrika( Friends of the Global Fund Africa)
Mwaka 2007, Shirika la afya duniani (WHO) lilimteua kuwa mwakilishi wa ngazi ya juu wa mpango wa chanjo ya ukimwi barani Afrika (AAVP), kuhakikisha wadau wa Afrika wanashirikiana kikamilifu katika maeneo ya utafiti wa chanjo ya HIV na Ukimwi na maendeleo.
Mwaka 2010, Bi. Kagame alipokea Shahada ya heshima ya sheria ya Chuo Kikuu cha Kikristo Oklahoma kwa mchango wake katika mapambano dhidi ya HIV/Ukimwi na umasikini. Na katika mwaka huo, aliteuliwa kama Mwakilishi maalum wa lishe ya mtoto na Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP).
Unawezaje kufanya shughuli zote hizi?
Akizungumza na jarida la Forbes kuhusu ni vipi anaweza kuhimili shinikizo la kuongoza taasisi mbalimbali , na wakati huo huo kuwa Mke wa Rais, na kuwa mama wa familia, Jeanette Kagame alijibu:
''Ili uwe na mfano wa usawa na maisha ya starehe, inabidi mtu aishi katika dunia ambayo inawajali watu wake…kwahiyo siwezi kujihisi mkamilifu kama sikuhusika katika majukumu yote hayo…''
Aidha alipoulizwa kuhusu anavyomsaidia mumewe kufanya kazi yake Bi Jeanette alisema: ''Huwa ninamuangalia wakati wote na kujaribu kuelewa maono yake , na kuyafanya rahisi kama yalivyo kwa ajili yake ili aweze kuchukua hatua. ''
Unaweza pia kusoma
Haiba na muonekano

Chanzo cha picha, FirstLadyRwanda/Twitter
Wanaofanya kazi karibu naye, wanamuelezea Jeanette Kagame kama mwanamke mchangamfu, mcheshi, anayesilikiza na kuyajali maoni ya walio karibu naye, lakini pia mwenye haiba ya juu hususan inapokuja katika utekelezaji wa malengo na ajenda zake:
''Anasikiliza kwa kweli na anatoa fursa kwa kila mtu kuchangia mawazo na katika mikutano yake ana ucheshi, lakini yote katika muktadha wa kazi na kwasababu yeye ni mchapakazi, inatubidi sisi pia kuwa wachapa kazi na ni mtu anayetoa mazingira mazuri ya kazi kwa wafanyakazi wake'', aliiambia makala hii mmoja wa watu waliofanya kazi naye katika ofisi ya Mke wa rais.

Chanzo cha picha, Imbuto Foundation
Kwa wanawake wa maeneo ya mashinani, Bi Jeanette Kagame anafahamika kama ''umubyeyi'', mama mwenye maono, anayepigania hali bora za maisha ya wanawake na wasichana na mwingi wa huruma.
Mara nyingi ameonekana hadharani akitokwa machozi kwa huzuni hasa anapotembelea na kutoa usaidizi kwa familia za wanawake wenye matatizo mbali mbali, na wajane wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambao baadhi yao wanaishi peke yao.

Chanzo cha picha, Jeanetter Kagame Foundation
Kwa wanawake wasomi, Bi Jeanette Kagame ni mama ambaye ni mfano wa kuigwa kutokana na bidii katika kazi anazozifanya na kutekeleza maono yake.
''Mimi ni mfanyakazi wa serikali, lakini kulingana na ninavyomuona Mke wa rais anavyofanya kazi kulijenga taifa letu, inanifanya nihisi kuwa na msukumo na wakati wote kuongeza bidii kazini'', anasema Aline Mbabazi mkazi wa Kigali na kuongeza kuwa '' Kama mwanamke kwa kweli najivunia kuwa na mama wa taifa kama Jeanette Kagame, kila mara anapozungumza anatutia sisi moyo wanawake na wasichana kwamba tunaweza kujikwamua kimaisha na vile vile tumeona jinsi anavyosaidia kimasomo hasa watoto kutoka familia masikini...ni mfano wa kuigwa''
Mitindo yenye mvuto

Chanzo cha picha, Jeanette Kagame
Muonekano wa umekuwa na mvuto kwa baadhi ya wanawake nchini Rwanda, wengi wakimsifu kwa haiba yake ya utulivu na mitindo ya kawaida ya mavazi.
Sawa na Bi Margret Kenyatta mke wa Rais wa Kenya, Bi Jeanette Kagame pia amekuwa akivaa baadhi ya mitindo iliyobuniwa na wabunifu wa mavazi wa Rwanda, hususan mavazi yake ya vitenge na suti.
''Ni mama ambaye mitindo yake inanivutia sana…anajua kuvaa kulingana na matukio, mtindo wake wa mavazi ni rahisi na ningependa sana kuvaa kama yeye baada ya kumaliza shule nikipata kazi'', anasema Mwanafunzi wa Chuo Kikuu mjini Kigali Louise Kagwesage Kanimba mkazi wa Kigali.
''Najivunia kuwa na ''mama'' yetu anayependeza kwa kuvaa mavazi ya heshima, anawakilisha muonekano wa mavazi ya akinamama wa Rwanda kimataifa'', anasema Havugimana Nzabandora , mkazi wa Ruhengeri kaskazini mwa Rwanda.

Chanzo cha picha, Invaho nshya

Chanzo cha picha, Paul Kagame/twitter

Chanzo cha picha, RwandFirstLady/Twitter
Licha ya kuwa mke wa rais, Bi Jeanette Kagame ambaye ni msomi mwenye Shahada ya Biashara na Sayansi ya utawala, ameonekana binafsi kuwa kiongozi na wengi wanamuona kama mwanamke aliyechangia kwa namna moja au nyingine katika mafanikio ya uongozi wa mume wake Rais Paul Kagame, hususan katika maendeleo ya wanawake na wasichana, pamoja na afya. Na ushawishi wake unaendelea kuongezeka.












