Wafahamu marais wa Afrika walioshindwa uchaguzi baada ya muhula mmoja

.

Chanzo cha picha, BBC NEWS

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili

Siasa za uchaguzi barani Afrika mara nyingi zimekuwa zikihusishwa na malalamiko ya uonevu na wizi wa kura. Si ajabu pia kusikia wapinzani wanasusia uchaguzi kwa kigezo cha kuminywa kwa demokrasia.

Lakini si mara zote hali huwa hivyo, japo ni kwa uchache, mara kadhaa imeshuhudiwa barani humo wagombea kutoka vyama vya upinzani (ama muungano wa vyama vya upinzani) wakifanikiwa kuangusha chama tawala madarakani.

Katika baadhi ya uchaguzi, wapinzani wamefanikiwa kuwang’oa madarakani baadhi ya viongozi ambao wamehudumu kwa muda mrefu. Mwaka 2017 Rais Yahya Jammeh wa Gambia ambaye utawala wake wa miaka 20 ulikithiri shutuma za ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo kuminya demokrasia na siasa za upinzani aliangushwa ghafla katika uchaguzi na mpinzani Adama Barrow.

Lakini pia kuna mifano mingine ambapo rais aliye madarakani anashindwa kutetea nafasi yake baada ya kuhudumu kwa muhula mmoja tu. Wafuatao ni baadhi ya marais wa Afrika ambao wamehudumu kwa muhula mmoja na kushindwa uchaguzi wakiwa madarakani katika miaka ya hivi karibuni:

George Weah- Liberia

.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Rais wa Liberia George Weah ndio mfano wa hivi karibuni zaidi. Amekubali kushindwa jana Ijumaa Novemba 17, 2023 na kumpongeza mpinzani wake Joseph Bokai kwa kuibuka na ushindi.

Alikuwa anagombea kuchaguliwa kwa muhula wa pili wa miaka mitano, lakini sasa mshambuliaji huyo nyota wa zamani Liberia anaonekana kujifunga goli mwenyewe kwa kushindwa kufikia matarajio ya raia wa nchi hiyo.

Katika kampeni ya uchaguzi huu alikuwa akiahadi kuboresha elimu, ajira na kukabiliana na ufisadi huku mpinzani wake mkuu Joseph Boakai akiahidi kuinusuru Liberia kutoka kwa uongozi mbovu na usimamizi mbaya wa raslimali za nchi unaofanywa na Weah.

Rais Weah amekuwa madarakani tangu 2018 baada ya kumshinda Bokai mwaka 2017. Ataondoka uongozini mwezi Januari mwakani.

Uchaguzi huu ulikuwa wa kwanza tangu kuondoka kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliotumwa baada ya kumalizika rasmi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003.

Weah ni mwanasoka wa kimataifa wa zamani aliyecheza kwenye klabu za soka za juu barani Ulaya kama Paris St-Germain (PSG) na AC Milan, kabla ya kumalizia safari yake nchini Uingereza kwa kuchezea kwa muda mfupi klabu za Chelsea na Manchester City.

Ni Mwafrika pekee aliyewahi kushinda tuzo ya Fifa ya mchezaji bora duniani ya na tuzo ya Ballon D'Or, zote mwaka 1995.

Alijitosa katika ulingo wa siasa baada ya kustaafu kucheza soka mwaka 2002.

Edgar Lungu- Zambia

Edgar Lungu

Chanzo cha picha, AFP

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Edgar Lungu alitangaza kustaafu siasa 2021 baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu na rais wa sasa wa Zambia Hakainde Hichilema.

Upinzani baina ya Lungu na Hichilema ulianza mwaka 2015 katika uchaguzi mdogo wa urais baada ya rais Michael Satta kufariki madarakani Oktoba 2014. Lungu akamgaragaza Hichilema kwa mara ya kwanza. Lungu akahudumu kutoka Januari 2015 mpaka Agosti 2016, kipindi ambacho kikatiba kikahesabika kama kumalizia awamu ya Satta.

Lungu na Hichilema wakakutana kwa mara ya pili kwenye kinyang’anyiro cha urais Agosti 2016 na Lungu akashinda kwa mara ya pili akiwa na 50% dhidi ya 47% za Hichilema, lakini kikatiba ikahesabaka kama ushindi wa muhula wake wa kwanza madarakani mpaka mwaka 2021.

Hata hivyo kipindi chake cha uongozi kilighubikwa na mdororo wa kiuchumi na kuliacha taifa hilo katika deni kubwa. Pia akiwa madarakani alishutumiwa kwa kuwaminya upinzania hasa bwana Hichilema.

Katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2021 kikawakutanisha tena Lungu na Hichilema kwa mara ya tatu lakini safari hii Hichilema alinyakuwa madaraka kwa kupata 59% ya kura dhidi ya 38.7% za Lungu.

Tangu Lungu aondolewe mamlakani miaka miwili iliyopita, amekuwa akibanwa mbavu na serikali ya Hichilema, kwa kile yeye mwenyewe anachodai kuwa ni sababu za kisiasa.

Mapema mwezi huu serikali ya Zambia ilimuondolea marupurupu ya kustaafu na mafao mengine rais huyo wa zamani kufuatia uamuzi wake wa kurejea katika siasa.

Inatazamiwa atamenyana tena na Rais Hichilema katika uchaguzi mkuu wa 2026. Endapo Lungu atashinda, atamuingiza Hichilema katika safu hii ya marais waliohudumu kwa muhula mmoja na kushindwa uchaguzi wakiwa mamlakani. Na hilo wala halitakuwa jambo la kustaajabisha ikizingatiwa historia ya kisiasa ya Zambia na uwezekano wa upinzani kutwaa madaraka.

Peter Mutharika & Joyce Banda – Malawi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Peter Mutharika aliingia madarakani mwaka 2014 baada ya kumshinda rais Joyce Banda ambaye alidumu madarakani kwa miaka miwili tu.

Upinzani baina ya Bi Banda na Peter Mutharika ulianza kabla ya wote wawili kupata urais. Vita baina yao ilianza katika awamu ya pili ya hayati Bingu wa Mutharika ambaye akiwa rais, Bi. Banda alikuwa makamu wake. Bingu na Peter ni ndugu wa damu.

Kabla kufikwa na umauti, Bingu alijaribu kila namna kumng’oa Bi Banda kwenye umakamu ili nduguye amrithi akitoka madarakani. Hatua hizo ziligonga mwamba mahakamani na Bi. Banda licha ya kutimuliwa katika chama tawala alibaki kwenye nafasi yake na kuanzisha chama chake cha siasa.

Joyce Banda

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Joyce Banda alikuwa rais wa kwanza mwanamke wa Malawi - na wa pili barani Afrika

Rais Bingu alipofariki mwaka 2012 Bi Banda akaapishwa kuwa rais kwa mujibu wa katiba na kumalizia muhula mpaka mwaka 2014.

Uchaguzi mkuu ukafanyika mwaka 2014, na hapo Bi Banda na Peter Mutharika wakakutana rasmi kwenye kinyang’anyiro cha urais. Mutharika alimng’oa Bi Banda madarakani kwa ushindi wa 36.4% ya kura. Nafasi ya pili ikienda kwa Lazarus Chakwera akipata 27.8% ya kura huku Bi Banda akichukua nafasi ya tatu kwa kupata 20.2%.

Mutharika aliongoza Malawi baada ya ushindi huo mpaka mwaka 2019 ambapo ulifanyika uchaguzi mkuu. Katika uchaguzi huo Mutharika alishinda kwa 38% dhidi ya 35% za Lazarus Chakwera. Hata hivyo matokeo hayo yalipingwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa kura na hatimaye ushindi huo kufutwa.

Katika uchaguzi wa marudio wa 2020, wapinzani walilinganisha nguvu na kumng’oa madarakani. Chakwera akapata ushindi wa 59.4% dhidi ya 39.9% za Mutharika.

John Mahama – Ghana

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kama ilivyokuwa kwa Bi Banda wa Malawi, John Mahama alikwea urais wa Ghana mwaka 2012 (mwezi Juni) moja kwa moja akitokea kwenye umakamu baada ya kifo cha rais John Atta Mills.

Tofauti na Bi Banda, Mahama alifanikiwa kutetea nafasi ya urais kwa kuingia madarakani kwa muhula wa kwanza kupitia uchaguzi uliofanyika Disemba 2012 kwa kumshinda mpinzani wake Nana Akufo-Addo kwa ushindi mwembamba wa asilimia 50 dhidi ya 47.

Mahama ameweka historia ya kuwa rais wa kwanza wa Ghana kuzaliwa baada ya taifa hilo kupata uhuru na pia kuwa mwanasiasa aliyehudumu ngazi zote mpaka kufikia urais.

Hata hivyo rekodi hizo hazikufua dafu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016. Kinyang’anyiro kwa mara ya pili kilikuwa baina ya Mahama na Akufo-Addo, safari hii ushindi ukienda kwa upinzani. Akufo-Addo akipata 53.7% dhidi ya 44.5% za Mahama.

Vita vya kisiasa baina ya wawili hao havikuishia hapo. Katika uchaguzi wa 2020 walikutana tena kwa mara ya tatu. Akufo-Addo akafanikiwa kulinda urais wake dhidi ya mahama kwa ushindi wa 51.30% dhidi ya 47.3%.

Goodluck Jonathan

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan

Goodluck Jonathan- Nigeria

Ingawa ndoto yake ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili haikutimia uchaguzi wa Machi 2015, Goodluck Jonathan wa Nigeria alipanda kwa kasi katika ngazi ya siasa za nchi hiyo.

Hadi Novemba 2009, alikuwa akihudumu kama makamu wa rais kutoka kusini mwa nchi chini ya rais wa kutoka kaskazini Umaru Yar'Adua.

Lakini rais Yar'Adua alipougua na kupelekwa hospitalini nchini Saudi Arabia na hakuonekana tena hadharani hadi alipofariki tarehe 5 Mei 2010.

Baada ya miezi kadhaa ya malumbano ya kisiasa, vigogo wa siasa za Nigeria hatimaye walimkubali kama kaimu kiongozi mwezi Februari 2010 wakati rais huyo mgonjwa aliporejea nyumbani, lakini hakuweza kutekeleza majukumu yake.

Mnamo 2011, Jonathan alishinda uchaguzi wake wa kwanza - wa urais - licha ya madai ya upinzani kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

Hata hivyo baada ya kuhudumu kwa muhula mmoja madarakani Jonathan alishindwa katika uchaguzi wa urais wa 2015 na mkuu wa zamani wa jeshi Jenerali Muhammadu Buhari.

Jonathan alikuwa rais wa kwanza aliye madarakani katika historia ya Nigeria kukubali kushindwa katika uchaguzi.

Imeandikwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Athuman Mtulya