Hakainde Hichilema: 'Mchunga ng'ombe' aliyeibuka kuwa rais wa Zambia

Chanzo cha picha, Reuters
Ilikuwa kujaribu bahati ya mara ya sita kwa Hakainde Hichilema, ambaye hatimaye amekuwa rais wa Zambia baada ya majaribio matano yasiyofanikiwa.
Bwana Hichilema alimshinda mpinzani wake mkuu, Rais anayemaliza muda wake Edgar Lungu, kwa zaidi ya kura milioni.
Lakini rais mpya ni nani? Na kwa nini amefanikiwa baada ya miaka ya kutofaulu?

Bwana Hichilema, 59, amejielezea kama "kijana wa kawaida", ambaye alichunga mifugo ya familia yake katika ujana wake kabla ya kuwa mmoja wa watu tajiri zaidi nchini Zambia.
Rais mteule na kiongozi wa United Party for National Development (UPND) anajulikana sana kama HH. Alizaliwa katika maisha ya hali ya kawaida kabla ya kufanikiwa kupata udhamini kwa Chuo Kikuu cha Zambia, na baadaye alihitimu shahada ya uzamili ya uongozi wa biashara, MBA kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham nchini Uingereza.
Aliendelea kupata utajiri wa fedha, mali, ufugaji, utunzaji mifugo, afya na utalii.
Ametumia nyanja zote mbili za historia yake kuomba kura kwa wapiga kura.
Aliwaambia wapiga kura kwamba wanahitaji mfanyabiashara aliyefanikiwa kuelewa jinsi ya kupata uchumi katika taifa lenye utajiri wa shaba, ambapo kuna ukosefu mkubwa wa ajira. Alitumia pia mizizi yake ya kilimo kuwavutia wakulima wa nchi hiyo, akisema anaweza kugeuza Zambia kuwa kikapu cha kikanda.
Lakini ilikuwa uwezo wa Bw Hichilema kuungana na wapiga kura wachanga ambao labda ndio sababu kubwa katika mafanikio yake. Zaidi ya nusu ya wapiga kura milioni saba waliojiandikisha nchini Zambia wako chini ya umri wa miaka 35. Karibu mmoja kati ya watano kati yao hawana kazi.

Chanzo cha picha, EPA
Chama cha Patriotic Front (PF) kiliingia madarakani mnamo 2011 kwa ahadi ya "ushuru mdogo, pesa zaidi katika mifuko ya watu na ajira zaidi". Lakini hii haikutokea kwa vijana wengi na walijitokeza kwa mamilioni yao kwa Bwana Hichilema.
Njia moja aliyojiunga na vijana ilikuwa kupitia mitandao ya kijamii. Huu haukuwa uchaguzi wa kwanza ambao Bwana Hichilema alijaribu kutumia 'likes' za Facebook na Twitter kuungana na wapiga kura, lakini hivi karibuni ameongeza ushawishi wake.
Amekuwa tayari pia kucheza mchezo mchafu.
Mwaka jana alitoa video inayoitwa "Hadithi ya wataalamu wawili ...", ambayo ilimwonyesha Bwana Hichilema kama mfanyabiashara mjanja na anayewajibika, na Bw Lungu kama mtu ambaye alitumia pesa zake zote katika baa na vilabu vya usiku. "Ni yupi kati ya hawa wawili aliye nadhifu?" video iliuliza.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Bwana Hichilema mara nyingi alikuwa akitoa maoni yanayozunguka kwenye mitandao ya kijamii mbali na siasa, hasa mpira wa miguu - njia ya uhakika ya kuungana na wapiga kura. Wakati mwingine alikuwa akiwadharau mashabiki wa Manchester United na Arsenal timu yao ilipoteza.
Pia aliwapongeza wachezaji wa Zambia ambao walipata pesa nyingi kwenda Uropa, pamoja na Patson Daka, ambaye hivi karibuni alijiunga na Leicester City, na Fashion Sakala, aliyesaini kwa mabingwa wa Scotland Rangers. Alitoa maoni juu ya michezo yao ya kirafiki ya kabla ya msimu, akionekana kuonesha nia ya kweli katika kazi zao. Bwana Lungu alijaribu mbinu kama hizo, lakini wengi waliona kuwa alilazimisha.
Bwana Hichilema mara nyingi alikuwa akitumia misimu kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na neno "bally", njia isiyo rasmi ya kumuita mtu kama baba yako. Hashtags kama #BallyWillFixIt ilitumiwa katika juhudi za kuzungumza lugha ya watu katika masoko na vilabu vya pombe, sio tu wasomi wa biashara.
Ilionekana kufanya kazi.
Maelfu ya wafuasi wa Bwana Hichilema walimiminika katika mitaa ya Lusaka baada ya ushindi wake, wakiimba "twende Bally".Bwana Hichilema ameonyesha uthabiti na ukakamavu katika taaluma yake ya kisiasa.
Pamoja na kushindwa katika uchaguzi mara tano, mara nyingi huwakumbusha watu kwamba amekamatwa mara 15 tangu aingie kwenye ulingo wa siasa.
Mnamo mwaka wa 2016, alishtakiwa kwa makosa ya uhaini kwa madai ya kutotoa nafasi kwa msafara wa rais uliokuwa unapita.
Alikaa miezi minne jela kabla ya kufutiwa mashtaka.
Katika hotuba yake ya kukubali, Rais mteule Hichilema aliashiria maridhiano na amani kwa mtangulizi wake.
"Usijali, utakuwa sawa, hautakabiliwa na adhabu au kutoa machozi", alisema Bw. Hichilema, ambaye mara nyingi alishambuliwa kwa kile alichosema ni majaribio ya kumnyamazisha na kumtisha kama kiongozi wa upinzani.
Na hatimaye baada ya kupata kazi hiyo ya nafasi ya juu zaidi, Bwana Hichilema bila shaka atakuwa anasherehekea.
Lakini rais mteule mpya atahitajika kuanza kufanya kazi mara moja katika nchi inayokabiliwa na matatizo mengi.
Pamoja na ukosefu mkubwa wa ajira, gharama ya maisha pia imeongezeka kwa haraka sana.
Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, Zambia ilitumbukia kwenye mgogoro wa kiuchumi mwaka jana wakati janga la Covid-19 likienea ulimwenguni kote.
Kwa pesa ambayo nchi inadaiwa na wakopeshaji wa kigeni, inakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 12 (£ 8.6bn).
Hii inamaanisha kuwa serikali inaishia kutumia angalau asilimia 30 ya mapato yake kwa malipo ya riba, kulingana na kampuni ya makadirio ya mkopo ya S&P Global.
Mwaka jana, Zambia ilikosa ulipaji wa riba, na kuifanya kuwa nchi ya kwanza ya Kiafrika kukosa kulipa mkopo wakati wa janga hilo.
Pia inakabiliwa na ugumu wa kulipa mikopo mingine.
Wimbi la umaarufu wa Bwana Hichilema litapungua ikiwa hawezi kuanza kurekebisha shida hizi, kwa haraka.












