Mfumo wa siri unaotumiwa na Hamas kulipa mishahara ya watumishi wa serikali

Chanzo cha picha, EPA
Baada ya takriban miaka miwili ya vita, uwezo wa kijeshi wa Hamas umedhoofika sana huku uongozi wake wa kisiasa ukiwa chini ya shinikizo kubwa.
Hata hivyo, katika muda wote wa vita Hamas imefanikiwa kuendelea kutumia mfumo wa malipo wa siri wa pesa taslimu kulipa mishahara ya watumishi wa umma 30,000 ya jumla ya $7m (£5.3m).
BBC imezungumza na wafanyakazi watatu wa umma ambao wamethibitisha kupokea karibu dola 300 kila mmoja ndani ya wiki iliyopita.
Inaaminika wao ni miongoni mwa makumi ya maelfu ya wafanyakazi ambao wameendelea kupokea kiwango cha zaidi ya 20% ya mishahara yao ya kabla ya vita kila baada ya wiki 10.
Huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei, mshahara huo unasababisha kuongezeka kwa chuki kati ya waaminifu wa kundi hilo.
Kumekuwa na uhaba mkubwa wa chakula ambao mashirika ya misaada ya kibinadamu yanalaumu vikwazo vya Israel na kusababisha kuongezeka kwa visa vya utapiamlo huko Gaza, ambapo kilo moja ya unga katika wiki za hivi karibuni imegharimu kama dola 80 - ambayo ni bei ya juu sana.
Kwa kuwa hakuna mfumo wa benki unaofanya kazi huko Gaza, hata kupokea mshahara ni mchakato mgumu na wakati mwingine ni hatari.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Israel mara kwa mara huwatambua na kuwalenga maafisa wa Hamas waowapa maafisa wa serikali mishahara, ikitaka kuvuruga uwezo wa kundi hilo kutawala.
Kuanzia wafanyikazi, polisi hadi maafisa wa ushuru, mara nyingi hupokea ujumbe uliosimbwa kwa njia fiche kwenye simu zao wenyewe au za wenzi wao unaowaelekeza kwenda mahali maalum kwa wakati maalum "kukutana na rafiki kwa ajili ya kunywa kikombe cha chai".
Katika eneo wanapokutana, mwanamume au mara chache sana anakuwa mwanamke – huja kwa mfanyakazi aliyekuja kunywa chai - ambaye hukabidhi kwa busara bahasha yenye pesa kabla ya kutoweka bila kuwa na mazungumzo zaidi.
Mfanyakazi katika Wizara ya Masuala ya Kidini ya Hamas, ambaye hataki kutaja jina lake kwa sababu za kiusalama, alielezea hatari iliyopo wakati wa kupokea mshahara.
"Kila nikienda kuchukua mshahara huwa namuaga mke na watoto wangu, ninajua kuwa huenda nisirudi tena," alisema. "Mara kadhaa, mashambulizi ya Israel yametokea katika sehemu za kupokea mishahara. Nilinusurika shambulio moja kwenye soko lililokuwa na shughuli nyingi katika jiji la Gaza."
Alaa, ambaye jina lake tumelibadilisha ili kulinda utambulisho wake, ni mwalimu wa shule aliyeajiriwa na serikali inayoongozwa na Hamas na mlezi pekee wa familia ya watu sita.
"Nilipokea shekeli 1,000 (kama dola 300) za noti zilizochakaa - hakuna mfanyabiashara ambaye anaweza kuzikubali. Ni shekeli 200 pekee ndizo zilizotumika - zilizosalia, sijui nizifanyie nini," aliiambia BBC.
"Baada ya miezi miwili na nusu ya njaa, wanatulipa pesa taslimu zilizochanika.
"Mara nyingi nalazimika kwenda kwenye vituo vya usambazaji wa misaada kwa matumaini ya kupata unga wa kulisha watoto wangu. Wakati mwingine nafanikiwa kuleta nyumbani kidogo, lakini mara nyingi sipati kitu."
Mnamo mwezi Machi wanajeshi wa Israel walisema wamemuua mkuu wa masuala ya fedha wa Hamas, Ismail Barhoum, katika shambulizi lililotokea kwenye hospitali ya Nasser huko Khan Younis ambaye walimshutumu kwa kupeleka pesa katika tawi la kijeshi la Hamas.
Bado haijafahamika jinsi Hamas imeweza kuendelea kulipa mishahara hasa ikizingatiwa kwamba kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu yake ya kiutawala na kifedha.
Mfanyakazi mmoja mkuu wa Hamas, ambaye alihudumu katika nyadhifa za juu na anafahamu shughuli za kifedha za Hamas, aliiambia BBC kwamba kundi hilo lilikuwa limekusanya takriban $700m pesa taslimu na mamia ya mamilioni ya shekeli chini ya mahandaki kabla ya shambulio baya ililotekeleza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023 kusini mwa Israel, ambalo lilisababisha kampeni mbaya ya kijeshi ya Israel.
Haya yalidaiwa kusimamiwa moja kwa moja na kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar na kaka yake Mohammed - ambao wote wameuawa na vikosi vya Israel.
Wafuasi wa Hamas wakasirishwa na malipo
Hamas kihistoria imekuwa ikitegemea ufadhili kutoka kwa ushuru mkubwa wa bidhaa na ushuru unaotozwa kwa wakazi wa Gaza, pamoja na kupokea msaada wa mamilioni ya dola kutoka Qatar.
Vikosi vya Qassam, tawi la kijeshi la Hamas ambalo linaendesha shughuli zake kupitia mfumo tofauti wa kifedha, unafadhiliwa zaidi na Iran.
Afisa mkuu wa chama kilichopigwa marufuku cha Muslim Brotherhood chenye makao yake nchini Misri, mojawapo ya mashirika ya Kiislamu yenye ushawishi mkubwa duniani, amesema karibu asilimia 10 ya bajeti yao pia ilielekezwa kwa Hamas.
Ili kupata mapato wakati wa vita, Hamas pia imeendelea kutoza ushuru wafanyabiashara na imeuza kiasi kikubwa cha sigara kwa bei iliyoongezwa hadi mara 100 ya gharama yake halisi. Kabla ya vita, kiboksi cha sigara 20 kiligharimu dola 5 – lakini sasa hivi kimepanda hadi zaidi ya $170.
Mbali na malipo ya pesa taslimu, Hamas imesambaza vifurushi vya chakula kwa wanachama wake na familia zao kupitia kamati za dharura za eneo ambazo uongozi wao hubadilishwa mara kwa mara kutokana na mashambulizi ya kila wakati ya Israel.
Hilo limechochea hasira miongoni mwa umma, huku wakazi wengi wa Gaza wakiishutumu Hamas kwa kusambaza misaada kwa wafuasi wake pekee na kuwatenga watu wengine.
Israel imeishutumu Hamas kwa kuiba misaada ambayo imeingia Gaza wakati wa usitishaji mapigano mapema mwaka huu, jambo ambalo Hamas imekanusha. Hata hivyo vyanzo vya BBC huko Gaza vimesema kuwa kiasi kikubwa cha misaada kilichukuliwa na Hamas wakati huu.
Nisreen Khaled, mjane aliyeachwa akiwalea watoto watatu baada ya mumewe kufariki kwa saratani miaka mitano iliyopita, aliambia BBC: "Njaa ilipozidi, watoto wangu walikuwa wakilia sio tu kutokana na maumivu bali pia kwa kuwatazama majirani zetu wanaoshirikiana na Hamas wakipokea vifurushi vya chakula na magunia ya unga.
"Je, wao sio sababu ya kuteseka kwetu? Kwa nini hawakuhakikisha wamepata chakula, maji na dawa kabla ya kuanzisha shambulizi lao tarehe 7 Oktoba?"
Imetafsiriwa na Asha Juma








