Simulizi ya baba wa Gaza ambaye mwanawe aliuawa katika shambulio la Israel akitafuta 'tama la maji'

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, David Gritten
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Jerusalem
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mahmoud Abdul Rahman Ahmed anasema mwanawe wakiume, Abdullah, alikuwa "akitafuta tama la maji" wakati alipochukuwa mitungi wa maji Jumapili asubuhi na kuelekea katika kituo cha usambazaji maji katika kambi ya wakimbizi za Nuseirat, katikati ya Gaza.
"Eneo hilo limefurika watu waliofushwa makwao, wengine wamechoshwa na vita, na wale amabo wamejionea mambo mabaya kutokana na kuzuiliwa mahali pamoja na mienendo yao kudhibitiwa kutokana na mzozo unaondelea Gaza," Mahmoud alisema katika mahojiano na mwandishi wa habari wa ndani anayefanyia kazi BBC.
"Watoto hao, miongoni mwa Abdullah, walipanga foleni wakiwa na njaa kupata walao tone la maji ya kunywa," aliongeza kusema.
"Dakika chache baada ya watoto na watu waliokabwa na kiua katika kambi hiyo kukusanyika, ndege za kivita zililiwashambulia watoto katika kituo hicho cha usambazaji maji bila kutoa ilani ya mapema."

Video iliyorekodiwa na mwandishi mwingine wa habari wa ndani na kuthibitishwa na BBC ilionyesha athari ya shambulio hilo la Israel katika barabara za kuelekea kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.
Anaishana na wanaume wawili waliowabeba watoto wadogo kabla ya kupata jengo lililoharibiwa, ambalo chini yake kuna makumi ya mitungi ya plastiki ya rangi ya manjano.
Wanawake wanapiga mayowe huku watu wa karibu wakimvuta mwanamume kutoka kwenye vifusi, huku wengine wakijaribu kumsaidia mwanamume mwingine aliyelowa damu. Watu wengine pamoja na watoto wanaonekana wakiwa wamelala chini bila ufahamu.
Hospitali ya Al-Awda huko Nuseirat ilisema watu 10, wakiwemo watoto sita, waliuawa katika shambulio hilo, na kwamba wengine 16 walijeruhiwa.
Kando na Abdullah, watoto waliofariki waliopoteza maisha ni Badr al-Din Qaraman, Siraj Khaled Ibrahim, Ibrahim Ashraf Abu Urayban, Karam Ashraf al-Ghussein na Lana Ashraf al-Ghussein.
Ilipoulizwa kuhusu shambulio hilo, jeshi la Israel lilisema lilimlenga "gaidi" wa Palestina wa Islamic Jihad lakini "kutokana na hitilafu ya kiufundi silaha hiyo ilianguka umbali wa mita kadhaa kutoka kwa lengo".
Jeshi lilisema "lina taarifa kuhusu watu waliojeruhiwa kutokana na shambulio hilo" na "linajutia madhara yaliyowafika raia ambao hawakuwa na hatia", na kuongeza: "Tukio hilo linachunguzwa."
Hata hivyo, Mahmoud alidai kuwa Israel "ilikusudia kuwasilisha ujumbe: haitaruhusu watu kuchota hata tone moja la maji ya kunywa."
Pia alisikitika kwamba ndoto za Abdullah na watoto wengine zilididimizwa.
"Walikuwa na matumaini kwamba siku moja hali yao itabadilika, ili na wao wajihisi kama watoto wengine ulimwenguni - kutekeleza jukumu lao la kawaida la kucheza, kusafiri, kula, kunywa, na kuishi kwa usalama," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Umoja wa Mataifa unasema uhaba wa maji katika Ukanda wa Gaza unazidi kuwa mbaya kutokana na ukosefu wa mafuta na vipuri kwa ajili ya kuondoa chumvi, pampu na vifaa vya usafi wa mazingira, pamoja na ukosefu wa usalama na kutofikika kutokana na operesheni za kijeshi za Israel dhidi ya Hamas na amri za wataka watu kuondoka eneo hilo.
Kutokana na hilo baadhi ya watu wanapokea chini ya kiwango cha dharura cha lita 15 kwa siku, kiasi ambacho Umoja wa Mataifa unakiita "mgogoro wa ukame unaosababishwa na binadamu".
"Unawaona watoto wakipanga foleni, kando ya barabara, wakiwa na mitungi kila asubuhi, wakisubiri lori la linalosambaza maji kila siku na wanapata maji lita tano hadi 10, yanayotumika kuosha, kusafisha, kupika, kunywa, nk," Sam Rose, kaimu mkurugenzi wa Gaza wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina (Unrwa), aliiambia BBC.
"Kila wakati mtu kuna mtu anayefariki kutokana na hali ngumu ya maisha. Lakini hii ni mojawapo ya sababu zingine nyingi," aliongeza.
Alhamisi iliyopita, watoto 10 na wanawake watatu waliuawa walipokuwa wakisubiri virutubisho vya lishe nje ya kliniki katika mji wa Deir al-Balah.
Jeshi la Israel lilisema lilikuwa likimlenga "gaidi" wa Hamas karibu na, kama ilivyokuwa tukio la Jumapili, lilisema kwamba linasikitika kuwaumiza raia katika operesheni hiyo.
"Tunazingatia matukio haya, lakini bila shaka hawa hawakuwa watoto pekee waliouawa huko Gaza [siku ya Jumapili]," Rose alisema. "Kila siku, tangu kuanza kwa vita, kwa wastani wa darasa lililojaa watoto wameuawa."
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (Unicef), Catherine Russell, wakati huo huo alitaja matukio yote mawili kuwa "ya kutisha" na kuzitaka mamlaka za Israel " kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu".

Baadaye wiki hii, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kujadili hali ya watoto huko Gaza, kufuatia ombi la Uingereza.
Hata hivyo, mwakilishi wa kudumu wa Israel Danny Danon alisema wajumbe wa baraza "wanatakiwa kuikemea Hamas kwa kurefusha mzozo huu".
"Watoto wa Gaza ni wahanga wa Hamas, sio Israel. Hamas inawatumia kama ngao za binadamu na UN iko kimya," alidai.
Mahmoud alisema ni Israel ambayo inapaswa kushinikizwa kumaliza vita.
"Hatuna nguvu. Sisi ni waathirika. Sisi ni raia kama watu wengine duniani, na hatumiliki silaha zozote za nyuklia au kitu chochote," aliongeza.
"Vita hivi vinahitaji kukomeshwa, na pia mauaji yanayoendelea kutokea katika Ukanda wa Gaza."
Imtafsiriwa na Ambia Hirsi












