Nini maana ya hati ya kukamatwa ya ICC kwa Hamas na Israel?

Chanzo cha picha, Reuters
Benjamin Netanyahu alijibu kwa hasira habari kwamba anaweza kukabiliwa na hati ya kukamatwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Ni uamuzi "mbaya na wa ajabu wa kihistoria", alisema. Israel imekuwa "ikiendesha vita vya haki dhidi ya Hamas, shirika la kigaidi la mauaji ya halaiki ambalo lilifanya shambulio baya zaidi kwa watu wa Kiyahudi tangu mauaji ya Holocaust."
Katika shambulio kali la kibinafsi, Bw Netanyahu alisema mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Karim Khan, ni mmoja wa "watu wanaopinga sheria za kisasa."
Netanyahu alisema Bw Khan, ni kama majaji katika Ujerumani ya enzi ya Nazi ambao waliwanyima Wayahudi haki za kimsingi na kuwezesha mauaji ya Holocaust.
Uamuzi wake wa kutafuta waranti wa kukamatwa kwa waziri mkuu na waziri wa ulinzi wa Israel "unamwaga petroliya hasira juu ya moto wa chuki dhidi ya Wayahudi ambayo imeshamiri duniani kote."
Bw Netanyahu alizungumza Kiingereza kwenye video hiyo ambayo ilitolewa na ofisi yake. Hufanya hivyo anapotaka ujumbe wake ufikie hadhira ya kigeni ambayo ni muhimu sana kwake, nchini Marekani.

Chanzo cha picha, LightRocket kupitia Getty Images
Hasira iliyoonyeshwa na waziri mkuu, na kuungwa mkono na uongozi wa kisiasa wa Israel, ilitokana na kurasa za lugha ya kisheria iliyochaguliwa kwa uangalifu katika taarifa iliyotolewa na Bw Khan, mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ambaye ni Wakili wa Mfalme wa Uingereza.
Neno kwa neno, mstari kwa mstari, zinaongeza hadi mfululizo mbaya wa tuhuma dhidi ya viongozi watatu mashuhuri wa Hamas pamoja na waziri mkuu na waziri wa ulinzi wa Israel.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Azimio la kutumia sheria za kimataifa na sheria za mizozo ya kivita kwa pande zote, haijalishi ni akina nani, liko katika kiini cha kauli ya Bw Khan ambapo anaweka wazi uhalali wake wa kuomba hati za kukamatwa.
"Hakuna askari wa miguu, hakuna kamanda, hakuna kiongozi wa kiraia - hakuna mtu - anayeweza kuchukua hatua bila kuadhibiwa." Sheria, anasema, haiwezi kutumika kwa kuchagua. Hilo likitokea, "tutakuwa tunatengeneza mazingira ya kuporomoka kwake".
Ni uamuzi wa kushikilia mienendo ya pande zote mbili hadi kiolezo cha sheria ya kimataifa ambayo inasababisha hasira nyingi, na sio tu katika Israeli.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema ilikuwa "ukasiri" kutuma maombi ya hati za kukamatwa. Hakukuwa na "usawa - hakuna - kati ya Israeli na Hamas".
Hamas ilitaka kuondolewa kwa madai dhidi ya viongozi wake, ikidai kuwa mwendesha mashtaka wa ICC "analinganisha mwathiriwa na mnyongaji". Ilisema ombi la kutoa hati za kukamatwa kwa uongozi wa Israel lilikuja miezi saba kuchelewa, baada ya "ukaaji wa Israel kufanya maelfu ya uhalifu".
Bw Khan hafanyi ulinganishi wa moja kwa moja kati ya pande hizo mbili, isipokuwa kuweka madai yake kwamba zote zimefanya msururu wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Pia anasisitiza kwamba vita hivi vya hivi punde vinakuja katika muktadha wa "mgogoro wa kimataifa wa silaha kati ya Israel na Palestina, na mgogoro wa silaha usio wa kimataifa kati ya Israel na Hamas".
Mahakama hiyo inaichukulia Palestina kama taifa kama ilivyo na hadhi ya mwangalizi katika Umoja wa Mataifa, jambo ambalo lilimaanisha kuwa iliweza kujiandikisha kwa Mkataba wa Roma uliounda ICC.
Bwana Netanyahu ametangaza kuwa Wapalestina kamwe hawatapata uhuru kwa macho yake.

Chanzo cha picha, Reuters
Badala ya kuona fedheha na uwongo , kama Rais wa Israel Isaac Herzog alivyosema, "magaidi hawa wakorofi na serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Israel", mashirika ya haki za binadamu yamepongeza jinsi mwendesha mashtaka wa ICC anavyotaka kutumia sheria kwa pande zote mbili.
Shirika kuu la kutetea haki za binadamu la Israel, Btselm, lilisema vibali hivyo vinaashiria "kuporomoka kwa kasi kwa Israeli katika dimbwi la maadili".
"Jumuiya ya kimataifa inaashiria Israeli kwamba haiwezi tena kudumisha sera yake ya ghasia, mauaji na uharibifu bila uwajibikaji," iliongeza.
Wanaharakati wa haki za binadamu wamelalamika kwa miaka mingi kwamba nchi zenye nguvu za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zinafumbia macho ukiukwaji wa sheria za kimataifa za Israel, hata kama zinalaani na kuyawekea vikwazo mataifa mengine ambayo hayako katika kambi yao.
Hatua zinazochukuliwa na Bw Khan na timu yake, wanaamini, zimepitwa na wakati.
Bw Khan anasema kwamba viongozi watatu wakuu wa Hamas walifanya uhalifu wa kivita ambao ni pamoja na kuangamiza jamii, mauaji, utekaji nyara, ubakaji na mateso.
Watu hao waliotajwa ni Yahya Sinwar, kiongozi wa Hamas huko Gaza, Mohammed Deif, kamanda wa Brigedi za Qassam, tawi lake la kijeshi, na Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas.
Kama sehemu ya uchunguzi wao, Karim Khan na timu yake waliwahoji waathiriwa na manusura wa shambulio la Oktoba 7.
Alisema Hamas imeshambulia maadili ya kimsingi ya binadamu: "upendo ndani ya familia,mafungamano ya ndani kabisa kati ya mzazi na mtoto vilivurugwa na kusababisha uchungu usiopimika kupitia ukatili ulioendelezwa kwa muda mrefu na mkubwa".
Israel, Bw Khan alisema, ina haki ya kujilinda. Lakini "uhalifu usio na fahamu" hau "kuiondolea Israeli wajibu wake wa kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu".
Kushindwa kufanya hivyo, alisema, kulihalalisha kutoa vibali vya kukamatwa kwa Bw Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na kusababisha njaa kwa raia kama silaha ya vita, mauaji, maangamizi na mashambulizi ya kukusudia dhidi ya raia.
Tangu kuanza kwa mashambulio ya Israel kama jibu dhidi ya mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, Rais Biden ametoa msururu wa tahadhari kwa Israel, akionyesha wasiwasi wake kwamba inaua raia wengi wa Palestina na kuharibu miundombinu mingi ya raia huko Gaza.
Lakini katika kitendo cha kusawazisha kwa uangalifu na mshirika wake wa karibu ambaye amekuwa akimuunga mkono kila wakati, Bw Biden na utawala wake hawajaeleza hadharani wanachomaanisha.
Bw Khan anaweka wazi tafsiri yake. Israel, anasema, imechagua njia za uhalifu kufikia malengo yake ya vita huko Gaza - "yaani, kusababisha vifo kwa makusudi, njaa, mateso makubwa na majeraha mabaya" kwa raia.
Jopo la majaji katika ICC sasa litazingatia iwapo litatoa hati za kukamatwa. Mataifa yaliyotia saini Mkataba wa Roma wa ICC basi yatalazimika kuwaweka kizuizini watu hao ikiwa watapata fursa.
Nchi 124 zilitia sani mkataba wa kuundwa kwa mahakama hiyo lakini Urusi, Uchina, Marekani na Israel hazijatia kwenye mkataba huo.
Lakini ICC imeamua kuwa ina mamlaka ya kisheria kushtaki vitendo vya uhalifu katika vita hivyo kwa sababu Wapalestina ni walisaini mkataba huo.
Ikiwa hati za kukamatwa zitatolewa, itamaanisha kuwa Bw Netanyahu, waziri mkuu aliyekaa mamlakani kwa muda mrefu zaidi wa Israel, hataweza kuwatembelea washirika wa karibu wa nchi za Magharibi bila hatari ya kukamatwa kwake.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema hatua za ICC "hazina msaada katika kusimamisha mapigano, kupata mateka au misaada ya kibinadamu." Lakini ikiwa vibali hivyo vitatolewa, Uingereza italazimika kuwakamata watu hao, isipokuwa kama inaweza kufanikiwa kudhihirisha kuwa Bw Netanyahu ana kinga ya ya kidiplomasia.
Muhimu zaidi kwa Bw Netanyahu na Bw Gallant ni Marekani. Ikulu ya White House inaamini kuwa ICC haina mamlaka katika mzozo huo, msimamo ambao unaweza kupanua mgawanyiko ndani ya chama cha Joe Biden cha Democratic kuhusu vita.
Washirika wakuu wa Israel miongoni mwa Wanademokrasia wanaweza kuunga mkono hatua ya Republican kupitisha sheria ya kuwawekea vikwazo maafisa wa ICC au kuwawekea marufuku ya kuingia Marekani.
Huku uvumi wa kufunguliwa mashtaka ukizidi kuenea Ulaya, Marekani na Mashariki ya Kati wiki kadhaa zilizopita, kundi la maseneta wa chama cha Republican walitoa tisho la aina hiyo kwa Bw Khan na wafanyakazi wake .
"Lenga Israel na tutakulenga wewe... umeonywa."
Yoav Gallant pia hangeweza kusafiri kwa uhuru. Maneno aliyotumia wakati akitangaza kuwa Israel itaizingira Gaza yamenukuliwa mara kwa mara na wakosoaji wa mwenendo wa Israel.
Siku mbili baada ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba, Bw Gallant alisema: "Nimeamuru kuzingirwa kabisa kwa Ukanda wa Gaza. Hakutakuwa na umeme, hakuna chakula, hakuna mafuta, kila kitu kimefungwa ... tunapambana na wanyama na kutenda ipasavyo".
Bw Khan ameandika katika taarifa yake kwamba "Israeli kwa makusudi na kwa utaratibu imewanyima raia katika maeneo yote ya Gaza vitu vya lazima kwa maisha ya mwanadamu".
Njaa, anasema, iko katika sehemu za Gaza na iko karibu katika zingine.
Israel inakanusha kuwa kuna njaa, ikidai kuwa uhaba wa chakula hausababishwi na kuzingirwa kwao - bali na wizi wa Hamas na uzembe wa Umoja wa Mataifa.
Iwapo hati ya kukamatwa itatolewa kwa Ismail Haniyeh, mkuu wa tawi la kisiasa la Hamas, itabidi afikirie zaidi kuhusu safari zake za mara kwa mara kukutana na viongozi wakuu wa Kiarabu. Ana uwezekano wa kutumia muda mwingi zaidi katika kambi yake nchini Qatar, ambayo kama Israel haikutia saini Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC.
Viongozi wengine wawili wa Hamas wanaoshutumiwa, Yahya Sinwar na Mohammed Deif, wanaaminika kujificha mahali fulani ndani ya Gaza. Hati ya kukamatwa haiongezi sana shinikizo kwao. Israel imekuwa ikijaribu kuwaua kwa muda wa miezi saba iliyopita.
Hati hiyo pia itamweka Bw Netanyahu katika kundi la viongozi wanaotuhumiwa kuwa ni pamoja na Rais wa Urusi Vladmir Putin, na marehemu Kanali Muammar Gaddafi wa Libya.
Bw Putin anakabiliwa na kibali cha kukamatwa kwa uhamisho wa raia wa Ukraine uliotekelezwa kinyume cha sheria na uhamisho wa watoto kutoka Ukraine hadi Urusi.
Kabla ya kuuawa, hati ya kukamatwa kwa Kanali Gaddafi ilikuwa ya mauaji na mateso ya raia wasio na silaha.
Hati ya masitaka ya ICC sio jambo la kufurahisha kwa Benjamin Netanyahu, kiongozi wa serikali ambayo inajivunia demokrasia yake.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












