Bobi Wine aiambia BBC akiwa mafichoni hatapinga matokeo ya uchaguzi wa Uganda mahakamani
Akizungumza na BBC akiwa mafichoni, Bobi Wine alisema ataendelea kumpinga Rais Yoweri Museveni licha ya hofu inayohusiana na usalama wake binafsi.
Muhtasari
- Mauritius yamkosoa Trump kuhusu umiliki wa kisiwa cha Chagos
- Togo yamrejesha rasmi Paul- Henri Sandaogo Damiba nchini Burkina Faso
- Uingereza yatetea makubaliano ya Visiwa vya Chagos baada ya Trump kuita makabidhiano hayo "kitendo cha ujinga mkubwa"
- FARDC yasema 'iliteka' Uvira... Je, hali ikoje katika jiji hili?
- Macron asema vitisho vya ushuru vya Marekani havikubaliki huku Trump akisisitiza mpango wa Greenland
- Bobi Wine aiambia BBC akiwa mafichoni hatapinga matokeo ya uchaguzi wa Uganda mahakamani
- Gen Z wa Korea Kusini wabuni mtindo mpya wa kuwadhihaki watu wa umri wa miaka ya 'arobaini'
- Bunge la Ulaya lawapongeza waandamanaji wa Iran kwa ujasiri wao
- Uwanja wa mpira wa watoto wa Kipalestina wakabiliwa na agizo la kubomolewa na Israel
- Mtoto wa Museveni 'anajigamba' jinsi alivyowaua watu 22 - Bobi Wine
- Tanzania yapanda katika orodha ya timu bora FIFA
- Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania aaga dunia, Rais Samia amuomboleza
- "Sihitaji kurekebisha uhusiano na familia yangu," asema Brooklyn Peltz-Beckham
- Mbunifu wa mitindo wa Italia, Valentino, afariki dunia akiwa na umri wa miaka 93
- Waziri Mkuu wa Hispania aahidi kutafuta chanzo cha ajali mbaya ya treni ya mwendo kasi
- Zaidi ya waumini 160 wametekwa nyara katika mashambulizi dhidi ya makanisa Nigeria – viongozi wa dini
- Trump asema atatekeleza kwa "asilimia 100" tishio la ushuru kwa Greenland, EU yaahidi kulinda maslahi yake
Moja kwa moja
Lizzy Masinga & Mariam mjahid
Mauritius yamkosoa Trump kuhusu umiliki wa kisiwa cha Chagos

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Diego Garcia, kisiwa cha mbali katika Bahari ya Hindi, ni mojawapo ya visiwa 60 hivi vinavyounda Visiwa vya Chagos. Mwanasheria mkuu wa Mauritius amejibu ukosoaji wa Donald Trump wa mkataba wa Chagos, akisisitiza kwamba bado inatarajia makubaliano hayo kuendelea.
Katika taarifa iliyoandikwa, Gavin Glover anasema "ni muhimu kukumbuka" kwamba mpango huo "ulijadiliwa, ulihitimishwa na kutiwa saini pekee kati ya Uingereza na Jamhuri ya Mauritius".
"Uhuru wa Jamhuri ya Mauritius juu ya Visiwa vya Chagos tayari unatambuliwa bila utata na sheria za kimataifa na haipaswi tena kujadiliwa," inasema.
"Tunatarajia mkataba huo kutekelezwa haraka iwezekanavyo, kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa."
Wapinzani wa serikali ya Uingereza wanahoji kwamba kujitoa kwa Visiwa vya Chagos kunawakilisha kitendo cha kujidhuru kitaifa na kuongeza kwa wapinzani wa Uingereza, haswa Uchina.
Hoja hizo ni pamoja na kipengele cha kukunja mikono baada ya ufalme lakini pia hofu kwamba kambi ya Diego Garcia, muhimu kwa Uingereza na Marekani, hivi karibuni itakuwa hatarini zaidi.
Eneo la mbali la kambi hufanya iwe vigumu sana kufuatilia, isipokuwa kutoka kwa anga za juu.
Soma pia:
Togo yamrejesha rasmi Paul- Henri Sandaogo Damiba nchini Burkina Faso

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Paul-Henri Sandaogo Damiba alifukuzwa kazi kutoka kwa jeshi mnamo Novemba 2024, pamoja na maafisa wengine 15, na mamlaka ya kijeshi ya Burkina Faso. Baada ya siku kadhaa za siutafahamu na taarifa zinazokinzana katika vyombo vya habari kuhusu uwezekano wa kukabidhiwa kwake, mamlaka ya Togo imethibitisha rasmi kuwa Paul-Henri Sandaogo Damiba amekabidhiwa kwa serikali ya Burkina Faso.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Haki ya Togo, aliyekuwa rais wa serikali ya mpito ya Burkina Faso alikabidhiwa rasmi tarehe 17 Januari 2026 kwa mamlaka za nchi hiyo.
“Tukizingatia maoni chanya ya chumba cha uchunguzi, Bw. Paul-Henri Sandaogo Damiba alikabidhiwa kwa mamlaka ya Jamhuri ya Burkina Faso tarehe 17 Januari 2026,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Waziri wa Haki wa Togo.
Luteni Kanali Damiba aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwezi Septemba 2022, na baada ya hapo alikimbilia mjini Lomé, Togo, ambako aliishi tangu kuangushwa kwake.
Kwa muda mrefu, mamlaka ya Burkina Faso zilikuwa zikimtuhumu kwa kujaribu kuyumbisha serikali iliyopo madarakani.
Katika taarifa yake, serikali ya Togo ilieleza kuwa ilipokea ombi rasmi la kumkabidhi Damiba tarehe 12 Januari 2026, kutoka kwa mamlaka ya mahakama ya Burkina Faso.
Ombi hilo lilimhusu Damiba, ambaye anakabiliwa na mashtaka mbalimbali, yakiwemo ubadhirifu wa fedha za umma, utajiri usiohalali, rushwa, kuchochea uhalifu na makosa ya jinai, kupokea mali iliyoibwa kwa uzito mkubwa, pamoja na utakatishaji fedha.
Soma pia:
Uingereza yatetea makubaliano ya Visiwa vya Chagos baada ya Trump kuita makabidhiano hayo “kitendo cha ujinga mkubwa”

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, kisiwa cha chagos Serikali ya Uingereza imetetea makubaliano ya Visiwa vya Chagos baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuyakosoa vikali na kuyaita “kitendo cha ujinga mkubwa”.
Katika chapisho aliloweka kwenye jukwaa lake la Truth Social, Trump aliandika: “Inashangaza kwamba mshirika wetu ‘mahiri’ wa NATO, Uingereza, kwa sasa inapanga kukabidhi Kisiwa cha Diego Garcia, eneo lenye kambi muhimu ya kijeshi ya Marekani kwa Mauritius, na kufanya hivyo bila sababu yoyote ile.”
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni “kitendo cha UJINGA MKUBWA”.
Kauli hizo zinaashiria mabadiliko ya msimamo wa Marekani kuhusu makubaliano hayo, ambayo yalitiwa saini Mei mwaka jana.
Wakati huo, utawala wa Trump ulikuwa umepongeza hatua hiyo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, akiitaja kama “mafanikio makubwa sana”.
Serikali ya Uingereza imesema ilichukua hatua hiyo “kwa sababu kambi hiyo ilikuwa iko hatarini”.
Waziri wa Amerika Kaskazini, Stephen Doughty, aliongeza kuwa Uingereza itaikumbusha Marekani kuhusu uimara wa makubaliano hayo katika siku zijazo.
Viongozi wa upinzani nchini Uingereza wamekuwa wepesi kurejesha ukosoaji wao dhidi ya makubaliano ya Chagos.
“Rais Trump yuko sahihi,” alisema kiongozi wa Chama cha Conservative, Kemi Badenoch, akiita makubaliano hayo “kujiharibia kabisa”.
Kwa upande wake, kiongozi wa Reform UK, Nigel Farage, alimpongeza rais wa Marekani kwa “kuyapiga kura ya turufu”.
Nchini Mauritius, Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo aliiambia BBC kuwa “kwa sasa hana maoni”.
Hata hivyo, mwaka jana maafisa wa serikali ya Mauritius waliyasifu makubaliano hayo wakiyataja kama “ushindi mkubwa” kwa taifa hilo.
Soma pia:
FARDC yasema 'iliteka' Uvira... Je, hali ikoje katika jiji hili?

Chanzo cha picha, MONUSCO
Maelezo ya picha, Mtazamo wa angani wa jiji la Uvira Jeshi la serikali ya Congo (FARDC) lilitangaza kuwa limeuteka mji wa Uvira katika jimbo la Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kwamba wanajeshi wake wamekuwa wakidhibiti eneo hilo tangu Jumapili, Januari 18, 2026.
FARDC ilithibitisha hilo katika taarifa yake, baada ya vuguvugu la M23 kujiondoa katika mji huo siku ya Jumamosi, huku wapiganaji wake sasa wakiripotiwa katika maeneo ya Sange na Luvungi, zaidi ya kilomita 10 kaskazini mwa Uvira.
Oscar Balinda, mwanaharakati wa M23 ambaye siku ya Jumatatu alikataa kuiambia BBC walikopiga kambi wapiganaji wa M23 waliokuwa wameondoka Uvira, alisema "bado wako kwenye harakati".
Mkazi mmoja wa mji wa Uvira aliiambia BBC Rwanda kwamba "watu wanafurahi kuwaona tena FARDC", na kuongeza kuwa "tangu wafike tumekuwa tukisikia milio ya risasi, na hadi leo bado tunasikia milio ya risasi".
FARDC iliwashutumu wapiganaji wa M23, wanaodaiwa kushirikiana na vikosi vya Rwanda, kwa kuharibu na kupora kabla ya kuondoka Uvira, madai ambayo Balinda alikanusha katika mahojiano na BBC, akisema kwamba uporaji wote wanaotuhumu M23 ulithibitishwa kuwa bado upo.
Soma pia:
Macron asema vitisho vya ushuru vya Marekani havikubaliki huku Trump akisisitiza mpango wa Greenland

Chanzo cha picha, EBU
Maelezo ya picha, Macron amevaa miwani ili kuficha tatizo la macho, anasema Rais Emmanuel Macron amesema kuwa Ufaransa na Ulaya kwa ujumla zinauthamini waziwazi uhuru na mamlaka ya kitaifa.
Amesema mtazamo huo si wa kizamani, bali ni njia ya kuhakikisha kuwa mafunzo ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia hayasahauliki, huku Ulaya ikiendelea kujitolea kwa ushirikiano kati ya mataifa.
Rais huyo wa Ufaransa amesema ni kwa kuzingatia misingi hiyo ndipo nchi yake imeamua kushiriki katika mazoezi ya kijeshi huko Greenland, akisisitiza kuwa hatua hiyo hailengi kumtishia yeyote, bali ni kumuunga mkono mshirika wake wa Ulaya, Denmark.
Macron pia amekosoa vikali ushindani wa Marekani katika mikataba ya kibiashara, akisema mikataba hiyo inahujumu maslahi ya mauzo ya nje ya Ulaya, inalazimisha Ulaya kutoa masharti mazito kupita kiasi, na kwa wazi inalenga kudhoofisha na kuiweka Ulaya chini ya udhibiti.
Ameongeza kuwa hali hiyo inazidishwa na ongezeko lisilo na kikomo la ushuru mpya, jambo alilolitaja kuwa halikubaliki kabisa.
Amebainisha kuwa hali hiyo inakuwa mbaya zaidi pale ushuru huo unapotumika kama shinikizo dhidi ya mamlaka ya maeneo ya nchi.
Macron amesema Wazungu ndio pekee wasioyalinda ipasavyo makampuni na masoko yao, hasa pale nchi nyingine zinapokiuka kanuni za ushindani wa haki.
Kwa mujibu wake, ushindani wa kiuchumi wa Ulaya uko nyuma ikilinganishwa na Marekani, na amesema kuna haja ya kushughulikia ukosefu wa ukuaji wa uchumi na uwekezaji mdogo.
Soma Pia:
Bobi Wine aiambia BBC akiwa mafichoni hatapinga matokeo ya uchaguzi wa Uganda mahakamani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Bobi Wine hajaonekana hadharani kwa siku kadhaa tangu uchaguzi wa Alhamisi iliyopita uliokuwa na utata Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema hatapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Alhamisi kupitia mahakama, akieleza kukosa imani na mhimili wa haki nchini humo.
Badala yake, amewahimiza wafuasi wake kutumia njia za amani, ikiwemo maandamano ya kisheria, kulinda demokrasia yao.
Akizungumza na BBC akiwa mafichoni, Bobi Wine alisema ataendelea kumpinga Rais Yoweri Museveni licha ya hofu inayohusiana na usalama wake binafsi.
“Mahakama nchini Uganda imepoteza uhuru wake, na tunawahimiza raia kutumia njia zote halali kupinga udhalimu na kulinda demokrasia,” alisema mwanamuziki huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 43.
Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo kwa ushindi mkubwa.
Ameishutumu kambi ya upinzani kwa kujaribu kubatilisha matokeo kwa kutumia vurugu, na kuwaita “magaidi”.
Katika mahojiano hayo, Bobi Wine pia alikosoa vikali vyombo vya usalama kwa kuzuia uingizaji wa chakula katika makazi ya familia yake, ambako mke wake na jamaa zake wanadaiwa kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa vitendo.
Alisema alilazimika kuondoka katika nyumba hiyo, iliyoko katika kitongoji cha mji mkuu Kampala, usiku wa Ijumaa kufuatia uvamizi wa vikosi vya usalama.
Pai Unaweza Kusoma:
Gen Z wa Korea Kusini wabuni mtindo mpya wa kuwadhihaki watu wa umri wa miaka ya 'arobaini'i

Chanzo cha picha, Instagram/@detailance
Maelezo ya picha, Jay anakiri kwamba amekuwa mwangalifu zaidi anapozungumza na vizazi vijana. Ji Seung-ryul, mwenye umri wa miaka 41, anajivunia sana ladha yake ya hali ya juu katika mitindo ya mavazi pamoja na uwezo wake wa kufuatilia mwelekeo wa kisasa.
Hujitahidi kuhakikisha anachapisha picha zake za kujipiga (selfies) mbele ya kioo kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, akiamini kama wengi kwamba kuongezeka kwa idadi ya waliopenda picha (likes) ni ishara ya ustaarabu na uelewa mzuri wa mitindo.
Hata hivyo, alifadhaika alipogundua kuwa wanaume wa rika lake wameanza kuwa walengwa wa dhihaka mtandaoni.
Wengi wanawashutumu kwa kujaribu kujiingiza katika tamaduni na mitindo isiyowahusu, hasa kwa kuvaa mavazi yanayohusishwa na Kizazi cha Gen Z na kizazi cha milenia wachanga.
Vibonzo vya kejeli (meme) vilivyoundwa kwa kutumia akili bandia (AI) vimesambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, vikimuonyesha mwanaume wa makamo aliyevaa mavazi ya mitaani huku akishika simu ya iPhone.
Taswira hii inawakilisha kundi ambalo vijana hulirejelea kwa jina la “walioko katika miaka ya arobaini”. Mitindo yao ya mavazi, hususan fulana, imegeuzwa kuwa chanzo cha dhihaka na chuki miongoni mwa baadhi ya vijana.
Kang, mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka arobaini anayejulikana kwa umaridadi wake, anaamini kuwa kiini cha meme ya “kijana wa miaka arobaini” kinatokana na hisia ya msingi ya kibinadamu.
Anasema: “Kadiri mtu anavyoendelea kuzeeka, ndivyo hamu ya kurejea au kudumisha ujana inavyoongezeka. Tamaa ya kuonekana kijana si ya kizazi kimoja pekee, bali ni jambo linaloshirikiwa na vizazi vyote.”
Soma Pia:
Bunge la Ulaya lawapongeza waandamanaji wa Iran kwa ujasiri wao

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku ya Jumatatu, Januari 19, Rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola aliwaambia wajumbe katika kikao cha hadhara.
"Najua wengi wenu mngependa kutoa heshima kwa maelfu ya watu waliouawa katika mitaa ya Iran kwa ukimya, lakini watu wa Iran hawana haja ya kunyamaza.Wamelazimishwa kufanya hivyo kwa miaka 47. Kwa hiyo leo ninawaomba kufanya kitu tofauti.
''Nataka ninyi muungane nami katika kupiga makofi na kutoa heshima kwa wale wote ambao wana ujasiri chini ya paa lao na kupongeza kwa ujasiri chini ya hili. kufa.”
Wabunge wa Bunge la Ulaya walisimama na kupiga makofi kwa takriban dakika moja kufuatia ombi hili.
Tarehe 12 Januari Bunge la Ulaya lilipiga marufuku wanadiplomasia na wawakilishi wengine wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuingia katika majengo yake.
Roberta Metsola, Rais wa Bunge la Ulaya, alitangaza kwamba alichukua uamuzi huu kutokana na ukandamizaji mkali wa maandamano ya kuipinga serikali nchini Iran.
Soma pia:
Uwanja wa mpira wa watoto wa Kipalestina wakabiliwa na agizo la kubomolewa na Israel

Maelezo ya picha, Mamlaka ya Israel imeamuru klabu ya soka kutenganisha uwanja, au wataubomoa Uwanja wa mpira wa watoto wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa unakabiliwa na tishio la kubomolewa hivi karibuni, licha ya kampeni ya kimataifa ya kuununua.
Wanaounga mkono wanasema uwanja huo unatoa fursa adimu ya michezo kwa wachezaji vijana wa Kipalestina.
Hata hivyo, Israel inasisitiza kuwa umejengwa bila vibali vinavyohitajika. Katika ardhi hii iliyogawanyika kwa kina, mambo mengi yanapinganiwa; kuanzia utambulisho na imani za watu wanaoishi hapa, hadi kila inchi ya ardhi wanayosimamia.
Hivi karibuni, mzozo huo umejumuisha pia kipande kidogo cha nyasi bandia kilichowekwa chini ya kivuli cha ukuta mkubwa wa zege unaoitenga Israel na sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Huko Bethlehem, klabu ya mpira, inayodai kuwa ilipata ruhusa ya mdomo mwaka 2020 kwa ajili ya uwanja huo inaamini kuwa tishio la kubomolewa linahusiana zaidi na mambo kuliko sheria za mipango miji.
“Waisraeli hawataki tuwe na aina yoyote ya matumaini, hawataki tuwe na fursa yoyote,” Mohammad Abu Srour, mmoja wa wajumbe wa bodi ya Kituo cha Vijana cha Aida, aliniambia.
Wazo, alidokeza, ni kufanya maisha kuwa magumu kwa makusudi.
“Mara tu tunapopoteza matumaini na fursa, tutaondoka. Hii ndiyo maelezo pekee kwetu.” Tuliwasiliana na chombo cha Israel kinachosimamia masuala ya kiraia katika Ukingo wa Magharibi ili kupata maoni.
Ingawa agizo la kubomolewa lilitolewa kwa niaba yake, tulielekezwa badala yake kwa jeshi la Israel, ambalo linasimamia kazi zake.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitupa taarifa ifuatayo: “Kando ya uzio wa kiusalama, kuna agizo la kutaifisha na marufuku ya ujenzi; kwa hiyo, ujenzi katika eneo hilo ulifanywa kinyume cha sheria,” ilisema.
Wanaposubiri kuona kitakachofuata, watoto wa Aida wanatumaini kuwa uangalizi wa kimataifa unaweza kutosha kubadilisha mawazo ya mamlaka.
Lakini kwa sasa, wakati mgogoro mpana ukiendelea, mustakabali wa uwanja mmoja mdogo wa mpira uko hatarini.
Soma zaidi:
Mtoto wa Museveni 'anajigamba' jinsi alivyowaua watu 22 - Bobi Wine

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, anadai kuwa watu zaidi ya 100 wameuawa tangu wiki iliyopita na sio 22 kama alivyoandika mtandaoni mtoto wa Rais Yoweri Museveni na Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
''Jana usiku mtoto wa Museveni alipokuwa akitoa vitisho vya kuniua alionekana ''kufurahishwa'' na hatua ya kuuawa kwa wafuasi wetu 22 (kwa kweli, amewaua zaidi ya 100 tangu wiki iliyopita)'', aliandika kwenye mtandao wa X, alipokuwa akijibu vitisho vilivyotolewa dhidi yake na Jenerali Muhoozi.
Bobi Wine pia anasema wanajeshi wamezingira boma lake na kuwaamuru watu wote waliokuwa ndani ya nyumba hiyo kutoka nje kama ni wanaume.
Wine hajaonekana hadharani kwa siku kadhaa na anasema amejificha, akidai alitoroka uvamizi wa polisi nyumbani kwake.
Jenerali Muhoozi Kainerugaba amempa saa 48 kiongozi huyo wa upinzani kujisalimisha kwa polisi.
Polisi wa Uganda hata hivyo wanasema kuwa Bobi Wine bado yuko nyumbani na amewazuia waandishi wa habari kukaribia makazi hayo.
Pia uanweza kusoma:
Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania aaga dunia, Rais Samia amuomboleza

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu mzee Edwin Mtei akimkumbuka kuwa mmoja wa watumishi na viongozi wenye mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa kwenye eneo la fedha, uchumi na mipango.
Mzee Mtei alihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (1966-1974).
Aidha Rais Samia amesema Mzee Mtei ataenziwa katika historia ya siasa ya vyama vingi kama miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, pia mmoja wa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Akizungumza na Mwananchi, Freeman Mbowe ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema, amesema Mzee Mtei ameugua kwa kipindi kirefu na hali yake ilibadilika ghafla na wakati wanamchukua kwa gari la wagonjwa kumpeleka hospitali ya Seliani alifariki dunia akiwa njiani. Mwananchi imeripoti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche imeeleza kuwa chama hicho kimepoteza moja ya nguzo imara.
Tanzania yapanda katika orodha ya timu bora FIFA

Chanzo cha picha, Taifa stars instagram
Shirikisho la kimataifa la soka FIFA limetoa orodha mpya ya timu bora za soka mwaka huu wa 2026.
Morocco wamepanda kwa kiwango kikubwa zaidi katika timu za wanaume wakifika hadi nafasi ya nane,licha ya kupoteza katika fainali ya michuano ya soka barani Afrika AFCON dhidi ya Senegal.
Senegal walipanda hadi kufika nafasi ya 12 kutoka nafasi ya 17 waliyopata mwaka 2024.
Mwaka jana Morocco walikuwa katika nafasi ya 11, na nafasi bora waliyowahi kushika katika orodha hiyo ya FIFA ni 10 ikiwa ni mwaka 1998.
Hata hivyo timu ya Afrika iliyowahi kuchukua nafasi bora zaidi kwenye orodha hiyo ni Nigeria iliyokuwa nafasi ya 5 Aprili mwaka 1994.
Michuano ya AFCON ya 2025 imekuwa na ushawishi mkubwa katika soka la kimataifa na hivyo kuchangia timu nyingi za Afrika kupanda orodha hiyo.
Washindi wa shaba katika dimba hilo Nigeria wameorodheshwa katika nafasi ya 26 ,Cameroon nao wako katika nafasi ya 45 nao Misri waliotolewa nusu fainali wameorodheshwa nafasi ya 31 wakiwa wamepanda kwa alama nne pia wakiwa nafasi tatu nyuma ya Algeria.
Gabon waliporomoka kwa alama nyingi hadi nafasi ya 86 baada ya kutolewa mapema kwenye dimba la Afcon.
Mabingwa wa Ulaya Hispania wanaongoza orodha hiyo mbele ya bingwa wa dunia Argentina walio nafasi ya pili.
Ufaransa ni watatu wakifuatwa na England nafasi ya 4 huku Brazil wakishikilia nafasi ya 5.
Ureno na Uholanzi wako nafasi ya sita na saba mtawalia.
Je timu za Arika Mashariki ziko wapi?
Taifa stars ya Tanzania imepanda kwa nafasi mbili na kufikia nafasi ya 110 baada ya kushamiri kwenye dimba la Afcon wakitoka hatua ya raundi ya16 mara ya kwanza kwenye historia.
Uganda nao wameshuka kwa nafasi tatu baada ya kuboronga kwenye AFCON,wameorodheshwa nafasi ya 88 baada ya kushindwa kushinda hata mechi moja kwenye michuano hiyo.
Harambee star s wa Kenya wamedorora kwenye orodha hiyo baada ya kukosa kushiriki Afcon kwa mara ya tatu,wako nafasi ya 113.
Unaweza kusoma;
“Sihitaji kurekebisha uhusiano na familia yangu,” asema Brooklyn Peltz-Beckham

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Sir David na Lady Victoria Beckham hawajawahi kuthibitisha hadharani mgogoro uliokuwa ukiripotiwa sana na mtoto wao mkubwa na mke wake, Nicola. Brooklyn Peltz-Beckham amesema kuwa hataki “kurekebisha” uhusiano wake na familia yake, katika maoni yake ya kwanza hadharani akijibu ripoti kuhusu uhusiano wake na wazazi wake.
Katika mfululizo wa machapisho kwenye Instagram, mtoto wa kwanza wa Sir David Beckham na Lady Beckham aliwalaumu wazazi wake kwa “kumshambulia” yeye na mkewe kwenye vyombo vya habari, akisema walijaribu “bila kuchoka kuharibu” uhusiano wake na Nicola Peltz Beckham.
Baada ya miezi ya uvumi kuhusu mgogoro katika familia yenye hadhi kubwa, alisema kuwa alijaribu kuweka hali hiyo kuwa ya faragha lakini hakuwa na namna isipokuwa kuzungumza mwenyewe na kusema ukweli.
BBC imewasiliana na wawakilishi wa Sir David na Lady Beckham kwa maoni. Wawili hao hawajawahi kuthibitisha kuwepo kwa mgongano huo.
“Nimekuwa kimya kwa miaka na nimefanya kila jitihada kuweka mambo haya kuwa ya faragha,” alisema mwanamitindo mwenye umri wa miaka 26 katika mfululizo wa machapisho kwa wafuasi wake milioni 16.
“Kwa bahati mbaya, wazazi wangu na timu yao wameendelea kwenda kwa vyombo vya habari, na kuniacha bila chaguo ila kuzungumza mwenyewe na kusema ukweli kuhusu baadhi tu ya uongo uliochapishwa.
“Sihitaji kurekebisha uhusiano na familia yangu. Siko chini ya udhibiti wowote, ninasimama kwa ajili yangu mwenyewe kwa mara ya kwanza maishani mwangu.”
Aliongeza: “Hivi karibuni, nimeona kwa macho yangu binafsi jitihada wanazofanya kueneza uongo mwingi katika vyombo vya habari, mara nyingi kwa kuharibu watu wasio na hatia, ili kuhifadhi taswira yao wenyewe. Lakini naamini ukweli daima hujitokeza.”
Mbunifu wa mitindo wa Italia, Valentino, afariki dunia akiwa na umri wa miaka 93

Chanzo cha picha, Reuters
Mbunifu mashuhuri wa mitindo kutoka Italia, Valentino Garavani, anayejulikana kama Valentino, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93.
Akiwa mmoja wa magwiji wa mitindo ya karne ya 20, mavazi ya Valentino yalivaliwa na watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa, akiwemo Elizabeth Taylor, Nancy Reagan, Sharon Stone, Julia Roberts na Gwyneth Paltrow.
Alishiriki kuanzisha jumba la mitindo la Valentino mwaka 1960, na alihesabiwa pamoja na Giorgio Armani na Karl Lagerfeld kama miongoni mwa wabunifu wakubwa kabisa katika taaluma hiyo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye Instagram, Taasisi ya Valentino Garavani na Giancarlo Giammetti ilisema: “Alifariki kwa amani nyumbani kwake mjini Roma, akiwa amezungukwa familia yake.”
Taasisi hiyo ilisema kuwa mwili wa Valentino utapatiwa heshima ya mwisho katika Piazza Mignanelli mjini Roma kati ya tarehe 21 na 22 Januari.
Ibada ya mazishi ya Valentino itafanyika siku inayofuata katika Basilika ya Mtakatifu Maria wa Malaika na Mashahidi, kwa mujibu wa taasisi hiyo.
Valentino alizaliwa katika eneo la Lombardy mwezi Mei mwaka 1932, na alijulikana kwa mitindo iliyodhihirisha anasa, utajiri na fahari kubwa.
Waziri Mkuu wa Hispania aahidi kutafuta chanzo cha ajali mbaya ya treni ya mwendo kasi

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, ameahidi kufuatilia kwa kina sababu za treni mbili za mwendo kasi kugongana kusini mwa Hispania, ajali iliyosababisha vifo vya takribani watu 40, huku waokoaji wakiendelea kuchunguza mabaki ya treni hizo.
Baada ya kutembelea eneo la ajali, Sánchez pia alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya waathiriwa.
Zaidi ya watu 120 wengine walijeruhiwa baada ya mabehewa ya treni iliyokuwa ikielekea Madrid kuacha reli na kuvuka hadi njia ya reli ya upande wa pili, kisha kugongana na treni nyingine iliyokuwa ikisafiri kuelekea Adamuz, Jumapili jioni.
Ajali hiyo ni mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Mwendeshaji wa mtandao wa reli, Adif, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 19:45 kwa saa za huko (18:45 GMT) siku ya Jumapili, takribani saa moja baada ya moja ya treni kuondoka Málaga kuelekea kaskazini hadi Madrid, ilipoacha reli katika sehemu ya reli iliyonyooka karibu na mji wa Córdoba.
Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Óscar Puente, nguvu ya mgongano ilisukuma mabehewa ya treni ya pili hadi kwenye tuta la udongo. Aliongeza kuwa wengi wa waliopoteza maisha na kujeruhiwa walikuwa katika mabehewa ya mbele ya treni ya pili, ambayo ilikuwa ikisafiri kusini kutoka Madrid kuelekea Huelva.
Timu za uokoaji zilisema mabaki ya treni yaliyopinda na kuharibika vibaya yalifanya iwe vigumu kuwaokoa watu waliokuwa wamenaswa ndani ya mabehewa.
Sánchez alitembelea eneo la ajali hiyo pamoja na maafisa wakuu wa serikali siku ya Jumatatu alasiri.
Zaidi ya waumini 160 wametekwa nyara katika mashambulizi dhidi ya makanisa Nigeria – viongozi wa dini

Chanzo cha picha, Getty Images
Makundi yenye silaha yamewateka nyara makumi ya watu waliokuwa wakihudhuria ibada katika makanisa mawili katika jimbo la Kaduna, Nigeria, kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa kanisa alisema waumini zaidi ya 160 walitekwa nyara na watu wenye silaha wakati wa ibada ya Jumapili.
Hili ni tukio la hivi karibuni katika wimbi la utekaji nyara wa halaiki nchini Nigeria, ambapo Wakristo na Waislamu wote wamekuwa wakilengwa.
Makundi hayo, yanayojulikana kijijini kama “bandits”, mara kwa mara hufanya mashambulizi kama hayo katika maeneo ya kaskazini na kati mwa nchi ili kupata fedha za fidia.
Akielezea shambulio la Jumapili, polisi wa eneo hilo walisema watu waliokuwa na “silaha za kisasa” waliingia kwa nguvu katika makanisa hayo mawili yaliyopo Kurmin Wali, jamii ya msituni katika kata ya Afogo, mnamo saa 11:25 kwa saa za huko.
“Washambuliaji walikuja kwa idadi kubwa, wakaziba njia za kuingia makanisani na kuwalazimisha waumini kutoka na kuingia porini,” alisema Mchungaji Joseph Hayab, mkuu wa Shirika la Kikristo la Nigeria (CAN) kwa kanda ya kaskazini, alipoliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu.
Akizungumza na Reuters, Hayab aliongeza: “Taarifa nilizopokea kutoka kwa wazee wa makanisa zinaeleza kuwa waumini 172 walitekwa nyara, huku tisa wakifanikiwa kutoroka.”
Mwezi Novemba, wanafunzi na walimu zaidi ya 300 walitekwa nyara kutoka shule moja ya Kikatoliki. Baadaye waliachiliwa kwa makundi mawili tofauti. Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa msururu wa matukio ya utekaji nyara yaliyopewa uzito mkubwa na vyombo vya habari vya kimataifa.
Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama, zikiwemo utekaji nyara wa kuomba fidia unaofanywa na magenge ya kihalifu, uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kaskazini-mashariki, ghasia za kujitenga kusini-mashariki, pamoja na mapambano kati ya wafugaji na wakulima katika eneo la kati juu ya upatikanaji wa ardhi na maji.
Unaweza kusoma;
Trump asema atatekeleza kwa “asilimia 100” tishio la ushuru kwa Greenland, EU yaahidi kulinda maslahi yake

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Kaja Kallas, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), alisema kuwa umoja huo “hauna nia ya kuanzisha mzozo, lakini utasimama kidete kulinda msimamo wake.” Donald Trump ameapa "100%" kutekeleza tishio lake la kutoza ushuru kwa nchi za Ulaya zinazopinga ombi lake la kuchukua udhibiti wa Greenland.
Washirika wa Ulaya wameungana kuunga mkono uhuru wa Greenland.
Waziri wa mambo ya nje wa Denmark alisisitiza kwamba rais wa Marekani hawezi kutishia kumiliki eneo la Denmark.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper alisisitiza msimamo wa Uingereza kwamba mustakabali wa Greenland ni kwa "Wagreenland na Wadenmark pekee" kuamua.
Siku ya Jumatatu, Trump alikataa kuondoa mpango wa matumizi ya nguvu na akasisitiza kwamba ataendelea na ushuru unaotishiwa kwa bidhaa zinazofika Marekani kutoka Uingereza na nchi nyingine saba washirika wa NATO.
Alipoulizwa na NBC News kama angeweza kutumia nguvu kuiteka Greenland, Trump alijibu: “Hakuna maoni.”
Rais wa Marekani alisema atatoza Uingereza ushuru wa asilimia 10 kwa “bidhaa zote bila ubaguzi” zitakazopelekwa Marekani kuanzia tarehe 1 Februari, na ushuru huo utaongezeka hadi asilimia 25 kuanzia tarehe 1 Juni, hadi pale makubaliano yatakapofikiwa ya Washington kuichukua Greenland kutoka Denmark.
Trump alisema hatua hiyo hiyo itatumika kwa Denmark, Norway, Sweden, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Finland, nchi zote ambazo ni wanachama wa muungano wa Nato ulioanzishwa mwaka 1949.
Alipoulizwa kama atatekeleza tishio hilo la ushuru, Bw Trump aliambia NBC News: “Nitafanya hivyo, asilimia 100.”
Unaweza kusoma;
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo
