Qatargate: Netanyahu ahojiwa na kitengo maalum, washauri wake wakamatwa. Nini kiini cha kashfa hii?

Chanzo cha picha, AFP
Katika siku za hivi karibuni, matukio kadhaa yametokea nchini Israel ambayo yanahusiana moja kwa moja na kashfa hiyo inayojulikana kwa jina la Qatargate. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliulizwa kuhusu kesi hii Jumatatu jioni.
Alitoa ushahidi katika ofisi yake mjini Jerusalem kwa wachunguzi kutoka Kitengo cha Uhalifu Mkubwa. Ilimbidi aondoke katika Mahakama ya Wilaya ya Tel Aviv mapema Jumatatu asubuhi, ambako alikuwa akitoa ushahidi katika kesi nyingine ya jinai dhidi yake ya mashtaka ya rushwa.
Hata hivyo, mchakato huo sasa unaonekana kuwa mdogo ukilinganisha na Qatargate, uchunguzi wa madai ya kuhusika kwa washauri wa waziri mkuu katika kuishawishi Qatar.
Netanyahu mwenyewe kwa sasa ameorodheshwa katika uchunguzi kama shahidi, sio mshukiwa. Hata hivyo, siku ya Jumatatu, polisi waliwakamata wasaidizi wake wawili wakuu, Jonathan Urich na Eli Feldstein, ambao ni washukiwa wakuu.
Kulingana na vyanzo vya habari vya Israel, ushahidi wa Netanyahu utachunguzwa kwa makini, na baada ya hapo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itaamua iwapo kuna sababu za kubadilisha hadhi ya waziri mkuu katika kesi hii.
Ni nini kilikuwa msukumo kwa Qatargate?

Chanzo cha picha, NurPhoto
Uchunguzi huo ulianzishwa baada ya kuibuka tuhuma kwamba msemaji wa sasa wa IDF na ofisi ya mahusiano na vyombo vya habari, Eli Feldstein, aliwahi kuwa kama daraja la kuunganisha kampuni ya kimataifa iliyosajiliwa na ile ya Doha inayokuza maslahi ya Qatar na serikali ya Israel.
Kulingana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu, kupitia kwake, bidhaa za Qatar zilipandishwa kwa kutumia vyombo vya habari vya Israeli ambavyo viliboresha sura ya nchini Israeli. Aidha alisaidia kuwasilisha miradi ya biashara ya Qatar kwa njia nzuri kwa biashara za Israeli.
Kulingana na wachunguzi, mshauri mwingine wa ngazi ya juu wa Waziri Mkuu, Jonathan Urich, aliletwa hivi karibuni katika mpango huo, na wote wawili walipokea pesa kwa huduma zao kutoka kwa Mmarekani, Jay Footlick, ambaye aliiwakilisha kampuni huko Doha.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mapema mwezi Machi, polisi waliwahoji Feldstein na Urich kwa tuhuma za mawasiliano na wakala wa kigeni, ulaghai, utakatishaji fedha na hongo. Kutokana na amri ya mahakama kuzuia kufichuliwa kwa taarifa nyeti zinazohusiana na kesi hiyo, maelezo zaidi hayajajulikana.
Hata hivyo, Feldstein anaripotiwa kukabiliwa na mashtaka ya kuharibu usalama wa taifa la Israel kuhusiana na uvujaji wa nyaraka za siri za IDF.
Pamoja na Urich na Feldstein, Israel Einhorn, mshauri mkuu wa zamani wa kampeni ya uchaguzi ya chama cha Netanyahu cha Likud, pia anahusika katika kesi hiyo.
Uchunguzi huo ulichochewa na kuchapishwa na mfanyabiashara wa Israel Gil Birger, mtu mwenye maslahi makubwa katika Ghuba, ambaye ilionyesha kwamba alisaidia kuhamisha fedha kwa Feldstein kutoka kwa mshawishi wa serikali ya Qatar.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu ilianza uchunguzi, ambapo waandishi wa habari kadhaa walihojiwa. Mmoja wao anashukiwa kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na washawishi wa Qatar, ambaye anatajwa katika kesi kama "wawakala wa kigeni."
Kulingana na vyanzo vya polisi vilivyoliambia gazeti la Times of Israel, uchunguzi huo umejikita zaidi katika madai ya malipo ya Qatari kwa jamaa wa Netanyahu kati ya Mei 2022 na Oktoba 2024.
Waliohusika katika uchunguzi wamefutwa kazi

Chanzo cha picha, AFP
Mshirika wa karibu wa Benjamin Netanyahu anakanusha shutuma zote, lakini hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa za serikali kujaribu kuzima uchunguzi huo huku tuhuma za wapinzani wa waziri mkuu zikiendelea kuongezeka.
Mnamo Machi 21, ilijulikana kuwa Netanyahu alimfukuza kazi mkuu wa kitengo cha ujasusi cha Shin Bet, Ronen Bar, na alifanya hivyo licha ya agizo la Mahakama ya Juu.
Kufutwa kazi kwa mkuu wa shirika la ujasusi katika nchi kama Israel ni hatua mbaya sana.
Sababu rasmi zilizotolewa kwa hili ni kupoteza uaminifu na "kutofaulu kwa operesheni" ambayo iliwezesha shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7, 2023.
Lakini Bar mwenyewe na wafuasi wake wanaamini kutimuliwa kwake kumechochewa kisiasa na kuhusishwa na ukweli kwamba Shin Bet anachunguza kuhusika kwa washauri wa waziri mkuu katika kushawishi maslahi ya Qatar.
Mahakama ya Juu iliamuru uamuzi wa Bar kusimamishwa, lakini hivi karibuni Netanyahu alimtaja mkuu mpya wa ujasusi.
Jaribio lililofuata la hadhi ya juu la kuwaondoa waliohusika katika uchunguzi huo lilikuwa ni kuanzishwa kwa mchakato wa kumwondoa madarakani Mwendesha Mashtaka Mkuu Gali Baharav-Miaru.
Baraza la mawaziri la Israel kwa kauli moja liliidhinisha kura ya kutokuwa na imani na mwanasheria mkuu mnamo Machi 23, siku mbili baada ya mkuu wa Shin Bet kufutwa kazi.
Netanyahu mwenyewe hakushiriki katika kura hiyo. Kutokana na mgongano wa kimaslahi, haruhusiwi kushiriki katika mijadala inayohusiana na mfumo wa sheria.
Badala yake, utaratibu wa kumwondoa Baharav-Miara madarakani uliongozwa na Waziri wa Sheria wa nchi hiyo, Yariv Levin.
Alikuwa Baharav-Miara ambaye, mwishoni mwa Februari mwaka huu, aliagiza Shin Bet na polisi kufanya uchunguzi kuhusu Qatargate.















